Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Kwaheri Trump karibu rais mpya wa Marekani Joe Biden

Rais mteule wa Marekani Joe Biden anatarajiwa kula kiapo saa chache zijazo

Moja kwa moja

Asha Juma

  1. Hapa ndio tunatamatisha matangazo ya moja kwa moja ..mpaka hapo kesho

  2. Kamala Harris ala kiapo kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke

    Kamala Harris ala kiapo kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke katika historia ya Marekani.

    Ameapishwa na Jaji wa Mahakama ya Juu Sonia Sotomayor, ambaye aliweka historia mwaka 2009 kuwa mtu wa kwanza mwenye asili ya latini kushika nafasi ya juu katika mahakama hiyo.

  3. Kuapishwa kwa Joe Biden: Harris na mumewe waingia katika ukumbi

    Kamala Harris na mume wake , Doug Emhoff, wametangazwa rasmi kuingia katika majengo hayo ya bunge la Congress na katika jukwaa ambalo anatarajiwa kuapishwa muda mfupi ujao.

    Dakika chache zijazo atakuwa mwanamke wa kwanza mwenye asili ya mtu mweusi na ile ya Kihindi kuwa Makamu wa Rais katika historia ya Marekani.

    Alisimama kando ya Makamu wa rais Mike Pence na kuwasalimia waliofika katika jukwa hilo.

  4. Viapo vya rais si rahisi kama inavyoonekana

    Viapo vya rais sio rahisi kama inayoonekana Kabla ya kulipa kiapo , katiba inahitaji kila rais kula kiapo.

    Franklin D Roosevelt alikula kiapo hicho na kuweka rekodi mara nne , baada ya kushinda uchaguzi mara nne.

    Lakini anayeshikilia rekodi hiyo na rais Obama ambaye alihudumu kwa mihula miwili. Hivyobasi tunauliza inakuwaje?

    Mwaka 2009, wakati alipokuwa akiapishwa kwa mara ya kwanza , Obama aliruka mshororo muhimu baada ya makosa ya Jaji mkuu John Roberts ambaye alikuwa akimuapisha.

    Obama alikula kiapo wakati wa sherehe ya faragha katika Ikulu ya Whitehouse na mara ya pili hadharani siku iliofuata.

    Yeye si rais wa kwanza kukosea wakati wa kula kiapo Marais wengine watano pia wametatizika. Lakini yeye ndio rais wa pekee kula kiapo kwa mara nyingine kama marekebisho.

    Mwaka 1929, makosa katika kiapo cha Herbert Hoover yaligunduliwa na msichana mwenye umri wa miaka 13 , Helen Terwilliger, ambaye alikuwa amekariri maneno na alikuwa akisikiliza redioni.

    Baadaye alimuandikia Jaji mkuu William taft , ambaye alikiri makosa yake lakini akasisitiza kwamba haikuharamisha urais wa Hoover.

  5. Kuapishwa kwa Joe Biden: Kiapo cha kwanza kufanyika saa moja ijayo

    Tunatarajia Kamala Harris kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke baada ya chini ya saa moja.

    Ataapishwa na Jaji wa Mahakama ya Juu Zaidi Sonia Sotomayor ikiwa hafla ya kihistoria kwa njia tofauti.

    Mwanamke wa kwanza mwenye asili ya Kihindi na mtu mweusi , na Makamu wa Rais atakula kiapo kutoka kwa Mmarekani mlatinI wa kwanza.

    Imeripotiwa kuwa Harris alimchagua Sotomayor kuchukua jukumu hilo pia atatumia biblia mbili kula kiapo hicho, moja ikitoka kwa Thygood Marshall jaji wa kwanza mweusi katika mahakama ya juu zaidi.

    Joe Biden ataapishwa na Jaji mkuu John Roberts kama ilivyo utamaduni.

  6. Kuapishwa kwa Joe Biden: Wageni waanza kuwasili

    Wageni wameanza kuwasili US Capitol saa chache kabla ya shughuli ya kuapishwa kwa Biden.

    Idadi ya watu si kubwa mwaka huu kutokana na tahadhari ya virusi vya corona.

    Miongoni mwa walioonekana kuwasili ni Rais wa zamani Barack Obama na mkewe Michelle Obama na Seneta mteule wa Georgia Jon Ossof,ambaye anatarajiwa kuapishwa baadae hii leo.

  7. Kenya 'kupokea dozi milioni 24 za chanjo ya corona mwezi ujao'

    Kenya inatarajia kupokea dozi milioni 24 za chanjo ya ugonjwa corona iliyotengenezwa na kapuni ya Astrazeneca na chuo kikuu cha Oxford mwezi ujao, kulingana na shirika la habari la Reuters.

    Waziri wa Afya Mutahi Kagwe nchini Kenya amesema kuwa chanjo hizo ziliagizwa kupitia mpango wa Umoja wa Afrika.

    Waziri wa mambo ya nje Uingereza, Dominic Raab, ambaye yuko nchini humo kwa ziara ya siku moja, amenukuliwa akisema Uingereza ilikuwa inasaidia Kenya kujitayarisha kuanza kutoa chanjo hiyo.

    "Ni wajibu wetu sio tu kimaadili, lakini ni kwa maslahi ya Uingereza kuona raia wa Kenya wakipata chanjo hiyo haraka iwezekanavyo kadri ya uwezo wetu," Bwana Raab amenukuliwa akisema.

    Kenya ina idadi ya watu takriban milioni 48, kulingana na takwimu ya idadi ya watu mwaka 2019. Na hadi kufikia sasa nchi hiyo imethibitisha maambukizi 99,308 ya virusi vya corona huku watu 1,130,707 wakifanyiwa vipimo vya virusi hivyo.

    Pia, watu 82,478 wamethibitishwa kupona ugonjwa huo wa corona huku idadi ya vifo ikiwa 1,734.

  8. Kuapishwa kwa Joe Biden kuna maana gani kwa Afrika?

    Dunia itakuwa inatazama Joe Biden akiapishwa kama rais wa 46 wa Marekani baadaye hii leo.

    Ushindi wake katika uchaguzi wa Novemba uligonga vichwa vya habari barani kote kwasababu kitakachotokea kwa Marekani kinaathiri nchi zote duniani.

    Marekani ina wanajeshi waliopo katika maeneo mbalimbali kote barani Afrika na uchumi wetu unafungamana kupitia biashara na uwekezaji.

    Rais anayeondoka madarakani, Donald Trump, hakuwa kila siku akizungumza mazuri juu ya bara hili.

    Je sera zake zilikuwa na malengo mazuri kwa Afrika? vipi sasa kuhusu utawala mpya?, na je Biden huenda ana maanisha nini kwa nchi za Afrika?

    Soma hapa kujua matarajio ya Afrika kwa Biden:

    Pia tazama:

  9. Aliyekuwa askofu mkuu wa Kianglikana avuliwa cheo kwa tuhuma za uzinzi

    Kanisa la Kianglikana nchini Uganda limemvua cheo aliyekuwa askofu mkuu wa kanisa hilo, Stanley Ntagali, na kusitisha utendaji wa majukumu ya uaskofu pamoja na kuzuiwa kuwakilisha kanisa hilo kabisa kwasababu ya madai ya uzinzi.

    Bwana Ntagali alistaafu mwaka jana Machi baada ya kuhudumu kwa miaka 43 kama askofu.

    Katika taarifa ya Januari 13 kwenye tovuti ya kanisa la Kianglikana mrithi wake Dkt. Stephen Samuel Kaziimba, amesema Bwana Ntagali alijihusisha na mahusiano na mwanamke mmoja aliyekuwa kwenye ndoa na hilo alilifahamu.

    "Alisaliti ofisi ya Askofu, kiapo alichokula wakati wa kuapishwa, na maadili mema aliyotekeleza kwa kujitolea," Dkt. Kaziimba ameongeza.

    Dkt. Kaziimba amesema kanisa la Uganda limejitolea kuwa na uwazi pamoja na kutoa uangalinzi wa uchungaji kwa wale ambao wameathirika na hali hiyo na kutoa wito wa maombi kwa wanandoa wote, kuomba msahama na maridhiano.

    Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana Amerika Kaskazini, Foley Beach, pia naye alitoa taarifa yake akionesha kusikitishwa na tukio hilo.

    "Stanley ni ndugu katika Yesu ambaye nimekuwa nikifurahia kufanya kazi naye kwa miaka mingi na inanisikitisha sana kusikia mambo hayo. Ni maombi yangu mbele ya Mungu kuwa ataendelea na njia ya kuomba msamaha na kwamba Mungu atafariji wote walioathirika na dhambi hii."

    Stanley Ntagali, aliyekuwa Askofu hakupatikana kutoa maoni yake kuhusiana na kusimamishwa uaskofu.

    Lakini raia wengi wa Uganda watamkumbuka kwa kuzungumzia kile ambacho alikiona kama maadili mabaya nchini humo, 2019 aliyenukuliwa na gazeti la eneo akishauri watu “kudhibiti matamanio yao ya kingono”.

    Kanisa la Kianglikana nchini Uganda limekadiriwa kuwa na wafuasi milioni 13.

  10. Shule ya UWCEA Tanzania yasitisha masomo ya ana kwa ana kutokana na corona

    Shule ya kimataifa ya UWCEA kampasi ya Moshi, kaskazini mwa Tanzania imesitisha mafunzo ya ana kwa ana baada ya mwanafunzi mmoja kuthibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na tovuti ya shule hiyo, Januari 18 mwanafunzi huyo alithibitishwa kuwa na corona na jana Jumanne mwanafunzi mwingine ameonesha dalili za maambukizi ya virusi hivyo, lakini bado haijathibitishwa kama ana maambukizi.

    Kutokana na hali hiyo, shule hiyo ambayo ilikuwa ikitambulika awali kama International School of Moshi (ISM) imesitisha mafunzo ya ana kwa ana na kugeukia mafunzo kwa njia ya kidijitali hadi Februari mosi.

    Kumekuwa na wasiwasi mitandaoni hivi karibuni nchini Tanzania kuwa maambukizi ya virusi hivyo yamerejea kwa kasi nchini humo. Hata hivyo taarifa rasmi kutoka serikalini ni kuwa "ugonjwa huo umekwisha".

    Akiwa mkoani Kagera jana Jumanne rais John Magufuli amesihi wakulima nchini humo kuongeza kiwango cha uzalishaji wa chakula akibashiri uhaba wa chakula duniani baadaye mwaka huu kwasababu ya janga la virusi vya corona.

    "Mwaka huu kuna uwezekano wa kutokea kwa baa kubwa la njaa duniani kwa sababu watu wengi wanazingatia hatua za kutotoka nje kujikinga dhidi ya corona, lakini hilo halistahili kutukatisha tamaa kwasababu hata sheria hizo zikiwekwa bado watahitaji kula, tutakuza mazao na kuyauza."

    Takwimu rasmi ya idadi ya maambukizi na vifo vya corona ilitolewa kwa mara ya mwisho mwezi Aprili 2020, kufikia mwezi Juni rais Magufuli akatangaza kuwa "corona imekwisha Tanzania kutokana na maombi ya wananchi."

    Tanzania imekosolewa vikali kutoka pande mbalimbali ikiwemo na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa namna ilivyokabiliana na janga hilo.

  11. Kuapishwa kwa Biden: Nyimbo ya Burna Boy kuimbwa wakati wa kuapishwa kwa Biden

    Msanii wa Nigeria Burna Boy amejumuishwa katika orodha ya miziki itakayochezwa wakati wa sherehe ya kuapishwa kwa rais mteule Joe Biden.

    Nyimbo ya Burna kwa jina Destiny itakuwa miongoni mwa nyimbo za wasanii wengine wa kimataifa.

    Orodha ya nyimbo hizo 46 zimeandaliwa katika sherehe ya kuapishwa kwa Biden, taarifa hiyo imesema.

    "Wasanii na nyimbo zilizochaguliwa ujumuisha taswira ya kila mmoja Marekani. Wanafungua ukurasa mpya na watasaidia kuleta watu pamoja wakati utawala wa Biden na Harris unaanza kazi yake muhimu ya kuunganisha nchi yetu," taarifa hiyo imesema.

    Nyimbo nyingine zilizochaguliwa ni pamoja na wasanii wakubwa kama Beyoncé na nyimbo yake Find Your Way Back, Kendrick Lamar na Mary J. Blige‘s na wimbo wao Now Or Never, Bob Marley na Wailers na nyimbo yao Could You Be Loved pamoja na Levitating hit ya Dua Lipa.

  12. Kuapishwa kwa Biden: Vyombo vya habari Afrika vyaangazia kumalizika kwa utawala wa Trump

    Wakati Marekani inajitayarisha kumuapisha rais mteule Joe Biden, vyombo vya habari Afrika vimekuwa vikiangazia mwisho wa utawala wa Donald Trump na kile wanachotarajia katika utawala mpya.

    Leo hii gazeti la Kiswahili la Taifa Leo nchini Kenya limeandika kichwa cha habari, "Trump aicha Marekani kwa aibu na uharibifu mkubwa".

    Mwandishi wa makala Nigeria Hannatu Musawa ameandika kuwa, dunia inasubiri kwa hamu kitakachotokea kwa Donald Trump baada ya urais, alimuelezea Trump kiongozi kama mwenye “kujisifu na jeuri”.

    “Asante Mungu tunakaribia kuona mwisho wa ukurasa huu wenye kuchosha, mtu ambaye angefanya lolote kwa pesa zake na anachokipenda, mwenye majivuno na angetaka umiliki wakati wowote ule!” ameandika katika makala ya Premium Times.

    Mwandishi wa makala ya ThisDay, Chidi Amuta, ameandika Januari 17 kwamba “Trump anakaribia kuanza maisha yasio na nguvu yoyote”.

    Katika gazeti la Daily Nation sehemu ya maoni, Profesa Makau Mutua mwanasheria msomi alisema kuwa Trump anaondoka Ikulu ya Marekani akiwa na “damu mkononi mwake” – akirejelea kilichotokea Januari 6 katika uvamizi wa jengo la bunge la Capitol Hill.

    Katika makala ya vichekesho iliyochapishwa na gazeti la Afrika Kusini la Africa’s Daily Maverick Januari 19, Pieter-Dirk Uys alisema kuwa ingawa Trump anaondoka madarakani, “hataondoka tu kama moshi”.

    “Atatafuta namna ya kurejea, pengine kama kiongozi aliyeibiwa anayeishi ughaibuni katika eneo la nyumbani.”.

    Katika mitandao ya kijamii, maneno yanayoandikwa zaidi ni #InaugurationDay, #Presidency, #Trump yanatumika sana kwasababu watumiaji wakionesha matarajio yao kabla ya kuapishwa kwa Biden.

  13. Jose Chameleone kwenye kinyang'anyiro cha umeya Kampala

    Nyota wa muziki wa Hip hop nchini Uganda Joseph Mayanja maarufu kama Jose Chameleone ni miongoni mwa wagombea wa nafasi ya meya wa jiji la Kampala.

    Uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa unafanyika leo nchini Uganda, pamoja na Meya wa majiji kukiwa na ushindani mkali katika jiji la Kampala.

    Meya anayetetea kiti chake ni Elias Lukwango wa chama cha FDC anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa msanii Jose Chameleon ambaye ni mgombea wa kujitegemea, na msanii mwingine anayewania kiti hicho ni Danel Kazibwe maarufu kama Ragga D kutoka chama tawala na mgombea mwingine ni Nabilah Naggayi kutoka chama cha Bobi Wine.

    Wakati huo huo tume ya uchaguzi ikiwa imepokea matokeo ya vituo 1200 vya kupiga kura ambavyo havikujumuishwa wakati akitangazwa rais Museveni kuwa mshindi.

  14. Trump amsamehe aliyekuwa mshauri wake dakika za mwisho madarakani

    Rais anayeondoka madaraka Donald Trump amsamehe aliyekuwa mshauri wake Steve Bannon, ambaye anakabiliwa na mashitaka ya udanganyifu.

    Tangazo hilo linawadia saa kadhaa kabla ya kuapishwa kwa rais mteule Joe Biden.

    Bwana Trump pia amewahurumia watu wengine zaidi ya 140 saa zake za mwisho madarakani.

    Miongoni mwa waliosamehewa ni rapa Lil Wayne huku rapa mwingine Kodak Black na aliyekuwa meya wa Detroit Kwame Kilpatrick wakipunguziwa vifungo vyao.

    Kwa ujumla watu 73 wamepewa msahamaha huku wengine 70 vifungo vyao vikapunguzwa, taarifa kutoka Ikulu ya Marekani imesema. Bwana Bannon, ambaye alikuwa mshauri mkuu wa Rais Trump wakati wa kampeni yake mwaka 2016, alipatikana na hatia mwaka jana kwa makosa ya udanganyifu juu ya kampeni ya kuchangisha pesa kujenga ukuta katika mpaka ya Marekani na Mexico.

    Waendesha mashitaka Bwana Bannon na wengine watatu walilaghai wengine mamia ya maelfu ya wafadhili kuhusiana na mradi wa "Tujenge Ukuta" kampeni ambayo ilikusanya dola milioni 25.

    Inadaiwa kuwa Bwana Bannon alipokea zaidi ya dola milioni 1 ambazo baadhi ya pesa hizo alizitumia kwa matumizi yake binafsi.

    Alikanusha makosa hayo na alikuwa ahukumiwe. Ikulu ya Marekani imesema Bwana Bannon amekuwa "kiongozi muhimu na anajulikana kwa hekima yake katika siasa".

    Taarifa hiyo ilisema kwamba waendesha mashitaka walikuwa wamemfungulia mashitaka yenye kuhusishwa na ulaghai kutokana na kujihusisha kwake kwenye mradi wa siasa.

  15. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja ya BBC Swahili Jumatano 20/01/2021