Yanga yavunja ‘uteja’ wa miaka 30 kwa soka la Tanzania

Chanzo cha picha, Yanga SC
Baada ya miongo mitatu, klabu ya Yanga imekuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kutinga fainali ya mashindano makubwa ya vilabu barani Afrika.
Sasa, klabu hiyo itaminyana na klabu ya USM Algiers katika fainali za Kombe la Shirikisho la CAF. Kombe hilo ni la pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya Klabu Bingwa.
Mechi ya fainali itapigwa katika mikondo miwili, mechi ya kwanza ikichezwa jijini Dar es Salaam na ya pili nchini Algeria.
Hii ni mara ya kwanza pia kwa USM Alger kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho. Timu hiyo imewahi kucheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2005 ambapo ilifungwa na miamba ya DRC TP Mazembe.
Hivyo fainali hizi ni muhimu kwa klabu zote mbili ambazo zinataka kuweka rekodi ya kunyakua ubingwa wa Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza. Kwa klabu zote mbili haya ndiyo yatakuwa mafanikio makubwa zaidi.
Kwa Yanga fainali hii ni mchezo muhimu zaidi katika historia yao, kwani ushindi wao utakuwa ni rekodi mpya kwa Tanzania. Hakuna klabu ya Tanzania ambayo imewahi kushinda taji la vilabu vya Afrika.
Rekodi ya juu zaidi ilikuwa inashikiliwa na wapinzani wao Simba ambayo ilikuwa ni kucheza fainali ya mashindano kama haya miongo mitatu iliyopita.
Sasa Hii ni fursa kwa Yanga kujikita katika kilele cha ubora wa kuwa ndiyo klabu yenye mafanikio zaidi nchini Tanzania.
Safari ya Yanga kutinga fainali
Yanga imefika fainali baada ya kuichapa klabu ya Gallants FC kutoka Afrika Kusini jumla ya mabao 4-1. Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0 jijini Dar es Salaam katika mechi ya nusu fainali ya kwanza na kisha hapo jana kushinda mkondo wa pili kwa mabao 2-1 nchini Afrika Kusini.
Katika hatua ya robo fainali, Yanga ilifuzu kwa ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Rivers United ya Nigeria. Mechi ya kwanza Yanga ilishinda ugenini goli hizo mbili na kisha kutoka sare ya kutofungana jijini Dar Es Salaam.
Nyota ya Yanga ilianza kung’ara toka katika hatua ya makundi ambapo walimaliza katika nafasi ya kwanza kwa kushinda michezo minne kati ya sita, huku wakitaka sare mchezo mmoja na kupoteza mchezo mmoja tu.
































