Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

NEC: Tumepokea majina ya viti maalum kutoka Chadema

Tume ya taifa ya uchaguzi nchini Tanzania (NEC) imesema ilipokea barua zenye majina ya mapendekezo ya wanawake wabunge na madiwani wa viti maalum kutoka Chadema.

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo. Tukutane tena Jumatatu ijayo

    Tunakuaga kwa video hii ya ssichana wa miaka 10 tu aliyewanunulia wazazi wake nyumba:

    Akiwa na umri wa miaka 10 tu Emmanuella Samuel ametumia mapato yake aliyoyatengeneza kupitia mtandao wake wa You Tube kuwajengea wazazi wake nyumba. Amekuwa nyota katika chaneli ya You Tube maarufu ya mchekeshaji Mark Angel, tangu alipokuwa na umri wa miakamitano. Akimshukuru mama yake Emmanulla amesema mama yake anafaa kupewa nyumba nyingi.

  2. NEC: Tumepokea majina ya viti maalum kutoka Chadema

    Tume ya taifa ya uchaguzi nchini Tanzania (NEC) imesema ilipokea barua zenye majina ya mapendekezo ya wanawake wabunge na madiwani wa viti maalum kutoka chama cha demokrasia na maendeleo-Chadema.

    Tume imesema imepokea majina hayo tarehe 19, Novemba mwaka huu kutoka Chadema huku chama cha mapinduzi- CCM walikuwa wametuma majina yao Septemba 26.

    Na Novemba 20, kikao kilikaa kuteuwa wabunge hao 19 kutoka katika chama hicho kwa mujibu wa katiba na sheria ya Tanzania.

    Awali, Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika aliiambia BBC kuwa Chadema haijafanya uteuzi wa wabunge hao na vikao vya juu vya chama hicho vitakaa ili kufanya maamuzi.

    Hata hivyo Chadema iligoma kuteua wabunge wa viti maalumu wakidai kuwa hawatambui matokeo ya uchaguzi uliopita wakisema ulikuwa na kasoro lukuki, tuhuma ambazo hata hivyo zimekanushwa na mamlaka nchini humo.

  3. Abiy Ahmed akutana na ujumbe wa AU lakini ameuzuwia kwenda Tigray

    Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amekutana na Tume ya Muungano wa Afrika ambao uliwasili mjini Addis Ababa kujaribu kuleta upatanishi baina ya serikali na vikosi vya Tigray People's Liberation Front (TPLF) baada ya zaidi ya wiki tatu za mzozo.

    Awali Bw Abiy alisema juhudi za kimataifa za kuleta pande mbili mezani kwa ajili ya mazungumzo "hazikaribishwi", na tume ya AU haitaruhusiwa kukutana na maafisa wa Tigray.

    Baada ya mkutano wa Ijumaa na wajumbe watatu maalum wa AU, Bw Abiy amesema kuwa serikali yake inataka kuhakikishaulinzi wa raia, inafungua njia ya misaada ya kiutu, na itawakaribisha tena wakimbizi Waethiopia waliokimbilia Sudan.

    Hata hivyo, waziri mkuu huyo amesema serikali yake itaendelea na juhudi zake dhidi ya za kile alichokiita"kundi la TPLF ".

    Wajumbe wa AU envoys –Marais wa zamani Joaquim Chissano wa Msumbiji, Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia na Kgalema Motlanthe wa Afrika Kusini- hawataruhusiwa kusafiri kuelekea Tigray, serikali tayari imesema.

  4. Mzozo wa Tigray Ethiopia: Waziri Mkuu Abiy Ahmed ni nani?

    "Kwa mtazamo wangu, siamini Ethiopia inahitaji vita. Sitaki kujumuishwa miongoni mwa watu wanaopendelea suluhisho la kijeshi.

    Hiyo ilikuwa kauli ya Waziri Mkuu Abiy mwezi Septemba wakati jimbo la Tigray linaloongozwa na TPLF iliamua kufanya uchaguzi kupinga amri iliyotolewa na serikali kuu...Soma zaidi taarifa hii.

  5. Jimbo lateua ujumbe kwa ajili ya mazungumzo ya upatanishi

    Uongozi wa jimbo la Ethiopia la Tigray unasema kuwa umewateua wawakilishi wake kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Muungano wa Afrika (AU) pamoja na mashirika mengine ya kimataifa kuhusu usitishwaji wa mara moja wa mapigo na serikali ya Ethiopia.

    Katika taarifa yake, pia umetoa wito wakuwezeshwa kwa shughuli za misaada ya kiutu na kufanyika kwa uchunguzi kuhusu madai ya uhalifu wa kivita.

    Waziri Mkuu Abiy Ahmed anatarajiwa kukutanza na ujumbe wa Amani wa AU, lakini amekataa upatanishi wa kimataifa katika mzozo huo.

    Mapigano yameripotiwa baina ya vikosi vyaWatigray na wanajeshi wa serikali katika maeneo kadhaa ya Tigray, lakini mji mkuu wa jimbo hilo Mekelle unasemekana kuwa katika hali ya utulivu.

  6. Darasa la mapishi linalookoa maisha ya watoto Tanzania

      • Author, Aboubakar Famau
      • Nafasi, BBC News, Dar es Salaam

    Nchini Tanzania, tatizo la utapiamlo kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano bado ni kubwa.

    Miongoni mwa mikoa yenye idadi kubwa wa watoto hao ni mkoa wa Shinyanga uliopo kaskazini Magharibi mwa Tanzania, ambapo asilimia kumi na tano ya watoto wana uzito pungufu huku asilimia 32 wakiwa na udumavu. Hii ni kwa mujibu Tafiti ya Taifa ya Lishe yani Tanzania National Nutrition Survery ya mwaka 2018/2019.

    Kundi la kina mama lenye watoto wanaosumbuliwa na tatizo la utapiamlo uliosababishwa na upungufu wa madini chuma na vitamin A hivyo kuwa na utizo pungufu limekamilisha mafunzo ya wiki mbili ya mapishi bora yanayojumuisha makundi matano ya vyakula vyenye virutubishi kwa watoto.

    Baadhi ya akina mama kutoka kijiji cha Wijiteleja kilichopo mkoani Shinyanga kaskazini magharibi mwa Tanzania, wanaelezea jinsi mafunzo hayo yalivyoongeza uzito wa watoto wao.

    Magdalena John Kumalia awali mtoto wake alikuwa na kilo ambazo sio nzuri, lakini baada ya kumpikia vyakula vyenye virutubishi hali ilibadilika.

    “Mwanangu alikuwa na kilo saba tu, tukaanza darasa la mapishi, tukaanza kumpikia. Tulikuwa tunapika uji, tunaweka karanga, maziwa, tukiivisha, tunaepua na kuweka mbogamboga za majani, mpaka leo tumepima, mwanangu ana kilo tisa,” anasema Magdalena.

    Nae Agnes Ngelela anasema mbali na mtoto wake kuwa na kilo moja alipozaliwa lakini pia aliandamwa kwa magonjwa kama vile kuharisha na kutapika, lakini sasa magonjwa yote yameisha baada ya kupata lishe bora.

    Christian Ngowi ambae ni mganga mfawidhi wa zahanati ya Mundo mkoani humo anasema mafunzo hayo yalilenga zaidi kutumia vyakula, mbogamboga na matunda ambayo upatikanaji wake ni rahisi katika jamii inayozunguka.

    “Tuliona katika kundi la mbogamboga, kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa kundi hili kutokana na hali ya ukame inayozunguka wilaya yetu. Kwa hiyo, tulishauriana na afisa kilimo na mtendaji wa kijiji na wahudumu wa afya tukawafundisha kina mama kuwa na bustani za majumbani, kwa hiyo lile kundi la mbogamboga sasa hivi kina mama wanalipata kwa wingi bila gharama na kupoteza muda kwa kwenda sokoni,” anasema Dk. Ngowi.

    Wakati huo huo, Dk Frank Mtimbwa kutoka Shirika la World Vision nchini Tanzania ambalo ndilo linalodhamini mradi huu wa mafunzo ya mapishi kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine wa afya, anasema ili kutokomeza tatizo la utapiamlo katika jamii imewalazimu kuwashirikisha na kina baba.

    “Kwa jamii hizi tulizonazo, mwanaume anaweza akalima na mwanamke na akauza chakula chote na kwenye familia ukasikia kuna njaa, lakini wakati wa msimu wa kulima, walilima pamoja na walivuna sana. Kwa hiyo, sasa hivi wanafanya kazi pamoja na mwisho wa siku wanaamua wauze nini na pesa inayopatikana ifanye nini,” anasema Dk. Mtimbwa.

    Mbali na darasa la mapishi, wanakijiji pia wamehamasishwa kuanzisha bustani za nyumbani ili kurahisisha upatikani wa mbogamboga pamoja na viazi lishe ambavyo wataalamu wanadai vina asilimia kubwa ya virutubishi kwa watoto.

  7. Wakenya waliokuwa wakielekea Dubai wakamatwa na stakabadhi gushi za corona

    Maafisa wa uwanja wa ndege nchini Kenya wamewakamata wasafiri 21 ambao waliokuwa wakielekea mjini Dubai, katika Muungano wa falme za kiarabu (UAE), kwa kutumia vyeti gushi vya Covid-19.

    Wasafiri waliokamatwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani.

    Wasafiri hao wamekamatwa wakati wa msako wa vyeti hivyo uliokuwa ukifanyika katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta katika mji mkuu, Nairobi.

    Hii inakuja saa kadhaa baada ya UAE kupiga marufuku utoaji wa vibali vya kusafiria (visa) kwa wasafiri wanaotoka nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Kenya.

    Vyombo vya habari nchini Kenya vinaripoti kuwa marufuku hiyo iliwekwa baada ya wasafiri kutoka Kenya kupatikana na vyetu gushi vya Covid-19 walippowasili katika taifa hilo la Ghuba.

    Kenya imekuwa ikirekodi ongezeko la maambukizi ya Covid-19, huku jumla ya watu wenye maambukizi ikifikia 80,102 vikiwemo vifo vya watu 1,427.

  8. Binti wa Jerry Rawlings aonya kuhusu uchangishaji wa pesa za mazishi

    Binti mkubwa wa rais wa zamani wa Ghana Jerry Rawlings ametoa onyo dhidi ya wezi wa mtandaoni wanaodai kuwa wanachangisha pesa kwa ajili ya mazishi ya baba yake.

    Katika taarifa yake aliyoituma kwenye mtandao wa Facebook siku ya Alhamisi Zanetor Rawlings, alisema akaunti gushi za mitandao ya kijamii zimebuniwa kwa ajili ya kukusanya rambirambi ya baba yake.

    Amesema kuwa wezi wanawalenga wale wanaomtumia salamu za rambirambi kufuatia kifo cha baba yake.

    Bi Rawlings ni mbunge wa jimbo la Klottey Korle katika bunge la Ghana.

  9. Tume ya uchaguzi Uganda yawataka polisi kutowazuia wagombea urais

    Tume ya uchaguzi nchini Uganda imewatahadharisha polisi nchini humo dhidi ya kuwazuia wagombea wa urais kuendesha kampeni zao.

    Tume hiyo imesema kuwa imepokea baadhi ya malalamiko kutoka kwa wagombea wa urais na pia kuona taarifa za vyombo vya habari kwamba polisi inazuia na kuvuruga kampeni zao .

