Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vatican yajitolea kuwa mpatanishi katika mizozo ya Sudan Kusini na DR Congo
Vatican imeelezea kujitolea kwake kusaidia utatuzi wa mizozo katika mataifa ya Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidomokrasia ya Congo.
Moja kwa moja
Vatican yajitolea kuwa mpatanishi katika mizozo ya Sudan Kusini na DR Congo
Vatican imeelezea kujitolea kwake kusaidia utatuzi wa mizozo katika mataifa ya Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidomokrasia ya Congo
Mwezi uliopita Papa Francis alilazimika kuahirisha ziara yake katika nchi hizo mbili kkufutaia jeraha la goti - na katibu wa mambo ya nje wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, alichukua nafasi yake.
"Nilifurahishwa na kwamba watu wa Sudan Kusini kwa mapokezi yao," aliambia BBC. Aliongeza kuwa nchi hiyo ina "mustakhbali mwema" lakini akasema utekelezaji wa makubaliano ya amani ni muhimu.
"Kanisa Katoliki - hasa Papa Mtakatifu - daima yuko tayari kuingilia kati, kwa mfano upatanishi. Tulifanya hivyo Ulaya, kwa mfano wakati wa vita vinavyoendelea nchini Ukraine," aliongeza.
"Nadhani pia barani Afrika tuko wazi ikiwa wahusika [katika migogoro] wako tayari kufanya hivyo."
Papa Francis bado ana nia ya kuzuru Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini baadaye, na Kadinali Paolin ametoa wito kwa jumuiya za Sudan Kusini kutii wito wa Papa wa kuishi pamoja "kama ndugu na dada".
Wanaanga wagundua nyota inayozunguka duniani kwa kasi kubwa zaidi
Wataalamu wa masuala ya angaza juu wamegundua mojawapo ya nyota yenye kasi zaidi duniani zenye uwezo wa kuzunguka shimo jeusi kwa muda mfupi zaidi.
Nyota S4716 inazunguka Sagittarius Shimo jeusi karibu na galaksi ya Milky Way katikati ya ulimwengu wetu.
Watafiti wamegundua kuwa nyota hiyo hukamilisha mzunguko wa shimo jeusi lenye ukubwa wa kilomita milioni 23.5 ndani ya miaka minne pekee, muda mfupi zaidi ambao nyota yoyote imewahi kuzunguka katika obiti yake.
Kulingana na watafiti, hii inamaanisha kuwa nyota hiyo inasafiri kwa kasi ya maili milioni 18 kwa saa (kilomita milioni 29 kwa saa) au karibu maili 5000 kwa sekunde.
Nyota S4716 iligunduliwa na watafiti katika Chuo Kikuu cha Cologne na Chuo Kikuu cha Masaric.
Jumla ya darubini tano zilihitajika kufuatilia nyota hiyo, nne kati yake ziliunganishwa na kuunda darubini kubwa ya anga ili kutoa maelezo sahihi na wa kina zaidi wa nyota hiyo.
Darubini hizi za anga zilijumuisha NIR2 na OSIRIS mjini Hawaii, pamoja na darubini za Uangalizi wa Kusini mwa Ulaya SINFONI na NACO na Gravity.
Pia unaweza kusoma:
- Fahamu siri ya 'shimo jeusi' lililoonekana katikati ya bahari ya Pasifiki
- Shimo jeusi angani linavyofanya kazi bila kujulikana
Uchaguzi Kenya 2022: Wagombea wa kiti cha Gavana wa jiji la Nairobi Kenya wanashiriki mdahalo.
Wagombea wa walioidhinishwa na Tume ya Uchaguzi nchini Kenya IEBC, wanashiriki mdahalo unaopeperushwa mubashra kwenye vyombo vya habari muda huu nchini humo.
Jumla ya wagombea tisa waidhinishwa kuwania kiti cha ugavana chenye ushindani mkubwa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 9 mwaka huu.
Mdahalo wa wagombea wa ugavana utafuatiwa na ule wagombea wa kiti cha Makamu rais na Wagombea wanne wa urais watashiriki mdahalo wao tarehe 27 Julai.
Katika midahalo hii Wakenya wanatarajia kupata fursa ya kuelewa zaidi sera na mipango ya wagombea kuhusu masuala mbali mbali ya kitaifa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kanisa Katoliki lashutumu mzozo wa kabla ya uchaguzi nchini Kenya - ripoti
Kanisa Katoliki nchini Kenya limeonya majibizano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto huenda yakavuruga harakati za kutafuta amani, kwa mujibu wa gazeti la Nation.
