Vita vya Ukraine: Urusi yathibitisha kurefusha mkataba wa nafaka

Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imethibitisha kwamba mkataba wa nafaka umeongezwa muda kwa miezi miwili.

Moja kwa moja

  1. Mafanikio ya ulinzi wa anga ya Ukraine ni mshangao usio na furaha kwa Urusi - Uingereza

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Kombora la Kinzahl

    Ujasusi wa Uingereza, katika ripoti yake ya kila siku kuhusu vita vya Urusi- Ukraine, inachambua hali katika anga, na kumalizia kwamba hivi karibuni imekuwa na faida kidogo kwa jeshi la anga la Urusi, pamoja na. katika maeneo ya mpaka wa Urusi yenyewe.

    Maafisa wa ujasusi wa Uingereza wanasema kwamba mnamo Mei 13, 2023, magari manne ya Kikosi cha Wanaanga wa Urusi (VKS) - helikopta mbili na ndege mbili – zilishambuliwa katika la Bryansk la Urusi (kumbuka kwamba vyanzo vya Urusi vilitoa habari inayopingana juu ya hili, na Urusi. Wizara ya Ulinzi haikuripoti tukio kwa ujumla).

    Mnamo Mei 3, Ukraine ilitungua kombora la anga la Kinzhal lililorushwa na Urusi kwa mara ya kwanza. Katika siku zilizofuata, Urusi ilikuwa ikijaribu kwa uwazi kupunguza uwezo wa ulinzi wa anga wa Ukraine ulioongezeka, lakini ilipoteza Kinzhals chache zaidi

    Kuongezeka kwa tishio la anga kwenye mpaka wa Urusi hakuwezi lakini kuwa na wasiwasi wa kipekee kwa Vikosi vya Anga, kwani maeneo haya hutumiwa kwa operesheni za kijeshi dhidi ya Ukraine.

    Udhaifu unaoonekana wa kinzhal unaonekana kuishangaza Urusi: Rais Putin amerudia tena kusema kwamba makombora hayo hayawezi kuzuilika.

  2. Watoto wanane kati ya 10 wa Afrika Kusini wanatatizika kusoma wanapofikisha umri wa miaka 10

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Waziri wa elimu wa Afrika Kusini alisema matokeo ya kukatisha tamaa yanatokana na kufungwa kwa shule wakati wa janga la Covid-19.

    Watoto wanane kati ya 10 wa shule nchini Afrika Kusini wanatatizika kusoma kufikia umri wa miaka kumi, utafiti wa kimataifa umegundua.

    Afrika Kusini iliorodheshwa ya mwisho kati ya nchi 57 zilizofanyiwa tathmini katika Utafiti wa Kimataifa wa Kusoma na Kuandika, ambao ulijaribu uwezo wa kusoma wa wanafunzi 400,000 duniani kote mwaka wa 2021.

    Kiwango cha kutojua kusoma na kuandika miongoni mwa watoto wa Afrika Kusini kilipanda kutoka 78% mwaka 2016 hadi 81%.

    Waziri wa elimu nchini humo alilaumu matokeo hayo kwa kufungwa kwa shule wakati wa janga la Covid-19.

    Akielezea matokeo hayo kuwa "ya chini na ya kukatisha tamaa", Angie Motshekga pia alisema mfumo wa elimu nchini unakabiliwa na changamoto kubwa za kihistoria, ikiwa ni pamoja na umaskini, ukosefu wa usawa na miundombinu duni.

    Katika shule nyingi za msingi "maelekezo ya kusoma mara nyingi huzingatia tu utendaji wa kuzungumza, huku yakipuuza ufahamu wa kusoma na kuleta maana ya maneno yaliyoandikwa", aliongeza.

    Utafiti ulionyesha kuwa 81% ya watoto wa Afrika Kusini hawakuweza kusoma kwa ufahamu katika lugha yoyote kati ya 11 rasmi nchini humo.

    Pamoja na Morocco na Misri, Afrika Kusini ilikuwa mojawapo ya nchi tatu za Afrika ambazo zilishiriki katika tathmini za kufuatilia mienendo ya kusoma na kuandika na ufahamu wa kusoma wa watoto wa miaka tisa na 10.

    Kulingana na majaribio yanayofanywa kila baada ya miaka mitano mwishoni mwa mwaka wa shule, utafiti mpya unaweka nchi katika jedwali la ligi ya kimataifa ya elimu.

    Singapore ilijihakikishia nafasi ya kwanza katika viwango hivyo ikiwa na wastani wa alama 587, huku Afrika Kusini ikishika nafasi ya mwisho kwa pointi 288 - chini ya Misri iliokuwa na alama 378. Alama hizo zimewekwa dhidi ya wastani wa alama 500 za kimataifa.

    Utafiti pia ulionyesha kuwa kwa ujumla, wasichana walikuwa mbele ya wavulana katika ufahamu wao wa kusoma katika karibu nchi zote zilizotathminiwa, hatahivyo pengo la kijinsia limepungua katika duru ya hivi karibuni ya majaribio.

    Mapambano ya Afrika Kusini na mfumo wake wa elimu ni ya muda mrefu, na ukosefu mkubwa wa usawa kati ya wanafunzi weusi na weupe ni matokeo ya kutengwa kwa watoto chini ya ubaguzi wa rangi.

    Elimu ni moja ya gharama kubwa zaidi za bajeti ya serikali, ambayo huenda ikakatizwa tamaa na matokeo duni katika masomo kama haya.

    Ukosefu wa nyenzo zinazofaa za kusoma na miundombinu duni shuleni, kama vile vyoo, kumechangia tatizo hilo.

  3. Mackenzie :Miili 10 zaidi yagundulika kuhusiana na dhehebu tata la msitu wa Shakahola Kenya

    h

    Chanzo cha picha, EPA

    Miili 10 zaidi imegundulika katika msitu wa Kenya wa shakahola ambapo waumini wa dhehebu tata walifunga hadi kufa ili ‘’kumuona Yesu’’ haraka .

    Mchungaji wa dhehebu hilo Paul Nthenge Mackenzie anashikiliwa na ngazi za kisheria, kuhusiana na vifo vya watu katika msitu wa Shakahola.

    Zaidi ya miili mia mbili hadi sasa imekwishafukuliwa, huku polisi wakiendelea kuchunguza vifo vya waumini hao.

    Baada ya mapumziko ya siku mbili, shughuli ya kufukua miili katika msitu huo mkubwa uliopo pwani ya Kenya imeendelea.

    Kulingana na maafisa wa uchunguzi wa maiti, miili ya watoto wawili ni miongoni mwa ile iliyofufuliwa, na hivyo kupelekea jumla ya miili iliyopatikana kwa sasa kufikia 211.

    Wafuasi watatu wa dhehebu tata pia waliokolewa wakiwa katika mfungo wa hadi kufa. Walikuwa katika hali mahututi na kupelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu .

    Jumla ya watu 610 wanaoripotiwa kupotea wanasakwa katika vituo vilivyowekwa kwa ajili ya kutafuta watu wanaodhaniwa kuwa walipotea baada ya kujiunga na dhehebu tata katika msitu wa Shakahola.

    g

    Unaweza pia kusoma:

    • Paul Makenzie: Mama yangu alikufa, dada yangu sijui kama yupo hai’’
    • Paul Mackenzie: Ni kipi kinachojulikana kuhusu kiongozi wa dhehebu la kufa njaa nchini Kenya?
    • Paul Makenzie: '' Alisema yeye na familia yake watakua wa mwisho kuaga Dunia na kwenda mbinguni''
  4. Wanawake 65 watumiwa kondomu zilizotumika katika bahasha

    .

    Chanzo cha picha, WIKIPEDIA COMMONS/ANDREW OWENS

    Maelezo ya picha, Waathiriwa wanadhaniwa wote walisoma shule moja ya kibinafsi

    Polisi wa Australia wanachunguza kisa kimoja baada ya wanawake wasiopungua 65 kupokea kondomu zilizotumika kwenye bahasha

    Barua hizo, ambazo pia zilikuwa na jumbe zilizoandikwa kwa mkono, zilitumwa kwa anwani za kusini-mashariki na mashariki mwa Melbourne.

    Polisi wanaamini kuwa waathiriwa ni sehemu ya shambulio lililolengwa.

    Wanawake wote wanaaminika walisoma shule ya kibinafsi ya wasichana ya Chuo cha Kilbreda mnamo 1999.

    Muathiriwa wa kwanza alijitokeza mnamo Machi, na hivi karibuni waliripoti matukio kama hayo , polisi walisema.

    Gazeti la Herald Sun la Melbourne liliripoti kwamba wanawake hao wanashuku kuwa anwani zao zilipatikana kutoka kwa kitabu cha mwaka cha shule.

    Bree Walker aliliambia jarida hilo kuwa "hakulala" usiku alipopokea barua hiyo, ambayo ilikuwa na "ujumbe wa picha (ulioandikwa kwa mkono) ". Baadaye aliwasiliana na marafiki kuona iwapo walikuwa wamepokea bahasha kama hizo.

    Polisi wanaamini kuwa wanawake wengi walipokea barua nyingi, zote zikiwa na kondomu zilizotumika.

    Uchunguzi unaendelea na polisi wamemtaka yeyote mwenye taarifa kujitokeza. Wanatarajiwa kutoa Taarifa zaidi kuhusu kesi hiyo baadaye Jumatano.

    Chuo cha Kilbreda, shule ya wasichana ya Kikatoliki inayojitegemea, ilianzishwa na Brigidine Sisters mnamo 1904 na ina wanafunzi wapatao 900 waliosajiliwa.

  5. Mauzo ya Man Utd : Mfanyabishara wa Qatari Sheikh Jassim afanya maboresho ya ofa kununua klabu

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mfanyabiashara maarufu wa Qatar Sheikh Jassim bin Hamad Al Thani amefanya maboresho ya ofa yake ili aweze kuinunua klabu ya soka ya Manchester United.

    Vyanzo vya habari vimeiambia BBC Sport kwamba dau jipya liliwasilishwa Jumanne asubuhi huku mazungumzo na Raine Group, wanaoshughulikia mauzo yakifanyika.

    Mfanyabiashara huyo wa Qatar ambaye ni mwekezaji katika benki pamoja na Sir Jim Ratcliffe's Ineos Group ndizo pande mbili kuu zinazotazamia kuinunua klabu hiyo ya Old Trafford.

    Makundi hayo yote mawili yaliwasilisha dau la tatu mwishoni mwa mwezi Aprili.

    Inafahamika kuwa dau jipya ambalo ni kwa ajili ya kuinunua 100% ya klabu , litalipa deni lote na kujumuisha pesa nyingine za kando ambazo zitaelekezwa moja kwa moja katika klabu na shughuli za kijamii za eneo.

    Takwimu za mwezi Machi zilionesha kuwa United walikuwa wanadaiwa deni la pauni milioni 969.6, likijumuisha deni la jumla, mikopo ya benki, na ada za kutuma pesa zinazohusiana na malipo.

    Familia ya Glazer ilitangaza mwezi Novemba kuwa wanaangalia uwezekano wa kuiuzaManchester United huku waki "angalia mikakati mbadala".

  6. Vita vya Ukraine: Kyiv inasema imeyadungua makombora ya masafa ya hypersonic ya Urusi

    d

    Chanzo cha picha, Mitandao ya kijamii

    Maelezo ya picha, Video ya vilipuzi imekuwa ikisambazwa kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii

    Ukraine imesema kuwa imeyadungua makombora ya masafa ya hypersonic ya Urusi katika "shambulio lenye ukubwa wa kipekee "yaliyokuwa yamefyatuliwa mjini Kyiv Jumanne.

    Kyiv imesema mifumo ya ulinzi ya Ukraine ilizuia makombora sita ya masafa aina ya Kinzhal hypersonic, ambayo Urusi ilidai yanaweza kuhimili mifumo yote iliyopo ya ulinzi wa anga.

    Yalikuwa ni miongoni mwa makombora 18 ya aina tofauti yaliyokuwa yamefyatuliwa mjini Kyiv katika kipindi kifupi, wamesema maafisa.

    Urusi inakanusha kuwa makombora yake ya Kinzhal yalizuiwa na ilisema moja liliangamiza mfumo wa ulinzi wa anga wa Marekani wa Patriot.

    Ukraine ilikanusha kauli hiyo. BBC hatahivyo haijaweza kuthibitisha madai haya ya nchi mbili kwa vyanzo huru.

    Urusi ilianza mashambulio yake ya anga katika wiki za hivi karibuni – kwa kuupiga makombora mji mkuu wa Ukraine mara nane hadi sasa mwezi huu- kabla ya shambulio linalotarajiwa la Ukraine.

    Jumanne jioni wazairi wa ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu alisema Moscow haijafyatua makombora mengi ya Kinzhal kama ambayo Kyiv imedai kuyadungua.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  7. Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu ya mubashara ya leo Jumatano tarehe 17.05.2023