Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo Ukraine: Kwa nini mji wa bandari wa Ukraine Odesa unaonekana kuwa shabaha kuu ya Urusi
Moshi mnene mweusi umefunika anga juu ya mji wa bandari wa Odesa, baada ya mashambulizi ya anga ya Urusi.
Urusi inadai ililenga vituo vya mafuta katika eneo ambalo Ukraine ilikuwa ikitumia kusambaza wanajeshi wake. Afisa wa Ukraine alisema makombora yamegonga "miundombinu muhimu" na hakukuwa na majeruhi au waliouwawa.
Odesa iliyoko kusini-magharibi mwa Ukraine- inayojulikana kama 'Pearl of the Black Sea' - ni eneo la tatu la mji mkuu wa nchi hiyo, na limedhaniwa kuwa lengo kuu la kimkakati kwa vikosi vya Urusi.
Meya wa jiji hilo, Gennadiy Trukhanov, alionya kuwa vikosi vinaweza kuizingira bandari ya kusini kwa pande tatu.
Alisema vikosi vya Urusi vinaweza kuangalia kusogea eneo ambalo wapo katika mkoa jirani wa Mykolaiv.
Bw Trukhanov anaamini kwamba wanajeshi wa Urusi walioko katika eneo la Transnistria linalodhibitiwa na watu wanaotaka kujitenga nchini Moldova wanaweza kisha kuhamia - jambo ambalo kimsingi lingemzuia Odesa kutoka katika maeneo mengine ya nchi.
Iko kando ya mpaka wa kusini-magharibi mwa Ukraine, Transnistria inatambulika kimataifa kama sehemu ya Moldova lakini inatawaliwa na serikali inayoungwa mkono na Moscow.
Bw Trukhanov anafikiri kwamba upande wa tatu unaweza kutoka baharini: "Watajaribu wakati huo huo kutuvuruga kutoka kwa mwelekeo wa Transnistria, ili kuunda tatizo huko, na bila shaka kuondoka kutoka baharini."
Odesa ina umuhimu gani?
Kama mji wa tatu kwa ukubwa wa Ukraine, ni muhimu kwa uchumi wa nchi.
Andrey Ryzhenko, nahodha wa zamani wa jeshi la majini na Waziri Msaidizi wa zamani wa Ulinzi wa Ukraine, aliiambia redio ya BBC World Service kwamba Odesa ni "mji mkuu wa bahari wa Ukraine," na inawajibika kwa karibu "20% ya Pato la ndani la Ukraine."
Katika nyakati za kawaida sehemu kubwa ya mauzo ya nje ya Ukraine - kama mahindi, nafaka na madini - hupitia Odesa na bandari ndogo za karibu za Youjni na Illytchyivsk.
"Ni kitovu ambacho karibu asilimia 70 ya biashara ya baharini nchini inategemea," Dk Sidharth Kaushal, Mtafiti katika taasisi ya masuala ya usalama ya Royal United Services, aliiambia BBC.
Pia ni kituo maarufu cha watalii shukrani kwa fukwe zake na usanifu wa kuvutia wa Karne ya 19, na ilikuwa maarufu kwa watalii wa Urusi.
"Raia wa Urusi kila mara walikuwa wakija Odesa na walijua ukarimu wa watu wa hapo lakini hiki ni nini sasa? Artillery, mabomu dhidi ya Odesa," Bw Zelensky alisema katika moja ya taarifa zake za hivi karibuni za video.
"Hii itakuwa uhalifu wa kivita."
Unaweza pia kusoma
- YA MSINGI:Viongozi wa kimataifa walaani mauaji 'ya kikatili' ya Bucha
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine
Kwa nini Odesa ni muhimu kwa Urusi?
Kambi kuu ya jeshi la majini la Ukraine iko katika Odesa.
Hapo awali ilikuwa huko Crimea, lakini ilihamishwa baada ya kuingizwa kwa Urusi kwa peninsula mnamo mwaka 2014.
Bandari hiyo itakuwa shabaha ya kimkakati ya kijeshi kwa Rais Putin. "Kuzuia uchumi wa Ukraine na biashara yake ya baharini kunaweza, angalau kimsingi, kuipa Urusi uwezo wa kulazimisha serikali ya Ukraine," Dk Kaushal alisema.
Kama moja ya bandari muhimu za Dola ya zamani ya Urusi, pia inashikilia nafasi ya mfano katika tamaduni na historia ya Urusi.
Jiji lilianzishwa mnamo mwaka 1794 na Catherine the Great - mfalme wa mwisho kutawala Urusi.
Akiwa jiji kubwa linalozungumza Kirusi, Rais Vladimir Putin amekuwa akilitazama kwa muda mrefu.
Katika hotuba yake tarehe 21 Februari, kabla ya uvamizi wa Ukraine, alitaja haswa Odesa na "janga kubwa" ambao ulifanyika mnamo 2014, wakati waandamanaji 48 wengi wao wakiwa wanaoiunga mkono Urusi walikufa katika jiji hilo baada ya mapigano na wazalendo wa Ukraine.
Ngome 'isiyoweza kupingwa'
Shirika la habari la AFP linaripoti kuwa takriban 100,000 kati ya wakaazi milioni moja wa jiji hilo wanakisiwa kuwa tayari wamekimbia.
Maelfu ya wengi wao wakiwa wanawake na watoto wanaelekea magharibi, huku wakilia kuwaacha baba zao, waume zao, kaka zao na watoto wao, wakilia kwenye kituo cha treni cha jiji hilo.
Lakini wale wanaokaa wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii kusaidia kulinda jiji lao. Meya Trukhanov alisema eneo hilo "limegeuka kuwa ngome, isiyoweza kupingwa".
Watu wamekuwa wakiweka mchanga kutoka kwa fukwe za Odesa kwenye mifuko, ili kuimarisha ulinzi wa jiji hilo.
Mwandishi Jana Kopko alisema angependa kusaidia, "Nadhani ni muhimu kwa sababu ninalipenda jiji langu, ninaipenda nchi yangu, na ninataka nchi yangu ishinde vita hivi."
Waandaaji wanakadiria karibu tani 700 za mchanga hukusanywa kila siku.
Victor Skrypnik, mpiga picha wa ndani, alisema: "Tunafanya kazi hapa kwa sababu hatujui jinsi ya kuua. Sisi si wapiganaji wa kitaalamu lakini tunaweza kusaidia jeshi letu."
Meya Trukhanov anaamini kushikilia safu kubwa ya ulinzi kwa pande tatu itakuwa "vigumu" - lakini amedhamiria kulinda jiji lake.
"Odesa ni ishara, ishara ya uhuru ... ni jiji ambalo linapendwa duniani kote. Na wakazi wa Odesa ni watu wa amani."