Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Urusi yafanya shambulio la tisa la makombora ya masafa marefu ndani ya Ukraine mwezi huu
Mji mkuu wa Ukraine unakabiliwa na mashambulio ya anga ya urusi, amesema meya ya kyiv, likiwa ni shambulio la tisa mwezi huu.
Moja kwa moja
Watu wanne wamekamatwa kufuatia shambulio la sinagogi huko Tunisia
Watu wanne wamekamatwa nchini Tunisia kuhusiana na shambulizi nje ya sinagogi wakati wa ibada ya kila mwaka ya Kiyahudi.
Shambulizi hilo lilifanyika wiki moja iliyopita kwenye kisiwa cha kihistoria cha Djerba.Watu watano walikufa kwa jumla.
Mshambuliaji huyo alikuwa afisa wa polisi, ambaye aliwaua maafisa wengine watatu na waumini wawili wa Kiyahudi.
BMshambuliaji huyopia aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi. Mamlaka ya Tunisia haijaliita kuwa shambulizi la kigaidi.
Lakini siku ya Jumatano, Rais Kais Saied alikutana na viongozi wa dini ya Kiislamu, Kiyahudi na Kikristo, akisisitiza kuwa Tunisia ni nchi yenye "ustahimilivu".
"Harry na Meghan walitia chumvi tukio la kufukuzwa na wapiga picha" -Dereva wa teksi aliyewabeba
Dereva wa teksi Sukhcharn Singh, ambaye aliwabeba Mwanmfalme Harry na Meghan Markle huko New York Jumanne iliyopita, anasema kwamba hadithi yao ya wapiga picha (paparazzi) kuwafukuza na kutishia maisha yao ''imetiwa chumvi''.
Msemaji rasmi wa Harry na Meghan alisema hapo jana kwamba wanandoa hao walikaribia kuanguka na gari walipokuwa wakifukuzwa na paparazzi kwa saa mbili.
Tukio hilo, alisema, lilitokea New York, baada ya wanandoa hao kuhudhuria hafla ya jioni ya shirika la hisani ambapo Megan alipokea tuzo kwa kazi yake kutoka kwa Ms Foundation Women of Vision.
Dereva wa teksi anasema huenda alishuhudia sehemu tu ya tukio hilo, lakini wakati wanandoa hao walipokuwa kwenye teksi yake (kama dakika 10), hakukuwa na mikimbio au kisa cja kuendesha gari kwa kasi ya hatari kama ilivyoripotiwa.
Kulingana na Singh, Harry na Meghan walikuwa na wasiwasi sana, lakini hakukuwa na tishio dhidi yao.
"Sidhani [hadithi yao] ni ya kweli, wanatia chumvi sana. Hakukuwa na kitu kama hicho," dereva wa teksi aliwaambia waandishi wa habari.
Alithibitisha kuwa paparazzi waliendesha gari nyuma ya teksi yake, lakini hawakufanya kwa fujo, walidumisha umbali na hakukuwa na hatari.
Sonny Singh aliwachukua karibu na kituo cha polisi cha Manhattan, ambapo mwakilishi wa wanandoa hao alisema walikuwa wakijaribu kujificha wapiga picha ambao walianza kuwaandama mara tu walipoingia kwenye gari baada ya kuondoka kwa hafla hiyo.
Mafuriko yakumba mji katikati mwa Somalia
Takriban watu 250,000 katikati mwa Somalia wamelazimika kuyahama makazi yao baada ya maji mafuriko kusomba mji wa Beledweyne.
Watu walilazimika kujificha chini ya miti baada ya mto Shebelle kuvunja kingo zake,
Asilimia 99 ya watu wanaoishi katika mji huo na maeneo ya karibu hawana makazi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jimbo la Hirshabelle Abdirahmaan Dahir Gure aliambia BBC Somali.
Umoja wa Mataifa unaonya kuwa mafuriko yanaweza pia kuukumba mji wa Bulo Burde, umbali wa kilomita 110 (maili 68).
Mabadiliko ya hali ya hewa yanaaminika kuwa chanzo kikuu cha mafuriko hayo.
Kulingana na maafisa wa serikali ya Somalia, mvua kubwa iliyonyesha nchini Somalia na sehemu ya juu ya miinuko ya Ethiopia ilisababisha mafuriko ambayo yalisomba nyumba, mazao na mifugo.
