Urusi na Ukraine: Hatuwezi kuruhusu nguvu ya kikatili itawale ulimwengu - Zelensky

Rais huyo wa Ukraine alifungua hotuba yakekwa kuwataka waliohudhuriakatika kongamano la kiuchumi duniani la World Economic Forum kufikiria kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu: History at a turning point.

Moja kwa moja

  1. Mashirika ya haki za kibinadamu yataka wagombea waliokiuka maadili kuzuiwa kushiriki katika uchaguzi Kenya

    Kundi la mawakili nchini Kenya limezitaka taasisi zinazowachunguza wagombeaji wa uchaguzi kuwaondoa wanasiasa 25 kuwania nyadhifa zao kwa madai ya uadilifu.

    Muungano wa National Integrity Alliance (NIA) ulisema kuwa kukosa kufutilia mbali wawaniaji hao 25 ​​kutamaanisha kuwa Wakenya wana hatari ya kuwachagua wafisadi kwenye nyadhifa za umma.

    Kati ya wanasiasa hao 25, wanane ni washirika wa muungano wa Naibu Rais William Ruto wa Kenya Kwanza, huku 10 wakitoka muungano wa Azimio la Umoja wa Raila Odinga.

    Mgombea mwenza wa Bw Ruto Rigathi Gachagua ni miongoni mwa walioorodheshwa.

    Bw Gachagua anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi mahakamani ingawa hapo awali alikana kuhusika.

    NIA ilisema ilitegemea ripoti za uchunguzi za kweli na zinazoweza kuthibitishwa kuja na orodha hiyo.

    Wanasiasa hao hawajajibu hatua hiyo ya NIA.

    Sura ya Sita ya Katiba ya Kenya inataja kwamba watu ambao mienendo yao inachukuliwa kuwa isiyo na heshima au inayodhuru imani na uadilifu wa umma wanapaswa kuzuiwa kushikilia nyadhifa za umma.

    Wanasiasa wengi, wakiwemo wabunge wa viti maalum na magavana, wanawania kuchaguliwa tena licha ya kesi za ufisadi au tuhuma dhidi yao.

    Bw Odinga, mmoja wa walio mstari wa mbele katika kinyang’anyiro cha urais, ameahidi kupambana na ufisadi iwapo atachaguliwa.

    Wakenya watapiga kura kumchagua rais, magavana, maseneta, wabunge na viongozi wa kiraia tarehe 9 Agosti.

  2. Waziri asema 'watu maskini hawatakwenda mbinguni' - ripoti

    .

    Chanzo cha picha, kahinda Otafire/facebook

    Maelezo ya picha, kahinda

    Gazeti la New Vision la Uganda linamnukuu mwanasiasa mmoja mkuu akisema "maskini hawataenda mbinguni kwa sababu wanamtukana Mungu kwa njia ya maombolezo na shutuma kila siku".

    Waziri wa Masuala ya Ndani Kahinda Otafiire aliripotiwa kutoa maoni hayo katika hafla ya shule huko Kyenjojo, magharibi mwa Uganda, huku akiwaambia wanafunzi kuwa kufanya kazi kwa bidii ndio dawa ya umaskini.

    "Ikiwa hutumii zana alizokupa Mungu, usimlaumu unaposalia kuwa maskini. Jitahidi kuushinda umaskini kwa sababu kuwa tajiri ni utukufu," anaripotiwa kusema.

    Ukosefu wa ajira kwa vijana na ukosefu wa ajira ni mkubwa nchini Uganda, ambayo ina moja ya idadi ya watu changa zaidi duniani ikiwa na 75% ya raia chini ya umri wa miaka 30.

  3. Joe Biden: China 'inacheza na moto' Taiwan

    Joe Biden

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Joe Biden

    Rais wa Marekani Joe Biden alionya Jumatatu kwamba China "inacheza na moto" akizungumzia vitendo vyake nchini Taiwan na kuahidi kuingilia kijeshi kulinda kisiwa hicho iwapo kitashambuliwa.

    Wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Tokyo, pamoja na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida, rais wa Marekani pia alifananisha uvamizi wa Taiwan na ule wa Urusi dhidi ya Ukraine, lilivutia jibu kali kutoka kwa Beijing.

    Biden ametoa matamshi hayo akiwa katika katikati ya ziara yake ya kwanza barani Asia kama rais wa Marekani, ambapo pia aliitembelea Korea Kusini, mshirika mwingine wa Marekani katika eneo hilo.

    Rais wa Marekani alianza hotuba yake kwa kusema kwamba sera ya nchi yake kuhusu Taiwan "haijabadilika."

    Hii ni mara ya pili katika miezi ya hivi karibuni ambapo amedai Marekani itailinda Taiwan ikiwa China itashambulia, hatua inayoonekana na wataalamu kama mabadiliko msimamo wake

  4. Habari za hivi punde, Kylian Mbabe kusalia PSG, aipa 'pole' Real Madrid

    Mbappé kuhusu Real Madrid: “Nina heshima kwa Real Madrid na Florentino Perez. Walinifanyia kila kitu na walijaribu kunifurahisha sana, ndiyo maana ilibidi nimpigie simu yeye binafsi, tuna uhusiano wa karibu”.

    "Niliamua mwenyewe na nilifanya uamuzi bora"

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

  5. Watu 87 waliuawa katika shambulizi moja huko Desna, Ukraine

    Kifaru

    Chanzo cha picha, UNIAN

    Mnamo Jumatatu, Mei 23, Rais Volodymyr Zelensky alisema kuwa watu 87 walikufa chini ya vifusi katika kijiji kilichoshambuliwa na makombora ya Urusi cha Desni katika mkoa wa Chernihiv.

    Hii ni moja ya hasara kubwa kwa wakati mmoja ya Ukraine katika vita hivi, ambavyo viliripotiwa rasmi na wakuu wa nchi.

    Mnamo Machi kutokana na moto wa roketi katika utawala wa kikanda huko Nikolaev zaidi ya watu 50 walipotea.

    Zaidi ya watu 20 waliripotiwa kuuawa katika shambulio la makombora la mnara wa TV na kambi ya Walinzi wa Kitaifa karibu na Rivne, na pia makumi ya watu waliuawa katika shambulio kwenye kambi katika vitengo vya jeshi katika mikoa mingine ya nchi.

    Baada ya hapo, wanajeshi na wataalamu walizungumza juu ya hitaji la kubadilisha mazoezi ya makazi ya jeshi kwenye kambi.

    Zelensky alisema kuwa kama rais wa nchi inayopigana, alifikiria juu ya hali ya sasa ya Ukraine na ni watu wangapi wanaokufa kila siku.

    Siku moja kabla, rais alisema kwamba wanajeshi 50 mpaka 100 wa Kiukreni waliuawa katika vita kila siku.

    • Mzozo wa Ukraine: Fahamu Jinsi Finland ilivyojiandaa kwa miongo kukabiliana na Urusi
    • Vita vya Ukraine: Fahamu chombo kipya cha propaganda kinachotumiwa na Urusi
  6. Ukraine kushikilia mali ya watu watakaobainika kusaidia vita dhidi ya Ukraine

    Siku ya Ijumaa, viongozi wa G7 walikubali kuipatia Ukraine msaada kwa ajili ya kujilinda

    Chanzo cha picha, EPA

    Bunge la Ukraine limetangaza sheria mpya ambayo inaruhusu serikali kukamata mali ya watu wanaounga mkono vita vya Urusi.

    Yeyote atakayepatikana kuwa mfuasi wa mapigano hayo ana hatari ya kupelekwa katika Mahakama ya Juu ya Kupambana na Ufisadi ya Ukraine, ambapo maafisa watapeleka mali zao "katika mapato ya serikali", taarifa hiyo inasema.

    Uchumi wa Ukraine umepata pigo wakati wa mzozo na Urusi.

    Siku ya Ijumaa, viongozi wa G7 walikubali kulipatia taifa hilo lililokumbwa na vita $19.8bn (£15.7bn) kama msaada wa kiuchumi ili kuhakikisha kuwa linaendelea kujilinda.

    • MLRS: Kwanini Ukraine inazitaka 'kwa udi na uvumba' Silaha hizi?
    • Mzozo wa Ukraine: Usambazaji wa silaha za Magharibi nchini Ukraine unavyobadili hali ya mapambano ya vita
    • Mzozo wa Ukraine: Madai ya mashambulizi ya kemikali ya Urusi yathibitishwa
  7. Habari za hivi punde, Nyati mwingine mweupe aonekana mbuga ya Tarangire Tanzania

    Tarangire National Park

    Chanzo cha picha, Tarangire National Park

    Maelezo ya picha, Nyati mweupe katika mbuga ya wanyama pori ya Tarangire Tanzania

    Nyati mwingine mweupe ameonekana katika hifadhi ya Taifa ya Tarangire nchini Tanzania ndani ya wiki moja.

    Nyati wa kwanza alionekana tarehe 14 na kuvutia watalii wengi kutaka kumuona mnyama huyo, Wizara ya Maliasili na Utalii imesema.

    Kwa hifadhi ya Tarangire,hii ni mara ya kwanza kwa Nyati weupe kuonekana ingawa tayari walishuhudia twiga weupe mara mbili.

    Muongoza hifadhi ameeleza kuwa kwa muonekano wa kwanza ni albino ila watafiti wataweza kumbainisha zaidi.

    Nyati kwa kawaida ana rangi nyeusi na kuwa rangi nyeupe kunaonesha utofauti wake.

    Nyati wa kwanza ambaye ni dume, anakadiriwa kuwa na miaka 19 au 20, na kwa kawaida nyati hutembea kwa makundi hivyo hawezi kuwa ametoka hifadhi nyingine.

    Ili kujiridhisha na matukio haya mawili ndani ya wiki moja, na kwa nini Nyati hao ni wawili , na iwapo ni albino au la; Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) imetuma watafiti wake kuwafuatilia kwa kina, ikiwemo kukusanya taarifa zao na kuchukua sampuli ili kujiridhisha iwapo ni albino au la.

    Aidha , Watafiti wanawafuatilia Wanyama hao kwa karibu ili kujua maendeleo yao, ikiwemo kuwafunga mikanda ya mawasiliano ili kurahisisha ufuatiliaji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA).

    Muonekano na viashiria vya awali vinaonyesha kuwa nyati hawa wana tatizo la ualbino.

    Hata hivyo kuonekana kwa nyati wawili wenye ualbino ndani ya wiki moja katika hifadhi moja wakati ualbino katika wanyama wenye uti wa mgongo ni tukio la nadra linaleta maswali mengi na hivyo kuhitaji utafiti wa kina.

    Ualbino ni tukio linalotokea kwa mnyama mmoja kati ya wanyama 20,000 hadi milioni moja na kwa kawaida ni nadra kutokea.

  8. Hatuwezi kurusu 'nguvu ya kikatili' kututawala - Zelensky asema

    Zelensky
    Maelezo ya picha, Rais Zelensky

    Rais huyo wa Ukraine alifungua hotuba yakekwa kuwataka waliohudhuriakatika kongamano la kiuchumi duniani la World Economic Forum kufikiria kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu: History at a turning point.

    Mwaka huu ,kauli mbiu ya kongamano hilo ni maneno matupu, alisema Zelensky, badala yake ni ishara ya vita vinavyoendelea ‘hivi sasa’.

    Anasema kwamba ulimwengu unaweza kutawaliwa na ‘nguvu ya kikatili’, kabla ya kugeukia ‘jumba la uhalifu wa kivita la Urusi’, lililojengwa mjini Davos kama Ushahidi wa taifa hilo alilodai lina ‘wahalifu wengi wa kivita’.

  9. Habari za hivi punde, Mwanajeshi wa Urusi aliyemuua raia wa Ukraine apewa kifungo cha maisha jela

    Shishimarin

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Vadim Shishimarin

    Mahakama chini Ukraine imempatia kifungo cha maisha jela kamanda wa kitengo kimoja cha Urusi kwa kumuu raia ,katika uamuzi wa kesi ya kwanza dhidi ya uhalifu wa kivita dhidi ya mwanajeshi wa Urusi tangu uvamizi wa Ukraine.

    Mwanajeshi huyo aliyekamatwa, sajenti Vadim Shishimarin alihukumiwa kwa kumuua Oleksandr Shelipov ,62, katika Kijiji cha kaskazini mashariki cha Chupakhivka tarehe 28 mwezi Februari.

    Alikiri kumpiga risasi bwana Shelipov lakini akasema alikuwa akifuata amri na kuomba msamaha kwa mjane wake. Visa kadhaa vya uhalifu wa kivita vinachunguzwa na Ukraine.

    Moscow imekana kwamba wanajeshi wake waliwalenga raia wakati wa uvamizi wa taifa hilo huku Ukraine ikisema kwamba zaidi ya visa 1000 vya uhalifu wa kivita huenda vilifanyika.

    Kesi hii iliofanyika katika mji mkuu wa Ukraine Kyiv ilikuwa inatazamwa kuthibitisha bila shaka , kwamba mwanajeshi wa Urusi alimuua raia bila kujali sheria za vita.

  10. Sayad Khodai : Kanali wa jeshi la Iran auawa

    Familia ikiwa imekusanyika karibu na gari ambalo Kanali Sayad Khodai aliuawa

    Chanzo cha picha, EPA

    Kanali wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) ameuawa kwa kupigwa risasi katika mauaji ya nadra mjini Tehran.

    Watu wawili wenye silaha waliokuwa kwenye pikipiki wanaripotiwa kumpiga risasi Kanali Sayad Khodai mara tano kwenye gari nje ya nyumba yake.

    Kufikia sasa, hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi la Jumapili, na msako unaendelea kuwatafuta watu hao wenye silaha.

    Ni ukiukaji mkubwa zaidi wa usalama nchini Iran tangu 2020 wakati mwanasayansi mashuhuri wa nyuklia alipouawa.

    Picha kutoka eneo la tukio zinaonesha mwanaume aliyemwaga damu akiwa amejilaza kwenye gari huku akiwa amejifunga mkanda wa kiti.

    Kanali Khodai alikuwa mwanachama mkuu wa Kikosi cha wasomi cha Quds, tawi la IRGC ambao unaendesha operesheni nje ya nchi.

    Marekani inakishutumu kikosi hicho kwa kuunga mkono mashirika ya kigaidi na kuhusika na mashambulizi katika eneo la Mashariki ya Kati.

  11. Mwenyekiti wa umoja wa Afrika kuzuru Urusi na Ukraine

    w

    Chanzo cha picha, AFP

    Rais wa Senegal Macky Sall anasema atasafiri hadi Urusi na Ukraine hivi karibuni katika wadhifa wake kama mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika.

    Bw Sall alisema Jumapili kwamba amepokea mamlaka ya wakuu wengine wa nchi wa AU kufanya safari hizo.

    Katika mkutano wa pamoja na Kansela wa Ujerumani anayezuru Afrika Olaf Sholz, alisema Afrika ina nia ya kuona amani kupitia mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi.

    Rais huyo wa Senegal alisema Urusi imetoa mwaliko wa kufanya ziara huku rais wa Ukraine akieleza haja ya kuwasiliana na wakuu wa nchi za Afrika.

    Mgogoro wa Russia na Ukraine umekatiza usambazaji wa nafaka na mafuta ya kupikia, na hivyo kuzidisha uhaba wa chakula hasa katika nchi maskini za Afrika kutokana na kupanda kwa bei.

    Bei ya mafuta duniani pia imepanda kutokana na hilo, na kuongeza mzigo wa gharama kwa nchi nyingi.

  12. Ukraine inaweza kupoteza maisha ya wanajeshi 100 kila siku huko mashariki - Zelensky

    w

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ukraine huenda inapoteza maisha kati ya 50-100 eneo la mashariki kila siku, Rais Volodymyr Zelensky alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari Jumapili.

    Alisema waliouawa walikuwa wakiilinda Ukraine katika "mwelekeo mgumu zaidi".

    Zelensky hakufafanua zaidi lakini maoni hayo yanaonekana kuwa marejeleo ya hasara za kijeshi na ni ishara ya jinsi mapigano yalivyo makali mashariki.

    Vikosi vya Urusi vimeongeza juhudi zao za kuteka miji ya eneo la Donbas mashariki, kwa kuzingatia mji wa Severodonetsk.

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  13. Polisi wa Nigeria wachunguza kisa cha mbunge kukatwa kichwa

    w

    Chanzo cha picha, Okechukwu Okoye/Facebook

    Polisi nchini Nigeria wanachunguza kisa cha kukatwa kichwa kwa mbunge wa eneo hilo katika jimbo la kusini-mashariki la Anambra muda wa wiki moja baada ya watu wenye silaha kumteka nyara pamoja na msaidizi wake.

    Kupatikana kwa mwili wa Okechukwu Okoye uliokatwakatwa wikendi kumezua hasira.

    Gavana wa jimbo la Anambra Charles Soludo alielezea mauaji hayo kuwa ya kinyama, ya kinyama na ya kushtua.

    Alitangaza zawadi kwa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa wauaji. Haijabainika ni nani alikuwa nyuma ya shambulio hilo.

    Maafisa wamelilaumu kundi lililopigwa marufuku la kujitenga kwa kuongeza ghasia katika eneo hilo.

    Wenyeji wa Biafra, ambao wanafanya kampeni ya kutaka jimbo lililojitenga, wamekanusha kuhusika na mashambulizi ya hivi majuzi.

    Kiongozi wake, Nnamdi Kanu, amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za ugaidi na uhaini ambayo ameyakanusha.

  14. Mamia wahamishwa Afrika Kusini kufuatia mafuriko mapya

    Wakazi wameripoti uharibifu wa miundombinu baada ya mvua kubwa kunyesha hivi punde

    Chanzo cha picha, AFP

    Maelezo ya picha, Wakazi wameripoti uharibifu wa miundombinu baada ya mvua kubwa kunyesha hivi punde

    Mamia ya wakazi wamehamishwa kutoka mkoa wa KwaZulu-Natal huko Afrika Kusini baada ya mafuriko kuzuka upya.

    Mkoa huo ulikumbwa na mafuriko mabaya mwezi uliopita.

    Mvua kubwa imekuwa ikinyesha katika eneo hilo wikendi iliyopita na mamlaka zimetoa tahadhari kuzuia maafa yoyote.

    Maya wa jiji hilo Mxolisi Kaunda anasema hakuna ripoti kamilifu iliyotolewa kuhusu athari za mvua kubwa iliyonyesha lakini wakazi wameripoti uharibifu mkubwa wa miundombinu, tuvuti ya News24 inaripoti.

    Tahadhari ya kiwango cha 10 - ngazi ya juu na kali zaidi - iliyotolewa na huduma ya hali ya hewa inaendelea kudumishwa.

    Wengi wa wale walioathiriwa na mafuriko ya Aprili hawajawahi kurejelea hali yao ya kawaida, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

    Nyumba zilifagiliwa na barabara kuharibiwa wakati wa mafuriko ya Aprili.

  15. Uganda haitadhibiti gharama za juu za maisha - Museveni

    Museveni

    Chanzo cha picha, AFP

    Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema serikali haitaingilia kati hali ya sasa ya kiuchumi na kupanda kwa gharama ya maishi nchini humo .

    Bei za bidhaa za mafuta, i mali ghafi inayoagizwa kutoka nje ya nchi, pamoja na chakula, zimekuwa zikipanda katika miezi michache iliyopita, mzozo ambao unashuhudiwa kute duniani kufuatia vita vya vinavyoendelea nchini Ukraine.

    Mfumko wa bei nchini Uganda umefikia asilimia 4.9, kiwango cha juu zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 2017.

    Katika hotuba yake kwa taifa kupitia televisheni usiku wa Jumapili, Museveni alisema ruzuku ya serikali au kuondolewa kwa ushuri wa bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi kutaporomosha uchumi..

    Kutumia kwa akiba ya kitaifa kwa ununuzi wa bidhaa hizo za bei ghali kutakuw ana athari kubwa, rais aliongeza.

    Akiba ya sarafu ya kigeni nchini Uganda kwa sasa ni zaidi ya bilioni nne

    Bw. Museveni alisema nchi inatakiwa kutumia bidhaa za kuagizwa kutoka ambazo inaweza kumudu pekee

    Pia aliwashauri wananchi kubadilisha ngano ya bei ghali badala ya vyakula vinavyopatikana nchini kama vile mtama, mahindi, ndizi mbichi na mihogo..

    Sehemu kubwa ya Uganda ina uwezo wa kuzalisha vyakula kwa wingi, na familia nyingi zinategemea kilimo cha kujikimu.

    Kati ya 2020 na 2021, kilimo kilichangia takriban asilimia 23.7 ya Pato la Taifa la nchi. Lakini hata bei za vyakula vinavyozalishwa nchini zimekuwa zikipanda, hasa mijini, kutokana na gharama za usafirishaji.

    Raia wa Uganda wanalazimika kununua kiasi kidogo cha vitu vya msingi au kuegesha magari yao ili kukabiliana na mzozo huo.

  16. Idadi ya wakimbizi yafikia milioni 100 kwa mara ya kwanza duniani

    w

    Chanzo cha picha, Reuters

    "Idadi ya watu waliolazimika kukimbia migogoro, ghasia, ukiukwaji wa haki za binadamu na mateso sasa imevuka hatua ya kushangaza ya milioni 100 kwa mara ya kwanza kwenye rekodi, iliyochochewa na vita vya Ukraine na migogoro mingine mibaya," Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi anasema.

    Katika taarifa, mkuu wa UNHCR Filippo Grandi anasema hii ni "takwimu kubwa na ya kutisha na. Ni rekodi ambayo haikupaswa kuwekwa kamwe.

    "Hii lazima iwe kama mwito wa kuamsha na kuzuia mizozo haribifu, kukomesha mateso, na kushughulikia sababu zinazowalazimisha watu wasio na hatia kukimbia makazi yao."

    UNHCR inasema vita vya Ukraine vimepoteza makazi milioni nane ndani ya nchi hiyo, na zaidi ya watu milioni sita wamekimbilia nje ya nchi.

    Mwaka jana, idadi ya waliokimbia makazi ya Umoja wa Mataifa iliongezeka hadi milioni 90 kwa sababu ya ghasia na migogoro katika nchi zikiwemo Ethiopia, Burkina Faso, Myanmar, Nigeria, Afghanistan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

  17. Hakuna chochote cha kunitenganisha na mume wangu, 'hata vita haviwezi'- Mke wa Zelensky

    W

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mke wa Rais wa Ukraine Olena Zelenska amefanya mahojiano ya nadra akiwa na mumewe Volodymyr Zelensky.

    Hii ni mara ya pili kwa wanandoa hao kuonekana wakiwa pamoja tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine.

    Familia ya Zelensky ilipelekwa mahali pasipojulikana kwa sababu za kiusalama.

    Olena alieleza katika video kuwa, chochote hakiwezi kumchukua mumewe hata vita haviwezi.

    Aliongeza kama familia nyingine nchini Ukraine, wameathirika pia na vita hivi.

    Hawajaweza kumuona Zelesky kwa zaidi ya miezi miwili.

    Lakini alisisitiza kuwa anaelewa umuhimu wa kazi yake.

    ‘’Hatuaonana kwa zaidi ya miezi miwili, tunazungumza tu kwa simu, na nimefurahi sana kwa nafasi hii, kwani mahojiano haya angalau yanafanya tunakua pamoja’’ anasema Olena.

    Soma:

    • Mfahamu mke wa Rais wa Ukraine Olena Zelenask anayetafutwa na Urusi
    • Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
  18. Wataalamu wa mabomu kutoka Syria wamewasili nchini Urusi

    w

    Chanzo cha picha, EPA

    Zaidi ya wataalamu 50 wa Syria wenye uzoefu katika utengenezaji na utumiaji wa mabomu ya mapipa wamewasili na kufanya kazi nchini Urusi kwa wiki kadhaa pamoja na jeshi la Urusi.

    Hii iliripotiwa na gazeti la Guardian la Uingereza, likiwanukuu maafisa wa Ulaya.

    Kwa mujibu wao, wataalam katika utengenezaji wa silaha hii ya kiholela, ambayo iliharibu sehemu kubwa ya Syria wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, walitumwa Urusi kusaidia kuendeleza operesheni za matumizi yake huko Ukraine.

    Uwepo wao nchini Urusi unaweza kuwa moja ya sababu zinazoelezea maonyo ya Amerika na Ulaya kwamba jeshi la Urusi linaweza kuwa linajiandaa kutumia silaha za kemikali nchini Ukraine.

    Mabomu ya pipa - mlipuko mbaya, kawaida wa ufundi, umejaa kwenye pipa, wakati mwingine na kitu kimoja au kingine cha kushangaza, ambacho hutupwa kutoka kwa helikopta kwa kulenga "kwa jicho".

    Kulingana na wataalamu, kutokana na kiwango cha chini cha usahihi, mabomu ya pipa hutumiwa hasa katika hali ya rasilimali ndogo na ukosefu wa silaha nyingine. Silaha ya aina hii ilitumika kwa madhara makubwa katika muda wote wa vita vya Syria.

    "Tunajua kwamba kuna uwezekano wa kutumia mabomu ya pipa, lakini ikiwa jeshi la Urusi litatumia huko Ukraine, watapoteza; tutajua ni nani aliyefanya hivyo, na uwezekano mkubwa bado watauawa," maafisa wa Ulaya ambao hawakutajwa waliambia The Guardian.

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine