Takriban watu 45 wafariki Afrika Kusini huku mvua na maporomoko ya udongo vikisababisha uharibifu

Inakuja huku wanasayansi kuonya kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanachochea mvua kubwa kuliko kawaida kusini mwa Afrika.

Moja kwa moja

  1. Mafuriko ya Durban: Takriban watu 45 wafariki huku mvua na maporomoko ya udongo vikisababisha uharibifu

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takriban watu 45 nchini Afrika Kusini wamefariki katika mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha kwa siku kadhaa, mamlaka zimesema.

    Ilitokea katika jimbo la pwani la KwaZulu-Natal, ambapo watu wengi bado hawajulikani walipo na huduma za dharura zinawatafuta manusura.

    Baadhi ya watu katika jiji la Durban wamesimama juu ya paa wakisubiri kuokolewa, lakini vyombo vya habari vya nchi hiyo vinaripoti kuwa ni helikopta moja tu inayopatikana kuwaokoa watu.

    Barabara kuu kote jijini zimefungwa na maporomoko ya udongo yameharibu nyumba nyingi.

    Inakuja huku wanasayansi kuonya kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanachochea mvua kubwa kuliko kawaida kusini mwa Afrika.

    Meya wa jiji la Durban - ambalo ni eneo likiwemo la Durban na miji inayoizunguka - amewaomba radhi wakazi walioachwa baada ya kituo cha simu za dharura kuzidiwa usiku kucha.

    Meya Mxolisi Kaunda pia anasema juhudi zinaendelea za kurejesha huduma ya maji na umeme ambayo imekatika katika baadhi ya maeneo ya jiji, baada ya vituo vingi vya umeme vya jiji hilo kujaa maji Jumatatu jioni na mitambo kadhaa ya kusafisha maji kuharibika.

    Wakaazi wanaohofia nyumba zao zinaweza kuporomoka wanapaswa kutafuta hifadhi katika kumbi za jamii, Meya Kaunda ameshauri.

  2. Watu kadhaa wapigwa risasi katika njia ya chini ya ardhi jijini New York

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takriban watu 13 wamepigwa risasi katika kituo cha treni ya chini ya ardhi jijini New York.

    Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, risasi zilifyatuliwa katika kituo cha 36th Street katika Sunset Park karibu 0830 saa za ndani (1330 GMT) Jumanne asubuhi.

    Picha kutoka eneo la tukio zinaonyesha abiria waliokuwa wamevuja damu wakiwa wamelala kwenye sakafu ya kituo. Vifaa vya vilipuzi ambavyo havijatengenezwa pia vilipatikana kwenye eneo la tukio.

    Mtu anayeshukiwa kuwa na silaha bado yuko huru.

    Akitajwa kama mwanamume aliyevalia fulana ya rangi ya chungwa na ikiwezekana akiwa amevalia barakoa ya gesi, inaaminika alitoroka eneo la tukio. Nia ya vitendo vyake bado haijatambuliwa .

    Msemaji wa Meya wa Jiji la New York Eric Adams alitoa wito kwa wakazi wa New York "kukaa mbali na eneo hili kwa usalama wao’

  3. Habari za hivi punde, Johnson na Sunak kutozwa faini kwa karamu za wakati wa vizuizi vya Covid

    th

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri Mkuu Boris Johnson na Kansela Rishi Sunak watatozwa faini na polisi kwa kuhudhuria sherehe wakati wa sheria za kupambana na janga la Covid .

    Polisi wa Metropolitan wamekuwa wakichunguza mikusanyiko 12 katika Downing Street na Whitehall inayodaiwa kuvunja sheria za Covid.

    Kufikia sasa, jumla ya faini zaidi ya 50 zimetolewa kwa uvunjaji wa sheria za Covid katika majengo ya serikali.

  4. Uingereza inachunguza madai ya Urusi kutumia silaha za kemikali Ukraine

    Mariupol has been virtually wiped out by weeks of heavy Russian bombardment

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kumekuwa na "ripoti kwamba vikosi vya Urusi huenda vilitumia silaha za kemikali katika shambulio dhidi ya watu wa Mariupol", Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Liz Truss ameandika kwenye Twitter.

    "Tunafanya kazi na washirika kwa haraka ili kuthibitisha madai hayo. Matumizi yoyote ya silaha kama hizo itakuwa ni ongezeko la kutojali katika mzozo huu na tutamwajibisha [Rais wa Urusi Vladimir] Putin na serikali yake," Truss alionya.

    Haya yanajiri muda mfupi baada ya wapiganaji wa kikosi cha Azov cha Ukraine kinacholinda Mariupol kusema kwamba wanajeshi wa Urusi "walitumia sumu isiyojulikana asili yake dhidi ya vikosi vya Ukraine na raia" katika mji huo wa bandari uliozingirwa kusini mwa nchi.

    Haikutoa ushahidi wa kuthibitisha madai yake.

    Petro Andryuschenko, msaidizi wa meya wa Mariupol, aliandika kwenye mtandao wake waTelegram kwamba ripoti kuhusu shambulio la kemikali hazijathibitishwa na kwamba alitarajia kutoa ufafanuzi baadaye.

    Pentagon ilisema Marekani inafahamu "ripoti za mitandao ya kijamii" kuhusu madai ya vikosi vya Urusi kutumia silaha za kemikali huko Mariupol, lakini ikasema hilo haijathibitishwa.

    Msemaji wa idara ya ulinzi ya Marekani John Kirby alisema: "Hatuwezi kuthibitisha kwa sasa na tutaendelea kufuatilia kwa karibu hali ilivyo."

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aligusia suala hili katika hotuba yake ya video usiku wa Jumatatu.

    Soma zaidi:

  5. Vikosi vya Urusi vinafanya kazi kwa ujasiri na ufanisi mkubwa- Putin

    Urusi imepeleka maelfu ya wanajeshi nchini Ukraine katika kile inachoita "oparesheni yake maalum"

    Chanzo cha picha, Sputnik/Mikhail Klimentyev/Kremlin

    Maelezo ya picha, Urusi imepeleka maelfu ya wanajeshi nchini Ukraine katika kile inachoita "oparesheni yake maalum"

    Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema vikosi vyake vinavyoendesha oparesheni ya kijeshi nchini Ukraine vimekuwa vikifanya kazi kwa ushujaa, ufanisi na kutumia silaha za kisasa zaidi.

    Katika mwonekano wa nadra wa umma Bw. Putin alisema Urusi "hatukuwa na chaguo lingine" ila kuanzisha oparesheni ya kijeshi nchini Ukraine ili kujilinda, na vikosi vyake vitafikia lengo hilo, kulingana na shirika la habari la Interfax.

    "Hivi ndivyo itakavyokuwa. Hakuna shaka juu yake. Malengo yako wazi kabisa, na ni mazuri," Putin alisema katika hotuba aliyotoa kwenye kituo cha anga cha Vostochny katika hafla iliyoangaziwa kuadhimisha Siku ya Wanaanga ya Urusi.

    "Lengo kuu ni kusaidia watu huko Donbas," alisema.

    Alipoanzisha uvamizi wa Urusi mwezi Februari, Putin alisema lengo lake lilikuwa "kuondoa Majeshi na Wanazi nchini Ukraine" lakini tangu wakati huo amebadilisha lengo kuu la kijeshi kuwa "ukombozi wa Donbas".

    Mara kwa mara ametoa shutuma zisizo na msingi kwamba Ukraine imefanya mauaji ya kimbari mashariki na ametumia hii kama uhalali wa mashambulizi ya Urusi.

  6. Ethiopia yaondoa marufuku dhidi ya Boeing 737 Max baada ya ajali ya 2019

    Abiria na wafanyakazi wote waliokuwa kwenye ndege hiyo walifariki dunia

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Abiria na wafanyakazi wote waliokuwa kwenye ndege hiyo walifariki dunia

    Ethiopia imeruhusu ndege za Boeing 737 Max kurudi kwenye anga yake, mamlaka ya usafiri wa anga imesema, miaka mitatu baada ya moja ya ndege yake kuanguka muda mfupi baada ya kuanza safari kutoka mji kuu, Addis Ababa.

    Abiria wote 149 na wafanyakazi wanane waliokuwa kwenye ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kutoka mji mkuu wa Ethiopia kuelekea Nairobi nchini Kenya walifariki dunia.

    Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Ethiopia (ECAA) ilisema kuwa iliondoa marufuku hiyo baada ya kuridhishwa na maboresho katika muundo wa ndege na mpango wa mafunzo ya marubani wa mashirika ya ndege.

    Utawala wa Usafiri wa Anga wa Marekani (FAA) uliidhinisha ndege hizo kuanza tena safari zake mnamo Novemba 2020, lakini ikaamuru mafunzo ya lazima ya marubani na urekebishaji wa kompyuta ya angani.

  7. Zelensky aomba kuhutubia AU kuhusu uvamizi wa Urusi

    Zelensky

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewasiliana na Umoja wa Afrika (AU) ili kuunga mkono uvamizi wa Urusi na kuomba kulihutubia shirika la bara hilo.

    Bw Zelensky alimpigia simu Rais wa Senegal Macky Sall siku ya Jumatatu na mazungumzo yao yaligusia taarifa ya AU mwezi Februari iliyotaka kusitishwa mara moja kwa mapigano na kurejelewa kwa mazungumzo.

    Mataifa ya Afrika yameonyesha kutokuwa na umoja katika kukabiliana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

    Senegal ilikuwa miongoni mwa nchi 17 za Kiafrika ambazo hazikupiga kura katika Umoja wa Mataifa kuhusu azimio la kutaka Urusi ikomeshe operesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine.

    Katika mazungumzo hayo ya simu, Bw Zelensky alimfahamisha Bw Sall kuhusu "mapambano ya Ukraine dhidi ya uvamizi na uhalifu wa kutisha wa mchokozi wa Urusi", kulingana na ujumbe wa Twitter.

    Ruka X ujumbe, 1
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe, 1

    Bw Sall, rais wa sasa wa AU, alithibitisha mazungumzo hayo na ombi la Bw Zelensky kuhutubia Umoja wa Afrika.

    Ruka X ujumbe, 2
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe, 2

  8. Tembo amuua mtafiti wa Colombia nchini Uganda

    Temboo

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mtafiti kutoka Colombia amefariki dunia baada ya kukanyagwa na tembo katika mbuga ya wanyama ya Kibale nchini Uganda.

    Ramirez Amaya Sebastian, ambaye anahudumu katika chuo kikuu nchini Marekani, alikuwa akifanya utafiti wa kawaida akiwa na msaidizi wakati tukio hilo lilipotokea, kulingana na Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda (UWA).

    "Walikutana na tembo mmoja ambaye aliwashambulia na kuwalazimisha wawili hao kukimbia pande tofauti.

    Tembo alimfuata Sebastian na kumkanyaga na kusababisha kifo chake,” msemaji wa UWA Bashir Hangi alinukuliwa akisema.

    Shambulio hilo la tembo huko Kibale lilikuwa la kwanza katika mbuga hiyo katika miaka 50, UWA ilisema.

    Mnamo Januari, mtalii mmoja wa Saudia aliuawa na tembo katika bustani ya Murchison Falls, mbuga nyingine nchini humo, alipoacha gari alilokuwa akisafiria na marafiki zake.

  9. Mahakama ya DRC yabatilisha kifungo cha msaidizi wa rais

    Mshirika mkuu wa serikali ya rais Felix Tshisekedi nchini DR Congo Vital Kamerhe

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Mshirika mkuu wa serikali ya rais Felix Tshisekedi nchini DR Congo Vital Kamerhe

    Mahakama ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imebatilisha kifungo cha miaka 13 jela kwa aliyekuwa mkuu wa wafanyakazi wa Rais Felix Tshisekedi, Vital Kamerhe, ambaye alipatikana na hatia ya matumizi mabaya ya fedha, tovuti binafsi ya Radio Okapi imeripoti.

    Mahakama ya Cassation ilisema hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Rufaa ya Kinshasa/Gombe "ilitiwa dosari za kiutaratibu".

    ''Mahakama ya Uchunguzi iligundua kuwa Mahakama ya Rufaa ya Kinshasa/Gombe ilikiuka Kifungu cha 104 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kwa kuchunguza kesi hiyo wakati haikuwa sawa,” ilisema Radio Okapi.

    Kamerhe alikuwa amepinga muundo wa mahakama na tayari alikuwa amewasilisha kesi hiyo kwa Mahakama ya Kikatiba, kwa mujibu wa tovuti.

  10. Mtoto wa Museveni Jenerali Muhoozi Kainerugaba afunga akaunti yake ya Twitter

    Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Uganda, Lt Jenerali Muhoozi Kainerugaba
    Maelezo ya picha, Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Uganda, Lutenit Jenerali Muhoozi Kainerugaba

    Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu la Uganda, Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mtoto wa rais Yoweri Museveni amefunga akaunti yake ya Twitter.

    Msemaji wake, Maj. Chris Magezi amethibitisha hilo na kuongeza kuwa Muhoozi alichukua uamuzi wa kufunga akaunti yake ya Twitter kwa sababu za kibinafsi.

    Hatua hiyo hata hivyo imezua gumzo katika mitandao ya kijamii huku baadhi ya tovuti zikidai kuwa Jenerali Muhoozi alifungiwa na Twitter.

    Anasemekana kuwa mrithi wa baba yake ambaye amekuwa uongozini tangu mwaka wa 1986 na ni mtumiaji mahiri wa Twitter.

    Soma zaidi:

  11. Vita vya Ukraine: EU yaelekea Nigeria kwa usambazaji zaidi wa gesi

    Nigeria

    Chanzo cha picha, NNPC

    Umoja wa Ulaya unaimarisha uhusiano na Nigeria huku ukijaribu kubadilisha vyanzo mbalimbali vya uagizaji wa gesi asilia katika jaribio la kupunguza utegemezi wa nishati ya Urusi.

    Nigeria ni muuzaji mkuu wa nne wa gesi asilia iliyosafishwa barani Ulaya. Angalau 40% ya gesi ya Nigeria kwa sasa inauzwa Ulaya.

    EU inataka kupunguza matumizi ya gesi ya Urusi ili kukabiliana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine

    Wanadiplomasia hao walitembelea kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali ya Nigeria siku ya Jumatatu kwa mikutano ya kuongeza ushirikiano katika sekta ya nishati

    "Sisi sio tu wateja wakuu wa Nigeria, sisi pia ni washirika wakuu katika sekta ya mafuta na gesi kwa sababu baadhi ya makampuni ambayo yanafanya kazi nanyi yanatoka Ulaya. Kwa hivyo tunashiriki maslahi sawa na malengo sawa," Balozi wa EU nchini Nigeria Samuela Isopi alisema.

    Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kitaifa la Petroli la Nigeria (NNPC) alihakikishia wajumbe wa Ulaya kwamba kampuni hiyo ina nia ya kuongeza usambazaji wa gesi kwenye soko la kimataifa.

    Mamlaka ya Nigeria inasema kuwa nchi hiyo ina hifadhi ya gesi asilia iliyothibitishwa ya futi za ujazo trilioni 209.5 (TCF) kufikia Januari 2022.

    Mapato kutoka kwa mafuta na gesi yanachukua takriban theluthi mbili ya ufadhili wa Nigeria.

    Soma zaididi:

    • Mzozo Ukraine: Je dunia inategemea vipi mafuta na gesi ya Urusi?
    • Mzozo wa Ukraine na Afrika: Athari kwa mafuta,wanafunzi na mkate
    • Ukraine na Urusi: Bidhaa ambazo zitaguswa na jinsi Afrika itakavyoathirika
  12. Vita vya Ukraine: Warusi 'waliacha mabomu kila mahali' - Zelensky

    Zelensky

    Chanzo cha picha, handou

    Urusi inaendelea kutengwa na jumuiya ya kimataifa, Rais wa Ukraine Volodymr Zelensky amesema katika hotuba yake ya usiku wa kuamkia leo kwenye Facebook, akiongeza kuwa "uvamizi huo unaifanya [Urusi] kuwa na sumu zaidi kila siku".

    Zelensky ameonya kwamba "makumi ikiwa sio mamia kwa maelfu" ya mabomu hatari yameachwa nyuma na Urusi wakati ikijondoa maeneo ya karibu na mji mkuu.

    "Wavamizi waliacha vilipuzi kila mahali. Katika nyumba walizotumia kuzuilia watu. Barabarani na mashambani. Walipora mali za watu, magari na milango," anasema.

    Alionya kuhusu ripoti kwamba Urusi inaweza kuwa na mpango wa kupeleka silaha za kemikali nchini Ukraine, akiongeza kwamba wanachukulia uwezekano huo "kwa uzito iwezekanavyo" na kutoa wito kwa Waukraine kuimarisha azma yao.

    "Kipaumbele chetu leo ​​na kila siku kwa wakati huu ni hatua madhubuti za kujihami," aliwaambia raia wa Ukraine.

    Anasema kwamba wanajeshi wa Ukraine ni "jasiri" kuliko vikosi vya Urusi, na "wanawashinda wavamizi kwa hekima na mbinu zilizotathminiwa vyema".

    Lakini anasema Ukraine bado inawategemea washirika wake wa kimataifa kwa ajili ya silaha, na haina vifaa vinavyohitajika"kukomboa Mariupol".

    Urusi yaishambulia Ukraine:Mengi zaidi

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  13. Takriban watu 30 wauawa katika mashambulizi DRC

    Jeshi

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takriban watu 30 wameuawa katika siku mbili za mashambulizi ya watu wenye silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Shirika la Msalaba Mwekundu limesema.

    Ilitokea katika jimbo la Ituri, ambalo pamoja na jirani ya Kivu Kaskazini, wako chini ya hali rasmi ya kuzingirwa katika juhudi za serikali kukomesha mashambulizi ya makumi ya makundi yenye silaha.

    Mashambulizi hayo yanakisiwa kutekelezwa na Allied Democratic Front (ADF), mojawapo ya makundi mabaya zaidi ya waasi wanaoendesha shughuli zao katika eneo hilo.

    Walifanya vitendo vya kikatili - baadhi ya waathiriwa walikutwa wakiwa wamefungwa - wengine walikuwa wamekatwa koo.

    Nyumba zilichomwa na mali kuporwa. Mwezi Disemba, zaidi ya wanajeshi 1,000 wa Uganda walivuka na kuingia DR Congo kwa kile kilichokusudiwa kuwa operesheni ya pamoja ya kijeshi kuwashinda ADF.

    Lakini licha ya kuahidiwa maendeleo, kundi hilo limeendelea kufanya mashambulizi ya mara kwa mara kwa jamii zilizo hatarini.

    Huko Kivu Kaskazini, kundi lingine la waasi linaloitwa M23 hivi karibuni limeanzisha upya uasi unaoviteka vijiji vinavyoongeza mzozo wa usalama.

  14. Wapenzi wa muziki wa injili Afrika wamuomboleza Osinachi

    Osinachi

    Chanzo cha picha, Osinachi Nwachukwu Singing Ministry Int’l/Facebook

    Kumekuwa na hisia kali baada ya taarifa za kifo cha mwimbaji wa nyimbo za Injili kutoka Nigeria Osinachi Nwachukwu.

    Ripoti za awali zilisema kuwa mwanadada huyo mwenye umri wa miaka 42 alikuwa anaugua saratani ya koo, lakini familia yake inakanusha hilo, kwa madai kuwa alikuwa mwathirika wa unyanyasaji wa nyumbani.

    Mumewe Peter Nwachukwu amekamatwa na polisi, na bado hajazungumza lolote.

    “Pumzika kwa amani mwana wa Mungu, nilipenda jinsi alivyomwabudu Mungu,” alisema shabiki wa Afrika Kusini, Hilda Motswatswa.

    Abel Phanuel akiwa Lagos aliandika: "Moyo wangu uko pamoja na familia yake katika nyakati hizi za majaribu. #SemaNoToDomesticViolence."

    "Kwa kweli alitoa moyo wake katika wimbo wa Ekuweme," alisema Caren Akoth, "labda ilikuwa njia yake ya kuelezea huzuni zake".

    Na huko Liberia, David Jacque Tarpeh aliandika: "Huu ni wakati wa wanawake wote wa Nigeria kukusanyika pamoja na kudai haki kwa kufanya maandamano ya amani".

    Ruka X ujumbe
    Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

    Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

    Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya nje

    Mwisho wa X ujumbe

  15. Hujambo na karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja