Afrika Kusini imetangaza rasmi kukumbwa na wimbi la pili la maambukizi baada ya hapo jana kurekodi visa 7,000 vya maambukizi mapya. Vijana ndiyo wanalaumiwa kwa kuchochea wimbi hilo la pili katika taifa ambalo ndilo lililoathiorika zaidi na Covid 19 barani Afrika.
Waziri wa afya nchini humo Zweli Mkhize amesema zaidi ya maambukizi mapya yanaathiri wale wenye umri kati ya miaka 15 na 19 na inahofiwa kuwa katika baadhi ya maeneo Afrika Kusini, maambukizi ni makubwa hata kuliko yaliyoshuhudiwa katika wimbi la kwanza la mwezi Julai.
Zaidi ya watu elfu 22 wamefariki dunia Afrika Kusini kutokana na Corona. Nchi nyingine za Afrika kama Zimbabwe na Kenya pia zinaripoti maambukizi mapya.
Hata hivyo mpaka sasa, bara Afrika kwa jumla limenusurika kutumbukia katika hali mbaya ya mamabukizi na vifo kama inayoshuhudiwa Marekani na barani Ulaya. Shirika la afya duniani WHO hata hivyo linaonya kuwa katika kipindi cha siku saba zilizopita, Afrika imerekodi ongezeko la zaidi ya asilimia saba ya maambukizi.
Visa vipya 100,000 vimerokodiwa na watu 100 wamefariki dunia wiki moja iliyopita. Nchi zinazojumiusha asilimia sabini ya maambukizi Afrika ni Afrika Kusini, Morocco, Misri, Tunisia na Ethiopia. Morocco imepokea dozi milioni mbili ya chanjo ambayo wahudumu wa afya na walio na matatizo ya kiafya watapewa kipaumbele. Chanjo hiyo itapeanwa bila malipo.
Kimataifa, Marekani imerekodi zaidi ya vifo elfu tatu katika kipindi cha siku moja pekee, hiyo ikiwa ni idadi ya juu zaidi ya vifo kwa siku vitokanavyo na Covid 19 kuwahi kurekodiwa kokote ulimwenguni. Nayo Afrika Kusini inaripoti wimbi jipya la maambukizi, vijana wakilaumiwa kwa kusababisha wimbi hilo.
Marekani inasalia kuwa nchi iliyoathirika zaidi na maradhi ya Covid 19 ulimwenguni, huku mamilioni wakiwa wameambukizwa na takriban watu laki tatu wakiwa wamefariki dunia nchini humo kutokana na virusi hivyo vya Corona ambavyo vimeutikisa ulimwengu kwa karibu mwaka mmoja sasa tangu vilipozuka nchini China mwezi Desemba mwaka jana.
Tukitupia macho muenendo wa Corona katika mataifa ya Ulaya, siku moja baada ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kuwatolea wito Wajerumani kukubali hatua kali zaidi za sitisho la shughuli ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi, visa elfu 23 mia sita sabini na tisa vipya vimerekodiwa katika taifa hilo imara zaidi kiuchumi barani Ulaya.
Waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Markus Soder amesema sitisho kamili linapaswa kutekelezwa kuanzia Krisimasi hadi tarehe 10 Januari.
Nchi jirani na Ujerumani, Waziri mkuu wa Ufaransa Jean Castex anatarajiwa kutangaza kulegezwa kwa masharti yaliyowekwa na serikali mwezi uliopita kudhibiti maambukizi, serikali ya Ufaransa ilikuwa imetarajia maambukizi yatapungua hadi chini ya elfu tano kwa siku lakini hapo jana, maambukizi mapya elfu kumi na nne yaliripotiwa nchini humo, kwa hiyo kumbi za burudani zitasalia kufungwa kwa muda kiasi.