Kiongozi wa Wagner Prigozhin yuko Belarus, Lukashenko asema

Kiongozi huyo wa Belarus amenukuliwa akisema "hakikisho la usalama limetolewa", kama alivyoahidi Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Raia wa Uganda waishataki kampuni ya TotalEnergies ya Ufaransa mjini Paris

    Kundi la raia wa Uganda limewasilisha kesi mahakamani dhidi ya kampuni kubwa ya mafuta ya Ufaransa, TotalEnergies mjini Paris, kuhusu miradi miwili mikubwa ya uchimbaji nchini mwao.

    Wanadai ukiukaji wa haki za binadamu na wanataka fidia kwa kunyimwa upatikanaji wa ardhi zao.

    TotalEnergies inaongoza muungano ambao unachimba mamia ya visima vya uchunguzi na kujenga bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,500 (maili 932) ambalo litavuka hifadhi kadhaa za asili nchini Uganda.

    Wakati huo huo, polisi wa Uingereza wamewakamata wanaharakati 27 wa mabadiliko ya tabianchi wanaoandamana kupinga miradi ya Uganda iliyopaka rangi kwenye makao makuu ya TotalEnergies’ London.

  3. Kenya: Awamu ya tatu ya uchunguzi wa maiti ya watu waliokufa Shakahola yakamilika

    Makaburi

    Chanzo cha picha, AFP

    Serikali ya Kenya imekamilisha awamu ya tatu ya uchunguzi wa miili inayoaminika kuwa wafuasi wa dhehebu tata inayoongozwa na Paul Mackenzie Nthenge.

    Shughuli ya uchimbaji wa maiti ilikuwa umesitishwa hadi kupatikane mahali pa kutosha wa kuhifadhi na kuchunguza miili zaidi.

    Kufikia sasa uchunguzui wa miili 338 iliyofukuliwa kwenye msitu mpana wa Shakahola ambao unahusishwa na dhahebu hilo umefanywa.

    Miili 201 kati ya hiyo ilikuwa ya watu wazima.117 ni watoto na 20 haikuweza kutambuliwa kwa sababu ilikuwa imeharibika vibaya.

    Miili 131 ilikuwa wanaume na 185 ilikuwa wanawake kulingana na ripoti ya uchunguzi.

    Maiti 22 ilikuwa imeharibika vibaya na ilikuwa vigumu kutambua jinsia.

    Takriban watu 600 bado hawajulikani walipo, kulingana na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya.

    Mwanapatholojia mkuu wa serikali ya Kenya, Dk. Johansen Oduor, alisema uchunguzi wa maiti ya mshukiwa wa kiongozi wa madhehebu ambaye alifariki akiwa mikononi mwa polisi utafanywa tu baada ya familia ya marehemu kutambua mwili wake.

    "Ni uzoefu wa kipekee ambao tumekuwa nao hapo awali.Kufanya uchunguzi wa miili 338 sio jambo rahisi. Tulichogundua ni kutusaidia kujifunza zaidi kuhusu chanzo cha kifo na mchakato wenyewe,” alisema.

    Ingawa baadhi ya miili ilikuwa na dalili za kunyongwa koo na kiwewe cha nguvu, njaa inasalia kuwa sababu kuu ya kifo.

    Uamuzi wa kujua ni muda gani Mackenzie na washukiwa wengine 28, akiwemo mkewe, watasalia chini ya ulinzi wa polisi itawasilishwa Julai 3.

    Soma zaidi:

    • Madhehebu ni nini na kwa nini watu hujiunga nayo?
    • Dhehebu la Mchungaji Mackenzie Kenya: Mama aliyetoroka msitu wa Shakahola kuokoa watoto wake
    • Paul Makenzi:Mhubiri huyu alianzaje safari tata ya kuwashawishi watu kufunga hadi kufa?
    • Matukio ya ibada hatari zaidi ulimwenguni
  4. Lukashenko asema Prigozhin yuko Belarus -Shirika la habari la serikali

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko amenukuliwa akisema kuwa mwanzilishi wa Wagner Yevgeny Prigozin yuko Belarus, kulingana na shirika la habari la serikali ya Belarus Belta.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Belarus vina maoni zaidi kutoka kwa kiongozi Alexander Lukashenko kuhusu kuwasili kwa mwanzilishi wa Wagner Yevgeny Prigozin nchini humo.