Somalia ndiyo inaanza kupata nafuu kutokana na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo kadhaa baada ya kukosa mvuo kwa misimu mitano mfululizo, na kutishiakutokea kwa janga la kibinadamu.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, mvua hiyo inahuisha vyanzo vya maji na kusaidia mimea kukua lakini mvua nyingi zaidi inahitajika ili kupunguza athari za ukame wa hivi majuzi. Mvua nyingi pia huongeza hatari ya mafuriko.
Mshambuliaji wa lori la New York ahukumiwa vifungo 10 vya maisha pamoja na miaka 260 jela
Mfuasi wa Islamic State aliyehusika na shambulizi baya zaidi la kigaidi mjini New York tangu tarehe 9/11 ameambiwa atafia gerezani akitumikia vifungo vingi vya maisha.
Sayfullo Saipov aliwaua watu wanane wakati alipoendesha lori na kuwagonga watembea kwa miguu na waendesha baiskeli kwenye barabara ya Manhattan mnamo 2017.
Alipewa vifungo 10 vya maisha - nane kati ya hivyo vinaendeshwa kwa mfululizo - pamoja na miaka 260, na hataachiliwa kamwe.
Alipokuwa akihukumiwa, aliambiwa "ameharibu maisha ya watu wengi" - lakini hakuonyesha majuto wakati wa kesi hiyo.
Saipov alikabiliwa na familia za waathiriwa na walionusurika mahakamani, huku hakimu akibainisha "hali yake ya kutotubu" wakati wa hukumu siku ya Jumatano.
Raia huyo wa Uzbekistan, ambaye sasa ana umri wa miaka 35, alitumia lori la kukodi kushambulia waendesha baiskeli na watembea miguu kwa ghafla katikati mwa jiji la Manhattan Upande wa Magharibi wa jioni ya Halloween 2017.
Alipiga kelele "Mungu ni mkuu" kwa Kiarabu na akapigwa risasi na polisi alipokuwa akitoka kwenye gari.Alitarajia ukatili huo ungemfanya awe mwanachama wa kikundi hicho, kikao cha awali kiliambiwa.
Anatarajiwa kuzuiliwa katika gereza la "supermax" la Colorado, ambapo wafungwa husalia hadi saa 23 kwa siku katika seli zao.
Monica Missio, mama wa mwathiriwa Nicholas Cleves, aliambia mahakama: "Inanichukiza kwamba yeye huamka kila siku wakati mwanangu haamki."
Biblia ya kale ya Kiebrania yauzwa kwenye mnada kwa dola milioni 38
Biblia ya kale ya Kiebrania imenunuliwa huko New York Marekani kwa dola milioni 38.1, na kuwa hati ya thamani zaidi kuuzwa kwa mnada.
Codex Sassoon inasadikiwa kuwa iliandikwa miaka 1,100 iliyopita.
Ni kielelezo cha mapema zaidi cha hati moja iliyo na vitabu vyote 24 vya Biblia ya Kiebrania yenye alama za uakifishaji, vokali na lafudhi.
Mwanasheria wa Marekani na balozi wa zamani Alfred Moses aliinunua kwa ajili ya Jumba la Makumbusho la ANU la Watu wa Kiyahudi huko Tel Aviv, Israel.
"Biblia ya Kiebrania ndiyo yenye ushawishi mkubwa zaidi katika historia na ni msingi wa ustaarabu wa Magharibi," Bw Moses alisema katika taarifa.
Zabuni iliyoshinda ilizidi dola milioni 30.8 iliyolipwa na mwanzilishi mwenza wa Microsoft Bill Gates mnamo 1994 kwa Codex Leicester, daftari la kisayansi la Leonardo da Vinci.
Lakini haikufikia rekodi ya hati ya kihistoria iliyouzwa kwa mnada iliyowekwa na meneja hazini ya wawekezaji Ken Griffin, ambaye alinunua nakala ya kwanza iliyochapishwa ya katiba ya Marekani kwa dola milioni 43.2 miaka miwili iliyopita.
Codex Sassoon imepewa jina la mmiliki wa awali, David Solomon Sassoon, ambaye aliipata mwaka wa 1929 na kuweka mkusanyiko mkubwa zaidi wa kibinafsi wa hati za Kiebrania duniani nyumbani kwake huko London.
Maandishi ya Biblia ya Kiebrania - ambayo vitabu vyake 24 vinajumuisha kile ambacho Wakristo wanakiita Agano la Kale - yaliendelea kubadilika-badilika hadi Enzi za mapema za Kati, wakati wasomi wa Kiyahudi wanaojulikana kama Wamasora walipoanza kuunda maandishi kadhaa ambayo yalisawazishwa.
Pia unaweza kusoma:
- Wayahudi wanaovalia kama Waislamu ili kuepukaa marufuku ya maombi
- Mauaji ya Wayahudi yaliyosahaulika: 'Kwa nini walituua?
Ajali ya ndege ya Colombia: Watoto wanne waripotiwa kunusurika kwa siku 16 msituni
Maafisa nchini Colombia wanasema watoto wanne waliotoweka tangu ndege yao kuanguka msituni wamepatikana wakiwa hai zaidi ya wiki mbili baadaye.
Mama yao na watu wazima wengine walifariki katika ajali hiyo.
Shirika la serikali la ustawi wa watoto, ICBF, limesema limepata taarifa "kutoka eneo hilo " kwamba watoto hao wamepatikana wakiwa na afya njema.
Rubani alisema pia alikuwa ameambiwa watoto hao wamepatikana na watu wa kiasili ndani ya msitu huo mkubwa.
Wanajeshi wanaoshiriki katika msako huo, hata hivyo, bado hawajawaona watoto hao wenyewe.
Ndege hiyo ndogo aina ya Cessna 206 waliyokuwa wakisafiria ilikuwa ikisafiri kutoka Araracuara, ndani kabisa ya msitu wa Amazon kusini mwa Colombia, kuelekea San José del Guaviare, ilipotoweka asubuhi ya tarehe 1 Mei.
Rubani wake alikuwa ameripoti mapema matatizo ya injini.
Baada ya msako mkubwa uliohusisha zaidi ya wanajeshi 100, hatimaye ndege hiyo ilipatikana Jumatatu, wiki mbili baada ya kutoweka.
Miili ya rubani, rubani msaidizi na Magdalena Mucutuy mwenye umri wa miaka 33, mama wa watoto hao wanne, ilipatikana katika eneo la ajali katika jimbo la Caquetá.
Lakini watoto hao ambao wana umri wa miaka 13, tisa na minne, pamoja na mtoto mchanga wa miezi 11, hawakupatikana.
'Nina furaha sana'- Wanawake wa kwanza wa Burundi waelekea Saudia kwa mpango rasmi wa kazi za ndani
Maelezo kuhusu taarifa - Author, Prime Ndikumagenge
- Nafasi, BBC Africa, Bujumbura
Wanawake 11 wa Burundi wameondoka kwenye uwanja wa ndege wa Bujumbura na kuelekea Saudi Arabia kufanya kazi za nyumbani katika mpango wa serikali zote mbili zinazounga mkono mpango wa kuzuia uhamiaji haramu wa wafanyikazi.
Mamia ya wanawake wa Burundi, wengi wao wakiwa wasichana wadogo, wamesafirishwa na makampuni ya biashara kwenda kufanya kazi za nyumbani katika nchi za Kiarabu, na baadhi yao wamesema kuwa walivumilia ukatili wa nyumbani uliokithiri.
"Nina furaha sana…baada ya takriban miaka minne ya kukosa kazi", Aline Niyokwizera, 22, kutoka kusini mwa Burundi aliambia BBC katika uwanja wa ndege wa Bujumbura muda mfupi kabla kuwajaondoka.
Sitini kati yao, wote wakiwa wamevalia mavazi ya wanawake wa Kiislamu, walikuwa kwenye uwanja wa ndege tayari kuondoka lakini kumi na moja pekee ndio waliokwenda, waliosalia watasafiri siku ya Ijumaa baada ya kukosa viti kwenye ndege ya Jumatano jioni.
Jean Bosco Bizuru kiongozi wa wakala wa kuajiri wafanya kazi wa ndani alisema wamewafunza wanawake kazi za nyumbani ambazo watakuwa wakifanya nchini Saudi Arabia.
Burundi inakabiliwa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, ambao ni zaidi ya nusu ya wakazi wa nchi hiyo.
Epimeni Bapfinda, afisa katika wizara ya mashauri ya nchi za kigeni alisema zaidi ya nafasi za kazi 75,000 kwa Warundi zitapatikana nchini Saudi Arabia.
Pia unaweza kusoma:
Mhubiri wa Kenya aliyetaka kukutana na rais akamatwa
Polisi magharibi mwa Kenya wamemkamata mtu anayejiita mhubiri ambaye hivi majuzi alisema alitaka kukutana na Rais William Ruto ili kuwasilisha ujumbe wa kinabii.
Joseph Chenge wa Kanisa la Jerusalem Mowar alikamatwa Jumatano jioni pamoja na waumini 11 wa kanisa lake katika kijiji cha Ruri, kaunti ya Homa Bay.
Afisa wa upelelezi wa jinai wa Homa Bay Abed Kavoo alisema wanamshikilia Bw Chenge kwa tuhuma za kuendeleza mafundisho ya kidini ya kutiliwa shaka.
Bw Kavoo alisema uchunguzi wa awali umefichua kuwa kasisi huyo alikuwa akiwazuilia wagonjwa katika kanisa lake kwa kisingizio cha kuwaombea.
Wagonjwa watano waliokolewa kutoka kwa kanisa la mhubiri huyo, vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti.
Polisi walisema shughuli za kanisa la Chenge ni zinakika sheria, kwa vile halijasajiliwa.
Mhubiri huyo na waumini wa kanisa lake waliokamatwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani siku ya Alhamisi.
Mnamo Jumapili, Bw Chenge aliambia wanahabari kwamba huenda jambo lisilopendeza likaikumba nchi iwapo atakosa kukutana na Rais Ruto ndani ya siku 21.
Kukamatwa kwa mhubiri huyo kunajiri huku kukiwa na msako mkali dhidi ya makanisa yanayoshukiwa kuwa nchini Kenya, kufuatia kifo cha zaidi ya watu 200 wa dhehebu tata la kidini kaunti ya Kilifi pwani ya Kenya.
Kati ya makombora 30 yaliyorushwa na Urusi Ukraine, 29 yalidunguliwa – Jeshi la UKraine
Siku ya Alhamisi usiku, wanajeshi wa Urusi walishambulia eneo la Ukraine kwa makombora 30 ya baharini, angani na ya ardhini, ulinzi wa anga wa Ukraine uliangusha yote isipokuwa moja, huduma ya vyombo vya habari ya Jeshi la Wanahewa la Kikosi cha Wanajeshi cha Ukraine ilisema.
Makombora 22 ya X-101/X-555 yalirushwa kutoka kwa ndege za kimkakati za anga - Tu-160 mbili na Tu-95 nane. Kutoka kwa meli kwenye Bahari Nyeusi - makombora sita ya kusafiri ya Caliber. Pamoja na makombora mawili ya kusafiri ya Iskander-K
Amri ya Jeshi la Anga la Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine
Kulingana na Kikosi cha Wanajeshi wa Ukraine, makombora 29 ya masafa marefu yaliharibiwa, pamoja na droni mbili za uchunguzi.
BBC haina uthibitisho huru wa habari hii.
Mkuu wa jeshi la Sudan anaonekana kwenye video ya kipekee akiwa na bunduki
Jeshi la Sudan limechapisha video inayoonyesha kiongozi wake, Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, akitembea kati ya wanajeshi waliokuwa wakishangilia katika eneo lisilojulikana katika mji mkuu, Khartoum.
Video hiyo ya nadra ya sekunde 23 iliyochapishwa siku ya Jumatano inaonyesha Jenerali Burhan akiwa na bunduki na bastola.Anaonekana akiwa amevalia mavazi ya kijeshi, akiwasalimia wanajeshi wanaomshangilia .
"Mpiganaji - Kamanda Mkuu wa Majeshi - kati ya askari wake uwanjani," kichwa cha habari cha video hiyo kilisema.
Hii ni video ya kwanza ya aina yake tangu mzozo unaoendelea wa kijeshi uanze tarehe 15 Aprili kati ya jeshi na na kikosi maalum cha (RSF).
Hata hivyo, katika siku za mwanzo za mapigano, Jenerali Burhan alionekana pamoja na viongozi wengine wa kijeshi wakiwaamuru askari kutoka ndani ya jengo lisilojulikana mjini Khartoum.
Mkuu wa jeshi na mpinzani wake kamanda wa RSF Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, maarufu kama Hemedti, wamejaribu kuongeza ari ya vikosi vyao vinavyopigana.
Hemedti pia alijitokeza katika eneo lisilojulikana huko Khartoum.Hivi majuzi pia alikanusha katika ujumbe wa sauti kwamba aliuawa.
Mapigano hayo ambayo yanachangiwa na mzozo wa madaraka kati ya Jenerali Burhan na Hemedti yameingia mwezi wa pili ambapo zaidi ya watu 800 wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa.