    Wakati huo huo katika taarifa ya pamoja ya mabalozi wa nchi za Muungano wa Ulaya nchini humo, wameeleza kutofurahishwa kwao na ghasia zilizotawala kampeni ya uchaguzi tarehe 18 na 19, Novemba nchini humo.

    Wamesema Uganda ilishuhudia ghasia na maandamano pamoja na matumizi yasiyofaa ya vikosi vya usalama dhidi ya raia na kuvitaka vyama vyote vya kisiasa na wagombea wake kuwataka wafuasi wao kuacha ghasia na matumizi ya lugha mbaya.

    Wametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kumaliza uchokozi unaolenga kuleta ghasia au kusababisha ukiukaji wa sheria.

    Hii inajiri huku Kiongozi wa upinzani nchini humo Robert Kyagulanyi al maarufu Bobi Wine akilalamikia kuzuiwa kuendesha kampeni zake katika mji wa Hoima magharibi mwa nchi hiyo.

    Katika ujumbe wake wa twitter Bobi Wine amesema kuwa polis walifunga barabara za kuelekea katika mji huo ili kumzuwia kufika katika hoteli aliyotarajia kupata malazi na kuziamuru hoteli zote katika mji huo zisimpokee na timu yake, na hivyo kuwalazimisha kulala ndani ya magari:

  10. Kenya yapunguza idadi ya wageni wanaohudhuria harusi kutokana na corona

    Idadi ya wageni watakaoruhusiwa kuhudhuria harusi nchini Kenya imepunguzwa hadi kufikia watu 50 pekee kutokana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini humo.

    Baraza linalojumuisha dini mbalimbali nchini humo limesema kuwa chakula kinachotolewa katika harusi kitakuwa kikiletwa kwa wazazi na ndugu wa karibu wa maharusi pekee.

    Mwezi Agosti Rais Uhuru Kenyatta aliongeza idadi ya wageni wanaoweza kuhudhuria harusihadi watu 100 alipolegeza masharti ya kudhibiti maambukizi ya Covid-19.

    Katika masharti mapya yaliyotangazwa Alhamisi wiki hii, chakula kimepigwa marufuku katika mazishi na idadi ya watu wanaoruhusiwa kuhudhuria mazishi imepunguzwa hadi watu 100 pekee.

    Muda wa mazishi pia umerekebishwa kwa kupunguzwa hadi saa moja pekee.

    Huduma za kanisa pia hazitatolewa kwa zaidi ya dakika 90.

    Wiki iliyopita mwenyekiti wa baraza la dini mbali mbali nchini Kenya, Anthony Muheria, alitibiwa virusi vya corona katika hospitali moja mjini Nairobi.

  11. Mwanasheria mkuu wa Tanzania aionya Chadema kuhusu wabunge walioteuliwa

    Mwanasheria Mkuu wa Tanzania Profesa Adelardus Kilangi amewaonya CHADEMA kutowabugudhi wabunge wa chama hicho wa viti maalumkutoka chama hicho.

    Profesa Kilangi amesema, mchakato wa Wabunge wa viti Maalum kutoka CHADEMA umefuata Sheria na Katiba, hivyo hawapaswi kubugudhiwa.

    Awali Spika wa bunge la Tanzania Job Ndugai alisema, kanuni za bunge zinamtaka kuwalinda Wabunge walio wachache na maslahi yao na kuahidi kufanya hivyo kwa nguvu zake zote.

    Kuhusu Wabunge 19 wa viti Maalum kutoka CHADEMA Bw Ndungai alisema wameteuliwa kihalali na kama CHADEMA wana matatizo nao walipaswa kuwaita kwa heshima na kuwasikiliza badala ya kuwahukumu.Amesema majina ya wabunge wa viti maalum alipewa na na Tume ya Uchaguzi, na kazi yake ni kuwaapisha Wabunge hao na ameshafanya hivyo.

  12. Hujambo na karibu tena kwa matangazo yetu mubashara ya leo tarehe 27.11.2020