Mkuu wa jeshi la Sudan azuia akaunti za benki za mpinzani wake wa RSF
Mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametoa agizo la kufungia akaunti za benki za kundi la wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) na kampuni zake tanzu.
Moja kwa moja
Rais Ruto apokea ombi la pamoja la Kenya,Uganda na Tanzania kuandaa Afcon 2027

Chanzo cha picha, Pool
Rais William Ruto wa Kenya Jumatatu alipokea ombi la pamoja la Kenya kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2027 pamoja na majirani Uganda na Tanzania.
Waziri wa Michezo wa nchi hiyo Ababu Namwamba na Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya Nick Mwendwa waliwasilisha hati hiyo kwa Dkt Ruto katika Ikulu ya Nairobi.
Kenya imeungana na majirani wake Tanzania na Uganda katika mpango uliopewa jina la "Pamoja" kuleta mashindano ya bara hilo yanayotamaniwa sana katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza katika historia.
Rais alimuagiza Waziri wa Michezo Ababu Namwamba kuwasiliana na wenzake kutoka Uganda na Tanzania ili mataifa hayo matatu ya Afrika Mashariki yaweze kufanikiwa kushinda ombi la kuandaa mashindano hayo makubwa zaidi ya kandanda barani.
Kariakoo:Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa akemea 'kamata kamata' ya TRA dhidi ya wafanyabiashara
Maelezo ya sauti, Kariakoo:Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa akemea 'kamata kamata' ya TRA Biashara katika soko la kimataifa la Kariakoo jijini Dar es Salaam, Tanzania zimekwama kufanyika hii leo kufuatia mgomo wa wafanyabiashara, wanaopinga kile wanachokiita taratibu zisizofaa za kudai na kukusanya kodi yakiwemo malimbikizo ya kodi za miaka iliyopita pamoja na ukaguzi wa maghala ya bidhaa.
Yote hayo yanadaiwa kutekelezwa na maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa njia za unyanyasaji. Hali hiyo imemlazimisha Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa kusafiri kutoka Bungeni Dodoma hadi Dar es Salaam ili kuzungumza na wafanyabiashara hao
Zelensky akutana na Waziri Mkuu huku silaha zaidi kwa Ukraine zikiahidiwa

Chanzo cha picha, PA Media
Uingereza imekubali kutuma mamia ya makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani zenye silaha nchini Ukraine.
Haya yanajiri juu ya uamuzi wa Uingereza wa wiki jana kuipatia Kyiv makombora ya Storm Shadow.
Hatua hiyo ina maana kwamba Uingereza inakwenda mbele zaidi kuliko nchi nyingine yoyote katika kutoa silaha zenye uwezo wa kuinua uwanja wa vita kwa upande wa Ukraine.
Hapo awali, Rais Volodymyr Zelensky alikutana na Rishi Sunak wa Uingereza kama sehemu ya ziara yake ya washirika wa Magharibi.
Ukraine inaendelea kujiandaa kwa mashambulizi ambayo yanatarajiwa dhidi ya majeshi ya Urusi.
Wiki iliyopita, Bw Zelensky aliambia BBC kuwa nchi yake inahitaji silaha zaidi kabla ya kufanya mashambulio hayo.
Siku ya Jumatatu, rais wa Ukraine alikuwa na takriban saa mbili za mazungumzo na Bw Sunak huko Checkers, karibu na London.
Aliwasili katika ardhi ya Uingereza kwa ziara ya ghafla baada ya ziara ya Ulaya Magharibi ambayo pia ilimpeleka Roma, Berlin na Paris.
Bw Zelensky alisema Ukraine na Uingereza ni "washirika wa kweli".
Makombora hayo mapya yanaweza kutumika kuharibu maeneo ambako kuna wanajeshi wa Urusi .
Iwapo Ukraine inaweza kuharibu vituo vya jeshi la Urusi, vituo vya vifaa na maghala ya risasi katika eneo linalokaliwa, basi inaweza kuwa vigumu kwa Moscow kuendelea kuwasambazia tena wanajeshi wake silaha na chakula katika mstari wa mbele .
Mpaka wa Kenya na Somalia kufunguliwa ndani ya siku 90

Chanzo cha picha, Kithure Kindiki/Twitter
Kenya na Somalia zimeazimia kufungua mpaka kwa awamu, ndani ya siku 90 zijazo.
Akitoa tangazo hilo Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Kithure Kindiki alisema kuwa mpaka wa Mandera/Belet Hawo (Belethawa) utakuwa wa kwanza kufunguliwa katika muda wa siku 30 zijazo.
Sehemu hii ya mpaka inatoa kiingilio kutoka upande wa Kenya katika Kaunti ya Mandera.
"Katika awamu ya pili ambayo ni siku 60 kutoka sasa, tunafaa kuwa na uwezo wa kufungua mpaka wa pili Liboi-Harhar/Dhobley. Hii itatoa kiingilio kutoka kaunti ya Gariisa," alisema.
Sehemu ya tatu ya mpaka itakayofunguliwa itakuwa Kiunga/Ras Kamboni huko Lamu.
Waziri Kindiki alithibitisha kuwa serikali ya Kenya itaendelea kushirikiana na Serikali ya Shirikisho la Somalia ili kuendeleza na kutekeleza mbinu na mikakati ya pamoja katika masuala ya kiuchumi na kupambana na ukosefu wa usalama katika mipaka ya nchi hizo .
Mwenzake kutoka Somalia, Mohamed Ahmed Sheikh Ali alisema Serikali ya Shirikisho imejitolea kukuza na kuimarisha ushirika na majirani zake ili kuimarisha usalama.
Wawili hao pia waliazimia kuimarisha mawasiliano ya mipakani na upashanaji habari kati ya nchi hizo mbili.
Mipaka ilifungwa mwaka 2011 katika kilele cha mashambulizi ya al Shabaab.
Treni ya Austria yacheza hotuba ya Hitler kupitia kipaza sauti

Chanzo cha picha, Getty Images
Wasafiri waliokuwa kwenye treni ya kusafiri mji mmoja mmoja hadi mwingine nchini Austria walishangazwa siku ya Jumapili wakati rekodi ya hotuba ya Adolf Hitler ilipochezwa kwenye treni hiyo .
Badala ya matangazo ya kawaida, umati wa watu pia ulisikika ukipiga kelele "Heil Hitler" na "Sieg Heil" juu ya mfumo wa spika za treni.
Mhudumu wa treni hizo amesema kumekuwa na matukio kadhaa kama hayo katika siku za hivi karibuni.
Abiria mmoja kwenye huduma ya Bregenz-Vienna aliambia BBC kwamba kila mtu kwenye treni hiyo "alishtuka kabisa".
David Stoegmueller, Mbunge wa Chama cha Kijani, alisema hotuba ya kiongozi wa Nazi wa Ujerumani ilichezwa kwenye spika za treni muda mfupi kabla ya treni, OEBB Railjet 661, kuwasili Vienna.
"Tulisikia vipindi viwili," alisema."Kwanza kulikuwa na sekunde 30 za hotuba ya Hitler, na kisha nikasikia 'Sieg Heil'."
Bw Stoegmueller alisema wafanyakazi wa treni hawakuweza kuzuia hotuba hiyo na hawakuweza kutoa matangazo yao wenyewe."mhudumu mmoja wa treni alikasirika sana," aliongeza.
Katika taarifa iliyotumwa kwa BBC, Shirika la Reli la Austria (OEBB) lilisema: "Tunajitenga wazi na kilichotokea'
"Kwa sasa tunaweza kudhani kuwa matangazo yalitolewa na watu moja kwa moja kwenye treni kupitia njia za mawasiliano. Tumeripoti suala hilo kwa polisi," OEBB ilisema.
Inafahamika kuwa malalamiko yamewasilishwa dhidi ya watu wawili.
Mwimbaji wa Afrobeats Seun Kuti akamatwa kwa madai ya kumshambulia Polisi

Chanzo cha picha, @BenHundeyin
Mwimbaji wa muziki wa Afrobeats wa Nigeria Seun Kuti amekamatwa kwa madai ya kumshambulia afisa wa polisi, msemaji wa polisi wa Lagos Benjamin Hundeyin ameandika kwenye Twitter., pamoja na picha ya mwanamuziki huyo akiwa na pingu.
Kuti alijisalimisha katika makao makuu ya Kamandi ya Polisi ya Jimbo la Lagos baada ya mkuu wa polisi Usman Alkali Baba kuamuru azuiliwe Jumamosi.
"Alinaswa kwenye video akimshambulia afisa wa polisi aliyevalia sare", msemaji wa polisi aliongeza.
Kuti - mtoto wa mwanzilishi wa Afrobeat Fela Kuti - alienda katika makao makuu ya polisi Jumatatu na wakili wake na mwakilishi wa familia, Hundeyin aliongeza.
Kabla ya kukamatwa, Kuti alisema kwenye Twitter kwamba polisi huyo alijaribu kumuua yeye na familia yake, lakini hakueleza jinsi gani.
Yeye na wakili wake hawajazungumza chochote tangu kukamatwa kwake.
Hilda Baci: Mpishi wa Nigeria anayepania kuvunja rekodi ya dunia

Chanzo cha picha, bb
Mpishi mmoja nchini Nigeria amekuwa maarufu baada ya kupika kwa zaidi ya saa 90 bila kikomo katika jaribio la kuvunja rekodi ya dunia.
Hilda Baci amepika zaidi ya vyakula 100 tofauti tangu awashe jiko lake saa 15:00 GMT siku ya Alhamisi.
Rekodi ya sasa ni ya saa 87 na dakika 45 iliyowekwa Rewa, katikati mwa India mnamo 2019 na mpishi wa India Lata Tondon.
Guinness World Records inasema inakagua ushahidi kabla ya kusema ikiwa amevunja rekodi.
Ingawa hakuna maafisa wa shirika walio katika eneo la soko la Lekki huko Lagos, kamera za CCTV zimewekwa kufuatilia tukio hilo.
Baci, 27, awali alipanga kupika kwa saa 96 - hadi 15:00GMT Jumatatu.
Lakini umati wa watu wenye ghasia ambao umepiga kambi nje ya ukumbi unamchochea kufikia muda wa saa 100.
Amebuni maelfu ya sehemu ya chakula, ambayo inatolewa kwa wageni waalikwa.
Anaruhusiwa msaidizi mmoja kwa wakati, na anaweza kuchukua mapumziko ya dakika tano kila saa, au sawa na saa kadhaa.
Mpishi anaonyesha dalili zinazoonekana za uchovu wa mwili na anapata mikanda baridi kichwani mwake, na kukandwa miguu wakati wa mapumziko.
Msaidizi wa matibabu pia anafuatilia ishara zake muhimu.
Jaribio lake limevutia nchi, huku wanasiasa na watu mashuhuri wakipita kumshangilia.
Profesa wa Florida avunja rekodi ya muda aliotumia kuishi chini ya maji

Chanzo cha picha, Reuters
Mtafiti wa Marekani amevunja rekodi ya dunia kwa muda mrefu zaidi aliotumia kuishi chini ya maji bila presha kutolewa katika kifaa kilichowekwa majini alimoishi .
Joseph Dituri amekaa zaidi ya siku 74 chini ya rasi ya 30ft-deep huko Key Largo, Florida.
Na hana mpango wa kuacha bado.Siku ya Jumapili, alisema angekaa katika hapo kwa angalau siku 100.
"Hamu ya ugunduzi imenifikisha hapa," alisema.
"Lengo langu tangu siku ya kwanza limekuwa kuhamasisha vizazi vijavyo, kuwahoji wanasayansi wanaosoma maisha chini ya bahari na kujifunza jinsi mwili wa binadamu unavyofanya kazi katika mazingira magumu," aliongeza.
Rekodi ya awali ya dunia ya siku nyingi za kuishi chini ya maji kwa presha ya mazingira - 73 - ilianzishwa na maprofesa wawili mwaka wa 2014 katika eneo sawa na Key Largo.
Mexico yapeleka ndege ya rais iliyokataliwa nchini Tajikistan

Chanzo cha picha, Reuters
Ndege ya kifahari ya rais ambayo Mexico ilikuwa ikijaribu kuiuza kwa zaidi ya miaka minne hatimaye imewasili katika makazi yake mapya - Tajikistan.
Rais López Obrador alifanya uuzaji wa ndege hiyo aina ya Boeing 787 Dreamliner kuwa moja ya ahadi zake za kampeni, akiiita ishara ya ubadhirifu wa serikali zilizopita.
Lakini ndege hiyo iliyokuwa na vifaa maalum ilikuwa ngumu kuiacha na jaribio la kuiuza mnadani lilikumbwa na changamoto nyingi .
Hatimaye iliuzwa kwa serikali ya Tajik kwa $92m (£73.7m).
Ndege hiyo ilipaa kutoka California, ambapo ilikuwa imehifadhiwa, na kufika katika mji mkuu wa Tajik, Dushanbe, mapema Jumatatu.
Awali ndege hiyo ilinunuliwa mwaka wa 2012 na rais wakati huo, Felipe Calderón, kwa $218m (£175m).Wakati huo ilitumiwa na mrithi wa Bw Calderón, Enrique Peña Nieto.
Bw López Obrador aliapa kutokanyaga kamwe ndani ya ndege hiyo.Amekuwa akitumia ndege za kibiashara tangu aingie madarakani.
Hata hivyo, uuzaji wa ndege hiyo ulikumbwa na matatizo.
Kwa nini nilimteua mkuu wa jeshi licha ya pingamizi - Rais wa Kenya

