Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Jackline Mengi asisitiza marehemu mumewe alikuwa na 'akili timamu'

Mjane wa Marehemu Reginald Mengi, Jackline Ntuyabaliwe ameonesha kutorodhika na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusu wasimamizi wa mirathi ya mali alizoacha marehemu mumewe.

Moja kwa moja

  1. Tumefika tamati ya taarifa zetu za moja kwa moja, mpaka kesho panapo majaaliwa.

  2. Bolt yamsimamisha kazi dereva Tanzania kwa kumshambulia abiria

      • Author, Elizabeth Kazibure
      • Nafasi, BBC News, Tanzania

    Kampuni inayotumia programu ya mtandao kwa ajili ya usafirishaji ya Bolt inasema imempiga marufuku mmoja wa madereva wake nchini Tanzania baada ya madai kwamba alikuwa amemshambulia abiria mmoja wa kike kitendo kilichosababisha ghadhabu mtandaoni.

    Ujumbe uliochapishwa sana kwenye mitandao ya kijamii ulielezea kwa kina jinsi mwanamke mmoja aliyesema kuwa alibaki na majeraha mengi baada ya kukataa kulipa pesa nyingi kuliko bei iliyooneshwa kwenye programu hiyo.

    Alisema alijaribu kukimbia lakini dereva alimsukuma na kuiba pesa zote zilizobaki kwenye mkoba wake, na kumuacha akiwa kwenye mshtuko.

    Kwa majibu ya chapisho hilo, watu walifafanua jinsi walivyokumbana na adha kama hiyo mikononi mwa baadhi ya madereva.

    Tukio hilo limesiuliwa na rafiki wa mwathiriwa ambaye alisema alitaka "kueneza ufahamu ili isiweze kutokea kwa mtu mwingine tena".

    Bolt imelizungumzia tukio hilo na imesema "haikubaliani na aina yoyote ya udhalilishaji kwenye jukwaa letu".

  3. Binti wa miaka 12 aendesha mtumbwi kumuwahisha mama yake hospitali ili akajifungue

    Binti wa miaka 12 katika kaunti ya Busia Magharibi mwa Kenya amepiga makasia kupita maji ya mafuriko akimuwahisha mama yake hospitali.

    Mama huyo, Judith Anyango Akala, amesema chupa yake ilipasuka majira ya saa tisa usiku na kumuomba binti yake ampeleke kwenye hospitali ya karibu kwa kuwa mume wa mama huyo alikwenda kazini zamu ya usiku.

    Kijiji chao,Rukala , kikiwa kimezungukwa na maji ya ziwa Victoria baada ya mvua kubwa, familia imekuwa ikiishi kwenye kambi pamoja na familia nyingine ambazo zimelazimika kuyaacha makazi yao.

    Binti huyo mdogo aliendesha mtumbwi gizani akitumia kurunzi ya simu ya mama yake kumsaidia kumuongoza.

    Bi Akala alisema walipiga makasia wakipita mimea na wakaendelea kupotea kabla ya kufika katika Kituo cha Afya cha Model cha Rukala. Safari ilichukua kama saa moja hivi, akaongeza.

    Mtaalamu wa afya katika kituo hicho, Felix Pambula, ameiambia BBC kuwa mwanamke huyo na mtoto aliyekuwa tumboni wangepoteza maisha kama angejifungulia nyumbani.

    ''Kichanga kilikuwa kimejiviringa na kitovu shingoni. Mama na mtoto walikuwa kweye hatari na walihitaji uangalizi mzuri,'' alisema.

  4. Watoto wanateseka kutokana na mashambulizi ya wanamgambo Msumbiji

    Shirika la misaada la kimataifa linasema watoto wanateseka sana na uasi wa wanamgambo wa Kiislamu kaskazini mwa Msumbiji.

    Katika ripoti mpya, shirika la Save the Children limesema watoto wengi hawajui wazazi wao wako wapi, hawawezi kwenda shule na wamepoteza hati zao za kitambulisho.

    Zaidi ya watoto 300,000 wamehama makazi yao kutokana na mzozo huo na karibu 2,500 wametenganishwa na wazazi wao.

    Shirika hilo limesema wengi wameshuhudia vurugu za kutisha.

    Wapiganaji wa kiisilamu wamekuwa wakifanya mashambulizi kaskazini mwa Msumbiji kwa zaidi ya miaka mitatu, wakishambulia miji na vijiji, na kuchoma nyumba.

  5. Jackline Mengi asisitiza marehemu mumewe alikuwa na 'akili timamu'

    Mjane wa Marehemu Reginald Mengi, Jackline Ntuyabaliwe ameonesha kutorodhika na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusu wasimamizi wa mirathi ya mali alizoacha marehemu mumewe.

    Aliandika katika mtandao wake wa Instagram:

    ''Imetosha.... Ripoti ya matibabu ya Dk Reginald Mengi imeambatanishwa kama ushahidi. Ukweli kwa wale wanaopenda ukweli. Mume wangu alitumia maisha yake yote kama mtu anayeheshimiwa, mwerevu mkarimu na msaidizi kwa maelfu ya Watanzania''. Aliandika Jackline.

    Hakuwa mwendawazimu! Unaweza kusema chochote unachotaka na uchukue kila kitu lakini kwa hili nitamtetea mpaka kifo.

    Aliandika katika mtandao huo akiambatanisha ripoti ya daktari wake aliyetoa mapendekezo kuhusu afya ya marehemu, kuwa ugonjwa wa kiharusi alioupata haukuathiri uwezo wake wa kiakili.

    Mahakama ilisema nini?

    Siku chache zilizopita akisoma hukumu yenye kurasa 72, Jaji Mlyambina alisema kuwa wosia wa mwisho wa Marehemu Dkt Mengi ulioandikwa tarehe 17 mwezi Agosti mwaka 2017 haukuzingatia misingi ya kisheria ya uandishi wa wosia.

    Katika shauri hilo watoto wa Marehemu Dkt. Mengi walikuwa wakipinga wosia uliodaiwa kuachwa na marehemu baba yao na saini iliyopo kwenye wosia ni tofauti na sahihi nyingine za marehemu na pia kwa wakati huo baba yao hakuwa na uwezo wa kuandika kutokana na matatizo ya kiafya aliyokuwa nayo tangu mwaka 2016.

    Watoto wakubwa wa marehemu walidai kuwa wosia uliwabagua na urithi wote aliachiwa mkewe mpya na watoto mapacha na hivyo wosia huo ulikuwa kinyume na sheria kwasababu uliwabagua watoto bila sababu za msingi na za kisheria.

  6. Viumbe, mimea na wadudu vamizi hugharimu Afrika dola trilioni 3.5 kwa mwaka

    Utafiti mpya unasema wadudu, minyoo, mimea vamizi ya magugu,zinagharimu Afrika zaidi ya $ 3.5tn (£ 2.5tn) kila mwaka.

    Watafiti walio Ghana, Kenya, Uingereza na Uswizi wameelezea athari mbaya za spishi zinazoletwa na shughuli za wanadamu.

    Nigeria, ambayo hasara yake inakadiriwa kuwa dola trilioni moja kwa mwaka, ni nchi iliyoathirika zaidi.

    Gharama nyingi zinatokana na kupalilia - kazi inayofanywa hasa na wanawake na watoto - lakini uharibifu unaosababishwa na wadudu unakadiriwa kuwa karibu na thamani ya dola bilioni 40.

  7. Waziri nchini Kenya akana kuwepo kwa mpango wa kuuza mbuga ya wanyama

    Waziri wa utalii wa Kenya amekanusha kuwa kuna mipango ya kubinafsisha mbuga za kitaifa za wanyama pori na akiba.

    Najib Balala alikuwa ameuliza wiki iliyopita kwanini serikali bado inasimamia mali muhimu za utalii, akibainisha kuwa "haya ni mambo ambayo yanahitaji kurekebishwa, na huu ni wakati wa kufikiria tena".

    Aliliambia baraza la diplomasia ya Kijani ya Umoja wa Ulaya kwamba nchi hiyo inaangalia uwekezaji mpya na mifano ya biashara ambayo itapunguza gharama za kuendesha bustani hizo.

    Matamshi ya waziri huyo yalizua ukosoaji, huku vyama vya watalii wa ndani na vyama vya watunzaji wa hoteli vikisema kuwa haikuwa busara kubinafsisha maliasili na tamaduni za nchi.

    Lakini Jumatano, Bw Balala aliambia Citizen TV kwamba hakuwa na mpango "wa kuuza mbuga hizo".

    "Mbuga haziwezi kuuzwa. Hizi ni urithi wa kitaifa, lakini zinaweza kusimamiwa kwa mtazamo tofauti," alisema.

  8. Wakazi wakosa malazi baada ya kukumbwa na mafuriko Kagera

      • Author, Munira Hussein
      • Nafasi, BBC Africa

    Kaya zaidi ya mia tisa mkoani Kagera magharibi mwa Tanzania hawana makazi kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha mwezi uliopita.

    Hivi sasa wanaishi kwenye kambi ambazo hawana mahitaji ya kibidamu kwa zaidi ya wiki mbili.

    Hivi sasa wanaishi kwenye kambi ambazo hawana mahitaji ya kibidamu kwa zaidi ya wiki mbili.

    Kanali Dennis Mwira, ni Mkuu wa Wilaya ya Misenyi amesema kuna kaya 964 zenye watu 1184 ambazo zimekosa makazi maana yake maji yamejaa kwenye nyumba hizo.

    ''Baada ya mafuriko tulikwenda Kagera Sugar kwa ajili ya kuomba mitambo ya kuchimba mitaro lakini moja ya mitambo hiyo ulizama hivyo inaonekana kuwa sasa hakiwezi kufanyika chochote wakati huu wa masika.'' Alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

    Lawama zimekuwa zikielekezwa kwa wakazi wa eneo hilo kwa kuharibu Misitu na kusababisha athari wakati huu wa mvua kubwa.

  9. Tanzania, Uganda zashuhudia utiaji saini mkataba wa kuanza ujenzi wa bomba la mafuta

    Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni leo yuko kwenye ziara ya kikazi ya siku moja nchini Tanzania kwa Mualiko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

    Akiwa nchini Tanzania Rais Museveni na Rais Samia wameshuhudia utiaji saini wa mikataba ya utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni za uwekezaji wa mradi huo.

    Shughuli hizo zinafanyika Ikulu ya Dar es Salaam.

    Bomba la mafuta lenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 4.1 linatarajiwa kuunda ajira za watu kati ya 10,000 na 15,000.

    Mazungumzo kuhusu mpango huu yalianza mwezi Mei mwaka 2017 kati ya Hayati Magufuli na Rais Yoweri Kaguta Museveni.

  10. Natumai hujambo. Ni siku nyengine ambayo tutaendelea kukuangazia mubashara yale yanayojiri