Karibu watu 130 wafariki kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini Rwanda

Idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini Rwanda imeongezeka hadi kufikia 127, maafisa wanasema.

Moja kwa moja

  1. Na kufikia hapa tunakamilisha matangazo ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Mkuu wa Umoja wa Mataifa atoa wito wa kukomeshwa kwa mapigano nchini Sudan

    Mji mkuu wa Sudan Khartoum umekumbwa na mapigano makali tangu tarehe 15 Aprili

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Mji mkuu wa Sudan Khartoum umekumbwa na mapigano makali tangu tarehe 15 Aprili

    Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa pande zinazozozana nchini Sudan kusitisha mapigano mara moja, kabla ya mzozo huo kuzidi kuwa vita kamili.

    Akizungumza nchini Kenya, Bw Guterres alisema watu nchini Sudan wanakabiliwa na janga la kibinadamu, huku hospitali zikiwa zimeharibiwa, maghala ya chakula na misaada yameporwa huku mamilioni wakikabiliwa na uhaba wa chakula.

    Hapo awali, mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu, Martin Griffiths, ambaye yuko Sudan, alisema anajaribu kupata ahadi kutoka pande zote kuruhusu misaada ya kibinadamu katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

    Pande za Sudan zimekubaliana mapatano mapya ya siku saba kuanzia siku ya Alhamisi, lakini usitishaji mapigano hapo awali umesambaratika.

    Bw Griffiths alisema malori sita ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani yaliporwa yakiwa njiani kuelekea eneo lenye matatizo la Darfur, licha ya kuhakikishiwa kuwa yatakuwa salama.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Sudan:Mahasimu wa Sudan wakubaliana 'kimsingi' kusitisha mapigano kwa wiki moja
    • Mapigano Sudan: Hakuna mazungumzo mpaka mashambulio ya mabomu yakome, Hemedti aiambia BBC
  3. Nyota wa muziki wa Tanzania aibuka tena baada ya kuugua kwa muda mrefu

      • Author, Alfred Lasteck
      • Nafasi, BBC News, Dar es Salaam

    Gwiji wa muziki wa Afrika Mashariki ambaye pia ni mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Joseph Haule, maarufu kwa jina la kisanii Profesa Jay, kwa mara ya kwanza ameandika kwenye mitandao ya kijamii baada ya zaidi ya mwaka mmoja kuhangaika kuhusu mahali alipo na afya yake.

    Rapa huyo wa Tanzania, mtunzi wa nyimbo na mbunge wa zamani alifichua kuwa alikuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa zaidi ya miezi minne.

    Yeye wala familia yake hawajasema alichokuwa akiugua. Profesa Jay anasema alipata matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam na baadaye akasaidiwa na serikali kupata matibabu zaidi nje ya nchi.

    Siku ya Jumanne, alishirikisha ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram kwa mara ya kwanza tangu Januari mwaka jana.

    Ruka Instagram ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa Instagram ujumbe

    Alishukuru kwa ushirikiano alioupata kutoka kwa serikali, chama chake cha Chadema, na wananchi wakati akipigania uhai wake.

    Profesa Jay anajulikana sana kama mmoja wa waanzilishi wa muziki wa kisasa wa Kiswahili wa Tanzania wa Bongo Flava

  4. Binti wa Mugabe ajikuta katika mgogoro wa talaka wa dola milioni 80

    Bona Mugabe alionekana akiwa na mumewe kwenye mazishi ya babake mnamo 2019

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Bona Mugabe akiwa na mumewe kwenye mazishi ya babake mwaka 2019

    Kesi ya talaka kati ya binti ya aliyekuwa Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe na mumewe imetoa taswira ya utajiri wa ajabu uliokusanywa na familia hiyo - ikiwa ni pamoja na nyumba za thamani ya karibu dola milioni 80 (£64m).

    Bona Mugabe, 33, aliwasilisha maombi ya talaka ya kuachana na rubani wa zamani wa shirika la ndege Simba Mutsahuni Chikore mwezi Machi, na kuomba kugawanywa kwa mali kushughulikiwa katika kesi tofauti mahakamani.

    BBC imeona nyaraka za mahakama zilizowasilishwa na Bw Chikore tarehe 28 Aprili kujibu zile za Bi Mugabe.

    Anadai ulezi wa pamoja wa watoto watatu wa wanandoa hao na sehemu ya mali, ambayo ni pamoja na mashamba yasiyopungua 21, ambayo baadhi yalichukuliwa na familia ya Mugabe wakati wa unyakuzi wa mashamba ya wazungu takriban miongo miwili iliyopita, na licha ya serikali kuwa na sera ya "mtu mmoja shamba moja".

    Bw Chikore pia anaorodhesha mali 25 za makazi ikiwa ni pamoja na jumba la kifahari huko Dubai - lenye thamani ya jumla ya karibu dola milioni 80, magari ya kifahari, vifaa vya kilimo na mamia ya maelfu ya dola taslimu.

    Anasema mali hizo walizipata kibinafsi na kwa pamoja wakati wa ndoa yao, kupitia mirathi na michango kutoka kwa marehemu rais kwa kazi iliyofanywa kwa niaba yake.

    Anaongeza kuwa mali ambayo ameorodhesha ni tone la bahari, ikilinganishwa na mali ambayo Bi Mugabe anamiliki moja kwa moja.

    Wazimbabwe wapokea kwa mshtuko na hasira taarifa za kiwango cha utajiri uliokusanywa na mtoto mmoja tu wa Bw Mugabe.

    Akijibu, George Charmba, ambaye alikuwa msemaji wa Bw Mugabe na sasa anahudumu katika ofisi ya Rais Emmerson Mnangagwa, alikanusha kuwa wanandoa hao walikuwa na mashamba 21.

    "Ardhi yote ya Kilimo ni ya Serikali, na wakulima wanaitumia kwa MSINGI WA KUKODISHA," aliandika kwenye ujumbe wa Twitter.

    Aliongeza kuwa hakuna mtu anayepaswa "kujenga siasa au mabishano kuhusu mashamba 21 yanayodaiwa kumilikiwa na Cde Bona na mumewe aliyeachana naye".

    Bona Mugabe akiwa na wazazi wake kwenye sherehe ya kuhitimu chuo kikuu nchini Singapore mwaka 2013

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Bona Mugabe akiwa na wazazi wake kwenye sherehe ya kuhitimu chuo kikuu nchini Singapore mwaka 2013

    Haijulikani ni lini kesi ya talaka - iliyowasilishwa mahakamani katika mji mkuu, Harare - itaisha. Bi Mugabe na Bw Chikore walifunga ndoa katika harusi ya kifahari mwaka 2014 ambayo ilihudhuriwa na wakuu kadhaa wa nchi za Afrika - na ilitangazwa moja kwa moja kwenye televisheni ya taifa.

    Mugabe alifariki mwaka wa 2019 akiwa na umri wa miaka 95, ikiripotiwa kuwa bila kuacha wosia.

    Ameacha mkewe Grace, Bona, watoto wawili wa kiume na mtoto mmoja wa kambo.

    Alikuwa madarakani nchini Zimbabwe tangu wakati wa uhuru mwaka 1980 hadi alipotimuliwa mwaka 2017 na aliyekuwa mpinzani wake, Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa.

  5. Nijel Amos: Mwanariadha wa Botswana apigwa marufuku ya miaka mitatu ya kutumia dawa za kusisimua misuli

    Amos

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mshindi wa medali ya fedha ya Olimpiki ya 2012 katika mbio za mita 800 nchini Botswana, Nijel Amos amepigwa marufuku kujihusisha na riadha kwa miaka mitatu baada ya kukutwa na dawa iliyopigwa marufuku.

    Amos, ambaye medali yake ya fedha mjini London ilikuwa ya kwanza ya Olimpiki kuwahi kushindwa na nchi yake, alisimamishwa na Kitengo cha Uadilifu cha Riadha (AIU) mnamo Julai 2022 baada ya jaribio la nje ya mashindano kugundua dawa iliyopigwa marufuku kwenye sampuli ya mkojo.

    Wakati wa kusimamishwa, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 alikuwa nchini Marekani akijiandaa kwa Mashindano ya Riadha ya Dunia huko Oregon. Marufuku itaisha tarehe 11 Julai 2025.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na AIU, metabolite, GW1516, "iliunganishwa awali na kutathminiwa kwa ajili ya matibabu ya fetma, kisukari na matatizo mengine yanayosababishwa na matatizo ya kimetaboliki lakini sasa haijaidhinishwa kwa matumizi ya binadamu."

    Nijel Amos was Botswana's flag bearer at the 2016 Olympics following his silver medal in the 800m in London in 2012

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Iliongezwa kwenye orodha iliyopigwa marufuku ya Wakala wa Dunia wa Kupambana na Dawa za Kulevya mwaka wa 2009 baada ya matumizi yake haramu kama wakala wa dawa za kusisimua misuli kuibuka.

    Amos, alishinda medali ya dhahabu ya mita 800 kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2014, matokeo yake tangu Juni 4, 2022 yameondolewa.

  6. Cristiano Ronaldo awa mwanaspoti anayelipwa zaidi duniani baada ya kuhama Al Nassr - Forbes

    th

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Cristiano Ronaldo amekuwa mwanaspoti anayelipwa kiasi cha juu zaidi cha fedha duniani kwa mara ya kwanza tangu 2017 baada ya kuhamia Al Nassr ya Saudi Arabia.

    Forbes wanaripoti kuwa mshambuliaji huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 38 alipata $136m (£108.7m) katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.

    Mkataba wake na Al Nassr unaripotiwa kuwa na thamani ya zaidi ya euro 200m (£176.5m) kwa mwaka.

    Nahodha wa Argentina aliyeshinda Kombe la Dunia Lionel Messi ni wa pili kwenye orodha ya Forbes akiwa amejishindia $130m (£103.9m).

    10 bora ya Forbes pia ina nyota wa mpira wa vikapu LeBron James na bondia Canelo Alvarez, huku bingwa mara 20 wa tenisi wa Grand Slam Roger Federer ndiye mwanaspoti pekee aliyestaafu katika orodha hiyo katika nafasi ya tisa.

    Dustin Johnson (wa sita) na Phil Mickelson (wa saba) ndio wachezaji wa gofu wa kwanza kuingia 10 bora tangu Tiger Woods mnamo 2020.

    Johnson hakuwa katika 50 bora mwaka wa 2022 lakini baada ya kuwa mchezaji wa kwanza wa hadhi ya juu kujiunga na Mfululizo wa Mwaliko wa Gofu wa LIV unaofadhiliwa na Saudia, amepanda katika orodha ya Forbes.

    Pia unaweza kusoma:

    • Kwanini kuishi pamoja kwa Ronaldo na mpenzi wake nchini Saudi Arabia kumezua gumzo?
    • Cristiano Ronaldo: Kwa mara ya kwanza anaongoza kwa mastaa wanaoingiza pesa kupitia Instagram
  7. Polisi wapekua nyumba ya Rais wa zamani wa Brazil Jair Bolsonaro

    Bolsonaro

    Chanzo cha picha, EP

    Polisi wamepekua nyumba ya Rais wa zamani Jair Bolsonaro katika mji mkuu wa Brazil, Brasilia.

    Upekuzi huo ni sehemu ya uchunguzi dhidi ya kundi linaloshukiwa kuhujumu hifadhidata ya serikali iliyo na habari kuhusu chanjo ya Covid-19.

    Polisi walisema hifadhidata hiyo imebadilishwa ili kubadilisha hali ya chanjo ya watu kadhaa ambao hawakutajwa.

    Msaidizi wa karibu wa Bw Bolsonaro, Mauro Cid, amekamatwa kama sehemu ya uchunguzi huo.

    Polisi wa walisema "data ya uwongo" ilikuwa imeingizwa kwenye rekodi za chanjo ya Covid-19 zinazoshikiliwa na Wizara ya Afya ya Brazil.

    Kulingana na polisi, hii ilifanyika ili watu ambao hali yao ya chanjo ilikuwa imebadilishwa waweze kupata vyeti vya chanjo muhimu kuingia Marekani wakati huo.

    Bwana Bolsonaro ni mpinzani mkubwa wa chanjo ya Covid, ambaye alieneza habari za uwongo mara kwa mara juu ya chanjo hiyo na athari zake zinazodaiwa.

    Katika matangazo yamoja kwa moja kwenye mtandao wa kijamii mnamo 2021, alidai kimakosa kwamba chanjo za Covid-19 ziliongeza nafasi ya kupata Ukimwi. Mnamo Oktoba 2021, alisema hatapata chanjo dhidi ya Covid.