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais wa Kenya William Ruto Rais wa Kenya William Ruto anasema alimteua mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya kwa sababu alikuwa bora zaidi, licha ya kuwa miongoni mwa watu waliojaribu "kupindua ushindi wangu" katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
"Nilimteua Jenerali [Francis] Ogolla, ni miongoni mwa watu waliokwenda Bomas kujaribu kupindua ushindi wangu... Lakini nilipotazama wasifu wake, alikuwa mtu bora zaidi kuwa jenerali," alisema.
"Nilipozungumza naye, ni nini kililiongoza akili yangu, ndio labda alifanya makosa... Nilipozungumza naye, aliniambia 'Sina utetezi...nilichofanya ni makosa'," Bw Ruto alieleza, akisema. alifanya uamuzi huo kwa uangalifu na kinyume na ushauri wa watu wengi.
Rais alikuwa akizungumza wakati wa mahojiano ya televisheni Jumapili usiku.
Alikuwa akijibu tuhuma kwamba kulikuwa na upendeleo wa kikabila katika uteuzi wa nyadhifa za serikali - ambayo alikanusha.
Wakati wa rufaa ya kupinga matokeo ya kura ya urais, aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini Kenya Wafula Chebukati alidai kuwa Jenerali Ogolla alikuwa sehemu ya wajumbe wa Baraza la Ushauri wa Usalama wa Kitaifa (NSAC) waliotaka kushawishi matokeo ya uchaguzi ili kumpendelea kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
Katika taarifa ya kiapo kwa Mahakama ya Juu, alisema kuwa Jenerali Ogolla na wengine katika NSAC walikuwa wametumwa katika kituo cha kujumlisha kura katika mji mkuu Nairobi.
NSAC ilikanusha madai hayo lakini ikakiri kufanya mkutano na mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi.
Mahakama ya Juu, ambayo iliidhinisha ushindi wa Bw Ruto, haikutoa uamuzi wowote wa uhakika kuhusu madai ya Bw Chebukati.
Pia unaweza kusoma:
- Ninajiweka sawa kiafya- kiongozi wa Kenya aeleza kuhusu kupungua kwa uzani wake
- Kiongozi wa Kenya aomba radhi kwa vifo vya watu walioangamia Shakahola
BBC Africa Eye: Tazama Wanaigeria wanavyolaghaiwa kwa kuwa wapenzi wa jinsia moja
Maelezo ya video, BBC Africa Eye: Wanaigeria wanavyoingia kwenye mtego na kulaghaiwa kwa kuwa wapenzi wa jinsia moja Mtandao ulikuwa mahali ambapo jumuiya ya LGBT nchini Nigeria kuungana na wengine kwa usalama zaidi - hadi magenge ya wahalifu yalipojiunga kidijitali pia.
Africa Eye inachunguza jinsi Wanaigeria wanavyoingia kwenye mtego na kulaghaiwa kwenye programu za uchumba kwa kuwa wapenzi wa jinsia moja.
Afrika Kusini haitaegemea upande wowote katika vita vya Ukraine - Ramaphosa

Chanzo cha picha, AFP
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema kuna "shinikizo la ajabu" kwa nchi hiyo kuacha msimamo wake wa kutofungamana na upande wowote kuhusu vita vya Ukraine.
Katika taarifa, Bw Ramaphosa alisema Afrika Kusini haitaunga mkono upande wowote katika kile alichosema ni "mashindano kati ya Urusi na Magharibi".
Matamshi yake yanakuja siku chache baada ya balozi wa Marekani nchini Afrika Kusini, Reuben Brigety, kuishutumu nchi hiyo kwa kutoa silaha na risasi kisiri kwa Urusi, licha ya kudai kutoegemea upande wowote.
Bw Brigety alisema ujasusi wa Marekani ulikuwa na uhakika kuwa silaha zilikuwa zimepakiwa kwenye meli ya Urusi katika kambi ya wanamaji mjini Cape Town mwezi Desemba.
Bw Ramaphosa amekubali kuchunguza madai hayo lakini anasema hakuna ushahidi thabiti wa kuunga mkono madai hayo.
Pia unaweza kusoma:
China yamhukumu raia wa Marekani kifungo cha maisha jela kwa kufanya ujasusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, John Shing-Wan Leung alikuwa mkazi wa kudumu wa Hong Kong, lakini haijulikani wazi alikuwa akiishi wapi alipokamatwa (picha ya maktaba) Mahakama ya China imemhukumu kifungo cha maisha jela raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 78 kwa makosa ya ujasusi.
John Shing-Wan Leung, ambaye ni mkazi wa kudumu wa Hong Kong, alifungwa jela siku ya Jumatatu.
Mahakama katika ya Suzhou kusini mashariki mwa nchi haikutoa maelezo zaidi kuusiana na tuhuma dhidi yake.
Leung alikamatwa mjini humo miaka miwili iliyopita na ofisi ya ndani ya shirika la kukabiliana na ujasusi la China, taarifa ya habari kutoka mahakamani ilisema.
"Alipatikana na hatia ya ujasusi, alihukumiwa kifungo cha maisha jela [na] kunyimwa haki za kisiasa za maisha", kulingana na taarifa kutoka Mahakama ya ambayo ilichapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa WeChat.
Haijulikani Leung alikuwa akiishi wapi wakati wa kukamatwa kwake.
Kiongozi wa Kenya aomba radhi kwa vifo vya watu walioangamia Shakahola

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Zaidi ya miili 100 imefukuliwa katika makaburi huko Shakahola Rais William Ruto amewaomba Wakenya msamaha kutokana na vifo vya Wakristo walioangamia katika kanisa la kufunga hadi ufe , akikiri ulegevu na kuridhika kutoka kwa upande wa serikali.
Zaidi ya miili 200 hadi sasa imetolewa katika msitu wa pwani wa Shakahola, ambapo waumini walilazimika kufa kwa njaa ili kukutana na Yesu. Zaidi ya watu 600 bado hawajulikani walipo.
"Ninachukua jukumu kwamba, kama rais, haya (mauaji ya Shakahola) hayakupaswa kutokea. Kwa hilo, nasema kweli, samahani," Bw Ruto alisema katika mahojiano ya televisheni na vyombo vya habari vya Kenya Jumapili.
Aliwalaumu polisi na maafisa wa ujasusi nchini kwa kushindwa kugundua shughuli za ibada hiyo kwa wakati.
Alisema maafisa husika watalazimika kutoa maelezo kuhusu mauaji hayo ya halaiki.
Rais alisema kwamba atafanya kila awezalo kuzuia vifo vya kidini siku zijazo.
Pia aliahidi kutembelea msitu wa Shakahola mara uchunguzi utakapokamilika.
Chama cha wamiliki wa matatu nchini Kenya kuongeza nauli kuendana na bei mpya ya mafuta
Chama cha wamiliki wa matatu nchini Kenya wamesema hawana budi bali kuwatwisha abiria mzigo huo wa bei ya mafuta kwa kuongeza nauli kuendana na bei mpya ya mafuta ya petroli na dizeli.
Mwenyekiti wa Chama cha wamiliki wa matatu (daladala) nchini Kenya, Samuel Kimutai amezungumza na Mwandishi wa BBC Carol Robi.
Maelezo ya sauti, Chama cha wamiliki wa matatu nchini Kenya kuongeza nauli kuendana na bei mpya ya mafuta Mkuu wa jeshi la Sudan azuia akaunti za benki za mpinzani wake wa RSF

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Burhan Mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan ametoa agizo la kufungia akaunti za benki za kundi la wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) na kampuni zake tanzu.
Katika amri siku ya Jumapili, Jenerali Burhan pia alistaafisha maafisa wanne wa kijeshi wanaohusishwa na kundi hilo.
Mmoja wa maafisa walioathiriwa ni Brig Jenerali Omar Hamdan Ahmed, kamanda wa RSF Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo, na ambaye kwa sasa anaongoza ujumbe wa jeshi la wanamgambo kwa mazungumzo ya amani na jeshi la Sudan huko Jeddah, Saudi Arabia.
Jenerali Burhan pia alimfuta kazi gavana wa benki kuu Hussain Yahia Jankol na kumteua Borai El Siddiq badala yake.
Hakutoa sababu ya kufutwa kazi kwa Bw Jankol.
Wakati huo huo, chaneli ya serikali ya Sudan TV ilianza tena matangazo yake ya satelaiti siku ya Jumapili, wiki moja baada ya kwenda hewani.
Usambazaji wa kituo hicho umeathirika mara kadhaa tangu mapigano kati ya jeshi na RSF kuanza tarehe 15 Aprili.
Ninajiweka sawa kiafya- kiongozi wa Kenya aeleza kuhusu kupungua kwa uzani wake

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Rais William Ruto Rais wa Kenya William Ruto anasema kupunguza uzani wake unaoonekana ni juhudi zake za makusudi za kujiweka sawa huku kukiwa na wasiwasi wa baadhi ya Wakenya kwenye mitandao ya kijamii kuhusu afya yake.
Akizungumza katika mahojiano na wanahabari Jumapili, Rais Ruto alieleza kuwa ameongeza uzito katika kipindi cha kampeni mwaka wa 2022.
Wakati huo, alisema, kulikuwa na shinikizo kubwa ambalo wakati mwingine lilisababisha mkazo wa kula.
Bw Ruto alisema alipunguza uzito baada ya kuanza tena programu yake ya utimamu wa mwili, lishe na afya njema.
“Kwa asili ya kazi yangu, sina budi kuwa macho,” akasema Bw Ruto.
Baadhi ya Wakenya walikuwa wameona kuwa Rais Ruto alikuwa amepungua uzito miezi kadhaa baada ya kuchukua wadhifa wa mtangulizi wake.
Wengine walikisia kwamba huenda mkuu huyo wa nchi alikuwa mgonjwa.
Martin Odegaard: Hakuna matumaini' katika mbio za ubingwa baada ya kushindwa na Brighton
Martin Odegaard: Hakuna matumaini' katika mbio za ubingwa baada ya kushindwa na Brighton
Ingawa kihesabu bado haijathibitishwa, nyuso za wachezaji wa Arsenal mwishoni mwa kichapo chao cha 3-0 kutoka kwa Brighton siku ya Jumapili ziliweka wazi kuwa walijua mbio za kuwania taji la Ligi Kuu ya Uingereza zimekamilika.
Wengine walisimama wakitazama kwa mbali, wengine walikaa uwanjani na kutazama chini huku wapinzani wao wakishangilia
Mchezo huu ulionekana kama fursa ya mwisho kwa Arsenal. Bado walihitaji Manchester City kuteleza katika mechi zao tatu zilizosalia, lakini ushindi ulihitajika iwapo wangesalia kupigania nafasi hiyo ya kwanza.
Badala yake, walisalimu amri huku Brighton wakifunga mabao matatu ya kipindi cha pili ili kuimarisha jitihada zao za kuhakikisha wanashiriki katika soka la Ulaya msimu ujao.
Kupoteza huko kunamaanisha kuwa Arsenal wako nyuma ya vinara Manchester City kwa pointi nne na wamebakiza mechi mbili pekee.
Vijana wa Pep Guardiola wanajua ushindi dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa Etihad Jumapili ijayo unamaanisha kuwa ubingwa utakuwa wao.
Lord Sentamu: Askofu mkuu za zamani wa York kujiuzulu

Chanzo cha picha, PA MEDIA
Maelezo ya picha, Lord Sentamu alidai barua aliyotumiwa na muathiriwa haikufichuliwa Askofu mkuu wa York amelazimishwa kujiuzulu wadhifa wake katika Kanisa la England baada ya tathimini kuhusu jinsi alivyoshughulikia madai ya unyanyasaji wa kingono.
Lord Sentamu tayari amekataa matokeo ya ripoti ambayo ilisema alishindwa kuchukua hatua kuhus madai yaliyotolewa na muathiriwa.
Amekuwa ni naibu askofu wa heshima katika Dayosisi ya Newcastle.
Askofu wa Newcastle amemtaka ajiuzulu katia kazi ya utume " hadi matokeo ya uchunguzi na jibu lake kuuhusu vitakapochunguzwa zaidi".
Kanisa limeomba radhi kwa mchungaji mstaafu Matthew Ineson, ambaye alikuwa na umri wa miaka 16 aliponyanyaswa kingono katika miaka ya 1980.
Mtu aliyemnyanyasa, Mchungaji Trevor Devamanikkam, alijiua mwenyewe kabla ya kuwasili mahakamani.
Mnamo mwaka 2013, Bw Ineson alimaambia viongozi wa kanisa wa ngazi ya juu kuhusu unyanyasaji, akiwemo Lord Sentamu ambaye wakati huo alikuwa Askofu Mkuu wa jimbo la York.
Lord Sentam ana asili ya Uganda.
