Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Polisi Tanzania waonya Chadema kuhusu maandamano na mikusanyiko
Polisi nchini Tanzania wametoa onyo kwa mtu au kikundi cha watu watakaojaribu kuhamasisha mikusanyiko isiyo rasmi au kuandamana kwa namna yoyote.
Moja kwa moja
Ambia Hirsi
Naibu wa rais wa Kenya William Ruto adaiwa kuzuiwa kufanya ziara nchi jirani ya Uganda
Naibu wa rais wa Kenya William Ruto amezeuiwa kufanya ziara ya kibinafsi katika taifa jirani la Uganda
Vyombo vya Habari nchini humo vinaripoti kuwa Ruto alizuiwa kuabiri ndege kwenda Uganda pamoja na washirika wake kadhaa wa kisiasa .
Katibu wake wa Habari David Mugonyi amesema jambo hilo ni geni kwani kwa miaka yote ambayo amehudumu kama naibu wa rais ,Ruto hajawahi kuhitaji idhini ya kusafiri nje ya nchi kutoka kwa mkuu wa utumishi wa umma .
Mugonyi ameiambia BBC kwamba Ruto alilazimika kungoja katika uwanja wa ndege kwa karibu saa tatu kabla ya kuamua kuondoka .
“ Tumeshangazwa kwamba naibu wa rais amenyimwa idhini ya kufanya ziara ya kibinfasi nchini Uganda . Ni maafisa wetu ambao hushughulikiamipango yake ya usafirina waliambiwa kwamba lazima apate idhini kutoka kwa mkuu wa utumishi wa umma ili kusafiri’ Mugonyi amesema
Ingawaje Ruto hajasema lolote moja kwa moja kuhusiana na tukio hilo ,ameandika ujumbe katika twitterakisema ‘Tumuachie Mungu’
Serikali ya Kenya haijatoa tamko lolote kuhusu madai hayo .
Ruto amekuwa akiendelea kufanya kampeni za kumrithi rais Uhuru Kenyatta tangu walipotofautiana kisiasa wakati rais alipoanza ushiriikiano na aliyekuwa Waziri mkuu wa nchi hiyo Raila Odinga kupitia mwafaka wa maridhiano BBI .
Ruto amekuwa akifanya ziara kwenda Uganda kwa mwaliko wa rais Yoweri Museveni bila matatizo yoyote katika uwanja wa ndege.
Olimpiki Tokyo:'Kahawa ndio imenisaidia kushinda dhahabu katika mbio za mita 5000'-Sifan Hassan
Sifan Hassan ameshinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 ikiwa ni mara ya kwanza kwa Sifan Hassan kushiriki na kusema ana kila sababu ya kushukuru kahawa baada ya ushindi huo wa Jumatatu.Mwanamke huyo wa Uholanzi anajinadi kuweka historia katika mbio za mita 1500, 5,000 na 10,000.
Mzaliwa huyo wa Ethiopia, Hassan, 28, alitimka mbio kwa kasi ya juu na kushinda kwa dakika 14 sekunde 36.79, lakini inaonekana alihitaji msaada kidogo akielekea kumaliza.
"Bila kahawa singekuwa bingwa wa Olimpiki", alisema kwa utani.Ratiba iliyokaribiana ya Hassan inamaanisha atakuwa amekimbia katika mbio mara sita za umbali wa wastani au za masafa marefu katika kipindi cha siku nane.Katika mbio za kufuzu za mita 1500 mapema Jumatatu, ilibidi apone haraka baada ya kuanguka punde tu baada ya kengele kupigwa lakini alijinyanyua upesi kutoka nafasi ya 11 aliyokuwa wakati huo na kufuzu katika nafasi ya kwanza.
"Siwezi kuamini. Ilikuwa mbaya wakati nilijikwaa. Wakati nilianguka chini na ikabidi niruke, nilihisi kama nilikuwa nikitumia nguvu nyingi. Sikuamini hisia katika miguu yangu. Nguvu zote zilionekana kuniishia", alisema."Nilikuwa nimechoka sana. Bila kahawa singewahi kuwa bingwa wa Olimpiki. Nilihitaji kahawa yote!".
