Putin anapaswa kuhukumiwa kwa 'vitendo vya uhalifu' - Zelensky

Zelensky pia aliishutumu Urusi kwa uhalifu 6,000 wa kivita mwezi Aprili pekee, na kusababisha vifo vya raia 207 wa Ukraine wakiwemo watoto 11.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo hya ya moja kwa moja. Hadi kesho kwaheri.

  2. Ezekiel Odero:Mhubiri wa televisheni nchini Kenya aachiliwa kwa dhamana huku uchunguzi ukiendelea

    th

    Chanzo cha picha, AFP

    Mmoja wa wahubiri maarufu wa televisheni nchini Kenya ameachiliwa kwa dhamana, baada ya kufika mahakamani kuhusiana na vifo vya zaidi ya watu 100 - wanaodhaniwa kuwa washiriki wa ibada ya siku ya mwisho duniani .

    Ezekiel Odero, mchungaji tajiri mwenye wafuasi wengi, anachunguzwa kuhusu madai ya mauaji, kusaidia watu kujiua, utekaji nyara na utakatishaji fedha.

    Hakimu Joe Omido anayesimamia kesi ya Mchungaji Odero alisema hakuna “taarifa za kutosha kuhusu hali ya uchunguzi” dhidi ya kiongozi huyo wa kanisa ili kuhalalisha kuendelea kumzuilia, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

    Waendesha mashtaka wanamshtumu kwa kuwa na uhusiano wa kibiashara na kiongozi wa dhehebu hilo, Paul Nthenge Mackenzie, ambaye yuko kizuizini akikabiliwa na mashtaka ya ugaidi kuhusu mauaji hayo.

    Wengi wa waliofariki, ambao walipatikana katika msitu wa Shakahola karibu na mji wa Malindi, Pwani mwa Kenya walikuwa watoto.

    Katika kesi wasilisho mahakamani mapema wiki hii, Mchungaji Odero alisema alijitenga na Bw Mackenzie.

    th

    Unaweza pia kusoma

  3. Meya azua gumzo Somalia baada ya kunaswa katika picha akiwapiga watu wakijivinjari

    p

    Chanzo cha picha, @MOHAMEDSELH

    Meya wa Mogadishu hana masihara linapokuja suala la kukabiliana na dawa za kulevya katika mji mkuu wa Somalia - kiuhalisia.

    Yusuf Hussein Jimale amethibitisha hilo - katika video ambayo inamuonyesha akipiga kundi la vijana wa kiume na wa kike.

    Vijana hao wanaonekana wakijaribu kujikinga huku akiwapiga kwa fimbo ndefu, kuwatuhumu kwa kuvuta bangi, shisha na kunywa pombe kwenye klabu ya burudani iliyopo kwenye ufuo maarufu wa Lido mjini humo.

    Madale ametetea hatua yake akisema vijana wanahitaji kuwa na nidhamu, na fimbo ni bora kuliko bunduki.

    "Kwa vile walikuwa wamelewa wengine walijaribu kupigana nasi tukawachapa viboko, kimaadili hatuwezi kuruhusu tabia tulizozishuhudia na hakuna anayeweza kuvumilia hilo," alisema siku 10 zilizopita.

    Baadhi ya watu wamekerwa na kile wanachokiona kama hoja ya meya - wakitaka kuona ushahidi wa makosa ya wahasiriwa wake na kutaka utaratibu ufuatwe.

    "Meya alijichukulia sheria mkononi badala ya kuziachia vyombo husika. Mtu anayefanya uhalifu anapaswa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria kupitia mfumo wa mahakama," Muna Hassan, mwanaharakati wa masuala ya kijamii mjini Mogadishu, aliambia BBC.

    Lido Beach ni sehemu inayopendwa na vijana mjini Mogadishu

    Chanzo cha picha, LEYLA JEYTE

    Maelezo ya picha, Lido Beach ni sehemu inayopendwa na vijana mjini Mogadishu

    Wengine wanasema hatua ya Meya ya kutumia viboko katika nchi ambayo kupiga watoto ni aina ya nidhamu inayokubalika.

    Mkazi wa Mogadishu, Mohamed Noor alitweet kwamba Madale alichukulia hatua kama mzazi.

    ''Aina hii ya nidhamu ilikuwa bora kuliko mbinu kali kama vile kuwakamata na kuwafungwa, ambazo "zingegeuza watu kuwa wahalifu wa maisha," alisema.

    Msemaji wa manispaa ya Mogadishu alisema njia bora ya kupambana na dawa za kulevya ni kufuta leseni za baa na migahawa zitakazopatikana na dawa hizo.

  4. Marekani 'haikuwa na jukumu lolote' katika mashambulizi la Kremlin - Kirby

    Kirby

    Chanzo cha picha, EPA

    Ikulu ya White House imekanusha vikali madai ya Urusi kwamba Marekani ilipanga shambulio la ndege isiyo na rubani dhidi ya Urusi hapo jana.

    Mapema leo, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alidai, bila ushahidi wowote, kwamba Marekani ilihusika na tukio hilo, akidai kuwa Ukraine ilifanya shambulio chini ya maelekezo kutoka Washington.

    Awali msemaji wa usalama wa taifa wa Ikulu ya White House, John Kirby, aliliambia shirika la utangazaji la MSNBC madai hayo ni ya uongo, na kwamba Marekani haihimizi Ukraine kufanya mashambulizi nje ya mipaka yake.

    Katika mahojiano tofauti, Bw. Kirby alisisitiza kuwa Marekani "haikuwa na jukumu lolote" katika tukio hilo.

    Aliiambia CNN: "Ningewaambia tu uwongo wa Bw. (Dmitry) Peskov. Namaanisha, ni wazi ni madai ya kejeli. Marekani haikuwa na uhusiano wowote na hili. Hata hatujui kilichotokea. Lakini naweza kukuhakikishia Marekani haikuwa na jukumu lolote katika hilo."

  5. Tazama: Wahasiriwa wa mafuriko Rwanda wazikwa maeneo tofauti

    Maelezo ya video, Wahasiriwa wa mafuriko Rwanda wazikwa

    Shughuli za mazishi zimekuwa zikifanyika katika maeneo tofauti yaliyokumbwa na mafuriko nchini Rwanda.

    Katika mji Wa Rubavu watu 13 wamezikwa leo katika kabiri la Rugerero na kuhudhuriwa na wakuu wa serikali akiwemo waziri mkuu Edouard Ngirente.

    Serikali inasema hadi sasa watu wasiopungua 130 wamefariki kutokana na mafuriko yaliyotikisa majimbo ya magharibi na kaskazini mwa Rwanda

    Mwandishi wa BBC, Yve Bucyana alihudhuria baadhi ya mazishi hayo.

  6. Papa Francis amvua upadre raia wa Rwanda

      • Author, Samba Cyuzuzo
      • Nafasi, BBC Great Lakes
    Papa Francis

    Chanzo cha picha, Reuters

    Papa Francis amemvua upadri mzaliwa wa Rwanda ambaye amekuwa akihudumu kama kasisi kaskazini mwa Ufaransa kwa takriban miongo mitatu.

    Taarifa inayosambazwa mtandaoni iliyotiwa saini na askofu wa Évreux inasema kwamba Wenceslas Munyeshyaka, 64, "anapoteza moja kwa moja haki za ukasisi" na "amezuiliwa" kutumikia "mahali popote" kama kasisi.

    Ofisi ya Dayosisi ya Evreux imeithibitishia BBC uhalisi wa taarifa hiyo ambayo inasema kuwa inatokana na agizo la Papa la Machi.

    Bw Munyeshyaka, ambaye alikimbilia Ufaransa baada ya mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994, hajazungumzia uamuzi huo.

    Alisimamishwa kazi na Dayosisi ya Evreux mnamo Desemba 2021 baada ya kuibuka kuwa amekiri kisheria kuwa baba wa mvulana wa miaka 10.

    Bw Munyeshyaka alitawazwa kuwa kasisi nchini Rwanda mwaka wa 1992 ambapo anatuhumiwa kuhusika katika mauaji ya mamia ya Watutsi waliokuwa wamekimbilia kanisani kwake katika mji mkuu wa Kigali wakati wa mauaji ya kimbari.

