Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Vita vya Ukraine: Urusi yathibitisha kurefusha mkataba wa nafaka

Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imethibitisha kwamba mkataba wa nafaka umeongezwa muda kwa miezi miwili.

Moja kwa moja

  1. Yanga yavunja ‘uteja’ wa miaka 30 kwa soka la Tanzania

    Baada ya miongo mitatu, klabu ya Yanga imekuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kutinga fainali ya mashindano makubwa ya vilabu barani Afrika.

    Sasa, klabu hiyo itaminyana na klabu ya USM Algiers katika fainali za Kombe la Shirikisho la CAF. Kombe hilo ni la pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya Klabu Bingwa.

    Mechi ya fainali itapigwa katika mikondo miwili, mechi ya kwanza ikichezwa jijini Dar es Salaam na ya pili nchini Algeria.

    Hii ni mara ya kwanza pia kwa USM Alger kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho. Timu hiyo imewahi kucheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2005 ambapo ilifungwa na miamba ya DRC TP Mazembe.

    Hivyo fainali hizi ni muhimu kwa klabu zote mbili ambazo zinataka kuweka rekodi ya kunyakua ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza. Kwa klabu zote mbili haya ndiyo yatakuwa mafanikio makubwa zaidi.

    Kwa Yanga fainali hii ni mchezo muhimu zaidi katika historia yao, kwani ushindi wao utakuwa ni rekodi mpya kwa Tanzania. Hakuna klabu ya Tanzania ambayo imewahi kushinda taji la vilabu vya Afrika.

    Rekodi ya juu zaidi ilikuwa inashikiliwa na wapinzani wao Simba ambayo ilikuwa ni kucheza fainali ya mashindano kama haya miongo mitatu iliyopita.

    Sasa Hii ni fursa kwa Yanga kujikita katika kilele cha ubora wa kuwa ndiyo klabu yenye mafanikio zaidi nchini Tanzania.

    Safari ya Yanga kutinga fainali

    Yanga imefika fainali baada ya kuichapa klabu ya Gallants FC kutoka Afrika Kusini jumla ya mabao 4-1. Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0 jijini Dar es Salaam katika mechi ya nusu fainali ya kwanza na kisha hapo jana kushinda mkondo wa pili kwa mabao 2-1 nchini Afrika Kusini.

    Katika hatua ya robo fainali, Yanga ilifuzu kwa ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Rivers United ya Nigeria. Mechi ya kwanza Yanga ilishinda ugenini goli hizo mbili na kisha kutoka sare ya kutofungana jijini Dar Es Salaam.

    Nyota ya Yanga ilianza kung’ara toka katika hatua ya makundi ambapo walimaliza katika nafasi ya kwanza kwa kushinda michezo minne kati ya sita, huku wakitaka sare mchezo mmoja na kupoteza mchezo mmoja tu.

  2. Manchester City yaicharaza Real Madrid 4 - 0 klabu bingwa

    Manchester City walifanya vyema kwa kiwango cha hali ya juu na kuwazidi nguvu mabingwa Real Madrid na kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Inter Milan mjini Istanbul.

    City wamepoteza nusu-fainali mbili zilizopita mbele ya Real lakini hawakufanya makosa katika Uwanja wa Etihad wenye furaha na sasa wamesimama hatua moja kutwaa taji hilo ambalo mara zote limekuwa likikaa bila kufikiwa na timu ya Pep Guardiola.

    Na mchezo wao katika kipindi cha kwanza cha ajabu, haswa, utaishi kwa muda mrefu kwenye kumbukumbu kwani wababe wa dimba hili waliachwa wakiwa wamechanganyikiwa na kipaji cha City.

    Iliendelea na msafara unaoonekana kutozuilika kuelekea mbio tatu za Ligi ya Mabingwa, Ligi ya Premia - ambayo inaweza kushinda kwa ushindi nyumbani kwa Chelsea siku ya Jumapili - na Kombe la FA, ambapo watacheza na Manchester United kwenye fainali huko Wembley.

