Mashirika ya haki za kibinadamu yataka wagombea waliokiuka maadili kuzuiwa kushiriki katika uchaguzi Kenya
Kundi la mawakili nchini Kenya limezitaka taasisi zinazowachunguza wagombeaji wa uchaguzi kuwaondoa wanasiasa 25 kuwania nyadhifa zao kwa madai ya uadilifu.
Muungano wa National Integrity Alliance (NIA) ulisema kuwa kukosa kufutilia mbali wawaniaji hao 25 kutamaanisha kuwa Wakenya wana hatari ya kuwachagua wafisadi kwenye nyadhifa za umma.
Kati ya wanasiasa hao 25, wanane ni washirika wa muungano wa Naibu Rais William Ruto wa Kenya Kwanza, huku 10 wakitoka muungano wa Azimio la Umoja wa Raila Odinga.
Mgombea mwenza wa Bw Ruto Rigathi Gachagua ni miongoni mwa walioorodheshwa.
Bw Gachagua anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi mahakamani ingawa hapo awali alikana kuhusika.
NIA ilisema ilitegemea ripoti za uchunguzi za kweli na zinazoweza kuthibitishwa kuja na orodha hiyo.
Wanasiasa hao hawajajibu hatua hiyo ya NIA.
Sura ya Sita ya Katiba ya Kenya inataja kwamba watu ambao mienendo yao inachukuliwa kuwa isiyo na heshima au inayodhuru imani na uadilifu wa umma wanapaswa kuzuiwa kushikilia nyadhifa za umma.
Wanasiasa wengi, wakiwemo wabunge wa viti maalum na magavana, wanawania kuchaguliwa tena licha ya kesi za ufisadi au tuhuma dhidi yao.
Bw Odinga, mmoja wa walio mstari wa mbele katika kinyang’anyiro cha urais, ameahidi kupambana na ufisadi iwapo atachaguliwa.
Wakenya watapiga kura kumchagua rais, magavana, maseneta, wabunge na viongozi wa kiraia tarehe 9 Agosti.