Wanawake Afghan kupata haki chini ya sheria ya Kiislam, Taliban imesema
Haki za wanawake nchini Afghanistan zitaheshimiwa "kulingana na mfumo wa sheria za Kiislamu", Taliban wamesema.
Katika mkutano wa kwanza na waandishi wa habari tangu Taliban walipochukua udhibiti wa nchi ya Afghanistan Jumapili, msemaji alisema wanawake watakuwa huru kufanya kazi lakini akatoa maelezo kidogo juu ya sheria na masharti mengine.
Msemaji wa kundi hilo Zabihullah Mujahid alirudia kwamba Waafghan wote lazima waishi "katika mfumo wa Uislamu".
Hata hivyo, vikundi vya kutetea haki vinahofia uhuru wa wanawake unaweza kukadamizwa tena chini ya Taliban.
Kundi hilo la wapiganaji lilianzisha au kuunga mkono adhabu kulingana na tafsiri yao kali ya mfumo wa sheria ya Kiislam, yaani Sharia, wakati walipodhibiti Afghanistan kati ya 1996 na 2001.
Wanawake walilazimika kuvaa burka inayofunika kila mahali, na Taliban pia hawakukubali wasichana wenye umri wa miaka 10 na kuendelea kwenda shule.
Katika mkutano huo na wanahabari Jumanne, Bw. Mujahid alijibu maswali kadhaa kutoka kwa wanahabari wa kimataifa juu ya haki za wanawake chini ya serikali ya Taliban.
"Tutaruhusu wanawake kufanya kazi na kusoma ndani ya mifumo yetu", alisema.
"Wanawake watakuwa wachangamfu sana katika jamii yetu".
Lakini hakufafanua alipoulizwa juu ya kanuni za mavazi na ni majukumu gani wanawake wataweza kuwa nayo ndani ya nguvukazi ya nchi.
Mapema Jumanne, Taliban ilitangaza msamaha wa jumla kote Afghanistan na kusema kwamba inataka wanawake wajiunge na serikali yake.
Wachambuzi wanasema kikundi hicho kinaendesha kampeni ya kisasa ya kuonesha uhusiano na umma katika juhudi za kutaka kuungwa mkono kwa dhati na Waafghan na jamii ya kimataifa.
Ujumbe wa watawala wapya umepokelewa kwa hisia tofauti ndani ya Afghanistan.
"Siamini wanachosema", mwanamke huko Kabul ambaye alimtazama Mujahid akizungumza kwenye televisheni aliambia BBC.
"Ni ujanja na tunavutwa nje kuadhibiwa. Ninakataa kusoma au kufanya kazi chini ya sheria zao", alisema mwingine.
Hata hivyo, wengine waliona ahadi za mapema.
Ikiwa tunaweza kufanya kazi na kupata elimu, huo ndio ufafanuzi wa uhuru kwangu. Na mstari huo haujavukwa na Taliban bado", mwanamke mmoja wa Afghanistan alisema.
"Maadamu haki yangu ya kusoma na kufanya kazi inalindwa, sijali kuvaa hijabu. Ninaishi katika nchi ya Kiislamu na niko tayari kukubali kanuni ya mavazi ya Kiislamu - maadamu sio lazima vazi la burqa kwasababu hiyo sio kanuni ya mavazi ya Kiislamu."