    Kiongozi huyo wa Belarus amenukuliwa akisema "dhamana ya usalama imetolewa", kama alivyoahidi Rais wa Urusi Vladimir Putin.

    "Ninaona Prigozhin amekuwa akisafiri kwa ndege hii - ndio, yuko Belarusi leo," alinukuliwa akisema, akiongeza kuwa atasalia nchini kwa gharama ya kampuni ya Wagner.

    Siku ya Jumamosi, baada ya kusitisha maasi nchini Urusi, Prigozin alikubali mpango wa kuhamia Belarus.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Kundi la Wagner linafadhiliwa na serikali ya Urusi - Putin

    Putin

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Urusi Vladimir Putin, amesema kuwa kundi la mamluki la Wagner "linafadhiliwa kikamilifu" na serikali ya Urusi.

    "Ningependa kila mtu afahamu kwamba kundi zima la Wagner lilifadhiliwa na serikali - na wizara ya ulinzi na bajeti ya serikali.

    Tunafadhili kikamilifu kundi hili," alisema wakati wa mkutano wake kwa vikosi vya usalama kupitia televisheni.

    "Kuanzia Mei 2022 hadi Mei 2023, serikali ililipa kampuni ya Wagner rubles 86.262bn swa na dola bilioni moja za Kimarekani katika malipo na ziada."

    Putin aliongeza mamlaka itachunguza jinsi pesa zilizolipwa kwa Wagner na kiongozi wake zilivyotumika, shirika la habari la Reuters linaripoti.

    Huku hayo yakijiri Rais wa Belarus Alexander Lukashenko amesema anataka kufuatilia uzoefu wa kundi la Wagner katika vita na kujifunza kutoka kwao.

    Makamanda na wapiganaji wa Wagner wataruhusiwa kwenda uhamishoni Belarus pamoja na kiongozi wao, Yevgeny Prigozhin, chini ya makubaliano na Moscow yaliyosimamiwa na Lukasjenko

    "Kama makamanda wao watakuja kwetu na kutusaidia... tuambie ni nini muhimu kwa sasa... hiyo ni ya thamani. Hilo ndilo tunalohitaji kuchukua kutoka kwa Wagner," Lukasjenko alisema wakati wa mkutano na waziri wake wa ulinzi, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.

    Ameongeza kuwa hana sababu yoyote ya kuogopa uwepo wao na kwamba mamlaka ya Belarus "itawafuatilia kwa karibu".

    Pia unaweza kusoma:

  6. Kenya yazindua sajili ya kidijitali ya wahalifu wa ngono

    Jaji Mkuu Martha Koome (kati) alipozindua sajili ya kidijitali Jumatatu

    Chanzo cha picha, Kenya Judiciary/Twitter

    Maelezo ya picha, Jaji Mkuu Martha Koome (wa kati) alipozindua sajili ya kidijitali Jumatatu

    Kenya imezindua sajili ya mtandaoni yenye rekodi ya wahalifu wote wa kingono waliopatikana na hatia ambayo inatarajiwa kuimarisha haki kwa waathiriwa.

    Jaji Mkuu Martha Koome alisema mfumo huu wa hifadhidata "utahakikisha ufikiaji rahisi wa habari kuhusu wahalifu wa ngono waliopatikana na hatia, kuwezesha haki ya haraka".

    Alisema hatua hiyo hii itasaidia mamlaka za haki kuwafuatilia wahalifu wa ngono baada ya kutoka gerezani.