  8. Mazungumzo ya kihistoria ya amani na OLA nchini Ethiopia yamalizika bila makubaliano

    TH

    Chanzo cha picha, Facebook/Qe'ee Oromoo

    Duru ya kihistoria ya mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Ethiopia na waasi wa Oromo Liberation Army (OLA) yamemalizika bila makubaliano ya kumaliza mzozo katika eneo kubwa la Oromia.

    Mpatanishi wa serikali Redwan Hussein alisema kupitia Twitter kwamba mazungumzo yamekuwa "ya kujenga kwa kiasi kikubwa", lakini "kwa bahati mbaya haikuwezekana kufikia makubaliano kuhusu baadhi ya masuala wakati wa duru hii ya mazungumzo".

    Maelewano yamefikiwa katika baadhi ya maeneo, lakini sio juu ya tofauti kuu za kisiasa, Bw Redwan alisema.

    Pia alikiri haja ya mazungumzo ili kuendelea kutatua mzozo huo kwa njia ya kudumu na kwa amani.

    Pande hizo mbili zilikutana nchini Tanzania katika hatua ya kwanza kuu ya kumaliza uasi wa Oromia.

    OLA inasema inapigania "kujitawala" kwa Oromia na imefanya msururu wa uvamizi dhidi ya vikosi vya serikali katika eneo hilo.

    Mazungumzo hayo yalikuja takriban miezi sita baada ya serikali ya Ethiopia kufikia makubaliano ya amani ya kumaliza vita vya miaka miwili katika eneo la kaskazini la Tigray.

    OLA ilikuwa imeungana na vikosi vya Tigraya katika jitihada ambazo hazikufanikiwa za kupindua serikali.

  9. Mvulana, 14, akamatwa baada ya watu tisa kuuawa kwa kupigwa risasi shuleni nchini Serbia

    Serbia

    Chanzo cha picha, EPA

    Wanafunzi wanane na mlinzi mmoja wameuawa baada ya kupigwa risasi katika shule moja katika mji mkuu wa Serbia Belgrade.

    Wanafunzi wengine sita na mwalimu mmoja walijeruhiwa katika shambulio hilo na wamepelekwa hospitalini, wizara ya mambo ya ndani ilisema katika taarifa.

    Polisi watayari wamekamata mwanafunzi mwenye umri wa miaka 14 katika shule ya Vladislav Ribnikar katikati mwa Belgrade kuhusiana na shambulio hilo la Jumatano asubuhi.

    Mshukiwa anadaiwa kutumia bunduki ya babake, maafisa walisema. Uchunguzi wa chanzo cha tukio hilo unaendelea.

    Maafisa waliovalia helmeti na fulana za kuzuia risasi walizingira eneo la karibu na shule hiyo, iliyoko kitongoji cha Vracar ya kati, muda mfupi baada ya 08:40 saa za nyumbani (06:40 GMT).

    Huku hayo yakijiri walimu, wanafunzi na wazazi wamekuwa wakifarijiana nje ya shule ya msingi katikati mwa Belgrade ambapo mkasa huo ulitokea. Hizi ni baadhi ya picha za hivi punde kutoka eneo la tukio:

    p

    Chanzo cha picha, Reuters

    p

    Chanzo cha picha, Getty Images

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

  10. Polisi nchini Zambia waizingira nyumba ya rais wa zamani mjini Lusaka

    Lungu

    Chanzo cha picha, getty

    Polisi wa Zambia wameizingira nyumba ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Edgar Lungu katika mji mkuu, Lusaka, na kutaka kuipekua.

    Wakili wa Bw Lungu, Jonas Zimba ameambia Diamond TV kwamba maafisa wa polisi wanafanya msako unaodaiwa kuhusishwa na umiliki wa magari matatu na hati miliki.

    Alisema msako huo unafuatia malalamiko dhidi ya aliyekuwa mke wa rais, Esther Lungu, juu ya umiliki wake unaotiliwa shaka wa magari hayo matatu.

    Polisi bado hawajatoa tamko kuhusiana na tukio hilo. Chama tawala cha zamani, Patriotic Front (PF), kimeelezea hatua hiyo kama ukiukaji wa kinga ya Bw Lungu kama inavyothibitishwa na sheria.

    Bw Lungu aliondolewa mamlakani na Hakainde Hichilema katika uchaguzi wa Agosti 2021.

  11. Tazama: Mwanaume akamatwa nje ya kasri ya Ufalme wa Uingereza Buckingham Palace

    Mwanaume amekamatwa nje ya Buckingham Palace baada ya kushukiwa kutupa kibweta cha bunduki ndogo katika uwanja wa kasri, wamesema polisi imesema.

    Eneo hilo lilifungwa mara moja kwa uzio na udhibiti wa kilipuzi hicho ukafanyika kufuatia tukio hilo, ambalo lilitokea saa moja jioni Jumanne kwa saa za Uingereza.

    Mwanaume huyo alikamatwa akishukiwa kumiliki silaha ya inayoua. Hakuna taarifa kuhusu majeruhi.

    Tukio hilo kwa sasa halihusishwi na ugaidi.

    Tazama mwanaume akikamatwa katika lango la Buckingham Palace

    Maelezo ya video, Tazama mwanaume akikamatwa katika lango la Buckingham Palace
  12. Seneta wa Minnesota anaonekana nusu uchi akipiga kura kupitia Zoom

    Maelezo ya video, Seneta wa Minnesota anaonekana bila shati wakati akipiga kura kupitia Zoom

    Mbunge wa Minnesota alionekana akiwa hana nguo wakati akipiga kura yake kupitia Zoom wakati wa mkutano wa bunge.

    Seneta wa chama cha Republican Calvin Bahr alionekana kuwa kitandani na nyuma yake kulikuwa na picha ukutani kutoka filamu ya katuni za Watoto ya "I'm Just a Bill.

  13. Karibu watu 130 wafariki kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini Rwanda

      • Author, Yves Bucyana
      • Nafasi, BBC Swahili
    h

    Chanzo cha picha, Rwanda Broadcasting Agency

    Maelezo ya picha, Mvua kubwa inatarajiwa kuendelea kunyesha katika mwezi wa Mei

    Idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini Rwanda imeongezeka hadi kufikia 127, maafisa wanasema.

    "Kipaumbele chetu kikuu sasa ni kufikia kila nyumba ambayo imeharibiwa ili kuhakikisha tunaweza kuokoa mtu yeyote ambaye anaweza kukwama," anasema François Habitegeko, Gavana wa Mkoa wa Magharibi wa Rwanda.

    Mafuriko na maporomoko ya ardhi pia yameripotiwa katika nchi jirani ya Uganda, ambapo watu sita wamefariki, kwa mujibu wa Chama cha Msalaba Mwekundu.

    Shirika la utabiri wa hali ya hewa la Rwanda limeonya juu ya mvua kubwa kunyesha mwezi Mei.

    Gavana François Habitekego alisema: "Tulikabiliwa na matatizo makubwa sana". Anasema kuwa hadi sasa takwimu za muda walizonazo ni kwamba watu 55 walikufa kwa sababu "nyumba nyingi na majengo yaliangukia watu".

    Habitekego anasema kuwa watu wengi walifariki katika wilaya ya Ngororero lakini “wapo pia waliopoteza maisha katika maeneo ya Rubavu, Rutsiro na Karongi”.

    Jimbo la Magharibi - na kaskazini mwa Rwanda - ni maeneo yenye milima ambayo mara nyingi huathiriwa na maporomoko ya ardhi wakati wa misimu ya mvua.

    g

    Chanzo cha picha, RBA

    Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Rwanda hivi majuzi ilionya kuwa kutakuwa na mvua kubwa mwezi huu wa Mei.

    Nayo Wizara ya Maafa iliwatahadharisha wananchi kuwa waangalifu mnamo wakati huu. Mvua kubwa ilinyesha katika maeneo tofauti nchini Rwanda jana usiku, idadi ya uharibifu na vifo inatarajiwa kuongezeka.

    Gavana Habitekego aliambia BBC kwamba "Barabara nyingi zimeharibika kwa kukatika na kufunikwa na matope hivyo sasa ni vigumu kutembea".

    Barabara kuu katika jimbo la magharibi ya Kivu Belt inayounganisha miji ya Rubavu – Karongi, Muhanga – Musanze na barabara ya Musanze – Rubavu zimeharibika.

    Alisema: "Sehemu nyingine zimefunikwa na matope, siwezi kusema kuwa barabara zote hizo zinaweza kutumika ."

    Hata hivyo, anasema, shughuli za usaidizi katika ngazi ya mitaa zinafanywa na kwamba "msaada wa ngazi ya kitaifa uko njiani"

    th
  14. Vita vya Ukraine: Urusi kupunguza matukio ya sherehe za Siku ya Ushindi

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mwaka jana, Rais Vladimir Putin aliongoza Siku ya Ushindi akiwa ameshikilia picha ya baba yake akiwa amevaa magwanda ya jeshi.

    Miji kadhaa ya Urusi imetangaza kuwa itapunguza sherehe za mwaka huu za siku ya Ushindi.

    Maafisa wa urusi wameelezea sababu za kiusalama na mashambulio kutoka kwa vikosi vinavyounga mkono Waukraine kama sababu ya mabadiliko hayo.

    Milipuko na moto vimetokea nchini Urusi katika wiki za hivi karibuni.

    Lakini baadhi wamedai kuwa kupunguzwa kwa matukio hayo inaonyesha kuwa Urusi inahofia sherehe hizo zitabadilika na kuwa maonyesho ya maoni tofauti dhidi ya uvamizi wake wa Ukraine.

    Sherehe hizo ambazo hutawaliwa na maonyesho ya kuvutia ya kijeshi kwa kawaida huadhimisha Siku ya Ushindi, ambayo ni kumbukumbu ya ushindi wa Muungano wa Usovieti dhidi ya Wanazi wa Ujerumani wa tarehe 9 Mei 1945.

    Mojawapo ya matukio yanayotambulika zaidi ni lile la maandamano ya Kikosi Kisichoweza Kufa, ambapo watu kote nchini huandamana huku wakiwa wameshika picha za ndugu na jamaa zao waliopigana Vita kuu ya pili ya dunia.

    Mwaka jana, Rais Vladimir Putin aliongoza maandamano kote katika eneo la Red Square mjini Moscow huku akiwa ameshikilia picha ya baba yake akiwa amevaa magwanda ya jeshi.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  15. Mapigano Sudan: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa awasili Kenya kutathmini mzozo wa Sudan

    g

    Chanzo cha picha, Kenyan foreign ministry

    Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewasili nchini Kenya kufuatilia hali ya kibinadamu na kuisalama nchini Sudan kufuatia wiki za makabiliano.

    Bw Guterres amepokelewa na Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Alfred Mutua katika uwanja wa ndege, Nairobi.

    Katika ziara yake ya siku mbili, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa atafanya mazungumzo na Rais William Ruto na kukutana na wakuu wote wa mashirika ya Umoja wa Mataifa mjini Nairobi.

    Makundi ya kijeshi yanayopigana nchini Sudan yamekubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa siku saba kuanzia Alhamisi.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Sudan:Mahasimu wa Sudan wakubaliana 'kimsingi' kusitisha mapigano kwa wiki moja
    • Mapigano Sudan: Hakuna mazungumzo mpaka mashambulio ya mabomu yakome, Hemedti aiambia BBC
  16. Nigeria yaanza uchunguzi kuhusu chapa maarufu ya chakula cha tambi

    g

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Mtengenezaji wa Indomie wa Indonesia ametetea usalama wa bidhaa zake

    Shirika la udhibiti wa viwango nchini Nigeria (Nafdac) linasema inachukua “hatua ya haraka” kuichunguza chapa maarufu ya noodles kuhusiana na na madai kwamba ina kiungo kinachohusiana na kuongezeka kwa hatari ya mtu kupata saratani.

    Shirika hilo limesema kwenye taarifa yake kwamba linafanya “uchunguzi wa sampuli na tathmini ya tambi za Indomie, ikiwa ni pamoja na viungo, ili kuangalia uwepo wa ethylene oxide".

    lilisema kuwa linapanua uchunguzi huo zaidi hadi kwa chapa nyingine za tambi zinazouzwa katika soko la Nigeria.

    Nafdac linasema kuwa uchunguzi huo unafuatia kuondolewa kwa Tambi ‘’maalum zenye ladha ya kuku’’ wiki iliyopita kwenye masoko ya Malaysia na Taiwan baada ya kiungo cha ethylene oxide kugundulika katika baadhi ya sampuli.

    Indofoods, ambayo ni kampuni kubwa ya chakula ya Indonesian inayotengeneza tambi za Indomie, hatahivyo imetetea usalama wa bidhaa zake.

    Shirika la viwango nchini Nigeria lilisema kuwa chapa zilizohusishwa hazikusajiliwa katika mauzo salama nchini Nigeria, ikisema kuwa maafisa wa bandari walikuwa wamefahamishwa kutoruhusu uangizwaji wa bidhaa hizo.

    "Tunauhakikishia umma kwamba katika kipindi chote cha uchunguzi wa bidhaa utakua ukifanyika kwenye viwango vya kiwanga na soko na matokeo yake yatatangazwa," ilisema.

  17. Muungano wa Ulaya wapanga kuongeza uzalishaji wa makombora ya mizinga hadi milioni moja kwa mwaka

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Muungano wa Ulaya unaazimia kutenga zaidi ya euro milioni 500 kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa makombora ya mizingaili kuisaidia Ukraine na kujaza hifadhi yake.

    Mpango wa kamati ya Muungano wa Ulaya, ambao utatangazwa kwa umma Jumatano ijayo unatoa ruzuku kwa makampuni ya silaha ya Ulaya, ambayo yataweza kuwekeza katika sekta ya makombora howitzer na ndege roketi, pamoja na uzalishaji silaha za kemikali na kuzibadilisha silaha za zamani kuwa za kisasa.

    "Inapokuja katika suala la ulinzi, sekta yetu lazima ibadilike na kuwa ya utawala wa uchumi wa vita," alisema Kamishna wa Ulaya anayehusika na soko la ndani, Thierry Breton.

    Iwapo mpango mpya utaidhinishwa nanchi zote wanachama wa Muungano wa Ulaya na Bunge la Ulaya, utakuwa ni sehemu ya juhudi kubwa za EU za kuipatia Ukraine silaha, hususan makombora ya mizinga ya 155mm ambayo Kyiv inayahitaji zaidi.

    Kamishna wa Muungano wa Ulaya alikiri kuwa, licha ya uwepo wa ukubwa wa sekta ya viwanda vya silaha barani humo, Muungano wa Ulaya "leo hauna kiwango cha silaha kinachoweza kukidhi mahitaji ya usalama wa Ukraine na nchi wanachama."

    "Lakini ni fursa ya kufanya hivyo," alisema Breton. "Na tunaweza na lazima tuidhinishe mpango huu ili kukidhi mahitaji ya mzozo mkubwa."

    Unaweza pia kusoma:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  18. Lionel Messi aadhibiwa na Paris St-Germain kwa wiki mbili kuhusiana na safari ya Saudi Arabia

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Lionel Messi alishinda Kombe la Dunia na Argentina mwezi Disemba

    Nahodha wa Argentina Lionel Messi amesimamishwa kucheza katika kablu yake ya Paris St-Germain kwa wiki mbili baada ya kusafiri kwenda nchi ya Saudia Arabia bila ruhusa ya klabu hiyo wiki hii.

    Safari yake ilifuatia kushindwa kwa klabu hiyo ya Ufaransa nyumbani na Lorient siku ya Jumapili, ambapo Messi alicheza kipindi chote cha dakika 90 za mechi.

    Messi hatafanya mazoezi wala kuichezea PSG katika kipindi cha kusimamishwa kwake.

    Inafahamika kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 - aliomba ruhusa kufanya ya kusafiri ili kufanya kazi za kibiashara lakini alikataliwa.

    Messi, ambaye pia alipigwa faini na klabu, ana kazi kama balozi wa utalii wa Saudi Arabia.

    Mkataba wa mshindi huyo wa Kombe la Dunia na PSG unaisha msimu huu.

    Makamu wa rais wa Barcelona Rafael Yuste alidai mwezi Machi kuwa klabu ya Uhispania inawasiliana na Messi kuhusu kurejea kwake katika Nou Camp.

    Messi alifunga mabao 31 na kuchangia ushindi wa mabao 34 katika mechi 71 za mashindano yote ya PSG, na alishinda taji la Ligi 1 msimu uliopita.

  19. Mwili wa mvuvi wa Australia aliyepotea wapatikana ndani ya mamba

    .

    Chanzo cha picha, getty images

    Mwili wa mwanamume mmoja raia wa Australia aliyetoweka wakati akivua samaki na marafiki zake umepatikana ndani ya mamba.

    Kevin Darmody alionekana mara ya mwisho Kennedy's Bend - makazi maarufu ya mamba wa maji ya chumvi katika sehemu ya mbali ya kaskazini mwa Queensland - Jumamosi.

    Baada ya msako wa siku mbili katika eneo hilo, polisi waliwaua mamba wawili wakubwa na kupata mabaki ya binadamu.

    Mwili wake bado haujatambuliwa rasmi, lakini polisi wanasema ni "mwisho wa kusikitisha" wa kumsaka mtu huyo mwenye umri wa miaka 65.

    Bwana Darmody alikuwa mvuvi mwenye uzoefu na mwanachama mashuhuri wa jumuiya huko Cape York.

    Mamba hao wawili, ambao walikuwa na urefu wa mita 4.1 (futi 13.4) na urefu wa mita 2.8, walipigwa risasi na kufa siku ya Jumatatu takriban kilomita 1.5 (maili 0.9) kutoka mahali alipoonekana mara ya mwisho.

    Mabaki ya binadamu yalipatikana ndani ya mnyama mmoja tu, lakini maafisa wa wanyamapori wanaamini wote walihusika katika tukio hilo.

    Wavuvi waliokuwa na Bw Darmody wakati huo hawakuona shambulio hilo, lakini waliripoti kumsikia akipiga kelele, na kufuatiwa na sauti kubwa.

    "Nilikimbia chini... lakini hakukuwa na dalili yoyote, ila kamba zake na si kitu kingine," rafiki yake John Peiti aliliambia gazeti la Cape York Weekly.

    Mamba ni wengi katika eneo la kaskazini mwa tropiki ya Australia, lakini mashambulizi kama hayo ni nadra. Kifo cha Bw Darmody ni shambulio la 13 huko Queensland tangu uwekaji rekodi uanze mwaka 1985.

  20. Kambi ya muda huko Koufroune, Chad yawapokea wakimbizi 8,000 wa Sudan

    h

    Chanzo cha picha, AYO BELLO/BBC

    Maelezo ya picha, Kambi ya muda katika Koufroune, Chad, sasa ina wakimbizi wa Sudan 8,000

    Nyuso zenye uchovu za watu ambao wamevuka mpaka wa Sudan na kuingia Chad zinadhihirisha masaibu waliyoyapitia.

    Haya sio tu matokeo ya mapigano ambayo yaliibuka tarehe 15 Aprili kati ya majenerali wawili wakuu bali pia miongo miwili ya mzozo katika jimbo la Darfur.

    Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi (UNHCR) linakadiria kuwa zaidi ya watu 100,000 waliotoroka katika ghasia za hivi karibuni – wengi wao wamekwenda Chad.

    Darfur imekuwa katika mtikisiko wa kiusalama kwa miaka kati ya Waafrika mbali mbali na jamii za Waarabu.

    Wakati jamii sizizo za Waarabu zilipoanza vita dhidi ya serikali mwaka 2003, zikilalamika kuhusu ubaguzi, serikali ilijibu kwa kuwakusanya wanamgambo wa Kiarabu ambao walishutumiwa kueneza ukatili.

    Sasa wanamgambo wa Kiarabu – wanaohusishwa na Rapid Support Forces (RSF), kikundi cha wanajeshi ambao wanapigana dhidi ya serikali – wanaonekana kutumia fursa ya ukosefu wa usalama. Wamekuwa wakishutumiwa kufanya ghasia ambazo zimewafanya watu waikimbie Darfur.

    Baadhi wameishia katika kambi za muda katika kijiji cha Chad cha Koufroune. Inakadiriwa kuwa 8,000 wako katika kambi hiyo.

    Unaweza pia kusoma:

    • Mzozo wa Sudan:Mahasimu wa Sudan wakubaliana 'kimsingi' kusitisha mapigano kwa wiki moja
    • Mapigano Sudan: Hakuna mazungumzo mpaka mashambulio ya mabomu yakome, Hemedti aiambia BBC