Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Chadema yamjibu Rais Samia, yasema amepotoshwa

Chama cha upinzani nchini Tanzania Chadema, kimesema rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan “aidha amepotoshwa au ameamua kusema uongo” katika baadhi ya mambo ambayo ameyatolea ufafanuzi katika mahojiano yake maalumu aliyofanya na BBC

Moja kwa moja

  1. Tumefika tamati ya taarifa zetu za moja kwa moja, mpaka kesho panapo majaaliwa

  2. Kipindupindu chaua watu 800 Nigeria

    Mlipuko wa kipindupindu nchini Nigeria umeua zaidi ya watu 800 katika miezi michache iliyopita, Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Nigeria kinasema.

    Waathiriwa wengi ni watoto, na vijidudu vinaendelea kuenea - na zaidi ya maambukizi ya watu 31,000 tangu Januari, lakini wengi wao ni wale waliorekodiwa mwezi uliopita.

    Mlipuko huo umeathiri takribani majimbo 22 kati ya majimbo 36 ya Nigeria, ukiwemo mji mkuu, Abuja.

    Kulingana na NCDC, kaskazini mwa nchi hiyo kumeathirika zaidi.

    Mfumo dhaifu wa huduma ya afya nchini Nigeria umekuwa ukipambana kukabiliana mlipuko huo - madaktari katika hospitali za umma wanagoma na idadi ya maambukizi ya Covid-19 inaongezeka.

    Mafuriko mabaya katika maeneo mengine pia yamefanya mambo kuwa mabaya zaidi.

    NCDC inasema imesambaza timu za matibibu kusaidia majimbo kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa kipindupindu.

    Lakini inasema serikali na umma lazima usafi uwe kipaumbele,usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji salama ya kunywa kama sehemu ya suluhisho la muda mrefu.

    Dalili za ugonjwa huo unaoambukiza ni pamoja na kutapika, kuharisha na kupungukiwa maji mwilini. unaweza kuua ndani ya saa chache kama matibabu hayatapatikana.

    • Kesi ya rushwa ya Zuma yaahirishwa kwa sababu za kiafya

      Kesi ya ufisadi ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma - ambayo ilikuwa inapaswa kuanza tena Jumanne - imeahirishwa kwa sababu za kiafya.

      Timu yake ya wanasheria iliomba kuahirishwa kwa kesi baada ya kiongozi huyo mwenye miaka 79 kulazwa hospitalini Ijumaa lakini haikuelezwa alikuwa akisumbuliwa na nini

      Kesi hiyo inahusisha mkataba wa silaha wa dola bilioni 5 miaka ya 1990.

      Zuma, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha miezi 15 kwa kudharau mahakama katika kesi tofauti, atatarajiwa kuwasilisha ushahidi kwa mahakama kuhusu ugonjwa wake.

      Timu ya kitabibu ya rais wa zamani imepewa hadi tarehe 20 mwezi Agosti kuwasilisha ripoti mahakamani.

      Serikali pia itamteua daktari wa kujitegemea kuchunguza kama yuko na afya njema kusimama mahakamani.

    • Msumbiji yatarajia kufunguliwa tena kwa miradi ya gesi

      Operesheni ya kijeshi dhidi ya vikundi vyenye silaha katika mkoa wa kaskazini mwa Cabo Delgado wa Msumbiji ni "hatua muhimu sana" kwa kuanza tena kwa miradi ya gesi asilia, waziri wa Msumbiji anasema.

      Utulivu ulikuwa muhimu ili kurudisha shughuli katika mkoa huo ambazo zilikatizwa na mashambulio ya wapiganaji wa jihadi, Waziri wa Nishati Max Tonela alisema.

      Mwezi Aprili, kampuni ya nishati ya nchini Ufaransa, Total ilisitisha mradi wake wa gesi asilia wa thamani ya pauni bilioni 14.6 kaskazini mwa Msumbiji- mradi mkubwa wa uwekezaji barani Afrika-kwasababu ya mashambulizi katika eneo hilo.

      Moja kati ya masharti yaliyowekwa na Total ni kurejeshwa kwa usalama katika eneo la mradi katika bonde la Rovuma, waziri ameeleza.