    Umma pia unaweza pia, kupata hifadhidata hii kupiti amaombi. Jaji mkuu alisema hii itawawezesha kuchukua "hatua za tahadhari ili kujilinda wenyewe na watoto wao".

    "Tunatuma ujumbe bayana kwamba jamii yetu haitawavumilia wale wanaowadhulumu walio hatarini. Tutawawajibisha, na hawatafanya matendo yao bila kutambuliwa au kuadhibiwa,” alisema.

  7. Colorado: 'mpiga risasi wa kilabu cha LGBTQ' ahukumiwa vifungo 5 vya maisha na miaka 46 hadi 48 jela

    s

    Novemba 19 mwaka jana, mhalifu aliyepiga risasi na kuwaua watu watano katika klabu ya usiku ya wapenzi wa jinsi moja( LGBTQ) katika jimbo la Colorado, Marekani, alikiri mauaji na kujaribu kuua mnamo tarehe 26 na kuhukumiwa kifungo cha maisha.

    Waathiriwa waliokuwemo katika kilabu hicho kinachofahamika kama Club Q wakati huo walimkosoa mhalifu, Anderson Lee Aldrich (23), kama "mwoga" na "mnyama."

    Waliokuwepo kwenye klabu hiyo walimkabili Aldrich na kufanikiwa kuzuia ufyatuaji zaidi wa risasi kabla ya polisi kufika.

    Watu 17 walijeruhiwa katika tukio hilo, na wengine watano waliuawa: Daniel Aston (28), Derek Lump (38), Kelly Loving (40), Ashley Fau (34) na Raymond Vance (22).

    Aldrich alihukumiwa vifungo vitano vya maisha bila msamaha na vifungo 46 hadi miaka 48 kwa jaribio la kuua. Kwa kuongezea, alisisitiza "jibu la kutoshindana" na mahakama kuhusiana na shtaka kwamba alifanya uhalifu uliochochewa na chuki.

    "Ni uhalifu wa chuki kuwalenga na kuwatendea unyama watu fulani kwa ajili ya uwepo kwao," Jaji Michael McHenry alisema.

    Jaji McHenry alisema hatua za Aldrich "zinaonyesha uovu mkubwa zaidi katika moyo wa mwanadamu," akiongeza, "na ubaya karibu kila mara hutokana na ujinga na woga."

  8. Milionea wa China ashindwa jaribio la 27 la kufaulu mitihani ya kuingia chuo kikuu

    Liang Shi, pichani hapa mwaka wa 2018, amejaribu kufaulu mitihani hiyo mara kadhaa tangu 1983.

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Liang Shi, katika picha hii ya mwaka wa 2018, amejaribu kupita mitihani hiyo mara kadhaa tangu 1983.

    Milionea wa China anasema amefeli mitihani migumu ya kujiunga na chuo kikuu nchini humo kwa mara ya 27.

    Siku ya Ijumaa, Liang Shi mwenye umri wa miaka 56 aligundua kuwa alikuwa amepata alama 424 kati ya 750. Alama hiyo ni pungufu ya pointi 34 ya msingi unaohitajika ili kutuma maombi kwa chuo kikuu chochote nchini China.

    Karibu wanafunzi milioni 13 walifanya mitihani mwaka huu.

    Bw Liang amewahi kuvutia vyombo vya habari nchini hapo awali kuhusiana na juhudi zake za kutafuta elimu ya juu.

    Baada ya kufanyan mitihani hiyo mara kadhaa tangu 1983, Bw Liang aliambia vyombo vya habari vya nchini humo kwamba alisikitishwa na matokeo yake mwaka huu na alikuwa akijiuliza iwapo angewahi kutimiza ndoto yake.

    "Nilikuwa nikisema 'siamini kwamba sitafanikiwa', lakini sasa nimevunjika moyo," mwanamume huyo anayeishi Sichuan alikiambia chombo cha habari cha China Tianmu News.

    Gaokao, mtihani unaojulikana kuwa mgumu, huwajaribu wanafunzi wanaomaliza shule ya upili kwenye masomo yao ya Kichina, hisabati na Kiingereza na somo lingine la sayansi au lile wanalochagua.

    Takwimu za serikali ya China zinaonyesha ni asilimia 41.6 tu ya watahiniwa wa mitihani walifanikiwa kujiunga na vyuo vikuu au vyuo vya kiufundi mnamo 2021.

    Gaokao inaonekana kama fursa ya maisha, hasa kwa wale wanaotoka katika familia maskini, katika nchi ambayo shahada inachukuliwa kuwa muhimu kwa kazi nzuri.

  9. Ukraine huenda imetwaa tena ardhi iliyokaliwa na Urusi tangu 2014-wizara ya Ulinzi ya uingereza

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Vikosi vya Ukraine vina uwezekano mkubwa wa kutwaa tena ardhi katika eneo la Donbas mashariki mwa nchi hiyo linalokaliwa na Urusi tangu 2014, Uingereza inasema.

    Siku ya Jumamosi, kamanda wa Ukraine alisema ardhi ilichukuliwa tena karibu na kijiji kinachokaliwa na Urusi cha Krasnohorivka.

    Vikosi vya anga vimepiga 'hatua ndogo' mashariki kutoka kijiji hicho, huko Donetsk, MoD imesema .

    Inakuja wakati kiongozi wa Ukraine alisema kuwa mashambulio ya nchi yake yalikuwa yanapiga hatua katika nyanja zote.

    Akizungumza wakati wa hotuba yake ya usiku kucha, Volodymyr Zelensky alisema ilikuwa "siku ya furaha" kwa Ukraine lakini hakutoa maelezo au kuzungumza kuhusu maeneo yoyote haswa.

    Mnamo mwaka wa 2014 Urusi iliteka rasi ya Crimea kinyume cha sheria na vikosi vinavyoungwa mkono na Urusi vilichukua udhibiti wa maeneo ya Donetsk na Luhansk yanayopakana na Urusi mashariki.

    Katika taarifa yake ya kila siku ya kijasusi, wizara ya ulinzi ya Uingereza ilisema kuwa maendeleo ya Ukraine mashariki mwa Krasnohorivka ni "moja ya matukio ya kwanza tangu uvamizi wa Urusi Februari 2022 ambapo vikosi vya Ukraine vina uwezekano mkubwa wa kuteka tena eneo lililokaliwa na Urusi tangu 2014".

    Mashambulizi ya wakati huo huo ya Ukraine katika mstari wa mbele wa Donbas - sehemu ya juhudi zake za kukabiliana na mashambulizi - huenda yakazidisha nguvu kutoka kwa wanajeshi wanaotaka kujitenga wa Donetsk na Chechen wanaohudumu katika eneo hili, wizara ya ulinzi ya Uingereza ilisema.

  10. Wagner yajiandaa kukabidhi vifaa vya kijeshi - wizara

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema maandalizi yanaendelea kwa Wagner kukabidhi vifaa vyake vya kijeshi.

    Hii inafuatia uthibitisho wa Vladimir Putin kwamba wanachama wa Wagner, ambao alisema walikuwa wazalendo wa kweli ambao walikuwa wamepotoshwa katika tukio la uhalifu, wanaweza kuchagua kujiunga na jeshi la kawaida, kurudi kwa familia zao, au kwenda Belarusi.

    Wakati huo huo, kama tulivyoripoti ilitangazwa pia kwamba FSB ilikuwa ikiondoa mashtaka yote ya uhalifu dhidi ya wale walioshiriki katika uasi huo, ambao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka kwa uasi wa kutumia silaha.

    Masharti ya makubaliano yaliyofanywa kumaliza uasi wa Wagner sasa yanaibuka na inaonekana kundi hilo la mamluki linavunjwa.

    Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema maandalizi yanaendelea ili Wagner isalimishe silaha nzito na vifaa.

    th

    Vladimir Putin anasema wapiganaji wa kundi hilo wanaweza kuamua kujiunga na jeshi la kawaida, kwenda nyumbani au kuelekea Belarus, ambako ndege ya kibinafsi, inayohusishwa na kiongozi wa Wagner Yegeny Prigozhin ilitua leo asubuhi.Bado haijabainika kama alikuwa ndani ya ndege hiyo.

    Wakati huo huo, Idara ya Usalama ya Urusi, FSB, imesema kwamba wale ambao walikuwa sehemu ya uasi hawatakabiliwa na mashtaka.

    Kesi hiyo imefungwa.

    Hilo ni jambo la kushangaza, katika nchi ambayo wanaharakati wa upinzani wanatumikia vifungo virefu kwa sababu tu ya kuzungumza dhidi ya vita nchini Ukraine.

    Yevgeny Prigozhin na watu wenye silaha ambao walichukua mji wa Urusi, waliandamana hadi kuelekea Moscow na kuangusha helikopta za kijeshi na ndege iliyokuwa njiani wataruhusiwa kuwa huru.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Habari za hivi punde, Umoja wa Mataifa: Tangu kuanza kwa vita, Urusi imetekeleza mauaji ya kiholela ya zaidi ya 70 ya raia katika maeneo yanayokaliwa

    Tangu kuanza kwa vita, Urusi, imetekeleza mauaji ya kiholela ya zaidi ya raia 70, moingoni mwa wale waliokuwa kizuizini katika maeneo yanayokaliwa katika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu ya Uktaine, kulingana na ripoti iliyochapishwa Jumanne.

    Umoja wa Mataifa uliita "Kuwekwa kizuizini kwa raia katika muktadha wa shambulio la silaha la Shirikisho la Urusi nchini Ukraine".

    Utafiti huu unahusu kipindi cha kuanzia tarehe 24 Februari, 2022 hadi Mei 23, 2023.

    Kwa jumla, katika kipindi hiki, ujumbe wa ufuatiliaji wa Umoja wa Mataifa uliweza kuthibitisha kuzuiliwa kiholela kwa zaidi ya watu 800.

    "Tumeandika kunyongwa kwa jumla ya raia 77 ambao walizuiliwa kiholela na Shirikisho la Urusi," Matilda Bogner, mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu nchini Ukraine, alisema katika mkutano na Geneva.

    Kulingana na waandishi wa ripoti hiyo, watu hao ni wanaume 72 na wanawake watano.

    Ripoti hiyo inasema takriban mfungwa mwingine mmoja alikufa "kwa sababu ya mateso, hali ya kinyama ya kuwekwa kizuizini na/au kunyimwa huduma muhimu ya matibabu."

    Ripoti hiyo pia inasema kwamba Ukraine pia ilikiuka sheria za kimataifa kwa kuwaweka kizuizini raia kiholela, lakini kwa kiwango kidogo zaidi.

  12. Wanajeshi wa RSF Sudan watangaza kusitisha mapigano upande wao kwa ajili ya Eid

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Jenerali Dagalo ametangaza kusitisha mapigano siku ya

    Usitishaji vita wa upande mmoja uliotangazwa na mkuu wa Kikosi cha jeshi cha Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan utaanza kutekelezwa leo kwa sababu ya sikukuu ya Waislamu ya Eid-al-Adha, itakayoanza Jumatano.

    Kusitishwa kwa mzozo na jeshi la Sudan la RSF kulitangazwa katika rekodi ya sauti iliyotangazwa kwenye televisheni ya Al Arabiya na kiongozi wa RSF, Muhammad Hamdan Dagalo, anayejulikana zaidi kama Hemedti.

    Alisema hatua hiyo itatekelezwa Jumanne na Jumatano.

    Jenerali Hemedti pia alilaani dhuluma zinazofanywa dhidi ya raia - ikiwa ni pamoja na zile zinazotekelezwa na vikosi vyake mwenyewe.