Sakati ya sukari Kenya : ‘Sidhani kama kufikia sasa hivi Wakenya wanakabiliwa na hatari’- Waziri Kuria
Baada ya serikali kuwasimamisha kazi maafisa 27 kutoka taasisi kumi na mbili waliosaidia kuachiliwa kwa sukari iliyokwisha muda wake ambayo ilikuwa imepangwa kuharibiwa mwaka wa 2018 , serikali inasema Wakenya hawakabiliwi na hatari kwa sasa.
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei Jumatano alitangaza kwamba kusimamishwa kazi kumechochewa na wizara mbili, Hazina ya Kitaifa inayoongozwa na Njuguna Ndung'u na Uwekezaji na Biashara inayoongozwa na Moses Kuria ikisubiri kukamilika kwa uchunguzi wa kisa hicho.
Shirika la Viwango vya bidhaa nchini Kenya (Kebs) lilikuwa limeona kuwa mifuko 20,000 ya sukari haifai kwa matumizi ya binadamu na ikaagiza ibadilishwe kuwa ethanoli ya viwandani.
Lakini shehena hiyo badala yake iliingizwa sokoni kinyume na sheria. Akizungumza na mwandishi wa BBC Carol Robi, Waziri wa biashara na uwekezaji Moses Kuria anatolea ufafanuzi zaidi Sakata hilo pamoja na kuelezea taarifa kuwa pia kuna maziwa ya unga yaliyopitisha muda wa matumizi sokoni.
Msichana afariki Zimbabwe akiwakimbia wachezaji wa ngoma asili
Msichana mwenye umri wa miaka tisa alianguka na kufa nchini Zimbabwe wakati alipokuwa akiwakimbia wachezaji wa ngoma ya asili waliokuwa wakiicheza ngoma hiyo katika kitongoji cha Mabvuku, kilichopo katika mji mkuu, Harare.
Taarifa ya polisi iliyotolewa Jumatano imesema kuwa msichana huyo alifariki baada ya kuanguka chini alipokuwa akiwatoroka wachezaji wa ngoma ya Nyau katika shule iliyopo Mabvuku siku ya Jumatatu.
Uchunguzi unaendelea kuhusu tukio hilo, ilisema polisi bila kutoa taarifa zaidi.
Wachezaji wa ngoma ya Nyau, ambao pia hujulikana kama zvigure/izitandari katika kabila la Shona, mara nyingi huwatisha watoto kwa uchezaji na mavazi yao ya kutisha.
Licha ya uchezaji wake wa kuvutia, wanangoma huhusishwa na imani nyingi miongoni mwa watu wazima, lakini watoto wadogo, huwaona kama majitu ya kutisha, vinasema vyombo vya habari nchini humo.
Wachezaji wa ngoma ya Nyau wanatoka katika jamii ya Chewa inayopatikana kaskazini - magharibi mwa Zimbabwe. Jamii ya kabila hilo pia wanapatikana katika mataifa ya Malawi na Zambia.
Wachezaji wa ngoma hiyo husaidia kurithisha utamaduni na historia kwa watu wa jamii ya Chewa.
Utafiti mpya wakosoa nadharia iliyopo kuhusu asili ya binadamu katika Afrika
Wanasayansi nchini Canada na Marekani wamechapisha utafiti ambao unakosoa nadharia ya sasa kuhusu asili ya mwanadamu wa sasa kwamba ni katika Afrika.
Wakiangalia katika data za urithi, watafiti kutoka Chuo kikuu cha McGill na Chuo kikuu cha California - Davis wanasema kulikuwa na watu wengi waliokuwa wanaishi katika sehemu nyingi za Afrika, wakihamia kutoka kanda moja kuelekea nyingine na kuchanganyikana kwa zaidi ya miaka maelfu kadhaa.
Matokeo haya ya utafiti yanakinzana na nadharia kwamba binadamu wa sasa- Homo Sapiens ni kizazi cha mababu waliokuwa wakiishi Mashariki na Kusini mwa Afrika.
“Katika vipindi tofauti, watu walikubaliana na nadharia kwamba asili ya Homo Sapien inaonyesha kuwa binadamu kwanza walitokea mashariki au Kusini mwa Afrika,” alisema Brenna Henn, mtaalamu wa urithi katika chuo kikuu cha California, Davis ambaye pia ni mwandishi mkuu mwenza wa utafiti.
“Lakini imekuwa vigumu kukubaliana kuhusu nadharia hizi kutokana na uchache wa mabaki ya watu wa kale na rekodi za kiakiolojia za binadamu ambazo zinaonesha kuwa Homo Sapien walipatikana wakiishi kote barani Afrika kwa walau miaka 300,000 iliyopita,” alisema.
Yanga yavunja ‘uteja’ wa miaka 30 kwa soka la Tanzania
Baada ya miongo mitatu, klabu ya Yanga imekuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kutinga fainali ya mashindano makubwa ya vilabu barani Afrika.
Sasa, klabu hiyo itaminyana na klabu ya USM Algiers katika fainali za Kombe la Shirikisho la CAF. Kombe hilo ni la pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya Klabu Bingwa.
Mechi ya fainali itapigwa katika mikondo miwili, mechi ya kwanza ikichezwa jijini Dar es Salaam na ya pili nchini Algeria.
Hii ni mara ya kwanza pia kwa USM Alger kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho. Timu hiyo imewahi kucheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2005 ambapo ilifungwa na miamba ya DRC TP Mazembe.
Hivyo fainali hizi ni muhimu kwa klabu zote mbili ambazo zinataka kuweka rekodi ya kunyakua ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza. Kwa klabu zote mbili haya ndiyo yatakuwa mafanikio makubwa zaidi.
Kwa Yanga fainali hii ni mchezo muhimu zaidi katika historia yao, kwani ushindi wao utakuwa ni rekodi mpya kwa Tanzania. Hakuna klabu ya Tanzania ambayo imewahi kushinda taji la vilabu vya Afrika.
Rekodi ya juu zaidi ilikuwa inashikiliwa na wapinzani wao Simba ambayo ilikuwa ni kucheza fainali ya mashindano kama haya miongo mitatu iliyopita.
Sasa Hii ni fursa kwa Yanga kujikita katika kilele cha ubora wa kuwa ndiyo klabu yenye mafanikio zaidi nchini Tanzania.
Safari ya Yanga kutinga fainali
Yanga imefika fainali baada ya kuichapa klabu ya Gallants FC kutoka Afrika Kusini jumla ya mabao 4-1. Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0 jijini Dar es Salaam katika mechi ya nusu fainali ya kwanza na kisha hapo jana kushinda mkondo wa pili kwa mabao 2-1 nchini Afrika Kusini.
Katika hatua ya robo fainali, Yanga ilifuzu kwa ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Rivers United ya Nigeria. Mechi ya kwanza Yanga ilishinda ugenini goli hizo mbili na kisha kutoka sare ya kutofungana jijini Dar Es Salaam.
Nyota ya Yanga ilianza kung’ara toka katika hatua ya makundi ambapo walimaliza katika nafasi ya kwanza kwa kushinda michezo minne kati ya sita, huku wakitaka sare mchezo mmoja na kupoteza mchezo mmoja tu.
Beyoncé: Mashabiki wamiminika kwa ajili ya tamasha la nyota uwanjani Cardiff
Mashabiki wapatao 60,000 Beyoncé walimiminika Cardiff kushuhudia onyesho la uzunduzi wa tamasha la dunia muziki wake analotarajia kulifanya katika maeneo mbali mbali duniani.
Watu walisafiri kutoka maeneo mbali mbali duniani kumuona muimbaji huyo akiwa jukwani katika Uwanja wa Principality.
Walitoka maeneo ya mbali kama vile Marekani, Lebanon na Australia na walikuwa wameanza kupanga misururu saa 12 kabla ya onyesho kuanza Jumatano.
Mmoja wa mashabiki alisema anamkubali sana Beyonce na hata angefurahi "iwapo angenipaka jasho lake".
George Crocker, 15, ambaye alikuja kutoka Avoca Beach, New South Wales, Australia, alisema: "Ninashukuru sana kwamba fursa hii imekuja, kwamba hatimaye ninaweza kumuona.
"Ni muungu wa kike, ni mama yangu. Ni malkia kabisa…ni kila kitu katika mtu. Kila kitu kumuhusu ni kamili."
George Crocker, 15, alisafiri kutoka Avoca Beach nchini Australia na mama yake kushuhudia tamasha
Shabiki wa Beyonce tangu akiwa na umri wa miaka minne, alisafiri na mama yake Penny, na kuongeza : "Nitakuwa nimekodoa macho yang utu wakati wote , ninafahamu hilo kusema kweli."
Giovani Tana, 20, aliwasili katika mji mkuu wa Wales Jumamosi, baada ya kusafiri kwa ndege hadi London kutoka Beirut, Lebanon, na kupanda treni.
"Ni mara yangu ya kwanza kufika Uingereza, kwahiyo ni sababu kuu ya kuja," alisema.
"Nadhani London inafahamika zaidi na nilifikiria kuufahamu mji tofauti’’
"Kazi yake ni nzuri sana. Hakuna anayeweza kufanya ‘’shoo’’ kama anavyoifanya’’
"Ninaiheshimu kazi yake na kile anachokifanya kwa jamii ya wapenzi wa jinsia moja ni ya kufurahisha’’
"Kwake kuwa jukwaani kunawakilisha matamanio ya watu tofauti."
Madada Emma na Stephanie Dalton walisafiri kutoka Dublin kwa ajili ya tamasha na walikuwa katika msururuwa kuingia uwanjani mapema Jumatano
Emma, 28, alisema: "Tuna furaha kubwa, kwahiyo kuja mapema ni bora zaidi’’.
Tamasha la Renaissance World Tour ni la kwanza kufanywa na Beyoncé mwenye umri wa miaka 41-year-katika kipindi cha miaka saba.
Maafisa 27 wa serikali Kenya wasimamishwa kazi baada ya Sukari Iliotarajiwa kuharibiwa kutoweka
Serikali imewasimamisha kazi maafisa 27 kutoka taasisi kumi na mbili waliosaidia kuachiliwa kwa sukari iliyokwisha muda wake ambayo ilikuwa imepangwa kuharibiwa mwaka wa 2018, hatua ambayo ilihatarisha wananchi ambao huenda walinunua bidhaa hiyo.
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei Jumatano alitangaza kwamba kusimamishwa kazi kumechochewa na wizara mbili - Hazina ya Kitaifa inayoongozwa na Njuguna Ndung'u na Uwekezaji na Biashara inayoongozwa na Moses Kuria - ikisubiri kukamilika kwa uchunguzi wa kisa hicho.
Shirika la Viwango vya bidhaa nchini Kenya (Kebs) lilikuwa limeona kuwa mifuko 20,000 ya sukari haifai kwa matumizi ya binadamu na ikaagiza ibadilishwe kuwa ethanoli ya viwandani.
Lakini shehena hiyo badala yake iliingizwa sokoni kinyume na sheria .
"Ubadilishaji wa ethanoli ya viwandani ulipaswa kutekelezwa chini ya usimamizi wa pamoja wa mashirika ya Kebs na Nema chini ya mfumo wa mashirika mengi. Tangu wakati huo imethibitishwa kuwa shehena hiyo ilielekezwa kinyume na utaratibu na kutolewa bila utaratibu. Zaidi ya hayo, masharti yanayohusiana na uandikishaji wa wazi na wa ushindani wa bidhaa hiyo yalikiukwa na ushuru uliohitajika haukulipwa,” Bw Koskei alisema kwenye taarifa.
Taasisi ambazo maafisa wao wamesimamishwa kazi ni Kebs, Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA), Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Afisi ya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI), Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA), Huduma za Afya Bandarini.
Manchester City yaicharaza Real Madrid 4 - 0 Klabu bingwa
Manchester City walifanya vyema kwa kiwango cha hali ya juu na kuwazidi nguvu mabingwa Real Madrid na kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Inter Milan mjini Istanbul.
City wamepoteza nusu-fainali mbili zilizopita mbele ya Real lakini hawakufanya makosa katika Uwanja wa Etihad wenye furaha na sasa wamesimama hatua moja kutwaa taji hilo ambalo mara zote limekuwa likikaa bila kufikiwa na timu ya Pep Guardiola.
Na mchezo wao katika kipindi cha kwanza cha ajabu, haswa, utaishi kwa muda mrefu kwenye kumbukumbu kwani wababe wa dimba hili waliachwa wakiwa wamechanganyikiwa na kipaji cha City.
Iliendelea na msafara unaoonekana kutozuilika kuelekea mbio tatu za Ligi ya Mabingwa, Ligi ya Premia - ambayo inaweza kushinda kwa ushindi nyumbani kwa Chelsea siku ya Jumapili - na Kombe la FA, ambapo watacheza na Manchester United kwenye fainali huko Wembley.
Kipa wa Real Thibaut Courtois alifanya ushujaa kuokoa mashambulizi miwili ya vichwa ya Erling Haaland mapema kipindi cha kwanza lakini hakuwa na uwezo wa kuzuia shambulio la Bernardo Silva baada ya dakika 23, kiungo huyo wa Ureno akifunga bao la kichwa kwa dakika nane kabla ya kipindi cha kwanza kwenda mapumziko.
City walikumbana na vitisho vya mara kwa mara kutoka kwa Real baada ya kipindi cha mapumziko, Ederson akiokoa vyema kutoka kwa David Alaba na Karim Benzema, lakini hawakuweza kucheza na wakati mpira wa kichwa wa Manuel Akanji ulipopanguliwa na Eder Militao dakika 14 kabla ya sherehe kuanza.
Mchezaji wa akiba Julian Alvarez kisha akamalizia ushindi huo mnono kwa bao la dakika za mwisho baada ya kunyakua pasi nzuri ya Phil Foden.
City watacheza na Inter tarehe 10 Juni huku wakitarajia kushinda Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza.
FBI yamshitaki mwanaume kwa kuiba viatu vilivyovaliwa katika filamu ya Dorothy -The Wizard of Oz
Waendesha mashitaka nchini Marekani wamemshitaki mwanaume kwa kuiba viatu maarufu za rangi nyekundu vilizovaliwa na muigizaji wa filamu ya The Wizard of Oz, Judy Garland akiyecheza kama Dorothy mwaka 1939 .
FBI ilivipata Viatu hivyo vya thamani katika operesheni yake mwaka 2018 – baada ya kuchukuliwa kutoka katika makumbusho mwezi Agosti 2005 – lakini hakuna mtu aliyekamatwa wakati huo .
Jumanne, waendesha mashitaka wa shirikisho, walimshitaki mwanaume wa Minnesota Terry martin, mwenye umri wa miaka 76, kosa la wizi wa kazi kubwa ya sanaa.
Viatu hivyo vilivyopatikana ni moja ya pea nne zilizobakia.
Vilichukuliwa kutoka katika jumba la makumbusho la Judy Garland Museum lililopo Grand Rapids, Minnesota, na mwizi ambaye alivunja kioo na kupitia dirishani na kuingia ndani kupitia mlango wa nyuma ya jengo.
Hakuna alama za vidole zilizoachwa na hakuna king’ora kilicholia kuashiria wizi, kulingana na shirika la habari la CBC News, ambalo ni washirika wa BBC nchini Marekani.
Habari za hivi punde, Vita vya Ukraine: Urusi yafanya shambulio la makombora ya masafa ya tisa ndani ya Ukraine mwezi huu
Mji mkuu wa Ukraine unakabiliwa na mashambulio ya anga ya urusi, amesema meya ya kyiv, likiwa ni shambulio la tisa mwezi huu.
Huku ripoti zikitufikia kuhusu milipuko katika mji huo, Vitali Klitschko anasema moto uliowaka katika wilaya moja ya mji huo unasababishwa na kuwanguka kwa vifusi vya jengo.
Milipuko ilisikika pia katikati mwa Ukraine katika majimbo yaVinnitsa, Khmelnitsky na Zhytomyr.
Vyombo vya habari vya Ukraine vinaripoti kwamba makombora ya Ukraine yalifyatuliwa kutoka kwenye ndege katika jimbo la Caspian
Awali usiku wa kuamkia leo, tahadhari ya mashambulio ya ndege ilitangazwa tena nchini Ukraine. Kufikia saa kumi alfajiri kwa saa za eneo, tahadhari hiyo ilitolewa kwa maeneo yote ya nchi.
Maafisa wa mji mkuu wa Ukraine waliwaambia watu mjini humo watafute maficho
"Uvamizi wa anga unamaanisha mashambulizi, raia walishauriwa kuhamia katika maeneo ya kujificha aukuzingatia sheria ya 'kukaa kwenye sehemu zenye kuta za majengo' ili kuepuka kupigwa na mashambulio," taarifa ilisema ya utawala wa jiji la Kyiv.
Iliripoti kuwa mgumo wa ulinzi wa mashambulizi ya anga unafanya kazi katika majimbo mbali mbali ya nchi.
Wavuti wa habari wa Ukraine "Suspilne" unaripoti kuhusu vilipuzi katika majimbo yaVinnitsa ana Khmelnytsky .Wakazi pia wameripoti kuhusu vilipuzi katika jimbo Zhytomyr.
‘’Adui anashambulia kwa makombora ya kusafiri masafa tena! Vikosi vya ulinzi katika jimbo vinakabiliana na mashambulio ya anga kwenye maneo yanayolengwa," utawala wa kijeshi wa jimbo la Vinnitsa ulisema.
Vita vya Ukraine: Mengi zaidi
- MOJA KWA MOJA:Biden amuonya Putin: ''Madikteta watagharamika
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa