Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Uchaguzi Uganda 2021: Vyombo vya usalama vyaanza doria baada ya kura kupigwa Uganda

Raia wa Uganda hii leo wanashiriki katika shughuli ya kihistoria ya kumchagua rais na wawakilishi wa bunge lao

Moja kwa moja

Abdalla Seif Dzungu and Dinah Gahamanyi

  1. Matokeo ya uchaguzi Uganda 2021:Kura zikihesabiwa katika vituo mbalimbali

    Kura zinaendelea kuhesabiwa katika vituo mbalimbali huku maafisa wa usalama wakiwa katika mitaa mbalimbali kuhakikisha wanazuia wananchi kubaki kwa madai ya kulinda kura zao.

    Mwandishi wa BBC Munira Hussein ametuandalia picha zifuatazo;

  2. Matokeo ya Uchaguzi Uganda 2021: Vyombo vya usalama vyaanza doria

    Zoezi la kuhesabu kura limeanza katika baadhi ya vituo vya kupigia kura nchini Uganda.

    Idadi ya askari ilianza kuonekana kuongezeka saa moja kabla ya vituo vya kupigia kura kufungwa saa kumi jioni.

    Malori yakiwa yamewabeba wanajeshi wakizunguka mjini huku polisi na vikundi vya usalama vikiwa vinafanya doria.

    Katika baadhi ya maeneo, watu bado wanapiga kura kwa kuwa taratibu za uchaguzi zinaruhusu watu wote waliokuwa wamepanga foleni kabla ya muda wa vituo vya upigaji kura kufungwa kupiga kura.

    Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 35 anawania tena kuchaguliwa kwa muhula wa sita.

    Rais Museveni mwenye umri wa miaka 76-anakabiliana na wapinzani 10 huku mpinzani wake mkuu akiwa mwanamuziki aliyeamua kuwa mwanasiasa Bobi Wine, mwenye umri wa miaka 38.

    • Uchaguzi Uganda 2021: Museveni apiga kura muda mfupi kabla ya vituo kufungwa

      Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, 76, amepiga kura ikiwa zimesalia chini ya dakika 15 kabla ya vituo vya kupiga kura kufungwa.

      Vituo vya kupiga kura vimefungwa saa kumi jioni ingawa watu waliokuwa kwenye foleni wanaruhusiwa bado kupiga kura.

      Rais Museveni, amekuwa madarakani tangu mwaka 1986, na sasa anawania muhula wa sita.

      Mpinzani wake mkuu akiwa Bobi Wine,38, mwanamuziki aliyeamua kuwa mwanasiasa.

      Rais amepiga kura katika mji wa Rushere Magharibi mwa nchini Uganda.

    • Uchaguzi Uganda 2021: Mashine za uhakiki wa wapiga kura zashindwa kufanya kazi

      Mashine za uhakiki wa wapiga kura nchini Uganda zimeshindwa kufanya kazi katika baadhi ya vituo vya kupigia kura ambavyo BBC ilivitembelea.

      Msemaji wa Tume ya uchaguzi, Paul Bukenya, amesema kuwa walipokea taarifa kwamba baadhi ya vifaa hivyo havifanyi kazi.

      Vifaa hivyo vya kieletroniki hutumiwa kunasa na kuhakiki taarifa za wapiga kura kabla ya kutolewa kwa karatasi za kupiga kura.

      Foleni ndefu ilionekana katika vituo vya kupigia kura ambavyo BBC ilivitembelea BBC, japo kulikuwa na ucheleweshaji wa vifaa vya kupigia kura katika baadhi ya vituo.

      Upigaji kura ulipangwa kuanza saa moja asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki ingawa kwa baadhi maeneo ulichelewa.

    • Magufuli asema 'Maalim Seif amefanya maamuzi ya kishujaa'

      Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amempongeza mwanasiasa wa upinzani Maalim Seif Shariff kwa kukubali kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) visiwani Zanzibar.

      Rais Magufuli amesema kuwa uamuzi huo wa Maalim Seif ulikuwa ni wa busara na ulioangalia maslahi ya Zanzibar.

      "Uliacha maslahi yako binafsi, ukafanya uamuzi mkubwa na wa busara kwa maslahi ya Wazanzibari," ameeleza Magufuli na kuongeza: "Kuna ndoa zilivunjika, hasa Pemba kutokana na uchaguzi kwa kuwa mwanamke kapigia kura CCM na mume ACT, lakini baada ya maamuzi ya Maalim Seif wanandoa hao wakarudiana."

      Maalim Seif, kutoka chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo alipinga matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar mwezi Oktoba 2020 ambapo alipata 19.78% ya kura za urais huku mpinzani wake Hussein Mwinyi akipata ushindi wa 76.27% na kuapishwa kuwa rais.

      Hata hivyo, mwezi Disemba ACT ikatangaza kukubali kuingia katika serikali ya Zanzibar kama katiba ya visiwa hivyo inavyoelekeza na kupendekeza jina la Maalim Seif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais. Maamuzi hayo yalipokelewa kwa hisia mseto huku baadhi ya wanaharakati wakikikosoa chama hicho kwa 'kuwasaliti wananchi'.

      Rais Mwinyi na Maalim Seif wapo nyumbani kwa rais Magufuli wilayani Chato kwa ziara ya siku mbili.

    • Chuck Norris akana kushiriki ghasia katika jengo la Capitol Hill

      ‘Sio mimi!’, Chuck Norris akana kuwa katika ghasia za Capitol Hill.

      Msanii wa filamu Chuck Norris amelazimika kukanusha kutoshiriki katika vurugu zilizotokea wiki iliyopita katika jengo la bunge la seneti la Marekani- Capitol Hill, baada ya picha ya mtu aliyefanana na yeye kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

      Baada ya maandamano hayo, picha hiyo ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ya wafuasi wa Rais Donald Trump, ambao walimshirikisha picha ya mtu huyo Chuck Norris ambaye sasa ana umri wa miaka 80.

      Picha ya mwanaume huyo ambaye anafanana na Chuck Noris , ilisababisha mkanganyiko, huku wengi mtandaoni wakiamini nyota huyo wa filamu kweli alikuwa miongoni mwa watu waliosababisha vurugu katika Capitol Hill.

      Norris alipata umaarufu baada ya kuonekana katika filamu ya Bruce Lee ya Way of the Dragon na kuwa mchezaji filamu za stalwart ikiwa ni pamoja na Delta Force.

    • Uchaguzi Uganda 2021: Sanduku la kura laibiwa

      Msemaji wa Tume ya uchaguzi nchini Uganda amesema Sanduku la kura lililokuwa na kura ndani yake limeibiwa katika eneo la Rushenyi wilayani Ntungano Mashariki mwa nchini humo.

      Bw Paul Bukenya amesema tukio la wizi huo limeripotiwa kwa kitengo cha Tume ya uchaguzi cha malalamishi na kwamba polisi wanamtafuta mtu aliyeliiba.

      Bw Bukenya amesema kuwa watu wa eneo hilo wataweza kupiga kura yao licha ya kuibiwa kwa sanduku, lakini tukio kama hilo ni la bahati mbaya kwasababu linavuruga mchakato.

      "Tunalishughulia suala hili na tutawafahamisha mambo yatakavyokuwa", amesema Bw Bukenya.

    • Mchungaji wa Kenya ahukumiwa miaka 140 baada ya kuwabaka binti zake wawili

      Mahakama nchini Kenya imemfunga kifungo cha miaka 140 jela mchungaji aliyewabaka wasichana wake wawili wa miaka 14 na miaka 16 na kuwapatia mimba.

      Akitoa hukumu hiyo hakimu mkazi wa Baricho Anthony Mwicigi, alimuhukumu Mchungaji John Gichira

      kifungo cha miaka 70 kwa kila msichana . Mahakama iliamua kuwa hukumu hizo zitatekelezwa moja baada ya nyingine na hivyo mchungaji huyo ataishi jela miaka 140.

      Mchungaji huyo kutoka kaunti ya Kirinyaga kati kati mwa Kenya, mwenye umri wa miaka 51 alikiri kuwabaka watoto wake tarehe 5 Januari na kuwekwa jela tangu tarehe 7 Januari. Alimlaumu shetani kwa ubakaji huo watoto wake na akawaomba msamaha watoto wake na mahakama.

      Hakimu mkazi Anthony Mwicigi alisema kuwa mchungaji huyo alipataikana na hatia kwa kukiri mwenyewe kuwabaka watoto wake na akaagiza hukumu dhidi yake itolewe tarehe 14 Januari.

      Mchungaji huyo anayefahamika kwa jina la Gichina alikamatwa mahala alipokuwa amejificha baada ya polisi kuanzisha harakati za kumsaka.

      Msichana mmoja tayari ana mtoto wa miezi 7 na mwingine ana mtoto wa miezi 5.

    • Wanajeshi wa Msumbiji wawaokoa raia waliotekwa na Islamic State

      Wanawake 15 na watoto sita waliokuwa wametekwa na wanamgambo wa Islamic State katika jimbo lenye utajiri wa mafuta la Cabo Delgado nchini Msumbiji wameokolewa na jeshi.

      Wengi wao walikuwa wametekwa kutoka katika kisiwa cha Matemo wiki iliyopita, kulingana na mkuu wa polisi Bernardino Rafael.

      Mapigano ya hivi karibuni yanaonesha kua vikosi vya usalama vilifahamu ni wapi walipokuwa wanamgambo hao, kwa hiyo kwa usaidizi wa helikopta waliweza kuwazingira na kuwatenganisha na watekaji wao, alisema.

      Watarejeshwa tena Matemo, eneo ambalo limezongwa na mashambulizi tangu mwezi Oktoba.

      Lakini mkuu wa polisi amesema kuwa kisiwa hicho ni salama kwa sasa.

      Wanamgambo wa IS, wanaofahamika na wakazi kama al-Shabab, au vijana , wamefanya mashambulio kadhaa katika vijiji na miji katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka mitatu.

      Hivi karibuni zaidi waliahidi kulitii kundi la IS , na wanafahamika kwa mashambulio ya ukatili, ambayo huwa ni pamoja na kuwakata vichwa wanavijiji na kuchoma moto nyumba.

      Mara nyingi huwateka wanawake na watoto ambao hutumiwa kama watumwa wa ngono na kusafirisha bidhaa walizoiba kufuatia mashambulio.

      Mwishoni mwa juma, Waziri wa ulinzi wa Marekani alisema kuwa Anthony Tata, naibu waziri wa mashauri ya kigeni anayehusika na masuala ya sera alitembelea Msumbiji Ijumaa na kufanya mazungumzo na mawaziri juu ya umuhimu wa mpango wa kimkakati wa kuleta utulivu katika jimbo la Cabo Delgado.

      Taarifa kutoka ubalozi wa Marekani inasema kuwa Marekani itatoa msaada wa kibinadamu na kiuchumi wa dola milioni 42 kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika jimbo hilo lililopo kaskazini mwa nchi.

      Juhudi hizi na nyinginezo, kwa mujibu wa balozi Dennis Hearne, ni sehemu ya msaada wa kila mwaka wa dola milioni 500 ambao Marekani hutoa kwa Msumbiji.

    • Uchaguzi Uganda 2021: Bobi Wine athibitishwa kupiga kura Uganda

      Mgombea mkuu wa upinzani nchini Uganda Bobi amethibitishwa kupiga kura yake mapema leo .

      Bobi Wine anawania urais nchini Uganda kwa mara ya kwanza huku akidaiwa kutoa upinzani mkali kwa rais aliyepo madarakani Yoweri Museveni.

      Yupo katika kinyanganyiro hicho kwa ahadi ya kuvutia uwekezaji na kuwapatia ajira vijana iwapo atachaguliwa.

    • Uchaguzi wa Uganda 2021: Siku ya uchaguzi kwa picha

      Waandishi wa BBC waliopo nchini Uganda wametembelea maeneo mbali mbali kushuhudia shughuli ya upigaji kura iliyoanza saa moja kamili kwa saa za Afrika Mshariki.

      Hizi ni baadhi ya picha kuhusu uchaguzi wa Uganda na hali kwa ujumla ilivyo katika mji mkuu Kampala.

    • Wanaowatumia walemavu kujipatia kipato wafikishwa mahakamani Tanzania

      Watu 15 akiwemo mfanyabiashara, Sadikiely Meta (71) wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 41 yakiwemo ya kufanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu kinyume cha sheria, kukwepa kodi na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh31 milioni.

      Kulingana na mtandao wa mwnanchi nchini Tanzania , Meta na wenzake wanadaiwa kusafirisha wenye ulemavu 37, wakiwemo watoto wadogo wenye umri wa miaka saba na 11 kutoka mikoa ya Tabora, Shinyanga na kuwaleta Dar es Salaam na kisha kuwataka waombe fedha mitaani ili wao wajiingizie kipato.

      Kulingana na mtandao huo washtakiwa hao walisomewa mashtaka na wakili wa Serikali mwandamizi, Mkunde Mshanga akisaidiana na Wankyo Simon mbele ya hakimu mkazi mkuu, Kassian Matembele.

    • Uchaguzi wa Uganda 2021: Waganda wakosa huduma za intaneti mkesha wa uchaguzi

      Mamlaka nchini Uganda ilikatiza hudama za intaneti saa kadhaa kabla ya uchaguzi wa urais unaokumbwa na ushindani mkali kati ya nyota wa muziki na mmoja viongozi wa muda mrefu wa Afrika waliohudumu miaka mingi madarakani.

      Kundi la ufuatiliaji wa masuala ya Itaneti NetBlocks liliandika kwenye Twitter yake kwamba nchi hiyo ilizima mitandao yote ya intaneti Jumatano saa moja usiku majira ya Afrika Mashariki.

      Hatua hiyo ilifuatia agizo la serikali kufungia mitandao yote ya kijamii na programu tumishi za kutuma ujumbe.

      Rais Yoweri Museveni alisema alifikia uamuzi huo kwa sababu Facebook ilifunga akaunti kadhaa zinazounga mkono chama tawala.

      Mgombea wa urais,mwanamuziki aliyegeuka Bobi Wine aliandika katika Twitter yake kwamba huduma za intaneti zimekatizwa kama sehemu ya njama ya kuiba kura.

      "Watu wa Uganda wako imara na hakuna jambo lolote litakatiza azma yao ya kikomesha utawala wa kiimla," aliongeza.

      Shughuli za upigaji kura ilianza saa moja asubuhi ya leo Alhamisi, japo matokeo hayatarajiwi kutolewa kabla ya Jumamosi.

      Kampeni za uchaguzi zilikumbwa na ghasia ambazo zilisababisha vifo vya makumi ya watu.

      Bw. Museveni anagombea muhula wa sita baada ya kuwa madarakani kwa miaka 35.

    • Uchaguzi Uganda 2021: Milolongo mirefu yashuhudiwa kwenye vituo vya kupigia kura

      Milolongo mirefu imeshuhudiwa katika vituo vya kupigia kura katika mji mkuu Kampala, na maeneo menginge ya nchi

      Serikali imeamuru kufungwa kwa mitandao yote ya kijamii.

      Shughuli ya kupiga kura ilipangwa kuanza saa moja asubuhi na kukamilika saa kumi jioni kwa saa za Uganda, ingawa Tume ya uchaguzi nchini humo ilisema kuwa wapigakura wote waliojisajiri ambao watakuwa bado katika mstari wa kupiga kura wakati shughuli hiyo itakapofungwa, wataruhusiwa kupiga kura yao.

      Mgombea wa urais wa upinzani Bobi Wine anatarajiwa kupiga kura yake katika kituo kilichopo viungani mwa mji mkuu Kampala.

      Rais Yoweri Museveni atapiga kura yake kijijini kwao magharibi mwa Uganda.

      Baadhi ya wanadiploamsia wameelezea wasi wasi wao juu ya mchakato wa uchaguzi, wakielezea kukamatwa kwa wapinzani wakati wa kampeni zilizogubikwa na gasia.

      Pia wamezungumzia dhidi ya mashambulio dhidi ya uhuru wa kujieleza, baada ya serikali kuwaambia watoaji wa huduma za intaneti kukata huduma zao.

    • Yanga yaifunga Simba kutwaa Kombe la Mapinduzi

      Klabu ya Yanga imenyanyua Kombe la Mapinduzi baada ya kuwafunga watani wao wa jadi klabu ya Simba kwa mikwaju ya penati 4-3.

      Miamba hiyo ya soka nchini Tanzania ilimaliza dakika 90 za mchezo bila upande wowote kuliona lango la mwenzie katika dimba la Amaan visiwani Zanzibar.

      Matokeo ya mchezo huo yaliamuliwa kwa mikwaju ya penati ambapo Simba ilipoteza mikwaju miwili na Yanga ikapoteza mkwaju mmoja.

      Fainali hiyo iliyopigwa jana usiku ilikuwa ni ya pili kwa Yanga na ubingwa huo ni wa pili kwao. Simba imecheza fainali nane na kunyakua kombe hilo mara tatu.

      Kombe la Mapinduzi hufanyika kila mwaka mwezi Januari kuadhimisha Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

    • Uchaguzi wa Uganda 2021: Vifaa vya uchaguzi vyachelewa kufika katika baadhi ya vituo vya kupigia kura

      Waandishi wa habari walioko Uganda wanaripoti kuwa vifaa vya kupigia kura vimechelewa kufikishwa katika baadhi ya maeneo ya kupigia kura.

      Wale waliotweet kutoka vituo mbali mbali vya kipigia kura wamesema kuwa vifaa vilikuwa bado havijafikishwa katika vituo vya kupigia kura saa moja asubuhi, muda ambao upigaji kura ulitakiwa kuanza.

      Serikali imeamuru kufungwa kwa mitandao ya kijamii.

      Ufuatao ni baadhi ya ujumbe wa Twitter uliotumwa na waandishi wa habari kuhusu kuchelewa kwa shughuli ya kupiga kura.

    • Waziri wa zamani wa Masuala ya kigeni Ethiopia auawa na Jeshi

      Jeshi la Ethiopia limetangaza kwamba limemuua waziri wa zamani wa mambo ya nje Seyoum Mesfin, mmoja wa wanachama waanzilishi wa chama Tigray People’s Liberation Front (TPLF).

      Bw.Seyum, ambaye alihudumu kama waziri wa mambo ya nje wa kutoka mwaka 1991 hadi 2010, aliuawa pamoja na wanachama wengine wa ngazi ya juu TPLF kaskazini mwa jimbo la Tigray, wanajeshi walisema.

      Serikali ilikuwa imetoa waranti ya kukamatwa kwake- pamoja na viongozi wengine wa ngazi ya juu katika chama hicho – kufuatia oparesheni ya kijeshi ya mwezi Novemba eneo la Tigray. Zawadi ya birr milioni 10 sawa na ($254,000; £187,000) iliahidiwa kutolewa kwa wale watakaotoa taarifa zitakazosidia kukamatwa kwao.

      Jeshi linasema kwamba liliwaomba wajisalimishe lakini wakakata kufanya hivyo. Makumi ya wancahama wengine wa TPLF waliuawa na wengine kukamatwa katika oparesheni ya hivi punde, iliongeza kusema.

      Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliamuru oparesheni ya kijeshi dhidi ya jimbo la Tigray mnamo Novemba 4 na kuiondoa madarakani chama tawala, baada ya vikosi vyake kuvamia kambi ya majeshi ya serikali.

    • Uchaguzi Uganda 2021: Museveni akabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Bobi Wine

      Mwanamuziki nyota wa pop aliye na umri wa mika 38- anachuana kisiasa na mmoja wa viongozi wa Afrika aliyehudumu muda mrefu madarakani katika uchaguzi wa Uganda unaokabiliwa na ushindani mkali

      Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, anasema kuwa anawakilisha kizazi kipya cha vijana wa nchini humo, huku Yoweri Museveni, 76, akisema kuwa anasimamia ustawi.

      Kampeni zilikumbwa na vurugu ambazo zilisababisha vifo vya watu kadha.

      Serikali imeagiza kufungwa kwa mitandao yote ya kijamii.

      Rais Museveni anasema hii ni kwa sababu Facebook ilipiga marufuku akaunti kadhaa zinazounga mkono chama tawala.

      Sera ya polisi nchini Uganda inasema maafisa watapanda juu ya majengo marefu mjini Kampala siku ya uchaguzi, baaada ya magari yaliyo na silaha kuanza kuzunguka katika mitaa ya jiji hilo.

      Vituo vya kupiga kura vinafunguliwa saa moja kwa saa za Afrika Mashariki (04:00 GMT), lakini matokeo ya uchaguzi hayatarajiwi kutangazwa kabla ya Jumamosi.

      Rais Museveni anagombea muhula wa sita baada ya kuwa madarakani kwa miaka 35.

      Kampeni zilikuwa zimepigwa marufuku katika mji mkuu wa Kampala na katika baadhi ya wilaya.

      Upinzani unasema hatua hiyo ilichukuliwa kwasababu ya umaarufu wake lakini serikali inasema ilifikia uamuzi huo ili kudhibiti msambao wa ugonjwa wa Covid-19.

    • Uchaguzi Uganda 2021: Raia wa Uganda washiriki katika shughuli ya kihistoria leo

      Raia wa Uganda hii leo wanapiga kura kumchagua rais na wawakilishi wapya wa bunge .

      Akizungumza siku ya Jumatano mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini humo jaji Simon Byabakama aliserma kwamba wapiga kura wa kiume ni zaidi ya milioni tisa huku wenzao wa jiniai ya kike wakiwa zaidi ya milioni tisa.

      Katika uchaguzi huo rais Yoweri Museveni ambaye anatetea wadhfa wake anakabilia na upinzani mkali kutoka kwa mwanamuziki wa zamani maarufu Bobi Wine.

      Bobi Wine ni mgombea ambaye amevutia idadai kubwa ya vijana nchini humo.

      Rais Museveni anagombea muhula wa sita baada ya kuwa madarakani kwa miaka 35.

      Hatahhivyo rais Museveni anajivunia utawala wake wa muda mrefu ambapo amefanya baadhi ya maenedeleo.

      Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, anasema kuwa anawakilisha kizazi kipya cha vijana wa nchini humo, huku Yoweri Museveni, 76, akisema kuwa anasimamia ustawi.

    • Natumai hujambo. Karibu katika matangazo yetu hii leo moja kwa moja kutoka Uganda