Bingwa mara mbili wa ulimwengu wa Kenya Hellen Obiri alipata medali ya fedha baada ya kumaliza kwa 14: 38.36, huku Gudaf Tsegay wa Ethiopia akichukua shaba baada ya kukamilisha mbio hizo kwa muda was dakika 14: 38.87.Hassan ana muda kidogo zaidi wa kupona kabla ya kushiriki mbio yake inayofuata - nusu fainali ya pili ya mita 1500, ambayo inafanyika Jumatano.
Polisi Tanzania waonya Chadema kuhusu maandamano na mikusanyiko
Polisi nchini Tanzania wametoa onyo kwa mtu au kikundi cha watu watakaojaribu kuhamasisha mikusanyiko isiyo rasmi au kuandamana kwa namna yoyote.
Akizungumza na wanahabari leo Mkuu wa Jeshi la Polisi Simon Sirro alisema tuhuma dhidi ya Mbowe na wenzake ziko chini ya mamlaka ya mahakama.
"Jeshi la polisi halitegemei mtu au kikundi cha watu kwa namna yoyote kutoa shinikizo kwa mamlaka ya mahakama au kwa mtuhumiwa Freeman Mbowe aachiwe au kupewa dhamana,"alisema Bw. Sirro.
"Jeshi la polisi linatoa onyo kwa mtu au kikundi cha watu kitakachojaribu kuhamasisha mikusanyiko isiyo rasmi au kuandamana au namna yoyote ile kutoa shinikizo lolote,"aaliendelea kusema.
Mnamo Julai 31 Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika aliwataka wanachama wote ndani na nje ya Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza katika mahakama ya Kisutu siku ambayo kesi ya Mbowe itatajwa.
Amesema polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vimejipanga vizuri na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watu hao.
"Kabla ya uchaguzi nilisema kuna watu wamejipanga kulipua vituo vya mafuta na kuua viongozi wa Serikali hao wanaaopanga kuleta vurugu wajue Mbowe ni binadamu tumempeleka mahakamani tuache mahakama ifanye kazi yake.
Sirro aidha amewataka viongozi wa dini na taasisi nyingine ziache kusema Mbowe anaonewa na badaala yake wasubiri mahakama iamue kesi inayomkabili.
"Jambo usilolijua ni kama usiku wa giza, yeye kapelekwa mahakamani tusubiri maamuzi, mikoa iliyojipanga kufanya maandamano ni kuvunja sheria."
UN yataka msamaha wa Uingereza kwa unyakuzi wa ardhi Kenya
Ungereza imetakiwa kuomba msamaha na kuwalipa fidia watu kutoka jamii mbili za magharibi mwa Kenya ambao walinyanyaswa na ardhi zao zilichukuliwa enzi za ukoloni.
Ombi la Wakenya wazawa ambao walikuwa wamekaa katika maeneo yenye chai ya kaunti ya Kericho liliwasilishwa mbele ya mahakama ya Umoja wa Mataifa (UN).
Umoja umesema kuwa watu wa jamii ya Kipsigis na Tailai communities na wengine wazawa walidhulumiwa na na kutendewa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo mauaji, dhulma za kingono, kudhalilishwa, kuwekwa kizuizini kiholela, kuhamishwa kiholela na kunyimwa haki za faragha, maisha ya familia na mali.
Karibu watu 500,000 walidhulumiwa .
Sehemu kubwa ya ardhi katika eneo hilo sasa inamilikiwa na Uingereza na makampuni makubwa yakimataifa ya chai ikiwemo Findlay’s, Williamson Fine Tea na Unilever.
UN ilikuwa imeandikia serikali ya Uingereza mwezi Mei na kusema itachapisha matokeo ya uchunguzi wake ndani ya siku 30.
Watu Wanane wafariki katika mikasa ya moto ya misitu katika hoteli za kifahari Uturuki
Watu wasiopungua wanane wameuawa kwa moto wa mwituni ambao umesambaa kusini mwa Uturuki, na kuharibu vivutio vyautalii pwani ya nchi hiyo na kulazimisha watalii kukimbia.
Moto huo umekuwa ukiwaka kwa siku sita wakati Uturuki inakabiliana na janga kubwa la mikasa hiyo Siku ya Jumatatu maafisa wa Uturuki walisema zaidi ya visa mia tatu vya moto vilikuwepo wakati juhudi za kuzima moto zikiendelea.
Mahali pengine, wazima moto wanajaribu kuzuia moto wa mwituni katika sehemu za Ugiriki, Uhispania na Italia.
Huduma ya zima moto ya Italia ilisema ililazimika kushughulikia zaidi ya visa 1,500 nchini kote Jumapili.
Kenya yashindwa katika mbio mita 3000 kuruka viunzi na mita 5000 kwa wanawake
Kenya imeshindwa katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1984 katika michezo ya Olimpiki inayoendelea nchini Japan.
Hii ni baada ya mwanariadha wa Morocco Soufiane El Bakkali kushinda nishani ya dhahabu katika mbio hizo mjini Tokyo Jumatatu. Mwanariadha wa Kenya Benjamin Kigen alifanikiwa kupata nishani ya shaba.
Kigen alijikakamua na kuibuka wa tatu katika muda wa 8:11.45 baada ya kumshinda Getnet Wale katika kihunzi cha mwisho.
Soufiane El Bakkali ni Mmorocco wa kwanza kushinda mbi hizo.
Mwanariadha wa Ethiopia Lamecha Girma aliishindia nchi yake nishani ya fedha baada kuchukua nafasi ya pili kwa kumaliza katika muda wa 8.10.38.
Wakati huo huo Kenya pia ilikosa kupata dhahabu katika mbio za mita 5000 kwa upande wa akina dada baada ya Hellen Obiri kumaliza wa pili na kushinda medali ya fedha .
Mholanzi Sifan Hassan ndiye aliyeshinda dhahabu .Obiri hakuweza kumudu kasi ya Sifanna kulazimika kujishindia meali ya fedha ambayo aliinyakuwa tena miaka mitano iliyopita katika mashindano ya Rio . Muethiopia Gudaf Tsegay alishinda medali ya shaba
Agnes Tirop alimaliza katika nafasi ya nne ihaliLilian Kasait alimaliza katika nafasi ya 12 . Obiri hata hivyo yungalia atalenga kushinda dhahabukatka fainali ya mbio za mita 10,000
Kampuni ya mafuta ya Msumbiji yakana kumwaga mafuta baharini
Kampuni ya kusambaza mafuta inayomilikiwa na serikali ya Msumbiji, Petromoc, imekanusha kuhusika na umwagaji wa mafuta ulitokea mwishoni mwa wiki katika bandari ya Pemba, karibu na pwani ya mkoa wa Cabo Delgado.
Mwenyekiti wa bodi ya kampuni hiyo Hélder Chambisse amesema kuna maelezo finyu kuhusu chanzo cha mafuta hayo yaliyomwagika bahari.
Alisema laiti kampuni hiyo ilihusika mamlaka katika eneo hilo ingeliwaarifu.
Bw. Chambisse amesema uchunguzi unaendelea kufahamu kilichosababisha umwagikaji huo.
Inakadiriwa kwamba umwagikaji huo umesababisha hasara ya karibu lita 10,000 za mafuta.
Kisa hicho kimevutia umati mkubwa wa watu wakiwemo wanawake na watoto, ambao wanahatarisha maisha yao kuchota mafuta kwenye mitungi.
Polisi wamepelekwa eneo hilo kudhibiti watu.
Hatari:Bunduki za AK 47 na AR15 sasa zinatengezwa na teknlojia ya 3D kutumia plastiki na kuzua hofu Ulaya
Kuna hofu barani ulaya kuhusu matumizi ya teknolojia ya 3D Printing kutengeza silaha hatari na sasa sio bastola tu bali makundi ya itikadi kali za mirengo ya kulia yanayoeneza ubaguzi sasa yameanza kutengeza hadi bunduki hatari kama AK 47 na AR15.
Watu kadhaa wamekuwa wakikamatwa kote Ulaya kwa kupatikana na hatia ya kujitengezea bunduki kutumia teknolojia hiyo .
Watalaamu wanasema unachohitaji ni vifaa vya kutengeza bunduki vya gharama ya dola 50 pamoja na kupakua mtandaoni mfumo wa 3D unaokupa mwongozo jinsi ya kuzitengeza silaha hizo .
Stephan Balliet aliyehukumiwa maisha jela kwa kuwaua watu wawili ‘akifanya’ majaribio ya bunduki aliounda mwaka wa 2019 ameonekana kuwavutia watu wengi wenye misimamo mikali ya ubaguzi wa rangi tangu kesi yake ilipoangaziwa .
Ana itikadi za Kinazi ambazo zilimfanya kuwaonyesha wafuasi wake jinsi ya kuzitengeza bunduki kutumia vifaa vya palastiki na mwongozo wa 3D .
wakati akitekeleza mauaji yake hayo aliyapeperusha moja kwa moja mtandaoni .
Bunduki ya kwanza duniani kutengezwa na teknolojia ya 3D iliundwa mwaka wa 2013 na Cody Wilson, mwanaharakati wa haki za kumiliki bunduki mwenye umri wa miaka 25 huko Marekani .
Nchini Uingereza mwaka wa 2019 mshukiwa Tendai Muswere mwenye umri wa miaka 26 alishtakiwa kwa hatia ya kutengeza bastola kutumia teknolojia hiyo .Tendai kutoka katikati mwa London aliwaambia polisi wakati huo kwamba alikuwa akiitengeza bastola hiyo kwa ajili ya mradi wake wa shuleni .
Nchi nyingi za Ulaya zimekuwa zikisajili visa vingi vya kukamatwa kwa watu wanaomiliki bunduki zilizotengezwa na teknlojia hiyo ya 3D bila kuwa na leseni ya kumiliki silaha. Vifaa vinavyotengezwa na teknolojia hiyo vinaunganishwa na kuwa bunduki hatari .
Zambia yatuma jeshi kuzuia vurugu kabla ya uchaguzi
Rais wa Zambia Edgar Lungu ameidhinisha kutumiwa kwa majeshi kukabiliana na vurugu kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 12 – licha ya hatua hiyo kukosolewa na upinzani na makundi mengine.
Nimeruhusu majeshi ya Zambia, vikosi vya majeshi ya anga ya Zambia na vikosi vya huduma ya kitaifa ya Zambia kusadia polisi wa Zambia katika masuala ya usalama,” Bw. Lungu alisema.
Amesema wanajeshi hao tayari wamepelekwa katika maeneo tofauti ya mji mkuu wa Lusaka na pia watapelekwa katika maeneo mengine ya nchi “hali ikilazimu kufanya hivyo”.
Chama cha All People’s Congress (APC) kimesema hatua ya kuhusisha wanajeshi inalenga “kuwatia hofu na uwoga” wapinzani.
Kumekuwa na visa vya ghasia vinavyohusisha wafuasi wa chama tawala na wale wa upinzani katika maeneo tofauti nchini kuelekea uchaguzi.
Hatua ya rais kuwatumia wanajeshi, imetokana na mauaji ya wafuasi wawili wa chama tawala katika mji mkuu, akisema hawezi kuruhusu kutokea tena kwa mauaji kama hayo kwengineko nchini.
Tume ya uchaguzi inachunguza kisa hicho na itachukua hatua dhidi ya watakaopatikana na hatia.
Rais anagombea muhula wa pili madarakani katika uchaguzi huu ujao.
Mpinzani wake mkuu Hakainde Hichilema amewania urais mara tano bila mafanikio.
Shirika la ndege la Ethiopia linakanusha kusafirisha silaha Tigray
Shirika la ndege la Ethiopia limekanusha ripoti kwamba lilisafirisha silaha katika eneo la Tigray linalokumbwa na mzozo.
Shirika hilo limesema baada ya usafiri wa angani kurejeshwa katika eneo hilo ''limekuwa likitoa huduma muhimu za kibiashara kwa raia".
Usafiri wa kwenda na kutoka eneo la Tigray ulisitishwa ghasia zilipoanza mwezi Novemba 2020.
Usafiri ulirejeshwa mwezi Disemba 2020 na kufungwa tena wiki chache zilizopita wakati waasi wa Tigray walipoanza tena mapigano dhidi ya vikosi vinavyounga mkono.
Shirika la ndege la Ethiopian Airlines linasema hakuna"ndege uliyosafiri eneo hilo" tangu anga zilipofungwa hivi karibuni.
Linasema ripoti hizo zinatoka kwa watu ambao wanataka kuiharibia sifa na kuichafulia jina.
Pia linasema picha zinazoonesha maafisa waliovalia sare wakishuka katika ndege yake ni ya zamani na kuongeza kwamba ndege hiyo haijawahi kuwasafirisha wanajeshi katika maeneo yenye vita.
Tanzania yazindua usajili wa chanjo ya corona
Tanzania imezindua usajili wa mtandaoni wa chanjo ya Covid-19 baada ya kupokea dozi milioni moja ya chanjo hiyo Julai 24.
Wizara ya Afya imewaomba raia wanaoazimia kupewa chanjo bila malipo ''kuwasilisha maombi ya siku wanayotaka kuchanjwa kupitia simu zao za mkononi au kompyuta" kuanzia leo.
Serikali inatarajiwa kuanza shughuli ya kutoa chanjo kwa makundi maalumu, ikijumuisha maafisa wa afya kuanzia hapo kesho.
Nchi hiyo ya Afrika ilipokea dozi milioni moja ya chanjo ya Johnson & Johnson Julai 26 July kupiti ampango wa chanjo wa Covax
Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa afisa wa kwanza wa umma kupewa chanjo na ametoa wito wa raia kuchanjwa dhidi ya Covid-19.
Madagascar yawakamata majenerali waliopanga kumuua Rais Rajoelina
Maafisa wa kijeshi wa ngazi ya juu na polisi wamekamatwa nchini Madagascar kuhusiana na jaribio la kumuua rais lililotibuka.
Waliokamatwa ni pamoja na majenerali watano na maafisa kadhaa wa polisi na kufikisha 21 jumla ya watu ambao wanachunguzwa ufuatia tukio hilo a mwezi uliopita.
Mamlaka pia imepata bunduki moja na dola 250,000 za Kimarekani, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.
Jaribio la kumuua Rais Andry Rajoelina ni sehemu ya misukosoko ambayo imekuwa ikikumba taifa hilo la kisiwani.
Miongoni mwa waliokamatwa karibuni walikuwa 12 "wanajeshi na polisi wanaofanya kazi, ikiwa ni pamoja na majenerali watano, manahodha wawili na maafisa watano ambao hawajapewa kazi", Mwanasheria Mkuu Berthine Razafiarivony alisema.
Madagascar imekuwa ikitekeleza amri ya kutotoka nje tangu janga la Covid-19 lilipozuka mwaka jana huku sehemu ya kusini mwa nchi hiyo ikikabiliwa na hatari ya kukumbwa na baa la njaa.
Bwana Rajoelina, 47, alichukua madaraka mnamo 2009 kutoka kwa Marc Ravalomanana akiungwa mkono na jeshi.
Rajoelina aliapishwa kama rais wa nchi ya kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi mnamo 2019 baada ya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali na ambao ushindi wake ulipingwa katika mahakama ya kikatiba na mpinzani wake.
Soma zaidi:
Rais Samia awasili nchini Rwanda kwa ziara ya siku mbili
Rais wa Tanzania ,Samia Suluhu Hassan anafanya ziara ya siku mbili nchini Rwanda ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu kuingia madarakani mwezi wa tatu mwaka huu.
Ziara hiyo imeelezwa kuwa ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Hakuna maelezo yaliyotolewa na serikali ya Rwanda kuhusu ziara hiyo lakini kulingana na vyombo vya habari vya upande wa serikali, Rais Samia anatarajiwa kuzuru jumba la kumbukumbu ya mauaji ya kimbari la Gesozi mjini Kigali kabla ya kukutana kwa mazungumzo na mwenyeji wake Rais Paul Kagame.
Pande mbili zinatarajia kutia saini hati za makubaliano na kuzungumza na vyombo vya Habari.
Mkurugenzi wa sekta ya kibinfasi nchini Tanzania , bwana Francis Nanai amenukuliwa na gazeti la The Citizen nchini humo akisema kwamba ni fursa ya kuimarisha biashara kupitia bandari ya Dar es salaam.
‘’Tunaweza kutumia fursa ya ukaribu wetu na Rwanda kijiografia ili kuirai kutumia bandari yetu badala ya ile ya Mombasa Kenya.”
Pia alisema kwamba kuna haja ya kujengwa kwa kituo cha kimkakati kitakachohusika na usambazaji, wa mizigo ili Rwanda iagize mizigo kutoka Dar es salaam badala ya China , Japan na India.
Kulingana na takwimu za Umoja wa mataifa kuhusu biashara, Tanzania ilisafirisha hadi nchini Rwanda bidhaaza thamani ya $247m mwaka 2019.
Wakati wa kipindi kama hicho , Rwanda nayo ilipeleka nchini Tanzania bidhaa zenye thamani ya $5.04m .
Karibu katika matangazo mubashara leo Jumatatu 02.08.2021