Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Milipuko yatikisa bandari ya Ukraine saa kadhaa baada ya makubaliano ya mauzo ya nafaka

Milipuko sita ilipiga Odesa Jumamosi asubuhi, huku maafisa wa eneo hilo wakilaumu Urusi.

Moja kwa moja

  1. Kufikia hapo tunakamalisha matangazo haya ya moja kwa moja. Kwaheri.

  2. Wizara ya Ulinzi ya Uturuki: Urusi imesema haikuhusika na shambulio la Odessa

    Waziri wa Ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar anasema maafisa wa Urusi wameambia Ankara kwamba Moscow "haina uhusiano wowote" na mashambulizi ya makombora dhidi ya bandari ya Odessa.

    "Wakati wa mawasiliano yetu na Urusi, walituambia kwamba hawakuwa na uhusiano wowote na shambulio hili, na kwamba wanachunguza suala hili kwa uangalifu na kwa undani," Akar aliwaambia waandishi wa habari.

    Uturuki ina wasiwasi kwamba milipuko hiyo ilitokea mara tu baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya mauzo ya nafaka, ambayo Urusi na Ukraine zilihitimisha siku ya Ijumaa huko Istanbul, afisa huyo aliongeza.

    Makubaliano hayo yalitiwa saini mbele ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres.

    Jumamosi asubuhi, milipuko ilisikika katika bandari ya Odessa, huku Ukraine ikishutumu Urusi kwa kutekeleza mashambulizi hayo ya roketi.

    Kulingana na Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine, makombora manne yalielekezwa kwenye bandari, mawili kati ya makombora hayo yalidhibitiwa na ulinzi wa anga, mbili ziligonga miundombinu ya bandari, lakini uhifadhi wa nafaka haukuharibiwa.

  3. Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa alaani shambulio dhidi ya bandari ya Odessa

    Kitengo cha habari chaKatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kimetoa taarifa kwa niaba yake.

    Kinasema: "Katibu Mkuu analaani bila kusita shambulio lililoripotiwa dhidi ya bandari ya Odessa nchini Ukraine mapema leo.

    Hapo jana, pande zote ziliahidi kuhakikisha usafirishaji salama wa nafaka kutoka Ukraine na bidhaa zinazohusiana na masoko ya kimataifa.

    Bidhaa hizi ni muhimuna itasaidia kuondoa shida ya chakula duniani na kupunguza mateso kwa mamilioni ya watu wanaohitaji bidhaa hizo kote duniani.

    Utekelezaji kamili [wa masharti ya makubaliano] kati ya Urusi, Ukraine na Uturuki ni lazima."

  4. Zelensky: Urusi itatafuta njia za kutotimiza ahadi

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametoa tamko lake kuhusu shambulio la kombora la Jumamosi dhidi ya bandari ya Odessa.

    Bw Zelensky alisisitiza kuwa shambulio hilo lilitokea chini ya siku moja baada ya makubaliano ya Istanbul juu ya mauzo ya nafaka Kiukreni.

    "Hii inaonyesha jambo moja tu: haijalishi Urusi inasema nini na kuahidi nini, itapata njia za kutotimiza. Kijiografia, na silaha, umwagaji damu au la, ina vekta kadhaa, jinsi inavyofanya kila wakati," Zelensky alisema katika Kyiv. katika mkutano na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi la Marekani.

    Rais wa Ukraine pia aliishukuru Marekani kwa kifurushi cha usaidizi wa usalama kilichotangazwa hivi majuzi na kusisitiza kuwa nchi hiyo hasa inahitaji virushaji vya HIMARS, makombora na ndege zisizo na rubani.

    Zelensky aliufahamisha ujumbe wa Baraza la Wawakilishi juu ya kazi ya ujenzi mpya wa Ukraine baada ya vita, hatua ya kwanza ambayo ni utekelezaji wa Mpango wa Uokoaji Haraka - mpango wa kukarabati haraka makazi yaliyoharibiwa, miundombinu kielimu na matibabu.

    "Tunawaomba washirika wetu, ikiwa ni pamoja na Marekani, kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huu kabambe." huduma ya vyombo vya habari ya rais ilimnukuu rais akisema.

  5. Roman Abramovich aonekana kwenye hafla ya kutia saini mkataba wa mauzo nafaka nchini Uturuki

    Bilionea wa Urusi Roman Abramovich alikuwa miongoni watu waliokuwepo katika Ikulu ya Dolmabahce mjini Istanbul siku ya Ijumaa katika hafla ya kutia saini makubaliano ya mauzo ya nafaka kutoka Ukraine.

    Kulingana na taarifa katika gazeli la Kituruki la Haberler na Reuters, Abramovich alifufuatilia tukio hilo kutoka kwa watazamaji.

    Hii sio ushiriki wa kwanza wa bilionea huyo kushiriki katika mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine.

    Wakati msimu wa masika, Abramovich pia alikuja Uturuki wakati wa ziara za wajumbe kutoka pande zote mbili za mzozo wa kijeshi.

    Gazeti la Times mwezi uliopita liliripoti, Abramovich alituma nyaraka kwa Umoja wa Ulaya akijaribu kuthibitisha kwamba vikwazo alivyowekewa na Brussels ni vya kibaguzi, havina uwiano na kwamba vinatokana na tuhuma za uongo za kuwa karibu na Putin.

  6. Bosi mwanzilishi wa WWE Vince McMahon astaafu kutokana na madai ya dhuluma za kingono

    Mkuu wa kampuni ya mieleka (WWE) Vince McMahon, ambaye aligeuza kampuni hiyo kutoka katika ngazi ya kanda na kuwa gwiji la kimataifa, anasema atastaafu kutokana na madai mengi ya utovu wa nidhamu.

    Alijiondoa katika majukumu yake WWE mwezi uliopita kufuatia ripoti kuwa alilipa mamilioni pesa ili kufutilia mbali madai ya dhuluma za kingono na usaliti.

    Bwana McMahon anasalia kuwa mwanahisa mkuu wa WWE.

    Ameongoza WWE kwa miongo kadhaa, mara nyingi akionekana kama mmoja wa wapiganaji kwenye ulingo wa mchezo wa mieleka.

    Katika taarifa ambayo haikutaja madai dhidi yake, Bw McMahon alisema "anathamini zaidi na anavutiwa na mashabiki wa kizazi hiki kote ulimwenguni".

    "Mashabiki wetu kote ulimwenguni wawe na Imani kuwa WWE itaendelea kuwa burudisha kwa ari, bidii, na shauku kama kawaida," mzee huyo wa miaka 77 alisisitiza.

    Binti yake Stephanie atahudumu kama mwenyekiti wa muda na ataendelea kuwa Mkurugenzi Mtendaji mwenza.

    Mnamo mwezi Juni, gazeti la The Wall Street Journal liliripoti kwamba Bw McMahon alikubali kulipa dola milioni 3 sawa na (£2.5 milioni) kwa mwanasheria wa zamani ambaye alisema alimnyanyasa kingono kazini.

    Licha ya ripoti za awali kwamba angesalia katika wadhifa wa Mkurugenzi Mtendaji na mwenyekiti wa kampuni hiyo, bodi ya WWE ilitangaza uchunguzi dhidi yake baada ya kubainika kuwa alilipa zaidi ya dola milioni 12 (pauni milioni 10) kwa wanawake wengine wanne ili kuficha madai mengi ya uzinzi na usaliti.

    Wanawake hao – wote waliokuwa wafanyakazi wa WWE - walitia saini mkataba na Bw McMahon ambao uliwazuia kujadili mahusiano yao naye baada tu ya kupokea malipo.

    Bw McMahon alianzisha WWE katika miaka ya 1980 na amesimamia ukuaji wake katika ulimwengu wa vyombo vya habari ambapo maudhui ya kila wiki yanatangazwa katika zaidi ya nchi 180 na lugha kwa 30.

    Aliponunua Shirikisho la Mieleka Ulimwenguni wakati huo kutoka kwa baba yake mnamo 1982, mechi zilifanyika katika kumbi ndogo na matangazo yake ya nadra ya runinga yalifanywa kwa njia za kebo za Amerika.

    Lakini shirika hilo lilipata mabadiliko makubwa chini ya usimamizi wake, na mashindano kama vile WrestleMania, shindano la moja kwa moja lililowashirikisha nyota wakuu wa mchezo huo wa mieleka, linalo wavutia mamilioni ya watazamaji.

    Mnamo 2021 mapato ya kampuni yalizidi dola za kimarekani bilioni Moja (£833 milioni) kwa mara ya kwanza.

    Mchezo ulipo zidi kukuwa ulimwenguni, Bw McMahon alitumia utu wake wa kufoka na kuwa mmoja wa watu wanaotambulika zaidi.

    Na miongoni mwa matukio yake maarufu, ikiwa ni pamoja na kushambuliwa na Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump katika tukio la WrestleMania mwaka wa 2007, na ugomvi wake na nyota kama 'Stone Cold' Steve Austin na Hulk Hogan ukawa ndio kivutio zaidi.

  7. Vita vya Ukraine: Viongozi wa Afrika wakaribisha mkataba wa mauzo ya nafaka

    Viongozi wa Afrika Kusini na Ivory Coast wamekaribisha mkataba uliotiwa saini na Ukraine na Urusi kuruhusu usafirishaji wa nafaka kutoka bandari za Ukraine.

    Ni makubaliano makubwa ya kwanza yanayohusisha serikali za Moscow na Kyiv tangu mzozo huo kuanza mwezi Februari - na unalenga kupunguza bei ya juu ya nafaka, na kurejesha usambazaji kwa nchi zinazokabiliwa na uhaba wa chakula kwa sasa.

    Akizungumza mjini Pretoria katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na mwenzake wa Ivory Coast, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alisema kuzuiwa kwa nafaka kumewalazimu viongozi wa Afrika kufikiria kwa uzito kuhusu usambazaji wa chakula katika siku zijazo.

    "Kuendelea kutegemea kiasi kikubwa cha nafaka kutoka sehemu hiyo ya dunia, kunapaswa kuonekana kama hatari ya kweli kwa watu bilioni 1.3 wa nchi za Afrika"

    Rais Alassane Ouattara, ambaye yuko katika ziara ya kiserikali nchini Afrika Kusini, alisisitiza kuwa Afrika lazima iwe juu ya orodha ya wanaopokea nafaka.

    Kiongozi huyo wa Ivory Coast amesema amefurahishwa kuona kuwa Rais wa Urusi Vladimir Putin ameamua kutia saini pendekezo hilo chini ya uangalizi wa Umoja wa Mataifa na Uturuki.

    "Pia nilimuomba Rais wa [Ukraine] Volodymyr Zelensky kupatia kipaumbele bara la Afrika, kwa sababu ya kudorora kwa uchumi wake na hali ya kijamii katika nchi nyingi," alisema.

    Maelezo zaidi:

  8. Mzozo wa Ukraine: Urusi yaongeza orodha ya "nchi zisizo rafiki"

    Serikali ya Urusi imeongeza orodha ya "nchi zisizo rafiki" na kujumuisha Ugiriki, Denmark, Slovenia, Croatia na Slovakia.

    Serikali "imepanua" orodha ya mataifa ya kigeni yanayochukua "hatua zisizo za kirafiki" dhidi ya balozi za Urusi nje ya nchi, Waziri Mkuu Mikhail Mishustin alisema katika amri.

    Kwa jumla, Urusi ina orodha mbili kama hizo.

    Nchi hizo zimejumuishwa katika orodha ya kwanza iliyokuwa na Marekani na Jamhuri ya Czech pekee.

    Orodha ya pili ina mataifa 48.

    Hata kabla ya vita, mamlaka nchinUrusi ilianza kuchukulia hatu "nchi zisizo na urafiki" ikisema kwamba "zifanya vitendo visivyo vya kirafiki" dhidi ya yake.

    Mnamo Aprili 23, 2021, Rais wa Urusi alitia saini amri inayozuia haki ya nchi kama hizo kuajiri raia wa Urusi katika balozi zao mjini Moscow.

    Mapema mwezi Machi mwaka huu, baada ya kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, serikali ya Urusi iliidhinisha orodha nyingine ya nchi na wilaya "zisizo za kirafiki".

    Kisha orodha ya nchi 48 iliidhinishwa ilijumuisha- nchi zote wanachama wa EU, Australia, Albania, Andorra, Uingereza, Iceland, Kanada, Liechtenstein, Mikronesia, Monaco, New Zealand, Norway, Jamhuri ya Korea, San Marino, Macedonia Kaskazini, Singapore, Marekani. , Taiwan (Uchina), Ukraine, Montenegro, Uswisi na Japan.

  9. Milipuko yatikisa bandari ya Ukraine saa kadhaa baada ya makubaliano ya nafaka

    Milipuko imekumba bandari ya Ukraine siku moja baada ya Kyiv na Moscow kufikia mkataba wa kihistoria ulioruhusu kurejelewa tena kwa mauzo ya nafaka

    Milipuko kadhaa iligonga mji wa Odessa magharibi mwa Ukraine mapema Jumamosi. Chanzo cha milipuko hiyo hakijafahamika.

    Chini ya mkataba uliofikiwa siku ya Ijumaa, Urusi ilikubali kutoshambulia bandari wakati wa usafirishaji wa nafaka.

    Umoja wa Mataifa ulikuwa umetaja makubaliano, ya kuruhusu usafirishaji wa mamilioni ya tani ya nafaka kama "msingi wa matumaini".

    Oleksiy Honcharenko, mbunge wa eneo hilo, aliandika katika mtandao wa Telegram kwamba milipuko sita ilisikika katika mji huo na bandari yake ilikuwa imeshika moto baada ya shambulio.

    Bw Honcharenko aliongeza kuwa vikosi vya ulinzi wa Ukraine vilidungua makombora kadhaa na kwamba ndege za kivita zimekuwa zikiviziana katika anga za mji huo.

  10. Hujambo na karibu.