Baharia wa Ukraine huko Majorca akamatwa kwa kujaribu kuizamisha boti inayomilikiwa na bosi Mrusi kulipiza kisasi
Mbaharia mmoja wa Ukraine amekiri kujaribu kuizamisha boti inayomilikiwa na mkuu wa kampuni ya silaha ya serikali ya Urusi, kwa lengo la kulipiza kisasi kwa uvamizi wa Ukraine.
Boti hiyo yenye urefu wa mita 48 sawa na futi 157 inayoitwa Lady Anastasia, inayomilikiwa na mkurugenzi mkuu wa Rosoboronexport Alexander Mikheev, ilikuwa imetia nanga huko Majorca nchini Hispania wakati baharia huyo mtaalamu wa ufundi alipofungua ‘valves’ katika chumba chake cha injini.
Alikamatwa na maafisa wa ulinzi wa raia siku ya Jumamosi na baadaye kuachiliwa kwa dhamana.
Alimwambia jaji kwamba hajutii chochote na angeweza kufanya hivyo tena.
Mtu huyo alisema alijaribu kuizamisha boti hiyo ya Bwana Mikheev baada ya kutazama taarifa za habari kutoka Ukraine kwenye televisheni.
"Kulikuwa na video ya shambulio la helikopta katika jengo moja mjini Kyiv," alinukuliwa na vyombo vya habari nchini humo.
"Walikuwa wakishambulia watu wasio na hatia."
Siku ya Jumamosi, jengo la ghorofa ya juu karibu na uwanja wa ndege wa Zhuliany wa Kyiv lilipigwa na kombora, na kuacha shimo linalofunika angalau ghorofa tano.
Hakukuwa na maoni ya haraka kutoka kwa Bwana Mikheev au Rosoboronexport, ambayo husafirisha bidhaa za ulinzi za Urusi, ikiwa ni pamoja na mizinga, magari ya kivita, ndege, meli, silaha na risasi.