Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Milipuko Uganda: Sita wauawa wakiwemo washambuliaji watatu

Mmoja ulitokea karibu na kituo kikuu cha polisi ambacho pia kiko karibu na bunge.

Moja kwa moja

Ambia Hirsi

  1. Aung San Suu Kyi anatunzwa vyema: Jeshi Myanmar

    Jeshi la Myanmar limeambia BBC kwamba mamlaka haimtelekezi kiongozi aliyeondolewa madarakani Aung San Suu Kyi.

    Kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 76- hajaonekana hadharani tangu mapinduzi ya kijeshi ya Februari yaliyomuondoa mamlakani .

    Mahojiano ya BBC na msemaji wa jeshi Meja Jenerali Zaw Min Tun yanakuja baada ya kuachiliwa kwa mwanahabari wa Marekani Danny Fenster ambaye alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 11 gerezani.

    Makumi ya wanahabari na maelfu ya watu wamezuiliwa tangu mapinduzi hayo yalipofanyika.

    Meja Jenerali Zaw Min Tun amesema Bi. Suu Kyi anatunzwa vizuri kizuizini.

    "Namaanisha tulimuacha aishi na watu wake kwenye nyumba ingawa yuko chini ya kizuizi cha nyumbani," alisema. "Tunajaribu tuwezavyo kwa ajili yake, kile anachotaka au chochote anachotaka kula.

    Bi Suu Kyi ameshtakiwa kwa kuvunja sheria rasmi ya siri ya enzi ya ukoloni. Pia anakabiliwa na mashtaka ya ufisadi na kumiliki mazungumzo haramu.

    Siku ya Jumanne, vyombo vya habari vya serikali viliripoti kwamba alikuwa anakabiliwa na shtaka la ziada: udanganyifu katika uchaguzi, unaohusiana na uchaguzi wa 2020 ambapo chama chake kilishinda kwa kishindo.

    Amefikishwa mahakamani lakini hajatoa tamko lolote kando na maonyesho hayo mafupi.

    Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kuachiliwa kwake.

  2. Kenya yatangaza zawadi kwa habari za kukamatwa kwa wafungwa 'hatari' waliotoroka jela

    Mamlaka nchini Kenya imetangaza zawadi kwa atakayetoa taarifa zitakazosaidai kukamatwa kwa wafungwa "hatari" waliotoroka jela walimokuwa wakishikiliwa kwa tuhuma zinazohusiana na ugaidi.

    Watatu hao ni Mohamed Ali Abikar, Musharaf Abdalla,na Joseph Juma Odhiambo.

    Mmoja wao, Abikar alihusika katika shambulio la Chuo Kikuu cha Garissa April 2, 2015 ambalo lilisababisha vifo vya zaidi ya wanafunzi 100.

    Abdalla alikuwa anazuiliwa kuhusiana na shambulio lililofeli katika bunge la Kenya na Odhiambo alikuwa amekamatwa kwa kuwasajili vijana katika kundi la wanamgambo wa al-Shabab, ilani iliyotolewa na polisi ilisema.

    Wafungwa hao walitoroka kutoka kwa Gereza Kuu la Kamiti viungani mwa mji mkuu, Nairobi, Jumatatu saa 01:00 kwa saa za huko.

    Polisi wanatoa zawadi ya shilingi milioni 60 za Kenya sawa na ($535,000:£398,000) kwa habari zitakazowezesha kukamatwa kwa wote watatu.

    Kenya imewahi kukumbwa na mashambulizi ya kigaidi yaliyopangwa na kutekelezwa na wanamgambo wa al-Shabab.

  3. Mazungumzo ya Biden-Xi: Viongozi wahitimisha mkutano kwanza kupitia mtandaoni

    Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa China Xi Jinping wamehitimisha mkutano wao wa kwanza wa ana kwa ana wa mtandaoni, vyombo vya habari vya serikali ya China vilisema.

    Mkutano huo ulikuja huku mvutano ukiongezeka kati ya nchi hizo mbili kuhusu masuala kama vile Taiwan, biashara na haki za binadamu.

    Bw Biden alisema nchi zote mbili zina jukumu la kuhakikisha kuwa ushindani wao "hauendi kwenye mzozo wa wazi".

    Mazungumzo ya Jumanne ndio majadiliano muhimu zaidi ambayo viongozi wote wawili wamekuwa nayo tangu Bw Biden aingie madarakani Januari.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Hua Chunying aliuelezea mkutano huo kuwa "wenye kujenga na wenye tija", na kuongeza kuwa ulisaidia "kuongeza maelewano".

    Mkutano huo ulianza kwa viongozi wote wawili kusalimiana kwa furaha, huku Bw Xi akisema anafurahi kumuona "rafiki yake wa zamani" Biden.

    Kwa upande wake, Bw Biden alisema, "Labda nianze rasmi zaidi, ingawa mimi na wewe hatujawahi kuwa rasmi .." kulingana na ripoti ya Reuters.

  4. Genge linalotumia pikipiki lawaua watu 15 nchini Nigeria

    Watu waliokuwa wakiendesha pikipiki wamewaua kwa risasi raia 15 na kuwajeruhi wengine wengi katika jimbo la Sokoto, kaskazini magharibi mwa Nigeria.

    Mauaji hayo yametokea alfajiri ya Jumatatu.

    Gavana wa jimbo hilo, Aminu Tambuwal, ambaye alithibitisha mashambulizi hayo katika taarifa yake, alisema wahasiriwa 13 waliuawa katika mji wa Illela kwenye mpaka na Niger

    Wengine wawili waliuawa katika shambulio tofauti huko Goronyo - mji ambapo watu wenye silaha walifanya shambulio kubwa mwezi uliopita, na kuua zaidi ya watu 40 sokoni.

    Ripoti zilionyesha kuwa wakaazi wengi wamekimbia kutoka kwa nyumba zao kufuatia mashambulio ya hivi punde.

    Jimbo hilo linakabiliwa na wimbi la mauaji na utekaji nyara kwa ajili ya kulipwa fidia na magenge yenye silaha, ambayo yanaendelea licha ya kutumwa kwa maelfu ya vikosi vya usalama.

    Mwishoni mwa juma, wanamgambo wenye uhusiano na kundi linalojiita Islamic State waliwaua wanachama kadhaa wa vikosi vya usalama vya Nigeria akiwemo jenerali wa jeshi katika shambulizi la kuvizia katika jimbo la Borno.

  5. Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja hii leo Jumanne tarehe 16 Novemba 2021