    Mahakama nchini Ufaransa zimemuondolea mashtaka ya mauaji ya halaiki.

  7. Putin anapaswa kushitakiwa kwa 'vitendo vya uhalifu' - Zelensky

    Volodymyr Zelensky

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametoa wito wa kuanzishwa kwa mahakama maalum ambayo itawaijibisha Urusi kuhusiana na makosa yaliyotokana na "uchokozi wake" akijenga hoja yake kwa kutoa mfano uliowekwa na Nuremburg - kesi zinazoendeshwa na Washirika dhidi ya wawakilishi wa Ujerumani ya Nazi iliyoshindwa.

    Aliishutumu Urusi kwa uhalifu 6,000 wa kivita mwezi Aprili pekee, na kusababisha vifo vya raia 207 wa Ukraine wakiwemo watoto 11.

    Bw. Zelensky aliorodhesha uhalifu mwingine wa kivita unaodaiwa kufanywa na Urusi - ikiwa ni pamoja na "mamilioni" ya mashambulizi katika mikoa ya Donbas na wale waliouawa wakati ilipokuwa imekalia eneo la Bucha.

    Alisema "sote tunataka kuona Vladimir tofauti hapa", akimuashiria Rais wa Urusi Putin, ambaye alimwita "anayestahili kuhukumiwa kwa vitendo vya uhalifu katika mji mkuu wa sheria za kimataifa."

    Aliishukuru Uholanzi kwa kutoa silaha kwa Ukraine, na kuongeza kuwa vita vinashindwa kwa "nguvu ya silaha" - kutilia mkazo wito wake wa mara kwa mara wa kutaka silaha zaidi kutoka kwa washirika wake.

    Alisema mzozo wa Ukraine ulikuwa "vita ambavyo hatukuvitaka, vita ambavyo tunapaswa kuwa vya mwisho - na tutafanya hivyo."

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  8. Urusi yaishtumu Marekani kwa kuhusika na shambulio la Kremlin

    Urusi imeishutumu Marekani kwa kuhusika na shambulizi la ndege zisizo na rubani kwenye Ikulu ya Kremlin ambayo inasema ilikusudia kumuua Vladimir Putin.

    Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema kuwa "maamuzi juu ya mashambulizi hayo hayafanywi mjini Kyiv, bali Washington".

    "Kyiv hufanya tu kile inachoambiwa kufanya," aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano mfupi.

    Peskov hakutoa ushahidi wowote kuunga mkono madai hayo, lakini alisema kuwa uchunguzi wa dharura unaendelea.

    Hapo jana, maafisa wa Marekani walisema Ikulu ya White House haikuwa na taarifa yoyote kuhusu shambulio la ndege isiyo na rubani mjini Kremlin.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alitilia shaka shutuma za Kremlin kufuatia tukio hilo, na kusema: "Ningechukua kitu chochote kikitoka Kremlin kwa mashaka makubwa." Ukraine pia imekana kuhusika na shambulio hilo.

  9. Tazama: Dereva wa lori lililozungukwa na mafuriko aponea kifo

      • Author, Abdalla Dzungu
      • Nafasi, BBC Swahili, Nairobi
    Maelezo ya video, Dereva wa lori lililozungukwa na mafuriko aponea kifo

    Dereva mmoja wa lori la mafuta aliponea maisha chupuchupu baada ya kukwama katika lori lake ambalo lilikuwa linakaribia kuangamizwa na mafuriko.

    Kulingana na tovuti ya shirika la Shedrick Worldlife Trust, dereva huyo alikuwa anaendesha lori hilo katika barabara ya Gulana kulalu kaunti ya Tanariver nchini Kenya mwendo wa saa kumi jioni siku ya Jumatano wakati mto ulipofurika na kulizunguka lori hilo.

    Mafuriko ni tishio la mara kwa mara wakati wa msimu wa mvua nchini Kenya , na mara nyingi haiwezekani kutabiri ni lini au jinsi gani viwango vya maji vitaongezeka.

    Akiwa amekwama ndani ya lori hilo lililozungukwa na maji, hatari ya dereva na lori hilo ilionekana kuongezeka baada ya maji hayo yaliokuwa na nguvu kuliangusha lori hilo upande mmoja , hatua iliomfanya dereva kupanda juu yake akitafuta usaidizi.

    Watu waliokuwa wakishuhudia tukio hilo walitazama bila usaidizi wowote, huku dereva akiendelea kuomba usaidizi wowote.

    Kwa mujibu wa walioshuhudia dereva huyo alikua amekwama katika eneo hilo tangu mwendo wa saa nne asubuhi.

    Hatahivyo ilichukua juhudi za maafisa wa angani wa shirika la Shedrick Worldlife Trust, waliowasili na ndege yao katika eneo hilo ili kumuokoa.

  10. Mashambulizi makali ya mabomu huku mapigano yakiendelea nchini Sudan

    Moshi unaonekana kwenye mji mkuu wa Sudan, huku Umoja wa Mataifa ukionya majenerali wa nchi hiyo hawako tayari kusitisha mapigano.

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Umoja wa Mataifa umeonya kuwa majenerali wa nchi hiyo hawako tayari kusitisha mapigano.

    Milio ya risasi na milipuko imetanda katika mji mkuu wa Sudan Khartoum kwa siku ya 20 mfululizo.

    Mashahidi waliripoti milipuko mikubwa na kurushiana risasi kwa moto mitaani.

    Mashambulizi makubwa ya mabomu pia yalisikika katika miji inayopakana ya Omdurman na Bahri.

    Jeshi lilisema liko tayari kutii usitishaji vita mpya wa siku saba, lakini hakujakuwa na neno lolote kutoka kwa wanajeshi pinzani, Vikosi vya Msaada wa Dharura (RSF).

    Jeshi linaripotiwa kujaribu kuwarudisha nyuma RSF kutoka eneo linalozunguka ikulu ya rais na makao makuu ya jeshi.

    Mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa, Martin Griffiths, alisema azimio la pande zinazozozana kuendelea kupigana kunahatarisha kugeuza mzozo huo kuwa janga la kimataifa.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Sudan:Mahasimu wa Sudan wakubaliana 'kimsingi' kusitisha mapigano kwa wiki moja
    • Mzozo wa Sudan: Mgogoro wa Sudan unaweza kuisha kwa njia hizi tatu
    • Mapigano Sudan: Hakuna mazungumzo mpaka mashambulio ya mabomu yakome, Hemedti aiambia BBC
  11. Mapigano Sudan: Mwigizaji Asia Abdelmajid auawa katika mapigano Khartoum

    h

    Chanzo cha picha, ALFAITORY FAMILY

    Maelezo ya picha, Asia Abdelmajid alikuwa mmoja wa nyota wa maigizo ya jukwaani nchini Sudan

    Kifo cha mwigizaji maarufu, aliyefariki katika mapigano ya ufyatulianaji risasi kaskazini mwa mji wa Khartoum, kimewashitua wakazi wa mji huo huku wakisikia marafiki na jamaa zao wengi wakiuawa katika mapigano.

    Asia Abdelmajid, ambaye alitimiza umri wa miaka 80 mwaka jana, alikuwa maarufu kwa maigizo yake – ambapo alipata umaarufu zaidi mwaka 1965 kwa mchezo wa maigizo uliojulikana kama Pamseeka.

    Ulichezwa kwenye ukumbi wa maigizo katika mji wa Omdurman kuadhimisha mapinduzi ya kwanza ya Sudan dhidi ya kiongozi wa mapinduzi. Alifahamika kama mwanzilishi wa maigizo ya jukwaani – na mwigizaji wa kwanza aliyefanya maigizo ya jukwaani kama taaluma, baadaye alistaafu na kuwa mwalimu.

    Familia yake ilisema kuwa alizikwa katika kipindi cha saa kadhaa baada ya kupigwa risasi Jumatano asubuhi kwenye uwanja wa shule ya chekechea ambako amekuwa akifanya kazi zaidi hivi karibuni. Ilikuwa ni hatari kumpeleka makaburini.

    Haijajulikana ni nani aliyemuua kwa risasi katika makabiliano yaliyotokea katika kitongoji cha Bahri kilichopo kaskazini.