      Jumapili, jeshi lilithibitisha kudhibitiwa kwa mji muhimu wa bandari wa Mocimboa da Praia na vikosi vya Msumbiji na Rwanda.

      Rwanda ilituma kikosi cha wanajeshi nchini Msumbiji mwezi uliopita kusaidia katika vita dhidi ya vikundi vyenye silaha huko Cabo Delgado chini ya makubaliano ya nchi hizo mbili.

      Jumuiya ya kusini mwa Afrika, Sadc, ilizindua rasmi ujumbe wake wa kijeshi kupambana na "ugaidi na msimamo mkali wa vurugu" kaskazini mwa Msumbiji Jumatatu.

    • Chadema yamjibu rasmi Rais Samia, yasema rais amepotoshwa

        • Author, Aboubakar Famau
        • Nafasi, BBC News, Dodoma

      Chama cha upinzani nchini Tanzania Chadema, kimesema rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan “aidha amepotoshwa au ameamua kusema uongo” katika baadhi ya mambo ambayo ameyatolea ufafanuzi katika mahojiano yake maalumu aliyofanya na BBC.

      Kauli hiyo, imetolewa hii leo na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika pindi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

      Mnyika, amepinga baadhi ya hoja zilizotolewa a rais Samia ikiwemo zile zinazodai kwamba, Mbowe kwa muda mrefu alikuwa nje ya nchi baada ya kujua ana kesi inayomkabili, hivyo kusema, “hakuna wakati ambao kiongozi huyo ametoroka nchi au amekuwa nje ya nchi kinyume cha sheria.”

      Mnyika ameongeza kusema kuwa, wakati ukifika, “chama kitatoa vielelezo vitakavyoonyesha uhalali wa safari hizo.”

      Hata hivyo, rais Samia alipoulizwa iwapo kesi hiyo ya Mbowe ni ya kisiasa, alikataa kulitolea ufafanuzi wa kina kwa kusema kuwa, tayari kesi hiyo iko mahakamani, hivyo ni vyema kuachia mahakama kufanya kazi yake.

      Lakini tayari Chadema inamlaumu Rais Samia kwa madai kwamba ameingilia uhuru wa mahakama, na kusema, wameongeza na jopo la mawakili wao ili kuona ni hatua gani wanaweza kuchukua.

      Aidha miongoni mwa mambo mengine ambayo Chama hicho kimeyajibu ni pamoja na kauli ya rais aliposema kuna tofauti kati ya demokrasia ya kisiasa na fujo za kisiasa, hivyo kuashiria kwamba, baadhi ya maandamano yanayoitishwa na vyama vya kisiasa kama fujo za kiasa.

      Hata hivyo, kauli hii inaonekana kuwa mwiba kwa chama hicho cha upinzani ambapo Mnyika amesema kupiga marufuku mikutano hiyo ya hadhara ni kinyume cha katiba ya nchi na sheria za vyama vya kisiasa.

      Chadema pia imedai kwamba rais Samia amepotosha umma pale aliposema kwamba, wananchi wamekubali tozo za simu, ila kiwango cha tozo ndio hawajakikubali.

      Nchini Tanzania kumekuwa na maoni tofauti baada ya BBC kufanya mahojiano na rais Samia ambayo yamegusia nyanja mbalimbali ikiwemo masuala ya demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari pamoja na masuala mengine kadhaa.

    • Chanjo lazima kwa watumishi wa Umma nchini Kenya

      Watumishi wa Umma nchini Kenya wamepewa siku 13 kuhakikisha kuwa wanapata chanjo dhidi ya virusi vya corona au kukabiliwa na hatua za kinidhamu.

      Katika taarifa yake, mkuu wa utumishi wa umma alisema agizo hilo limetokana na idadi ndogo ya watumishi waliopata chanjo ya Covid-19 hasa waalimu na wale walio katika sekta ya usalama.

      Baadhi ya watumishi wa Umma kwa makusudi wamekwepa chanjo iliwaendelee kusalia nje ya kazi, hatua ambayo imezorotesha utoaji wa huduma, alisema.

      Jumatatu, Kenya iliripoti maambukizi mapya 745 ya virusi vya corona na kufanya idadi ya maambukizi iliyothibitshwa kufikia 212,573 tangu kuanza kwa janga hilo.

      Wiki iliyopita, serikali ilisema imetoa chanjo milioni 1.7 ya AstraZeneca, nyingi kati ya hizo ni dozi ya kwanza.

      Kenya inalenga kuchanja watu milioni 10 mwishoni mwa mwaka huu.

    • Guinea inathibitisha kisa cha kwanza virusi vya Marburg Afrika Magharibi

      Maofisa wa afya wa Guinea wamethibitisha mgonjwa wa kwanza kutoka Afrika Magharibi mwenye virusi vya Marburg, ugonjwa ambao unaweza kuambukiza sawa na ilivyo Ebola.

      Shirika la afya duniani (WHO) limesema, virusi hivi vinahitajika kuzuiliwa visisambae.

      Virusi vya Marburg vinasambaa kwa watu kutoka kwa popo kwenda kwa binadamu na binadamu wanaambukiza kwa njia ya majimaji ya mwili.

      Kesi za namna hii huwa ni chache, ugonjwa huu ulitokea mara ya mwisho huko Angola mwaka 2005. Unasababisha maumivu, uchovu, homa na kutokwa damu.

      Sampuli iliyochukuliwa kutoka kwa mgonjwa wa Guinea, ambaye amefariki tayari, ilipelekwa katika maabara ya taifa na kurudi na majibu ya virusi vya Marburg.

      Ugonjwa huo umepatikana Guéckédou,eneo ambalo lilikuwa na maambukizi ya Ebola hivi karibuni ingawa sasa yameisha.

      Mkurugenzi wa Shirika la Afya ukanda wa Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema virusi hivyo vimesambaa kwa kiwango kikubwa.

      Lakini amesifia angalizo na uchunguzi wa haraka uliofanywa na wafanyakazi wa afya wa Guinea.

      Jitihada zilizopo ni kubaini watu ambao walihusiana na mwanaume huyo aliyefariki kutokana na virusi vya Marburg.

      Watu wanne ambao walikuwa kwenye hatari zaidi ya maambukizi wameainishwa, wakiwemo wahudumu wa afya.

      Vile vile watu wengine 146 wanaweza kuwa katika hatari ya maambukizi ,mtaalamu Dkt.Krutika Kuppalli, ambaye amekuwa akifuatilia kesi hiyo ameiambia BBC.

      Mfumo ambao hukuepo Guinea na mataifa ya jirani ya namna ya kukabiliana na mlipuko wa Ebola umeanza kutumika tena ili kukabiliana na virusi vya Marburg.

      Barani Afrika, milipuko ya magonjwa ya mara kwa mara imeripotiwa Angola,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Afrika Kusini na Uganda, imesema WHO.

      Zaidi ya watu 200 wamefariki kutokana na virusi vya Marburg, wakati vilipotokea Angola mwaka 2005.

    • Mwanadiplomasia wa Nigeria ashambuliwa Indonesia

      Serikali ya Nigeria imelaani shambulio dhidi ya mmoja wa wanadiplomasia wa wake nchini Indonesia.

      Serikali inasema kuwa imeandika barua ya malalamishi kwa wenzao wa Indonesia kuhusiana na jinsi mwanadiplomasia wake alivyotendewa mjini Jakarta.

      Mwanadiplomasia huyo anayefanya kazi katika ubalozi wa Nigeria nchini Indonesia alionekana katika video iliyosambazwa mitandaoni akitendewa kama mhalifu na maafisa wa uhamiaji wa Indonesia.

      Aliropitiwa kwenda kununua bidhaa katika duka la jumla katika mji huio mkuu wakati alipokamatwa.

      Katika taarifa Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria imesema shambulio dhidi ya mwanadiplomasia huyo “inaenda kinyume na sheria ya kimataifa ya Vienna inayoongoza uhusiano wa kKidiplomasia kati ya nchi mbili”.

      Balozi wa Indonesia nchini Nigeria pia aliitakiwa kutoa ufafanuzi kuhusiana na suala hilo siku ya Jumatatu na inasemekana aliomba msamaha kwa niaba ya serikali yake.

      Mwaka 2015 serikali ya Indonesia iliwaua kwa kuwapiga risasi raia wawili wa Nigeria kwa madai ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

      Wizara ya Mambo ya nje ya Nigeria ilisema mauaji hayo yalitekelezwa licha ya ombi la msamaha la mara kwa mara kutoka kwa serikali, pamoja na bunge.

    • Waasi wa Tigray wakana kuhusika na shambulio baya dhidi ya hospitali jimbo la Afar

      Waasi wa Tigray wamekanusha kuhusika na shambulio kwenye kituo cha afya katika jimbo la Afar huko Ethiopia, ambalo liliwauwa watu wasiopungua 12.

      Utawala wa mkoa wa Afar unalaumu vikosi vya Tigray kwa shambulio hilo, wakati mapigano katika mzozo wa miezi tisa wa Ethiopia ukizidi hadi katika majimbo yanayopakana na Tigray.

      Daktari katika mkoa wa Afar wa Ethiopia aliambia BBC kwamba watu hao 12 walifariki kutokana na majeraha waliyoyapata katika shambulio kali la silaha katika kituo cha afya cha Galikoma.

      Watu zaidi ya 30 wakiwemo wanaume ,wanawake na watoto walihitaji matibabu ya dharura baada ya shambulio hilo .

      Msemaji wa utawala wa jimbo la Afar alisema raia wengi zaidi walifariki katika eneo la tukio lakini hakuweza kutoa idadi rasmi ya vifo.

      Alilaumu vikosi vya Tigray - lakini msemaji wa Tigray People's Liberation Front alisema kwenye Twitter kwamba ripoti za shambulio hilo "ni za kutisha".

      Alikana kuhusika kwa kundi hilo na kusema wako tayari kushirikiana na uchunguzi wowote kubaini ukweli

      Kituo hicho cha afya kilitumika kuwahifadhi watu waliokimbia makazi yao na kuweka msaada wa chakula.

      Wiki iliyopita mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths alizuru Ethiopia na kusema idadi ya wakaazi wa Afar walioachwa bila makao kwa sababu ya mapigano ya hivi karibuni ni 54,000.

    • Mkosoaji wa serikali ya Uganda aliye Uturuki kukabiliwa na mashtaka 15-Polisi

      Polisi nchini Uganda wanasema wana kesi 15 dhidi ya mwanablogu wa Uganda anayeishi Uturuki na mkosoaji wa serikali Fred Lumbuye.

      Hawajatoa maelezo kuhusu kesi hizo

      Bwana Lumbuye, ambaye huandika mengi katika lugha ya Kiganda, anahusishwa na uvumi ulioenea mwezi Juni kuhusu afya ya Rais Yoweri Museveni.

      Rais Museveni baadaye alitoa agizo la kukamatwa kwa watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuchapisha habari potofu na feki

      Wiki iliyopita, maafisa wa serikali ya Uganda walisema kwamba mwanablogu huyo, ambaye ni maarufu kwenye Facebook, alikuwa amekamatwa na atarudishwa nyumbani kukabiliwa na mashtaka.

      Lakini polisi na maafisa wa uhamiaji wameviambia vyombo vya habari kwamba Bw Lumbuye hayuko chini ya ulinzi wao .

      Bwana Lumbuye alikuwa akimkosoa sana Museveni katika kipindi cha kabla ya uchaguzi wa Januari 2021, na alitumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kumfanyia kampeni kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine.

    • R. Kelly: Uteuzi wa wanasheria wa kusikiliza kesi ya dhulma za kingono dhidi ya msanii R.Kelly waanza

      Msanii wa R&B R. Kelly amefika mahakamani mjini New York,huku uteuzi wa wanasheria katika kesi ya dhulma za kingono dhidi yake ukianza.

      Inajiri zaidi ya miaka miwili baada ya msanii huyo kushtakiwa kwa unyanyasaji wa wanawake na wasichana wadogo kwa karibu miongo miwili.

      Mwimbaji huyo aliyeshinda Tuzo ya Grammy anakabiliwa na mashtaka ya unyanasaji wa kingono dhidi ya watoto, ujambazi na rushwa. Amekanusha mashtaka

      Wanasheria wanaotarajiwa kuongoza kesi hiyo wanahojiwa ikiwa wanaweza kuwa na mawazo huru katika kesi hiyo.

      Baada ya majaji kuteuliwa, kesi inatarajiwa kuanza Agost18 na huenda ikaendelea kwa wiki kadhaa.Msanii huyo mwenye umri wa miaka 54 akipatikana na hatia huenda akafungwa jela kwa miongo kadhaa.

      Kesi dhidi yake pia imewasilishwa katika mahakama ya Illinois na Minnesota.

      Alipoulizwa jinsi anavyojihisi,wakili wa Kelly,Deveraux Cannick aliliambia shirika la Habari la AFP: "Ni sawa na Jumatatu nyingine."

      Kelly, mmoja wa wasanii nyota wa miondoko ya R&B miaka ya1990, amekuwa akizuiliwa tangu Julai mwaka 2019.

      Kesi ya New Yorki inamtuhumu mwimbaji huyo–ambaye jina lake halisi ni Robert Kelly –kwa kuongoza kundi la mameneja , walinzi wa kibinafsi na wengine ambao waliwaanda wanawake na wasichana kwa ajili ya kufanya ngono.

      Waendesha mashtaka wanasema wahasiriwa waliteuliwa katika matamasha na maeneo mengine.

      Soma zaidi:

      • R Kelly: Mwanamuziki maarufu wa Marekani ameshitakiwa kwa makosa ya unyanyasaji wa kingono
    • Mwanamuziki maarufu afariki dunia kutokana na Corona siku chache baada ya kujifungua

      Mwimbaji maarufu wa Malaysia amekufa kutokana na Covid-19, siku chache baada ya kujifungua mtoto wa kiume - mtoto wake wa nne.

      Siti Sarah Raisuddin aliyekuwa mja mzito alikuwa amekumbwa na uhaba waoksijeni na aliwekwa kwenye coma ili aweze kujifungua kupitia upasuaji.

      Mtoto aliokolewa, ingawa hakuweza kumshika mwanae.

      Mumewe alisema alimpigia simu ya mwisho ya video kabla ya kifo chake, ambapo machozi yalikuwa yakimtiririka mashavuni mwake.

      "(Ni) kana kwamba alielewa tunachomwambia," mchekeshaji Shuib Sepahtu aliwaambia waandishi wa habari. "Ni kwamba tu itakuwa vigumu sana kwangu kutoa habari kwa watoto wangu watatu juu ya kifo cha mama yao."

      Mbali na mtoto huyo mchanga, wenzi hao wana watoto wakubwa watatu wenye umri wa miaka sita hadi 10.

      Ripoti zinasema kwamba familia nzima ilikuwa imepatikana na Covid-19 mnamo 25 Julai, baada ya kuambukizwa kutoka kwa msaidizi wao wa nyumbani.

      Siku chache baadaye, Siti Sarah alikuwa ameweka video kwenye Instagram ya watoto wake wakilia baada ya kupata vipimo vya Covid.

    • ‘Wakati ukifika nitawatafuta viongozi wa upinzani..njooni tukae’ Rais Samia

      Rais waTanzania Samia Suluhu Hassan amesema yungali ana nia ya kukutana na viongozi wa upinzani nchini humo . Akizungumza na BBCkatika mahijiano ya kipekee ,rais Samia amesemaanataka kukutana na viongozi wa upinzani wakiwa na umoja .

      ‘Nilitaka kukutana nao ,lakini sio wakiwa wamechambuka chambuka.’ Amesema Rais Samia .

      Aliongeza kwamba lengo lake ni kukutana na viongozi hao wakiwa katika baraza lao na tayari uchaguzi wamabaraza umefanyikana kufungua milango ya uwezekano wa mkutano huo .

      ‘Kama wameshajiunda vziuri ,na hizi kamati zao ndogo ndogo zimejiunda vizuri basi nitatafuta siku tuitane tuzungume…hata mimi nataka kuzungumza nao niwaambie mwelekeo wangukwamba sasa tumemaliza uchaguzi twendeni tukajenge nchi’ aliongeza rais Samia .

    • Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja hivi leo Jumanne