"Vita dhidi ya nchi yangu"
Balozi wa Umoja wa Mataifa wa Ukraine Sergiy Kyslytsya anasema mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa Urusi amethibitisha kwamba rais wake ametangaza "vita dhidi ya nchi yangu", laripoti shirika la habari la Reuters.
Wizara ya mambo ya ndani ya Ukraine inaiambia CNN: "Uvamizi umeanza."
Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni kwa watu wa Urusi Alhamisi asubuhi, Rais wa Urusi Vladimir Putin alisema nchi yake "haina mpango" wa kuikalia kwa mabavu Ukraine.
Katika hotuba yake akitangaza "operesheni maalum ya kijeshi", Putin alisema kuwa watu wa Ukraine wataweza "kuchagua kwa uhuru" ambaye anaendesha nchi.
Shirika la habari la Reuters linamnukuu shahidi aliyesikia mlipuko katika mkoa wa Belgorod kusini-magharibi mwa Urusi, ambao hauko mbali na mpaka wa Ukraine.
Tunasikia ripoti - baadhi ambazo hazijathibitishwa - za milipuko katika maeneo mengine ya Ukraine.
Waandishi wa BBC hapo awali walithibitisha kusikia kishindo kikubwa katika mji mkuu wa Kyiv, pamoja na Kramatorsk katika eneo la Donetsk.
Lakini pia kumekuwa na ripoti kwenye mitandao ya kijamii za milipuko huko Kharkiv kaskazini-mashariki, Odesa kusini, na eneo la Mashariki ya Donetsk Oblast.