Mvinyo wa Pétrus uliokuzwa anga za mbali wauzwa dola milioni 1

Iliyochapishwa

Chupa la mvinyo nchini Ufaransa ambayo ilizunguka katika anga za juu kwa zaidi ya mwaka mmoja imewekwa sokoni baada ya kurejeshwa duniani.

Chupa ya Pétrus 2000 -iliyotengenezwa kutokana na zabibu katika mkoa wa Bordeaux - ilitembezwa katika obiti ya dunia kwa miezi 14 kama sehemu ya utafiti binafsi uliodhaminiwa kuhusu chakula na kilimo.

Jumanne, kampuni ya Christie ilitangaza kuwa mvinyo huo sasa upo sokoni kupitia mauzo yake ya kibinafsi.

Nyumba ya mnada inakadiria kuwa bei ya chupa hiyo ni dola milioni 1 (£720,000; €830,000).

Tim Triptree, mtaalamu wa mvinyo anayefanya kazi katika kampuni ya Christie, aliiambia BBC kuwa chupa ya kawaida ya mvinyo wa Pétrus 2000 pia itauzwa pamoja na chupa iliyosafiri katika anga za mbali, "kwa hiyo mnunuzi mwenye bahati ataweza kulinganisha chupa hizo mbili.

Chombo cha anga za mbali -Space Cargo Unlimited, kilituma chupa 12 za mvinyo katika Kituo cha kimataifa cha anga za mbali (ISS) mwezi wa Novemba 2019. Baada ya zaidi ya siku 400, kilitembea takriban kilomita milioni 300 (maili milioni 186 ) katika mvuto wa sifuri, mvinyo ulirejea dunaini Januari 2021.

Wanasayansi waliuchunguza mvinyo huo na kundi la waonjaji wa mvinyo waliweza kuonja baadhi yake katika Taasisi ya mvinyo ya Bordeaux mwezi Machi, kulinganisha mvinyo huo na ule uliotunzwa katika chupa dunaini. Jane Anson, mwandishi wa habari na mwandishi wa makala ya Inside Bordeaux, alikuwa mmoja wa watu wachache waliobahatika.

"Ni vigumu kwangu kusema kuwa ulikuwa bora au mbaya zaidi. Lakini ulikuwa tofauti kwa kweli ," aliiambia BBC . "Ladha yake ilikwa ya maua na yenye moshi zaidi - mambo ambayo yangetokea kwa vyovyote kwa Petrus wakati inapokaa kwa muda mrefu."

Bi Anson alisema kuwa lilikuwa ni chaguo bora kutuma mvinyo wa Pétrus katika uzio wa dunia - kwa sababu ya sifa ya ufahari wake, na uwezo wake wa kukaa miaka.

"Hakuna mivinyo mingi ambayo inaweza kudumu kwa miaka 60, 70, miaka mingi, na Petrus ni moja ya mivinyo hiyo ," alisema. Hakuwa na uhakika iwapo mvuto wa sifuri katika anga za mbali ulikuwa na atharai kwa mvinyo, au kama safari ya kwenda na kutoka na kuzunguka duniani ilikuwa na athari . "Lakini kulikuwa na utofauti wa wazi," aliongeza.

Unaweza pia kusoma:

Chupa zilitumwa katika anga za mbali kama sehemu ya safari ya WISE, mpango wa utafiti uliodhaminiwa kibinafsi ulioendeshwa na Space Cargo Unlimited. Nicolas Gaume, muasisi mweza na mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, alisema katika taarifa kwamba mpango huo unalenga "kusaidia katika ubunifu wa kilimo na chakula tunachohitaji siku zijazo duniani kwa kuchunguza athari za mvuto wa sifuri na anga za mbali."

Fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo ya mvinyo wa Christie zitasaidia kufadhili safari za anga za mbali za chombo cha mizigo- Space Cargo katika anga za mbali. Bw Triptree aliambia BBC utafiti ulionesha kwamba "mvinyo unakua katika anga za mbali ".

"Nani anafahamu, labda wanaanga wajao watakuwa wakienda na mvinyo katika safari zao!" alisema.

Hii ni chupa pekee ambayo itauzwa. Tatu zilifunguliwa kwa ajili ya kuonjwa, na nane zilizobakia zitatunzwa kwa ajili ya utafiti wa siku zijazo.

Makazi ya Bordeaux ya Château Pétrus huzalisha takriban chupa 30,000 za mvinyo kwa mwaka, na bidhaa zake zimekuwa bora kwa mwaka kila mara na ni ghali zaidi duniani. Chupa ya A 2000 ya Pétrus kwa kawaida huuzwa kwa takriban dola 6,000.

Unaweza pia kusikiliza: