Mafuriko ya Durban: Takriban watu 45 wafariki huku mvua na maporomoko ya udongo vikisababisha uharibifu
Takriban watu 45 nchini Afrika Kusini wamefariki katika mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha kwa siku kadhaa, mamlaka zimesema.
Ilitokea katika jimbo la pwani la KwaZulu-Natal, ambapo watu wengi bado hawajulikani walipo na huduma za dharura zinawatafuta manusura.
Baadhi ya watu katika jiji la Durban wamesimama juu ya paa wakisubiri kuokolewa, lakini vyombo vya habari vya nchi hiyo vinaripoti kuwa ni helikopta moja tu inayopatikana kuwaokoa watu.
Barabara kuu kote jijini zimefungwa na maporomoko ya udongo yameharibu nyumba nyingi.
Inakuja huku wanasayansi kuonya kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanachochea mvua kubwa kuliko kawaida kusini mwa Afrika.
Meya wa jiji la Durban - ambalo ni eneo likiwemo la Durban na miji inayoizunguka - amewaomba radhi wakazi walioachwa baada ya kituo cha simu za dharura kuzidiwa usiku kucha.
Meya Mxolisi Kaunda pia anasema juhudi zinaendelea za kurejesha huduma ya maji na umeme ambayo imekatika katika baadhi ya maeneo ya jiji, baada ya vituo vingi vya umeme vya jiji hilo kujaa maji Jumatatu jioni na mitambo kadhaa ya kusafisha maji kuharibika.
Wakaazi wanaohofia nyumba zao zinaweza kuporomoka wanapaswa kutafuta hifadhi katika kumbi za jamii, Meya Kaunda ameshauri.