    Kipa wa Real Thibaut Courtois alifanya ushujaa kuokoa mashambulizi miwili ya vichwa ya Erling Haaland mapema kipindi cha kwanza lakini hakuwa na uwezo wa kuzuia shambulio la Bernardo Silva baada ya dakika 23, kiungo huyo wa Ureno akifunga bao la kichwa kwa dakika nane kabla ya kipindi cha kwanza kwenda mapumziko.

    City walikumbana na vitisho vya mara kwa mara kutoka kwa Real baada ya kipindi cha mapumziko, Ederson akiokoa vyema kutoka kwa David Alaba na Karim Benzema, lakini hawakuweza kucheza na wakati mpira wa kichwa wa Manuel Akanji ulipopanguliwa na Eder Militao dakika 14 kabla ya sherehe kuanza.

    Mchezaji wa akiba Julian Alvarez kisha akamalizia ushindi huo mnono kwa bao la dakika za mwisho baada ya kunyakua pasi nzuri ya Phil Foden.

    City watacheza na Inter tarehe 10 Juni huku wakitarajia kushinda Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza.

  3. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo haya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  4. Mwanaridha wa Kenya anayeshikilia rekodi ya dunia asimamishwa kwa muda

    Mwanariadha wa Kenya anayeshikilia rekodi ya dunia amesimamishwa kwa muda kwa madai ya ukiukaji wa matumizi ya dawa za kusisimua misuli, Kitengo cha Uadilifu cha Riadha (AIU) kinasema.

    Mnamo 2020 Rhonex Kipruto alivunja rekodi ya dunia ya mbio kilomita 10 huko Valencia

    Pia alishinda medali ya shaba kwenye Mashindano ya Dunia ya 2019 kwa utendaji wake katika mbio za mita 10,000.

    Kesi itaamua hatima yake ya mwisho.

  5. Mzozo wa Ukraine: Urusi yathibitisha kurefusha mkataba wa nafaka

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imethibitisha kwamba mkataba wa nafaka umeongezwa muda kwa miezi miwili.

    Taarifa hii imeripotiwa na mashirika ya habari ya Urusi.

    "Kurefushwa kwa mkataba wa nafaka kunatoa nafasi ya kuhakikisha usalama wa chakula duniani," Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi ilisema katika taarifa iliyotolewa na shirika la habari TASS.

    Awali Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitangaza kuwa "mpango wa nafaka" - makubaliano ya kuzifungua bandari za Bahari Nyeusi za Ukraine na kuuza nje bidhaa za kilimo kutoka kwao - umeongezwa kwa miezi miwili.

    "Shukrani kwa juhudi za nchi yetu, msaada wa marafiki zetu wa Urusi, mchango wa marafiki zetu wa Ukraine, iliamuliwa kuongeza mkataba wa nafaka wa Bahari Nyeusi kwa miezi miwili," AFP ilimnukuu Erdogan akisema.

    Mkataba huo uliisha mnamo Mei 18 baada ya kuongezewa muda hapo awali.

    Hadi wakati wa mwisho uliyowekwa, Urusi haikuwa na mpango wa mkataba mpya, ndiposa masharti ya ziada. Haijabainika Moscow ilikubali kurefusha mpango huo katika mazingira gani.

  6. Harry na Meghan wahusika katika tukio hatari la 'magari kufukuzana kwa kasi' na wapiga picha - Msemaji

    Mwanamfalme Harry, Meghan na mama yake Meghan walihusika katika tukio la "hatari la kufukuzana na wapiga picha maarufu paparazzi, msemaji wa mwanamfalme huyo alisema.

    Tukio hilo lilitokea baada ya Duke na Duchess wa Sussex kuhudhuria sherehe ya tuzo huko New York Jumanne.

    Katika taarifa, msemaji wa mwana mfalme alisema "kufukuzana huko" kulidumu kwa zaidi ya saa mbili.

    Waliongeza kuwa tukio hilo lilisababisha karibu wagongane na madereva wengine barabarani, watembea kwa miguu na maafisa wa polisi.

    "Wakati umaarufu unavutia kiwango kikubwa cha maslahi kutoka kwa umma, haupaswi kuhatarisha maisha ya mtu yeyote," msemaji huyo alisema.

    "Usambazaji wa picha hizi, kwa kuzingatia njia ambazo zilipatikana, unahimiza tabia ya kuingilia faragha ambayo ni hatari kwa wote wanaohusika."

    Idara ya Polisi ya New York (NYPD) haikuthibitisha mara moja ufahamu wa tukio hilo.

    Tukio hilo linadaiwa kutokea baada ya wawili hao kuonekana hadharani kwa mara ya kwanza tangu kutawazwa kwa Mfalme Charlse mapema mwezi huu.

    Harry, Meghan na mama yake Meghan Doria Ragland, walikuwa wamehudhuria hafla ya maadhimisho ya miaka 50 ya Ms Foundation Women of Vision.

  7. Urusi yadai kuharibu ghala la silaha la wanajeshi wa Ukraine huko Nikolaev

    Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Urusi anadai kuwa jeshi la Urusi lilifanya shambulio kubwa la makombora dhidi ya ghala kubwa la rkuhifadhi risasi eneo la Nikolaev nchini Ukraine.

    Hapo awali, mkuu wa utawala wa kijeshi wa kikanda, pamoja na wawakilishi wa idara ya ndani ya Huduma ya Dharura ya Jimbo hilo la Ukraine (GSChS), waliripoti kwamba usiku wa Mei 16, kwamba kituo ch akuuza magari, kituo cha kibiashara, nyumba za kibinafsi, pamoja na majengo na miundombinu ya viwanda yaliharibiwa kutokana na shambulio la roketi dhidi ya Nikolaev.

    Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka kwa Huduma ya Dharura ya Serikali, mtu mmoja alijeruhiwa.

  8. Kenya: Odinga akanusha kufikia mapatano ya kisiasa 'Handshake' na Rais William Ruto

    Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amekana kufanya mazungumzo ya mapatano ya kisiasa na Rais William Ruto katika mikutano yao mitatu mwishoni mwa juma.

    Bw Odinga mnamo Jumanne alitaja mkutano wake na Rais Ruto katika mazishi katikati mwa kaunti ya Nyandarua na baadaye katika mechi mbili za kandanda za mashinani kama "mikutano ya bahati nasibu" ambayo haikuwa na uhusiano wowote na hali ya kisiasa nchini.

    Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya mnamo 2018 aliingia katika makubaliano ya baada ya uchaguzi maarufu "handshake" na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

    Amekuwa akishambuliwa mara kwa mara na utawala wa Kenya Kwanza kwamba maandamano yake dhidi ya serikali yalikuwa ni mpango wa kulazimisha ''handshake'' na Rais Ruto.

    "Hatukuzungumzia lingine lolote zaidi ya soka. Naomba ifahamike kwamba, hatutaki kushirikiana na serikali na hatujaomba," Bw Odinga alisema.

    Mikutano hiyo mitatu kati ya rais na waziri mkuu huyo wa zamani ilikuwa imezua tetesi za kuwepo kwa mapatano ya kisiasa kati ya wapinzani hao wawili.

    Pande zote mbili zilishiriki picha za Rais Ruto na Bw Odinga wakiwa wamekaa karibu, wakifuatilia mechi za soka kwa moyo mkunjufu.

    Haya yanajiri huku Bw Odinga akitishia kuitisha maandamano mapya kuhusu Mswada wa Fedha wa 2023 unaopendekeza Wakenya kutozwa ushuru zaidi.

  9. Zifahamu kashfa nne kubwa katika shirika la usambazaji vifaa vya matibabu na dawa nchini Kenya

  10. Kijana kutoka Tanzania ashinda tuzo ya kifahari ya kifalme mjini London

    Kijana mmoja kutoka Tanzania ameshinda Tuzo ya Uwezeshaji kwa Wanawake ya Amal Clooney huko London kwa juhudi zake za kusaidia elimu ya wasichana.

    Tuzo za kila mwaka za Prince's Trust hutambua vijana ambao wamefaulu dhidi ya hali ngumu , kuboresha nafasi zao maishani na kuwa na matokeo chanya kwa jamii zao

    Mshindi wa tuzo hizo Zamana alitambuliwa baada ya kuzindua kampeni yake ya kusaidia na kuhimiza wasichana kusalia shuleni nchini Tanzania.

    Kupitia kampeni yake ya “Niruhusu Nisome”, Zamana analenga kuwasaidia wasichana wa shule na wazazi wao kuelewa umuhimu wa kukamilisha masomo yao.

    “Tuzo hii ina maana kubwa sana kwangu.Kila msichana katika jamii yangu ana ndoto ya maisha yake ya baadaye, kama vile wasichana ulimwenguni kote.Ndoto yangu ni wasichana wengi kusalia shuleni,” Zamana alisema baada ya kupokea tuzo hiyo Jumanne usiku katika ukumbi wa michezo wa London Royal Drury Lane.

    Kufuatia hafla hiyo, Zamana baadaye Jumatano atakutana na Mfalme Charles III wakati wa mapokezi katika Jumba la Buckingham kusherehekea mafanikio ya washindi.

    Ilianzishwa na Mfalme, Prince's Trust International inasaidia vijana katika nchi 18 kupitia programu za ajira, elimu na biashara.

  11. Titanic: Wanasayansi watoa picha ya mabaki ya meli ambayo haijawahi kuonekana

    Ajali ya maarufu zaidi ya meli duniani imefichuliwa kwa njia ambayo haijawahi kuonekana hapo awali.

    Uchanganuzi wa kwanza wa kidijitali unaonyesha ukubwa wa mabaki ya Titanic, ambao uko mita 3,800 (futi 12,500) chini ya Atlantiki, umeundwa kwa kutumia ramani ya kina kirefu cha bahari.

    Inatoa mwonekano wa kipekee wa 3D wa meli nzima, na kuiwezesha kuonekana kana kwamba maji yametolewa.

    Matumaini ni kwamba hii itatoa mwanga mpya juu ya kile kilichokumba chombo hicho, ambacho kilizama mnamo 1912.

    Pia unaweza kusoma:

    • Titanic: Kwa namna gani redio iliokoa maisha ya watu 700?
    • Titanic: Siri nne zisizojulikana hata baada ya miaka 110 ya kuzama kwa Titanic
  12. KFC yakanusha kuiba wazo la vyakula vya nchini Afrika Kusini

    Kampuni kubwa ya vyakula-KFC imekanusha madai ya mjasiriamali kutoka Afrika Kusini akiishutumu kampuni hiyo kwa kuiba wazo lake la chakula cha kienyeji kinachojulikana kama kota, zinasema ripoti za vyombo vya habari nchini humo.

    Romeo Malepe anashutumu KFC kwa kutumia wazo lake la kota ya kuku ambayo KFC inazindua .

    Kota, inayojulikana pia kama Sphatlo, ni sandwichi kubwa iliyo na viambato vingi vilivyowekwa ndani ya robo ya mkate, imefungwa na inaweza kuliwa ukiwa njiani.

    Bw Malepe aliambia chapisho la eneo hilo kwamba wazo lake la "Streetwise Kota" liliibiwa alipokuwa akitafuta ushirikiano na KFC.

    Bw Malepe pia anasemekana kujitokeza kwenye mitandao ya kijamii hivi majuzi kulaani KFC kwa madai ya kuchukua wazo lake ambalo alisema alilitengeneza miaka minne iliyopita.

    Lakini KFC imekanusha madai hayo katika taarifa kwa vyombo vya habari vya Afrika Kusini, akisema kuwa "sio siri kwamba kota ni mlo maarufu wa Afrika Kusini na toleo dogo la KFC Sphatlho ni matokeo ya mchakato wa ndani wa kutengeneza bidhaa".

    Ilisema kuwa kwa zaidi ya miaka 50, msururu huo umechochewa na turathi na utamaduni wa Afrika Kusini kuendeleza bidhaa za kibunifu za ndani katika orodha yao.

    "Tutaendelea kutumia mitindo ya vyakula ya Afrika Kusini kama msukumo wa kuleta bidhaa muhimu kwa mashabiki wetu kote Afrika Kusini," KFC ilinukuliwa ikisema.

  13. Uchina yalitoza kundi la ucheshi faini ya $2m kwa mzaha kuhusu jeshi

    Kikundi cha vichekesho cha China kimepigwa faini ya Yuan 14.7m ($2.1m; £1.7m) kutokana na mzaha kuhusu jeshi lililoibua kauli mbiu ya Rais Xi Jinping.

    Kesi hiyo, ambayo ilifananisha tabia ya mbwa wa mcheshi na tabia ya kijeshi, iliwakasirisha viongozi.

    Walisema Shanghai Xiaoguo Culture Media Co na mcheshi Li Haoshi "wamelifedhehesha jeshi la watu".

    Kampuni hiyo ilikubali adhabu hiyo na kusitisha mkataba wa Bw Li.

    Matamshi hayo ya kuudhi yalitolewa wakati wa onyesho mjini Beijing siku ya Jumamosi, wakati Bw Li alipodokeza kuhusu mbwa wawili aliotumia ambao walikuwa wakimfukuza chindi

    "Mbwa wengine unaowaona wangekufanya ufikirie kuwa wanapendeza. Mbwa hawa wawili walinikumbusha tu... 'Pigana ili ushinde, ghushi mwenendo mzuri'," alisema Bw Li, ambaye jina lake la kisanii ni House.

    Mstari huo ni sehemu ya kauli mbiu ambayo Rais Xi aliizindua mwaka 2013 kama lengo la jeshi la China.

    Katika rekodi ya sauti ya uigizaji iliyoshirikiwa kwenye jukwaa la China linalofanana na Twitter la Weibo, watazamaji wanaweza kusikika wakicheka mzaha huo.

    Lakini haikukaribishwa sana kwenye mtandao, baada ya mshiriki wa watazamaji kulalamika kuhusu hilo.Mamlaka ya Beijing ilisema ilianzisha uchunguzi siku ya Jumanne.

    Kisha walinyang'anya yuan 1.32m ya kile kilichoonekana kuwa mapato haramu, na kuitoza kampuni hiyo faini ya yuan nyingine ya 13.35m, kulingana na Xinhua.

  14. Habari za hivi punde, Haiwezekani kuangamiza silaha ya Patriot ya Marekani kwa kutumia "Dagger" ya Urusi - Ukraine

    Mwakilishi rasmi wa Kikosi cha Wanahewa wa jeshi wa Ukraine aliita "propaganda" taarifa za Wizara ya Ulinzi ya Urusi, usiku wa Mei 16, kwamba mfumo wa kombora wa kupambana na ndege wa Patriot wa Marekani uliangamizwa na shambulio la roketi huko Kiev.

    Akizungumza kupitia chombo cha habari cha Kitaifa nchini Ukraine , Yuriy Ignat alihimiza "kutojali kuhusu hatima ya Patriot."

    "Kuharibu mfumo na aina ya "Dagger", haiwezekani. Kwa hivyo, kila kitu wanachosema hapo, nadhani, kibaki kwenye kumbukumbu zao za uenezi," mwakilishi wa amri ya Kikosi cha Wanajeshi wa Kikosi cha Wanajeshi wa Ukraine alisema.

  15. Shambulizi la kuvizia Nigeria: Wanne wauawa katika shambulio dhidi ya msafara wa Marekani mjini Anambra

    Watu wenye silaha kusini-mashariki mwa Nigeria wameshambulia msafara wa Marekani na kuua watu wanne, polisi wa eneo hilo wamesema.

    Wanasema wahasiriwa wawili wa shambulio la Jumanne katika jimbo la Anambra walikuwa wafanyikazi wa ubalozi wa Amerika, wakati wengine wawili walikuwa maafisa wa polisi.

    Washambuliaji waliwateka nyara watu wengine watatu, na kuchoma gari lao.

    Washington inasema hakuna raia wa Marekani aliyekuwa katika msafara huo, ambao ulikuwa ukisafiri katika jimbo hilo lililokumbwa na ghasia na uasi wa watu wanaotaka kujitenga.

    Polisi wa Nigeria wanasema shambulio hilo lilitokea katika barabara ya Atani-Osamale katika eneo la Ogbaru.

    Msemaji wa polisi DSP Ikenga Tochukwu anasema vikosi vya usalama kwa sasa vinaendelea na operesheni ya uokoaji .

    Katika taarifa kwa BBC, Marekani ilithibitisha kuwa "kulikuwa na tukio tarehe 16 Mei katika jimbo la Anambra", na kuongeza kuwa Washington ilikuwa ikishirikiana na idara za usalama za Nigeria kuchunguza shambulio hilo.

    "Usalama wa wafanyikazi wetu daima ni muhimu, na tunachukua tahadhari kubwa wakati wa kuandaa safari za kwenda uwanjani," idara ya serikali ya Merika ilisema.

    Mamlaka ya Nigeria mara nyingi hulaumu mashambulizi ya vurugu katika eneo hilo dhidi ya vuguvugu la watu wa asili la Biafra (Ipob).

  16. Misri yahutumiwa kuwatesa wanawake kwa madai ya kuwa na uhusiano na IS

    Mashirika mawili ya haki za binadamu yameshutumu mamlaka ya Misri kwa kuwaweka kizuizini kiholela - na katika baadhi ya matukio kuwatesa - wanawake na wasichana wanaohusiana na washukiwa wa kundi la Islamic State (IS).

    Human Rights Watch na Taasisi ya Sinai ya Haki za Kibinadamu zinasema kuzuiliwa huko mara nyingi kunaonekana kutumika kuweka shinikizo kwa wanafamilia wanaoshukiwa kuwa na uhusiano na wanajihadi wa Misri wanaohusishwa na IS.

    Mawakili na mashahidi waliohojiwa kwa ripoti hiyo wanasema lengo lilikuwa kutoa habari juu ya washukiwa wa kijihadi au kuwafanya wajisalimishe.

    Ripoti hiyo inasema baadhi ya wanawake na wasichana walikuwa waathiriwa wa kundi linalohusishwa na IS.

  17. Canada yakanusha kutoa fursa ya ajira kwa Wakenya

    Serikali ya Canada imekanusha ripoti kuwa Wakenya sasa wanaweza kusafiri hadi nchini humo kutafuta nafasi za kazi.

    Haya yanajiri kufuatia tangazo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Alfred Mutua Jumanne kwamba Wakenya sasa wataweza kwenda kuishi au kufanya kazi nchini Canada.

    Bw Mutua, ambaye alikuwa katika ziara rasmi nchini, alisema alifanya mkutano na Waziri wa Uhamiaji, Wakimbizi na Uraia wa Canada (IRCC) Sean Fraser na kukubaliana kuhusu fursa mbalimbali za uhamiaji.

    Alisema mchakato kwa wanaotaka kwenda Canada ni rahisi lakini unahitaji bidii. "Taarifa potofu zinasambaa ambazo zinapendekeza kuwa programu maalum zinakaribisha wahamiaji wa Kenya.

    Huu ni uongo, na programu za uhamiaji zilizotajwa hazipo," IRCC ilisema katika taarifa.

    IRCC ilisema kwa taarifa sahihi kuhusu jinsi ya kuhamia Canada, Wakenya wanapaswa kutembelea tovuti ya uhamiaji nchini humo.

  18. Kaka yake Mackenzie: 'Sikuwahi kuona jambo lolote baya kwake'

    Kaka yake na Mchungaji wa kanisa lenye utata nchini Kenya Paul Mackenzie anasema kwamba kaka yake alikuwa "mtu mwema" na mfano kwa jamii yake labda kama alibadilika baadaye.

    Paul Mackenzie anadaiwa kuwahimiza wafuasi wake kufa njaa. Zaidi ya miili 200 kufikia sasa imetolewa katika msitu wa Shakaholanchini Kenya huku wengine zaidi ya 600 wanaoripotiwa kuwa washiriki wa ibada ya siku ya mwisho bado hawajulikani walipo.

    Unaweza pia kusoma:

    • Paul Makenzie: Mama yangu alikufa, dada yangu sijui kama yupo hai’’
    • Paul Mackenzie: Ni kipi kinachojulikana kuhusu kiongozi wa dhehebu la kufa njaa nchini Kenya?
    • Paul Makenzie: '' Alisema yeye na familia yake watakua wa mwisho kuaga Dunia na kwenda mbinguni''
  19. Mapigano Sudan: Umoja wa Mataifa umetoa wito wa ufadhili wa dola bilioni tatu kwa ajili ya Sudan

    Umoja wa Mataifa umetoa wito wa ufadhili wa dola bilioni tatu kwa ajili ya Sudan kuweza kutoa misaada ya kiutu katika taifa hilo linalikumbwa na mzozo na mataifa jirani ambayo yanahifadhi wakimbizi kutoka Sudan.

    Maelfu ya watu wameachwa bila ya makazi tangu mzozo kuzuka kati ya Jeshi na kikosi maalum cha wanamgambo cha Rapid Support Forces mwezi uliopita na hivyo kusababisha janga la kibinadamu nchini humo.

    Mzozo huo unaendelea bila ya kusita licha ya makubaliano kadhaa kufikiwa ya kusitisha mapigano na kuruhusu misaada ya kibinadamu kufikia raia walioathirika. Inaaminika takriban watu milioni moja wamelazimika kuyahama makazi yao.

    Hospitali zimeshambuliwa na kuharibiwa,huduma za umeme na maji zimekatwa huku kukiripotiwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwmo kuuawa kiholela na wanawake kubakwa.

    Hata kabla ya mzozo huu,Sudan ilikuwa inakabiliwa na mahitaji makubwa ya kibinadamu kufuatia mizozo ya kipindi cha nyuma na imekuwa ikiwahifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka nchi jirani za Ethiopia na Sudan Kusini.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Sudan:Jitihada za wapatanishi kutuliza milio ya risasi na kumaliza mapigano
    • Mapigano Sudan: Hakuna mazungumzo mpaka mashambulio ya mabomu yakome, Hemedti aiambia BBC
    • Mzozo wa Sudan: Mgogoro wa Sudan unaweza kuisha kwa njia hizi tatu
  20. Polisi wa zamani wa Burundi kuwa mbunge wa kwanza mweusi Ugiriki

    Polisi wa zamani wa Burundi Spiros Richard Hagabimana anataka kuwa mbunge wa kwanza Mgiriki mweusi, katika nchi ambako wahamiaji ni nadra kushikilia nyadhifa za umma.

    Anagombea kiti cha ubunge cha wilaya ya kusini – mashariki ya Piraeus II kwa tiketi ya chama cha kihafidhina cha New Democracy, katika uchaguzi wa tarehe 21 Mei.

    "Piraeus ni mahala ambapo nilisomea, nilijifunza maneno ya kwanza ya Kigiriki, kufanya kazi na kuishi. Kupitia eneo hili, nilijifunza kuipenda Ugiriki," moja ya mabango ya uchaguzi ya Bw Hagabimana liliandikwa kwenye ukurasa wa Twitter.

    Habimana mwenye umri wa miaka 54-ameliambia shirika la habari la Reuters jinsi alivyofungwa alipokuwa afisa wa polisi nchini Burundi mwaka 2015 kwa kukataa kuwafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakiipinga serikali.

    Baadaye aliachiliwa huru kutoka gerezani kwa usaidizi wa maafisa wa Ugiriki na kurejea Athens mwaka 2016.

    Bw Hagabimana aliwasili Ugiriki mwaka 1991 kwa ajili ya masomo katika shule ya mafunzo ya jeshi la majini. Alihitimu mwaka 1996 lakini alilazimika kuomba ukimbizi nchini Ugiriki kwani Burundi wakati huo ilikuwa katika mzozo wa mapinduzi ya kijeshi, kulingana na ripoti za Reuters.

    Alipata uraia wa Ugiriki mwaka 2005 na katika mwaka huo huo alirejea Burundi kwa ajili ya juhudi za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.

    Alisema kuwa rangi ya ngozi yake haipaswi kuagaziwa katika uchaguzi ujao.