Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Serikali ya Tanzania yatoa tahadhari juu ya utoaji wa taarifa zinazohusu Umma
Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Dkt Hassan Abbas amewataka Watanzania kuzingatia misingi ya utoaji taarifa zinazohusu umma.
Moja kwa moja
Air Tanzania kuanza safari zake kuelekea Guangzhou China
Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) Linatarajia kuanza kufanya safari zake kuelekea jijini Guangzhou China ifikapo tarehe 20 Machi.
Hatua hiyo inakuja wakati kukiwa na vizuizi vya kusafiri vilivyowekwa duniani kutokana na janga la virusi vya corona.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Ladislaus Matindi aliliambia gazeti la Citizen Ijumaa kuwa safari za ndege kwenda china ambazo ziliahirishwa tangu mwezi Septemba mwaka jana kwa sababu ya janga la corona zitaanza rasmi mwezi huu.
''Tutasafiri kwa wiki mara moja Jumamosi saa 11 asubuhi kuelekea China na kurejea Tanzania siku ya Jumapili saa 11,'' alisema.
Shirika hili limeandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii taarifa kuhusu safari hizo zinazotarajiwa kuanza.
WHO: 'Hatari' ugonjwa wa Ebola kusambaa nchi jirani kutoka Guinea
Shirika la Afya Duniani limetahadharisha kuwa ''kuna hatari'' kuwa Mlipuko wa Ebola nchini Guinea unaweza kuenea nchi jirani.
"Kufikia jana jumla ya wagonjwa 18 waliripotiwa: 14 wakithibitishwa, pamoja na vifo vya watu wanne. Hii inatoa kesi ya vifo vya 44.4%," anasema Dkt Georges Alfred Ki-Zerbo, mwakilishi wa WHO nchini Guinea.
Shirika hilo limesema baadhi ya nchi jirani hazijaandaa kampeni yoyote ya chanjo.
Mpaka sasa zaidi ya watu 1,600 wamepatiwa chanjo ya dhidi ya ugonjwa wa Ebola nchini Guinea
Mlipuko wa ugonjwa huo ulioanza karibu wiki tatu zilizopita ni wa kwanza katika eneo hilo tangu mwaka 2014 ambapo ugonjwa huo uligharimu maisha ya watu 11,000 nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia.
Rais Bolsonaro awataka raia waache ''kulialia'' kuhusu Covid-19
Rais Jair Bolsonaro amewataka raia wa Brazil ''waache kulialia'' kuhusu Covid-19, akikosoa njia zinazotumika kupambana na virusi pamoja na kuwepo ongezeko la maambukizi na vifo.
Kauli yake imekuja siku moja baada ya Brazil kushuhudia ongezeko la vifo katika kipindi cha saa 24.
Brazili imeathirika vibaya na janga la corona, na kuacha mfumo wa afya ukiwa katika hali mbaya.
Katika kupambana na hali hiyo baadhi ya miji na majimbo yameweka mashati yao wenyewe.
Wizara ya Afya nchini humo imesema zaidi ya watu 260,000 wamekufa kutokana na Covid-19, ikiwa ni nchi ya pili duniani baada ya Marekani.
Pamoja na hali hiyo, Bw. Bolsonaro ameendelea kudhihaki tishio linalosababishwa na virusi hivyo.
''Acheni kulialia, mtalia mpaka lini?'' Bolsonaro alisema. ''mtakaa nyumbani mpaka lini na kufunga kila kitu? hakuna atakayeendelea kuvumilia. Tunasikitika kuhusu vifo, lakini tunahitaji ufumbuzi.
Rais Bolsonaro amekuwa akipinga hatua za kukaa karantini zilizowekwa na magavana, akisema kuwa ni hatari kwa uchumi wa taifa hilo kuliko hatari inayosababishwa na virusi vyenyewe.
Kenya yaanza kuwadunga watu chanjo ya Corona
Kenya imeanza kutoa chanjo ya Corona leo na mtu wa kwanza ambaye amedungwa chanjo hiyo ni kaimu mkurugenzi wa afya Patrick Amoth.
Watu kumi wa kwanza pia wamedungwa chanjo hiyo katika hospitali ya Kenyatta jijini Nairobi .
Wengine waliochanjwa ni afisa mkuu mtendaji wa hospitali ya Kenyatta Evanson Kamuri akifuatwa na muuguzi mmoja wa hospitali hiyo kisha Collins Tabu ambaye ni mkuu wa kitengo cha Chanjo katika wizara ya afya akachanjwa pia.
Wote walioachanjwa walitakiwa kusaini mkataba wa kuidhinisha kupewa chanjo hiyo na baadaye wakatakiwa kupumzika kwa dakika 30 kabla ya kuruhusiwa kuondoka .
Katibu wa kudumu wa wizara ya Afya Susan Mochache amesema chanjo itatolewa katika hospitali zote za rufaa za kaunti pindi uzinduzi katika hospitali ya KNH utakapokamilishwa .
Mwakilishi wa WHO nchini Kenya Rudi Eggers amesema Wakenya hawatagharamika wanapodungwa chanjo hiyo ya AstraZeneca.
Mzozo wa Tigray: Baraza la Usalama la UN lashindwa kukubaliana
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshindwa kufikia tamko la pamoja kuhusu mzozo wa Tigray kaskazini mwa Ethiopia, baada ya Urusi, China na India kuchukualia mgogoro huo kuwa suala la ndani.
Wanadiplomasia walionukuliwa na shirika la habari la AFP wamesema nchi tatu za Afrika katika baraza hilo- Kenya, Niger na Tunisia - zimeunga mkono rasimu ya taarifa iliyoandikwa.
Kamishena wa kutetea haki katika Umoja wa Mataifa katika awali alisema kulikuwa na ripoti za kusikitisha zinazoashitia huenda uhalifu wa kivita ulitekelezwa katika jimbo Tigray.
Michelle Bachelet aliangazia visa vya unyanyasajji wa kijinsia, mauaji ya kiholela na uharibifu mkubwa ulifanywa katika eneo hilo.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kutetea haki inataka kupewa idhini ya kuchunguza ripoti za ukatili uliotekelezwa na majeshi ya Ethiopia na Eritrea, wapiganaji wa Tigray People’s Liberation Front na vikosi vya jimbo la Amhara.
Maelezo zaidi:
- Jukumu la Eritrea katika mzozo wa Ethiopia
Televisheni za Senegal zafungwa kwasababu ya kuangazia maandamano
Mamlaka nchini Senegal zimesitisha matangazo ya vituo viwili vya televisheni za kibinafsi baada ya kuzilaumu kwa kuangazia zaidi maandamano yaliyosababishwa na kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani, Ousmane Sonko.
Vituo viwili vilivyoathirika na uamuzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Matangazo nchini humo ni Sen TV na Walf TV.
Vituo hivyo vimeshutumiwa kwa upeperushaji wa picha zinazoonesha maandamano baada ya Bwana Sonko kukamatwa, Shirika la habari la AFP limeripoti.
Siku ya Alhamisi, polisi walikabiliana na wafuasi wa Bw. Sonko mjini Bignona kusini mwa eneo la Casamance.
Serikali imethibitisha kuwa mtu mmoja aliuawa siku ya katika ghasia za Alhamisi zilizotokana na kukamatwa na Bw. Sonko mjini Dakar mapema siku hiyo.
Bw. Sonko amelaumiwa kwa kumbaka mwanamke mmoja katika saluni ambako alikwenda kusingwa.
Sokwe wafanyiwa majaribio ya chanjo ya corona
Sokwe kadhaa katika hifadhi ya wanyama ya San Diego wamepewa chanjo ya majaribio ya Covid-19 ziliyotengenezewa wanyama baada ya mlipuko wa ugonjwa huo kutokea miongoni mwa sokwe hao.
Sokwe wanane katika hifadhi hiyo walikuwa wa kwanza duniani kupatikana na virusi vya corona mwezi Januari. Kwa sasa wanaendelea kupokea matibabu.
Wahifadhi wa wanyama wana wasiwasi kuhusu tisho la ugonjwa wa corona kwa sokwe wa jadi.
Wana wasiwasi hasa juu ya baadhi ya spishi za sokwe wanaokabiliwa na tishio la kuangamia.
Wanayama wengine waliopatikana na virusi vya corona ni pamoja na simba katika mbuga ya Barcelona huko Barcelona na duma katika hifadhi ya wanyama ya Bronx huko New York.
Soma zaidi:
- Jinsi wanyama wanavyohusishwa katika mlipuko wa magonjwa mapya
Serikali ya Tanzania yatoa tahadhari juu ya utoaji wa taarifa zinazohusu Umma
Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Dkt Hassan Abbas amevitaka vyambo habari kuzingatia misingi ya utoaji taarifa.
Katika taarifa yake kwa umma Bw. Abbas amesema, katika siku za hivi karibuni kumekuwa na tabia ya baadhi ya vyombo vya habari na watu katika mitandao ya kijamii kujitolea taarifa bila kuzingatia mwongozo uliowekwa.
''Serikali ina mfumo wake wa kutoa taarifa mbali mbali kwa hiyo wale ambao hawahusiki na taratibu hizo hawafai kuingilia taratibu hizo’’ alisema Bw. Abbas.
Kauli yake inakuja siku kadhaa baada ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania kusema limepoteza mapadri 25, watawa na wauguzi 60 kwa matatizo ya kupumua kwa miezi 2.
Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Katoliki nchini Tanzania (TEC) liliwataka wananchi wa taifa hilo la Afrika Mashariki kuchukua tahadhari zaidi dhidi ya ugonjwa wa virusi vya corona.
Katibu wa TEC Padri Charles Kitima kupitia mkutano na wanahabari alisisitiza kuwa tishio la corona bado lipo Tanzania na Kanisa na ongezeko la vifo bado linaendelea kuripotiwa ikiwemo ndani ya Kanisa lenyewe ''Ndani ya miezi iliyopita Mapadri 25 wamepoteza maisha kwa matatizo ya kupumua. Masisita na manesi zaidi ya 60. Vifo vinaendelea, tuchukue tahadhari." alisema.
Kwa mujibu wa Dkt Kitima japo serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa waraka wa kuwataka watu kuchukua tahadhari bado kuna changamoto kwa kuwa watu hawabanwi kisheria kuchukua tahadhari. ''Changamoto tuipatayo kwa kuwa serikali haijasisitiza tahadhari, watu bado wana mtazamo kuwa corona haipo au imeisha kama ilivyokuwa mwaka jana.",alisisitiza.
Unaweza pia kusoma:
- Virusi vya Corona: Kanisa Katoliki Tanzania limesema limepoteza mapadri 25, watawa na wauguzi 60 kwa matatizo ya kupumua kwa miezi 2
Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu mubashara leo Ijumaa tarehe 05.03.2021