'Nawaomba kwa heshima kubwa mtuheshimu ndio tuwaheshimu'
Rais Uhuru Kenyatta hii leo amefungua rasmi kongamano la magavana kujadili mikakati ya kuboresha uchumi jijini Nairobi.
Moja kwa moja
Asha Juma
'Nawaomba kwa heshima kubwa mtuheshimu ndio tuwaheshimu', Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta hii leo amefungua rasmi kongamano la magavana kujadili mikakati ya kuboresha uchumi jijini Nairobi.
Katika hotuba yake, Rais Uhuru Kenyatta ametupia kidole cha lawama nchi za nje juu ya kile alichosema ni kujaribu kuingilia na kuelekeza Kenya namna ya kuendesha shughuli zake.
Kiongozi huyo wa nchi amesema, Kenya inashukuru uungwaji mkono na ushirikiano inayopata kutoka kwa nchi zingine lakini nchi yake haitakubali kulazimishwa cha kufanya na yeyote yule.
“Tunashukuru maafisa wa Umoja wa Mataifa na washirika wengine wa maendeleo ambao wamekuwa karibu sana lakini hadi kufikia sasa lazima niweke wazi, wakati tunawashukuru kwa ushirikiano wenu na kutajarajia ushirikiano zaidi, lazima mkumbuke Kenya ina wenyewe na wenyewe ni Wakenya milioni 50,” amesema Kenyatta.
Aidha, Rais Uhuru Kenyatta aliwaomba kujizuia kujaribu kuwaelekeza cha kufanya na njia ya kufuata.
“Tunakoelekea kuko wazi. Tunakuomba ujiunge nasi, utuunge mkono katika juhudi zetu hizo. Lakini usiingilie kwasababu hatutakuruhusu uamuru njia tunayostahili kufuata. Nawaomba kwa heshima kubwa mtuheshimu ndipo tutakapo waheshimu. Kila mtu yuko na shida zake hata wao wana shida zao wanazohitajika kuzitatua huko kwao. Nasema hivyo kwa nia njema tu. Sitaruhusu hilo na kama nchi hatutaruhusu hilo.”
Twiga waliokwama wahamishwa kwa njia ya maji

Wanamazingira, maafisa wa serikali na maafisa wa eneo nchini Kenya wameungana kuokoa twiga wanane waliokuwa wamekwama katika maeneo ya kisiwani.
Walijenga mashua za kusaidia wanyama kuvuka.
Na hadi kufikia sasa, wawili wamefanikiwa kupita salama.
Kwa mujibu wa David O’Connor wa Shirika la Save Giraffes, ameelezea BBC Newsday, kuwa juhudi hizo zilianza miaka mitatu iliyopita pale maji ya Ziwa Baringo yalipoanza kuongezeka.
Marais Barack Obama, George W Bush na Bill Clinton wajitolea kupata chanjo ya corona

Chanzo cha picha, Getty Images
Waliokuwa marais wa Marekani Barack Obama, George W. Bush na Bill Clinton wamejitolea kupewa chanjo ya ugonjwa wa corona kwa uwazi kabisa.
Watatu hao ambao wawili ni wa chama cha Democrat na mmoja wa Republican wamesema kuwa watapata chanjo hiyo punde tu itakapoidhinishwa na wadhibiti wa maafisa wa afya.
Hatua hiyo inakusudiwa kuimarisha imani ya raia juu ya usalama na ufanisi wa chanjo za virusi vya corona.
Kura za maoni zinaonesha kuwa idadi kubwa ya watu hawana haraka ya kupata chanjo hiyo.
Hadi kufikia sasa hakuna chanjo ambayo imeidhinishwa na Marekani lakini wadhibiti wa serikali wanaanza kufuatilia chanjo ya kampuni za kampuni za Pfizer na Moderna wiki zijazo.
"Nawaahidi itakapoanza kupatikana kwa watu walio katika hatari kubwa, nitaipata," Bwana Obama amesema katika mahojiano ya radio Jumatano SiriusXM.
"Huenda nikainywa kupitia televisheni au nichukuliwe video, ili watu wajue kwamba ninaamini sayansi."
Uchaguzi wa Uganda 2021:‘Museveni hajawahi kukutana na mpinzani jembe kama mimi’

Chanzo cha picha, Facebook/Bobi Wine
Mgombea urais wa upinzani nchini Uganda ambaye pia ni mwanamuziki, Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu kama Bobi Wine, amesema kuwa rais wa sasa Yoweri Kaguta Museveni hajawahi kukutana na mpinzani kama yeye.
Kyagulanyi amesema hayo wakati anarejelea tena kampeni zake jana Alhamisi maeneo ya Kibuku, Budaka na Manafwa.
Bobi Wine alivalia mavazi ya kujikinga na risasi kwa mara ya kwanza katika kampeni zake na kuwaarifu wafuasi wake kwamba kuanza wakati huo, anazungumza nao kama ‘Bobi Wine’ wala sio Kyagulanyi kwasababu yeye ni ‘upanga unaokata kote kuwili’.
“Mumemuona Kyagulanyi vya kutosha, sasa ni wakati wa Bobi Wine. Walipofyatulia gari langu risasi wengi walifikiria wakati umewadia wa mimi kusitisha kampeni zangu. Huu ni upanga unaokata kote kuwili. Na sasa ninajitokeza kama Bobi Wine,” mgombea huyo wa chama cha NUP alisema.
''Katika kipindi chake chote cha uongozi, miaka 34, Museveni hajawahi kukutana na mpinzani kama mimi na hii ndio sababu uongozi wake umeingiwa na wasiwasi,'' Bobi Wine alisema.
Aidha, Bobi Wine aliongeza, ‘Rais Museveni ana siku 40 pekee za kuwa madarakani na kumuhesabia siku hizo imeanza Desemba 4 ambazo zinaisha siku ya kupiga kura Januari 14, 2021.
Bobi Wine, pia katika kampeni yake, aliahidi Uganda mpya ambapo wahudumu wa afya watapewa kipaumbele na kupewa nyongeza ya mshahara hasa wakati nchi inapokabiliana na janga kama la virusi vya ugonjwa wa corona.
Soma zaidi:
'Aliyefariki akafufuka' kafariki kweli Kenya

Mwanaume mmoja nchini Kenya aliyedhaniwa amefariki dunia na kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti na "kupata tena fahamu" wiki jana, sasa amefariki kweli, kulingana na vyombo vya habari vya eneo.
Wiki iliyopita, inasemekana kuwa mhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti alikuwa anatayarisha mwili wake kuuweka kwenye chumba maalum kwa ajili ya wafu, kabla ya mwanaume huyo kupata fahamu ghafla na kuanza kupiga kelele.
Peter Kigen, 32, ambaye alikuwa ameugua kwa muda mrefu, alipekwa hospitali kupata matibabu na baadaye, akaruhusiwa kwenda nyumbani.
Akizungumza na gazeti la Kenya la Daily Nation, Alhamisi iliyopita, alisema kwamba ni mwenye furaha kuwa hai. "Hii ni kazi ya Mungu," ameliambia gazeti hilo.
Tukio hilo lilisabisha wengi kutoa maoni yao katika mitandao ya kijamii, na pia likajadiliwa katika bunge la kaunti ya Kericho.
Bunge hilo liliunda timu kuchunguza kile hasa kilichotokea taarifa ambayo iliwaondolea wahudumu wa afya lawama.
Alhamisi, msemaji wa familia alithibitisha kifo cha kweli cha mwanaume huyo kupitia gazeti za Kenya la Standard.
"Kigen alitangazwa kufariki dunia baada ya kufika hospitali ya kaunti ya Kericho alikopelekwa kutoka hospitali ya Kapkatet kwa matibabu zaidi," Hezbon Tonui amesema.
Gavana wa Nairobi Mike Sonko apigiwa kura ya kutokuwa na imani naye

Chanzo cha picha, MIKE SONKO/TWITTER
Madiwani 88 kati ya 122 wa kaunti ya Nairobi walipiga kura ya kutokuwa na imani na gavana wa Nairobi Mike Sonko hii ni idadi ambayo imepitisha kiwango cha thuluthi tatu kumuondoa gavana aliyemadarakani.
kitakacho fuata sasa ni wasilisho hilo matokeo hayo mbele ya bunge la Seneti ambapo hatma ya gavana wa Nairobi imo mikononi mwao.
Awali, gavana huyo alikuwa ametuma ombi katika mahakama kuu kusitisha hatua ya kuondolewa kwake akisema kwamba ni kinyume cha sheria na kinyume na katiba vilevile.

Chanzo cha picha, MIKE SONKO/TWITTER
Lakini je huu ndio mwisho wa Sonko kama gavana?
Kwa gavana ambaye kipindi fulani alikuwa mwenye nguvu na utawala wa aina yake, ikiwa bunge la seneti litadumisha matokeo ya kura ya kutokuwa na imani naye yaliyowasilishwa na bunge la kaunti, kitakachofuata itakuwa ni kuandaliwa kwa uchaguzi mpya katika kaunti hiyo kumchagua gavana na naibu wake na kutamatisha utawala wa gavana huyo aliyekuwa na madoido ya kipekee.
Na pia ikumbukwe, hadi anapigiwa kura ya kutokuwa na imani naye, Sonko alikuwa hana naibu gavana.
Mambo Muhimu kuhusu Mike Sonko
- Alizaliwa Februari 1975
- Alikuwa mbunge wa Makadara 2010-2013
- Alichaguliwa seneta wa Nairobi Machi 2013
- Alichaguliwa kuwa gavana wa Nairobi Agosti 2017
- Serikali ilitangaza kupunguza walinzi wake hadi watano 16 Mei, 2018
Soma zaidi kumhusu Sonko:
DR Congo yakumbwa na 'janga baya la njaa'

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu wapatao milioni 22 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanakabiliwa na ukosefu mkubwa chakula, hali hiyo ikiwa ni mbaya zaidi ikilinganishwa na mwaka jana, Shirika la Umoja wa Mataifa limeonya.
Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, “idadi hiyo imeongezeka kutoka milioni 15.6 mwaka 2019 hadi milioni 21.8.’’
Shirika hilo limesema hali hiyo imechangiwa na athari za janga la Covid-19 na kusababisha kupanda kwa bei ya chakula.
Wengi walioathirika na tatizo hilo ni kutoka kaskazini na kusini mwa mikoa ya Kivu, Ituri na Kasai, kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa -FAO.
Ukame wa Madagascar: Watu wanakula 'mchanga uliochanganywa na ukwaju'

Chanzo cha picha, EPA
Raia wa kusini mwa Madagascar wanakula mchanga uliochanganywa na ukwaju kwasababu ya kiangazi ambacho kimeharibu zao linalotegemewa na wenyeji, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.
"Tunauita udongo wenye kuhimili kiangazi kwasababu unaruhusu ukwaju kukua na kutusaidia kukabiliana na kiangazi," AFP imemnukuu mkulima wa eneo Doday Fandilava Noelisona.
"Siku hizi hatutafuti tena chakula bali tunatafuta mbinu za kupata kitu chochote cha kushikilia tumbo."
Matunda ya dungusi ambayo watu huyategemea yamekauka kwasababu ya ukosefu wa mvua.
Aidha, shirika la AFP limemnukuu mkulima mwingine, Avianay Idamy, ambaye anasema amegeukia uuzaji wa makaa kupata pesa za kukidhi mahitaji ya familia yake angalau waweze kula muhogo mara moja tu kwa siku.
Shirika la chakula dunia- WFP, linasema watu milioni 1.5 kusini mwa Madagascar wanahitaji msaada wa dharura wa chakula.
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja hii leo ikiwa ni tarehe 4/12/2020.
