Benjamin Netanyahu hospitalini kabla ya kura kuu ya mageuzi tata ya mahakama Israeli
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amefanyiwa upasuaji wa dharura wa kuweka kifaa cha kudhibiti moyo, baada ya kufikishwa hospitalini Jumamosi usiku.
Madaktari katika Kituo cha Matibabu cha Sheba walisema matibabu yalifanyika vizuri na hayuko katika hali ya kutishia maisha.
Kulazwa kwa Bw Netanyahu kunakuja kabla ya kura kuu ya bunge kuhusu marekebisho tata ya mahakama.
Maandamano ya kupinga mageuzi hayo yameikumba Israel, huku wafanyakazi wengi wakiahidi kugoma iwapo mswada huo utaendelezwa.
Katika hotuba yake ya video kabla ya upasuaji huo wa usiku kucha, Bw Netanyahu alisema alikuwa anahisi "vizuri" lakini anawasikiliza madaktari wake.
Kumekuwa na maswali juu ya afya yake baada ya kulazwa hospitalini wiki iliyopita akidaiwa kuwa na upungufu wa maji mwilini.
Operesheni hiyo ilifanyika vyema "bila matatizo yoyote," Profesa Roy Beinart kutoka Kituo cha Matibabu cha Sheba alisema, akiongeza kuwa Bw Netanyahu "hayuko katika hali ya kutishia maisha".
Ofisi yake ilisema Bw Netanyahu ataachiliwa Jumatatu, lakini safari zilizopangwa kwenda Cyprus na Uturuki zitapangwa upya.
Bw Netanyahu alisema anafaa kuwa mzima vya kutosha kuhudhuria bunge baada ya utaratibu huo. Saa 48 zijazo zinatarajiwa kupigiwa kura muhimu kuhusu mipango ya serikali yake kuhusu mabadiliko katika idara ya mahakama.
Kumekuwa na miezi kadhaa ya maandamano nchini Israel kuhusu mageuzi hayo, ambayo yanalenga kupunguza mamlaka ya Mahakama ya Juu.
Kura hiyo - inayotarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu - itakuwa sawa na mvutano kati ya muungano wenye msimamo mkali wa kidini-kitaifa na makundi ya jamii ya Israel.
Bunge lilianza kujadili mswada huo uliokuwa na upinzani mkubwa siku ya Jumapili.
Siku chache zilizopita zimeshuhudia makumi ya maelfu ya waandamanaji wakiandamana kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem kupinga mabadiliko ya mfumo wa haki, huku watu wakijaza barabara kuu.