Gazeti hilo linamnukuu Askofu wa Meru, Salesius Mugambi, akisema kwamba kutoelewana hadharani kati ya wanasiasa hao wawili kumeacha kanisa likiwa na mshangao, na kwamba lazima Wakenya wafanye kila wawezalo ili kuhakikisha kura ya amani na mageuzi ya kidemokrasia.
Bw Kenyatta tayari amehudumu kwa mihula miwili kama rais na atajiuzulu baada ya uchaguzi mwezi Agosti.
Kufuatia mpasuko hajaunga mkono azma ya Bw Ruto kumrithi. Badala yake, amemuidhinisha mpinzani wake wa muda mrefu Raila Odinga.
Azma ya awali ya Bw Odinga mwaka wa 2017 ilimfanya ashindwe na Rais Kenyatta, huku kukiwa na madai ya ulaghai na hofu ya kutokea tena ghasia za kisiasa.
Ujerumani inahofia kukatwa kwa gesi ya Urusi huenda kukawa kwa kudumu
Usambazaji wa gesi ya Urusi kwenda Ujerumani kupitia bomba la Bahari ya Baltic Nord Stream 1 umesimamishwa kwa siku 10.
Waendeshaji wa bomba hilo wanaoungwa mkono na Urusi wanasema hatua hiyo ni ya kazi ya kila mwaka ya ukarabati.
Lakini mawaziri wa Ujerumani wanaamini kuwa hatua hiyo inachochewa kisiasa kama shinikizo kwa Berlin.
Mwezi uliopita, Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Robert Habeck alisema Rais wa Urusi Vladimir Putin anatumia gesi "kama silaha" kujibu vikwazo vya Umoja wa Ulaya.
Katikati ya Juni kampuni ya gesi ya Urusi Gazprom, ilipunguza gesi inayaosafirishwa kupitia Nord Stream 1 hadi 40% tu ya uwezo wa bomba hilo. Ililaumu kucheleweshwa kwa urejeshaji wa vifaa vinavyohudumiwa na kampuni ya Nokia Energy ya Ujerumani.
Maelezo zaidi:
Kambi ya kijeshi yavamiwa karibu na mradi wa gesi wa Msumbiji
Wanamgambo wa Msumbiji siku ya Jumamosi walivamia kambi ya kijeshi iliyoko karibu na eneo la uchimbaji gesi katika jimbo la kaskazini la Cabo Delgado.
Lilikuwa ni shambulio la tatu la aina hiyo dhidi ya nafasi ya kijeshi katika jimbo hilo katika muda wa chini ya miezi miwili.
Washambuliaji hao waliripotiwa kutafuta silaha na chakula.
Vyombo vya habari vya ndani vinasema kulikuwa na makabiliano makali kati ya wanajeshi na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kiislam, huku majeruhi wakiripotiwa pande zote mbili.
Baadhi ya wanajeshi wanasemekana kukimbia kambi hiyo na kutafuta hifadhi katika mji wa karibu wa Palma.
Kambi hiyo ilikuwa pia na wanajeshi wa Rwanda, kwa mujibu wa ripoti, lakini majeshi ya Msumbiji na Rwanda hayajatoa tamko lolote kuhusiana na ripoti hizo.
Cristiano Ronaldo 'yuko kwenye mipango yetu'- Erik ten Hag
Mkufunzi wa Manchester United Erik ten Hag anasema mshambuliaji wa Ureno Cristiano Ronaldo "yuko kwenye mipango yetu" ya msimu mpya na "hauzwi".
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 atakosa sehemu ya kwanza ya ziara ya United ya kujiandaa na msimu mpya nchini Thailand na anataka kuondoka katika klabu hiyo.
Alirejea United msimu uliopita baada ya kuzichezea Real Madrid na Juventus.
"Hayupo nasi kutokana na masuala ya kibinafsi. Tuna mpango na Cristiano Ronaldo kwa msimu huu. Ni hayo tu," alisema meneja wa zamani wa Ajax Ten Hag.
"Natazamia kufanya kazi na yeye. Cristiano hauzwii. Yupo kwenye mipango yetu. Tunataka mafanikio pamoja."
Kukosekana kwa mshambuliaji huyo wa Ureno kwenye ziara hiyo kulizua uvumi kuhusu hatma yake baada ya pia kukosa kurejea kwa klabu hiyo kwa mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya huko Carrington.
Ronaldo badala yake alifanya mazoezi katika makao makuu ya timu ya taifa ya Ureno.
Maelezo zaidi:
Ukraine inaunda 'jeshi lenye nguvu'' ili kukomboa eneo la kusini - Waziri wa ulinzi
Ukraine inapanga "jeshi lenye nguvu" lililo na silaha za Nato kuchukua tena eneo la kusini mwa nchi kutoka mikononi mwa Warusi, waziri wa ulinzi anasema.
Kuchukua tena maeneo karibu na pwani ya Bahari Nyeusi ilikuwa muhimu kwa uchumi wa nchi, Oleksii Reznikov alisema.
Hata hivyo, kauli hiyo inachukuliwa kuwa wito wa hadhara kuliko mpango madhubuti, anasema mwandishi wa BBC Joe Inwood mjini Kyiv.
Matamshi ya waziri wa ulinzi yanakuja huku Urusi ikipiga hatua katika kuchukua eneo la mashariki mwa mkoa wa Donbas.
Shambulizi dhidi ya jengo la ghorofa siku ya Jumapili lilisababisha vifo vya watu 18 - huku zaidi ya 20 wakihofiwa kufukiwa chini ya vifusi.
Waokoaji bado wanatafuta manusura katika eneo la jengo la orofa tano huko Chasiv Yar, karibu na mji wa Kramatorsk, katika eneo la Donetsk ambalo limekuwa lengo la msukumo wa Urusi.
Soma:
Habari za hivi punde, Paul Pogba ajiunga tena na Juventus
Paul Pogba amejiunga tena na Juventus kwa uhamisho wa bila malipo baada ya mkataba wake Manchester United kumalizika.
Kiungo huyo wa kati wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 29 alishinda taji la Serie A mara mbili na miamba hao wa Italia kabla ya uhamisho wa rekodi ya dunia wa £89m kwenda United mwaka 2016.
Alisafiri kwa ndege hadi Turin siku ya Ijumaa kwa matibabu yake kabla ya kutangazwa ramsi Jumatatu.
Pogba hakuwa ameichezea United tangu Aprili baada ya kusumbuliwa na jeraha.
Juventus ilisema: "Tunapoagana baada ya tukio kubwa lililoshirikiwa pamoja, daima kuna matumaini kwamba tutaonana tena, mapema au baadaye.
"Aliondoka akiwa mvulana na anarudi kama mwanamume na bingwa, lakini kuna jambo moja ambalo halijabadilika - hamu ya kuandika kurasa zisizosahaulika za historia ya klabu kwa mara nyingine tena. Pogba amerejea na hatukuweza kuficha furaha."
United na Pogba hawakuweza kuafikiana kuhusu mkataba mpya na klabu hiyo ilithibitisha mwanzoni mwa Juni kwamba ataondoka kama mchezaji huru msimu huu wa joto.
Pogba alijiunga na akademi ya United kutoka Le Havre.
Soma zaidi:
Mali yawakamata wanajeshi wa Ivory Coast huku kukiwa na madai ya njama ya mapinduzi
Wanajeshi 49 wa Ivory Coast wanaosemekana kuwa walikuwa wakijiunga na kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Mali (Minusma) walikamatwa mjini Bamako siku ya Jumapili, huku kukiwa na uvumi wa jaribio la mapinduzi, vyombo vya habari vya Mali viliripoti.
Wanajeshi waliokamatwa inasemekana hawakuwa na kibali cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa na “wote waliletwa ndani ya mabasi mawili madogo na kisha kusafirishwa karibu saa 2000 ndani ya uwanja wa ndege,’’ tovuti ya aBamako iliripoti ‘’Uwanja wa ndege kwa sasa umewekwa chini ya uangalizi mkali na wanajeshi kadhaa wa vikosi vya usalama, ” tovuti iliongeza.
Tovuti ya Maliactu ilisema katika chapisho la Facebook kwamba wanajeshi ‘’hawakuwa wamebeba silaha’’ lakini ‘’walikuwa na mizigo chini ya uangalizi wa Minusma’’.