    Lakini wapiganaji wa kikundi cha jeshi la dharura - Rapid Support Forces (RSF), ambao wameweka ngome zao katika maeneo ya makazi kote mjini humo, wanaendelea kupigana na jeshi, ambalo hufanya mashambulio kutoka angani.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Sudan:Mahasimu wa Sudan wakubaliana 'kimsingi' kusitisha mapigano kwa wiki moja
    • Mzozo wa Sudan: Mgogoro wa Sudan unaweza kuisha kwa njia hizi tatu
    • Mapigano Sudan: Hakuna mazungumzo mpaka mashambulio ya mabomu yakome, Hemedti aiambia BBC
  12. Mwanaume wa Canada ashitakiwa kwa kuuza kemikali inayohusishwa na vifo Uingereza

    g

    Chanzo cha picha, PEEL REGIONAL POLICE

    Maelezo ya picha, Kenneth Law ameshitakiwa kuhusiana na vifo viwili nchini Canada, lakini polisi wanaamini huenda kuna wahanga wengi zaidi

    Polisi nchini Canada imemkamata nakumshitaki mwanamume anayeishi eneo la Toronto ambaye wanadai anahusika na vifo vya kujiua katika nchi za Canada, uingereza na Marekani.

    Kenneth Law, 57, anakabiliwa na mashitaka mawili ya kushauri na kusaidia mauaji ya kujitoa muhanga.

    Polisi ya kanda ya Peel inaamini huenda aliuza kemikali ya sumu mtandaoni, ambapo vifurushi vya sumu hiyo vilikwenda kwa watu katika zaidi ya nchi 40.

    Amekamatwa baada ya uchunguzi wa hivi karibuni wa gazeti la Times kumhusisha na vifo takriban vine nchini Uingereza.

    Polisi ilisema Jumanne kwamba walianza kuchunguza kisa hicho mwezi mmoja uliopita kufuatia kifo cha ghafla cha mwanaume mmoja anayeishi eneo la Toroto.

    Naibu mkuu wa kitengo cha polisi cha masuala ya kijamii katika kanda ya polisi ya Peel, amesema maafisa wanaamini kuwa mtu alimeza kemikali ya sumu ambayo aliuziwa na Bwn Law.

    Polisi ilisema inafahamu kuwa vifurushi 1,200 viliuzwa na Bw Law ambavyo vilisafirishwa kwa meli hadi katika nchi 40, ingawa hawajui ni vingapi vilijumuisha kemikali hiyo.

  13. Mapigano Sudan: Mahasimu wa Sudan hawana utashi wa kumaliza vita – Mkuu wa Umoja wa Mataifa

    f

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Mkuu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths anasema itakuwa vigumu kumaliza vita nchini Sudan

    Mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa itakuwa vigumu kumalizika kwa mapigano nchini Sudan, huku pande zinazohasimiana zikiwa makini "kuendelea".

    Martin Griffiths alikuwa akizungumza na BBC baada ya kutembelea bandari ya Port Sudan kwenye mwambao wa Bahari Nyekundu.

    Alisema kuwa aliwataka majenerali hasimu ambao wanapigania udhibiti wa nchi kukutana naye ana kwa ana kujadili upelekaji wa misaada ya dharura ya kibinadamu.

    Alisema kuwa pande mbili zinazohasimiana zilizungumzia kuhusu kuzingatia kanuni za msaada wa kibinadamu – lakini hawakuonekana kuwa na utashi wa kumaliza vita.

    Makubaliano mapya ya siku saba yanatariwa kuanza – lakini usitishaji mapigano wa awali ulivunjwa.

    Bw Griffiths alisema alisikia hadithi za ukatili wa kutisha ambazo zinaweza kupelekea kile alichokiita tatizo la maridhiano ya kizazi.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Sudan:Mahasimu wa Sudan wakubaliana 'kimsingi' kusitisha mapigano kwa wiki moja
    • Mzozo wa Sudan: Mgogoro wa Sudan unaweza kuisha kwa njia hizi tatu
    • Mapigano Sudan: Hakuna mazungumzo mpaka mashambulio ya mabomu yakome, Hemedti aiambia BBC
  14. Vita vya Ukraine: Zelensky yuko The Hague huku Kyiv ikipigwa na milipuko

    g

    Chanzo cha picha, SOCIA MEDIA

    Milipuko imesikika mjini Kyiv na miji mingine ya Ukraine, siku moja baada ya Urusi kuishutumu Ukraine kufanya shambulio la droni dhidi ya makao makuu ya serikali yake - Kremlin.

    Mashambulio yameripotiwa pia katika miji ya Zaporizhzhia na Odesa kusini mwa Ukraine.

    Mshambulio hayo ya anga yanakuja huku rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akitarajiwa kuzungumza mjini The Hague kama sehemu ya ziara yake ambayo haikutarajiwa nchini Uholanzi.

    Pia ataitembelea Mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC), ambayo inachunguza madai ya uhalifu wa kivita wa Urusi katika Ukraine.

    Urusi imeishutumu Ukraine kwa kujaribu kumuua Rais Vladimir Putin, lakini Bwn Zelensky amekanusha kwamba nchi yake ilifanya shambulio.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  15. Pep Guardiola: Halaand 'anastahili heshima aliyopewa'

    g

    Chanzo cha picha, reuters

    Pep Guardiola amedai lifanyike gwaride la heshima kwa ajili ya wachezaji wake na wafanyakazi wa klabu hiyo kuadhimisha bao la rekodi Erling Haaland la Primia Ligi – kumuonyesha mshambuliaji huyo jinsi mafanikio aliyoyapata yalivyo maalumu.

    Kufunga bao la 3 - 0 dhidi ya West Ham kwa Haaland kunamaanisha kuwa sasa ana mabao 35 ya ligi katika msimu.

    j

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Erling Haalandamefunga mabao 51 katika mechi zote za Manchester City msimu huu

    Amevunja rekodi ambayo awali ilimuweka katika kiwango sawa na Alan Shearer na Andy Cole.

    "Wakati kuna tukio maalumu, tunapaswa kuonyesha ni kwa jinsi gani lilivyo maalumu," amesema Guardiola.

    Wachezaji wenzake wa Manchester city, pamoja na Guardiola na wahudumu wengine wa klabu hiyo waliokuwa katika chumba cha mavazi, walijipanga mstari kumpatia heshima Haaland alipokuwa njiani kuelekea katika chumba cha kubadilisha mavazi.

    Unaweza pia kusoma:

    • Anaendelea kuvunja rekodi- Je Halaand anaweza kuwa mchezaji bora kuwahi kutokea Ulaya?
    • Kwanini Haaland anaweza kuipaisha Manchester City
  16. Ufyatuaji wa risasi Belgrade : Mvulana alitengeneza 'orodha ya kuua' kwa ajili ya shambulio la shule la Serbia

    g
    Maelezo ya picha, Mshukiwa wa ufyatuaji risasi wa Belgrade alipokamatwa na polisi

    Mvulana aliyewauwa wenzake wanane pamoja na mlinzi wa usalama katika shule nchini Serbia alipanga shambulio kwa wiki kadhaa na alikuwa na "orodha ya kuua", kulingana na polisi.

    Mvulana huyo mwenye umri wa miaka 13 alikamatwa kufuatia shambulio hilo lililotokea Jumatano asubuhi katika shule ya msingi ya Vladislav Ribnikar iliyopo katikati mwa mji mkuu Belgrade.

    Watoto wengine wa shule sita na mwalimu walijeruhiwa katika ufyatuaji huo wa risasi.

    Sababu ya shambulio hilo bado inachunguzwa, imesema polisi.

    Maafisa wa polisi waliovalia fulana za kujikinga na risasi walizingira eneo linalozunguka shule, iliyopo katikati ya makazi ya watu ya Vracar, muda mfupi baada ya saa mbili na dakika arobaini (06:40 GMT).

    Mshukiwa anadaiwa kuwa alitumia bunduki za baba yake, ambazo ni halali zikiwa na vibali vya kisheria.

    Inasemekana aliwahi kwenda na baba yake katika mchezo wa kufyatua risasi kwa kulenga shabaha kabla ya kutekeleza mauaji hayo.

    Mama yake mvulana huyo amekamatwa.

  17. Wabunge wa Nigeria waomba Uingereza imuhurumie seneta aliyepatikana na hatia

    h

    Chanzo cha picha, Met Police

    Maelezo ya picha, Seneta Ike Ekweremadu alipatikana na hatia mwezi Machi

    Wabunge nchini Nigeria wamewaomba maafisa wa mahakama nchini Uingereza “kucheza na sheria ili kutoa huruma” kuhusiana na hukumu ya mwanasiasa wa Nigeria aliyepatikana na hatia ya usafirishaji haramu wa viungo vya binadamu.

    Senata Ike Ekweremadu, mke wake pamoja na daktari "ambaye aliwasaidia’’ walipatikana na hatia mwezi Machi kwa njama ya kusafirisha viungo cha mwili, baada ya kumleta mwanaume mwenye umri wa miaka 21 nchini Uingereza kutoka Lagos.

    Hukumu yao inatarajiwa kutolewa Ijumaa.

    Spika wa bunge la wawakilishi nchini Nigeria, Femi Gbajabiamila, alimuelezea Ekweremadu kama "mtu mwema" ambaye hakuwahi kupatikana na hatia awali, huku akiomba ahurumiwe.

    Bunge la Jumuiya ya kiuchumi ya nchi zilizopo magharibi mwa Afrika (Ecowas) pia limeandika barua kwa mamlaka za Uingereza zikitaka msamaha utolewe kwa mwanasiasa huyo aliyepatikana na hatia.

    Vyombo vya habari vya Nigeria viliinukuu barua ya Spika wa Ecowas aliyomuandikia karani mkuu wa mahakama ya uhalifu ya Old Bailey iliyopo mjini London.

    Ilisema kuwa ingawa Ecowas “inapinga ”uhalifu ambao Ekweremadu alipatikana nao, ina “amini kuwa funzo limetolewa”.

    Barua hiyo pia ilimuelezea Ekweremadu kama “mtu muhimu katika kanda ya Ecowas”.

  18. Vita vya Ukraine: Zelensky akanusha kuwa Ukraine ilimshambulia Putin au Moscow

    d

    Chanzo cha picha, Social media

    Maelezo ya picha, Mitandao ya kijamii ya Urusi inaonyesha shambulio la droni la Kremlin

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amekanusha kuwa nchi yake ilifanya shambulio linalodaiwa kuwa ni la ndege isiyokuwa na rubani dhidi ya Kremlin, ambalo Urusi inasema lilikuwa ni jaribio dhidi ya maisha ya Vradimir Putin.

    "Hatumshambulii Putin wala Moscow. Tunapigania kwenye eneo letu. Tunalinda vijiji vyetu na miji yetu," alisema, akizungumza katika ziara nchini Finland.

    Ofisi ya rais wa Urusi ilisema kuwa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vilizidungua ndege mbili zisizo na rubani usiku.

    Ilitishia kulipiza kisasi wakati na mahala itakapona ni muhimu kufanya hivyo.

    Picha za video ambazo hajijathibitishwa zinazozunguka kwenye mtandao zinaonyesha moshi upipaa juu Kremlin - eneo kubwa la makao makuu ya serikali lililopo katikati ya mji wa Moscow – mapema Jumatano.

    Video ya pili inaonyesha mlipuko mdogo juu ya jengo la seneti, huku wanaume wawili wakionekana kupanda kwa shida juu kabisa ya jengo hilo la bunge.

    Ofisi ya rais wa Urusi ilisema Ukraine ilikuwa imejaribu kushambulia makazi ya Bw Putin yaliyopo ndani Kremlin na kuelezea shambulio hilo kama "kitendo cha ugaidi kilichopangwa na jaribio la kumuua rais".

    Maafisa wanasema kuwa droni mbili zilizolenga ofisi hizo za serikali zimezuiwa kwa kutumia rada za umeme, na kuongeza kuwa Rais Putin hakuwa kremlin wakati wa shambulio linalodaiwa.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  19. Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu ya mubashara leo ikiwa ni Alhamisi tarehe 04.05.2023