    RSF imeshutumiwa kwa kuhusika na ukiukaji wa sheria huko Darfur.

    Pia unaweza kutazama video hii:

  13. Raila Odinga kuongoza maandamano dhidi ya serikali ya Rais Ruto

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Kiongozi wa upinzani Raila Odinga anatarajiwa kuongoza maandamano nchini Jumanne.

    Haya yanajiri baada ya Rais William Ruto kutia saini mswada Fedha 2023 na kuufanya kuwa sheria.

    Kuporomoka kwa mazungumzo ya wanachama 14 ya pande mbili kati ya masuala mengine ndio yanayorejeshamuungano wa Azimio kwenye maandamano ili kushughulikia gharama ya juu ya maisha.

    Maafisa wa polisi wamesema wataruhusu mkutano wa leo wa Azimio kufanyika huko Kamukunji.

    Inspekta Jenerali wa Polisi wa Nairobi Adamson Bungei alisema wametuma maafisa zaidi barabarani kwa usalama.

    Alisema muungano huo umewaarifu kuhusu mkutano uliopangwa kufanyika katika Viwanja vya Kamkunji eneo la Muthurwa.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Mashambulizi ya Ukraine yanasonga mbele pande zote - Zelensky

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Rais Zelensky alitembelea wanajeshi wa Ukraine katika maeneo ya mapigano siku ya Jumatatu

    Rais Volodymyr Zelensky anasema mashambulizi ya Ukraine dhidi ya majeshi ya Urusi yamepiga hatua katika nyanja zote.

    Hakutoa maelezo yoyote, lakini wachambuzi wanaoiunga mkono Urusi wanasema wanajeshi wa Ukraine wamevuka mto Dnipro na kuchukua tena kijiji karibu na Kherson.

    Naibu waziri wa ulinzi wa Ukraine Hanna Maliar pia alisema jana kwamba vikosi vya Ukraine vimepata tena udhibiti wa Rivnopil, kijiji katika mkoa wa Donetsk magharibi mwa kundi la makazi lililorejeshwa tena katika operesheni za kukabili.

    Katika hotuba ya video ya usiku wa manane, iliyotolewa kutoka kwa gari moshi baada ya kutembelea maeneo ya mapigano, Zelensky alielezea Jumatatu kama "siku ya furaha" na akasema wanajeshi wake "wamesonga mbele kila upande" vitani.

    Soma zaidi:

  15. Putin athibitisha marubani wa Urusi waliuawa wakati wa uasi wa Wagner

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais Putin amethibitisha kuwa marubani wa jeshi la Urusi waliuawa katika mapigano na wanajeshi wa mamluki wa Wagner wakati wa maasi ya muda mfupi mwishoni mwa juma.

    Katika hotuba yake usiku wa kuamkia Jumatatu, Putin aliwashukuru wale wote "waliosimama kidete kukabiliana na waasi", na kubakia waaminifu kwa "wajibu wao, kiapo na watu wao", Reuters inaripoti.

    Rais wa Urusi aliendelea kuwashukuru mashujaa walioaga dunia ambao walionyesha "ujasiri na kujitolea" na "kuokoa Urusi kutokana na athari mbaya".

    Katika ujumbe wa awali wa sauti uliotumwa kwenye Telegram, kiongozi wa Wagner Yevgeny Prigozhin alidai kwamba "hakuna mwanajeshi hata mmoja aliyeuawa wakati wa "maandamano ya haki" ya Wagner, ingawa alionyesha masikitiko kwamba wanajeshi wake walifyatua ndege ambazo alisema zilikuwa zikiwashambulia.

    Soma zaidi:

  16. Mamluki wa Wagner: Wafuasi wakasirishwa na uasi wa Prigozhin

    .

    Chanzo cha picha, CONCORD PRESS SERVICE

    Yevgeny Prigozhin anaweza kuwa alijivunia kwamba alikuwa mwaminifu wa wanachama wote 25,000 wa jeshi lake la mamluki, lakini inaonekana kwamba huenda ilibadilika haraka jinsi uasi wa Kundi la Wagner ulipotimia.

    Katika jumbe za mtandaoni zilizochambuliwa na BBC Verify, wanajeshi wa Wagner na jamaa zao walikasirika dhidi ya uamuzi wa Prigozhin wa kusitisha maandamano yake kuelekea Moscow na kuondoka katika jiji lililotekwa la Rostov.

    "Bwana mwenye upara alipoteza nafasi ya Wagner kwa mikono yake mwenyewe.

    Akiwa amekasirisha wengi," mmoja aliweka ujumbe huo mtandaoni akidai kuwa mpiganaji wa Wagner kwenye mtandao wa Telegram wenye wafuasi 200,000.

    "Imekuwa uasi mwingine usio na maana," waliongeza.

    Telegram ni jukwaa la mtandao wa kijamii linalotumika sana na wanajeshi wa Wagner na wafuasi wa vita nchini Urusi, kuruhusu mawasiliano mara nyingi bila mtumaji kutambuliwa na maelfu ya wafuasi kwa wakati mmoja.

    Ilikuwa eneo ambapo Prigozhin alichagua kutangaza kile kinachojulikana kama "Maandamano ya Haki" dhidi ya utawala wa Urusi, lakini sasa imekuwa mahali ambapo wengi wamegeuka dhidi yake.

    Mark Krutov, mwandishi wa habari na Idhaa ya Kirusi ya RFE/RL, ana uwezo wa kufikia mazungumzo ya mtandao wa Telegram unaotumiwa na jamaa za wapiganaji wa Wagner.

    Alishirikisha baadhi ya jumbe zao na BBC.

    "Walisalitiwa tu," mwanamke mmoja aliandika. "Nilimwamini Prigozhin, lakini alichofanya hakikuheshimiwa."

    "Hakupaswa kufanya hivi. Huu ni usaliti mtupu," mtumiaji mwingine alikubaliana naye.

    Kwa muda mrefu Prigozhin alifurahia uungwaji mkono kutoka kwa mtandao wa washawishi wa Wagner.

    Kwa miezi kadhaa, wametetea hatua na vitendo vyake na kuwashambulia wapinzani wake katika Wizara ya Ulinzi - haswa adui yake aliyeapishwa, Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu.

    Lakini wakati maasi ya Wagner yalipokuwa yakiendelea, matendo yao yalinyamazishwa kwa namna ya kushangaza.

    Makundi mawili makubwa zaidi, Gray Zone na Reverse Side of the Medal- yenye wafuasi karibu 900,000 kati yao - hawakuharakisha kuidhinisha hatua yake, badala yake walilenga msingi usiopendelea upande wowote kwa kulaumu upinzani wa Bw Shoigu na wafuasi wake kwa umwagaji damu.

    Soma zaidi:

  17. Wakenya washtakiwa kwa jaribio la kusafirisha chungu kiharamu nje ya nchi

    .

    Chanzo cha picha, SPL

    Wakenya watatu washtakiwa kwa jaribio la kusafirisha chungu wenye thamani ya shilingi 300,000 za Kenya bila kibali kutoka shirika la Wanyama Pori nchini humo.

    Watu hao watatu, mwanaume, mkewe na mtu mwingine wanadaiwa kutaka kusafirisha chungu kinyume cha sheria kwa nchi za China na Ufaransa.

    Hata hivyo, watu hao walikanusha mashtaka dhidi yao ya kuhusika na spichi za wanyama walio hai bila idhini.

    Wakati wa kesi hiyo, mwendesha mashtaka alimtaka jaji kuharakisha usikilizaji wake kwa sababu maisha ya chungu hao yako hatarini.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Ukingo wa Magharibi: Marekani 'yakerwa' na mpango wa upanuzi wa makazi ya Israeli

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Picha inaonyesha makazi ya Wayahudi ya Kedar katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israeli mnamo Juni 2023.

    Serikali ya Israel imeanzisha mpango mpya wa ujenzi wa nyumba 5,700 katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa.

    Tangazo hilo linakuja licha ya shinikizo la Marekani kusitisha upanuzi wa makaazi, ambayo inaona kuwa kikwazo kwa amani na Wapalestina.

    Msemaji wa Marekani alisema Washington "imefadhaishwa sana" na mpango huo.

    Walowezi wanne wa Israel waliuawa kwa kupigwa risasi na Wapalestina wiki iliyopita, na kusababisha ghasia za walowezi kwa siku kadhaa.

    Ghasia kati ya Wapalestina na Waisraeli zimepamba moto tangu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuchaguliwa tena mwaka jana.

    Muungano wake wa kidini na wa kitaifa umeapa kuendeleza uwepo wake katika maeneo ya Wapalestina.

    Kulingana na kundi la Israel linalopinga makazi la Peace Now, miezi sita iliyopita imeshuhudia ujenzi zaidi ya nyumba 13,000 za walowezi katika Ukingo wa Magharibi – ikiwa ni mara tatu zaidi ya mwaka mzima uliopita.

    "Serikali ya Israeli inatusukuma kwa kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa kuelekea kunyakuliwa kamili kwa Ukingo wa Magharibi," shirika hilo lilisema katika taarifa.

    Nchi nyingi zinachukulia makazi hayo, ambayo yamejengwa katika ardhi iliyotekwa na Israel mwaka 1967 katika Vita vya Mashariki ya Kati, kuwa haramu chini ya sheria za kimataifa, ingawa Israel haikubaliani nayo.

    Msemaji wa usalama wa taifa wa Marekani alikashifu upanuzi wa makaazi hayo, akisema "inadhoofisha uwezekano wa kijiografia wa suluhisho la serikali mbili, inazidisha mivutano, na inadhuru zaidi uaminifu kati ya pande hizo mbili".

    Pia unaweza kusoma:

  19. Urusi bado inamchunguza mkuu wa Wagner Prigozhin kwa uhaini

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mkuu wa wapiganaji wa Wagner Prighozin

    Kiongozi wa mamluki wa Wagner Yevgeny Prigozhin bado yuko chini ya uchunguzi wa Urusi kwa uasi wake, licha ya Kremlin kusema mashtaka ya uhalifu yamefutwa, ripoti ya vyombo vya habari vya serikali.

    Prigozhin alisema siku ya Jumatatu lengo la kundi lake lilikuwa "kuepuka kuvunjika kwa Wagner", katika ujumbe wake wa kwanza tangu uasi wa Jumamosi.

    Wagner iliuteka mji wa Rostov-on-Don kusini, kisha wakasonga mbele kuelekea Moscow.

    Lakini masaa kadhaa baadaye walirudi nyuma na mashtaka yaliondolewa, Kremlin ilisema.

    Wengi waliona mpango huo wa kutomshtaki Proghozin kuwa udhaifu kutoka kwa Rais Vladimir Putin, ambaye hapo awali alishutumu "uhaini" wa Wagner katika hotuba ya televisheni.

    Badala yake, Prigozhin alipewa uhamisho katika nchi jirani ya Belarus, Kremlin ilisema, kufuatia upatanishi wa kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko.

    Kremlin ilijaribu kutoa taswira ya biashara kama kawaida Jumatatu.

    Waziri wa Ulinzi Sergei Shoigu alionyeshwa kwenye video, akidaiwa kuwa katika kituo kimoja cha mstari wa mbele cha vita dhidi ya Ukraine.

    Haijabainika ni lini hasa kanda hiyo ilirekodiwa.

    Wagner imekuwa ikitaka Bw Shoigu afutwe kazi kwa madai ya makosa yake katika uwanja wa vita nchini Ukraine.

    Pia unaweza kusoma:

  20. Natumai Hujambo