Tovuti ya Malijet ilisema kuwa vikosi maalum vya Mali vilitumwa kulinda uwanja wa ndege baada ya wanajeshi wa Ivory Coast kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii walidai kuwa wanajeshi hao wa Ivory Coast walihusishwa na jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali inayoongozwa na jeshi la Mali.
Madai hayo huenda yakazidisha mvutano kati ya utawala wa kijeshi wa Mali na Minusma, ambao mamlaka yao yalianzishwa tena hivi majuzi kwa mwaka mwingine.
Vile vile vinaendana na uzinduzi wa kampeni ya kundi maarufu la wanaharakati wanaoipinga Ufaransa kutaka kukiondoa kikosi cha Umoja wa Mataifa.
Uadui wa umma dhidi ya Minusma na mashambulizi ya wanamgambo dhidi ya walinda amani yameongezeka katika wiki za hivi karibuni.
Wakenya milioni 14 hawana lishe bora huku shida ya chakula ikiongezeka
Kenya ni mojawapo ya nchi 63 duniani zenye idadi kubwa ya watu wasio na lishe bora, ripoti ya “Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe Duniani” inasema.
Kulingana na ripoti hiyo, ambao data zao zilikusanywa kati ya 2019 na 2021, takriban Wakenya milioni 14.4 hawana lishe bora.
Inasema idadi ya watu walio na uhaba mkubwa wa chakula nchini katika kipindi hicho ilikuwa milioni 14.
Idadi ya watu walioathiriwa na njaa duniani iliongezeka hadi takriban milioni 828 mwaka 2021, ongezeko la milioni 46 tangu 2020 na milioni 150 tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona.
“Ongezeko la njaa mnamo mwaka 2021 linaonyesha ukosefu wa usawa uliokithiri kote na ndani ya nchi kwa sababu ya mtindo usio sawa wa kufufua uchumi kati ya mataifa na upotezaji wa mapato ambao haujarekebishika kwa wale walioathiriwa zaidi na janga hili,” ripoti hiyo inasema.
Soma zaidi:
Mahakama ya Uhispania yaidhinisha uchunguzi wa maiti ya aliyekuwa rais wa Angola
Mahakama mjini Barcelona imeidhinisha uchunguzi wa mwili wa aliyekuwa rais wa Angola, Jose Eduardo dos Santos ufanyike.
Alifariki katika jiji la Uhispania siku ya Ijumaa, alikokuwa ameenda kwa matibabu.
Uchunguzi wa maiti uliombwa na bintiye marehemu rais, Tchize dos Santos.
Amezungumzia njama ya kumuua babake ili kumzuia kuunga mkono upinzani katika uchaguzi ujao wa Angola.
Mawakili wa familia ya Dos Santos wameshutumu hatua za serikali ya Angola kurudisha mwili wa marehemu Angola kwa mazishi ya kitaifa, dhidi ya matakwa ya rais huyo wa zamani kuzikwa kwa faragha nchini Uhispania.
Dos Santos alikuwa rais wa Angola kwa karibu miaka 40, hadi mwaka 2017.
Roketi tatu zapiga Kharkiv usiku mmoja
Kharkiv imepigwa makombora mara tatu usiku wa leo.
Hii inaripotiwa na Huduma ya Dharura ya Jimbo na kuchapisha picha za uharibifu huo.
Roketi moja iligonga jengo la makazi la orofa sita katika wilaya ya Osnovyansk.
Kama matokeo ya mlipuko huo, mlango uliharibiwa kabisa.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 86, mkazi kwenye nyumba hiyo katika ghorofa ya 2, aliokolewa kutoka kwenye vifusi.
Kwa bahati nzuri, hakukuwa na wahasiriwa.
Makombora mengine mawili yalipiga yadi karibu na ghala katika wilaya ya Osnovyansky, pamoja na shule katika wilaya ya Slobidsky ya jiji.
Katika siku iliyopita, kulikuwa na moto 11 uliosababishwa na makombora katika Mkoa wa Kharkiv.
Jengo la makazi, majengo ya shamba, majengo ya viwanda, gari, jalala la uchafu na nyasi kwenye eneo la wazi viliteketea.
Soma zaidi:
Mashambulizi ya Urusi yasababisha vifo vya watu 15 katika makazi ya Chasiv Yar, Ukraine inasema
Takriban watu 15 wameuawa na zaidi ya 20 wanahofiwa kufukiwa chini ya vifusi, baada ya roketi za Urusi kushambulia jengo la ghorofa huko Chasiv Yar, mji ulioko mashariki mwa Ukraine, maafisa wanasema.
Baadhi ya waathiriwa wametolewa wakiwa hai. Idadi ya waliofariki ilitolewa na afisa wa huduma za dharura wa Ukraine.
Upande mmoja wa jengo hilo la ghorofa tano ulipasuliwa na kuacha mlima wa kifusi. Chasiv Yar iko karibu na mji wa Kramatorsk, katika mkoa wa Donetsk. Donetsk ni Eneo linalolengwa sana na Urusi.
Gavana wa eneo hilo Pavlo Kyrylenko alisema uharibifu huo ulisababishwa na makombora ya roketi za Uragan za Urusi.
Rais wa Ukrain Volodymyr Zelensky alisema mashambulizi kwenye jengo la makazi ilifanywa kimakusudi.
"Baada ya mashambulizi kama haya , hawataweza kusema hawakujua kitu au hawakuelewa kitu," alisema kwenye anwani ya video, na kuongeza kuwa "adhabu ni lazima kwa kila muuaji wa Kirusi".
Wakati huo huo, mama aliye na mtoto wa miaka tisa yuko chini ya vifusi, shughuli ya uokoaji inaendelea, ripoti inasema.
Kulingana na Kanali Vyacheslav Boytsov, naibu mkuu wa kwanza wa Huduma ya Dharura ya Jimbo la Ukraine katika mkoa wa Donetsk, ufyatuaji wa makombora ulifanyika takriban 9:00 Jumamosi.
Roketi nne kwa ujumla zilipiga, mbili zikigonga makazi ya malazi moja kwa moja.
Kuna habari kwamba mama mwenye mtoto wa miaka tisa ni miongoni mwa wahasiriwa wengine chini ya vifusi.
Idadi kamili ya waathiriwa ambao wanaweza kubaki chini ya vifusi haijulikani kwa sasa.
Watu sita waliofanikiwa kutolewa chini ya vifusi walipelekwa hospitalini.
Soma zaidi:
Afrika Kusini: Watu 15 wamepigwa risasi katika baa Soweto
Takriban watu 15 wameuawa kwa kupigwa risasi katika baa moja katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini, polisi wamesema.
Polisi walisema watu wenye silaha waliingia kwenye kilabu hicho asubuhi ya Jumapili na kuanza kufyatulia risasi ovyo kundi la vijana.
Kisha wakatoroka eneo hilo kwa basi dogo jeupe.
Hakuna sababu ya shambulio hilo ambayo imebainishwa, polisi walisema.
Watu kadhaa zaidi wako katika hali mbaya hospitalini, mwandishi wa BBC Nomsa Maseko anaripoti.
Waathiriwa wanaaminika kuwa na umri wa kati ya miaka 19 na 35.
"Miili ilikuwa juu ya kila mmoja huku damu zikiwa zimetapakaa. Tulikuwa tunawatafuta wapendwa wetu, ikabidi turuke miili kuwatafuta ndugu zetu," alisema mkazi wa eneo hilo Ntombikayise Meji.
Mkuu wa polisi wa jimbo la Gauteng, Lt-Jenerali Elias Mawela, aliiambia BBC kwamba ufyatuaji risasi huo unaonekana kuwa "shambulio la kinyama dhidi ya wateja wasio na hatia".
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ofisi yake ilisema watu hao wenye silaha walikuwa wamejihami kwa bunduki na bastola za 9mm walipoingia kwenye baa hiyo.
Polisi wanawasaka washukiwa hao, ambao bado hawajafahamika majina yao, ilisema.
Thaban Moloi, kiongozi wa jamii huko Soweto, alikasirishwa na muda ambao iliwachukua polisi kufika katika eneo la tukio.
"Ni baya sana, nakwambia. Watu hawajui la kufanya. Ungekuwa huko ungeona wanawake na watoto wakilia," alisema.
Bw Moloi alisema shambulio hilo lilitokea saa 23:00 kwa saa za huko (21:00 GMT) siku ya Jumamosi lakini polisi hawakufika hadi saa 04:00 siku ya Jumapili.
"Ilichukua saa tano kwa wao kuja, jamani," alisema.
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja