Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Lazaro Nyalandu azuiwa mpakani Namanga

Aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Singida Kaskazini, kwa tiketi ya Chadema, Lazaro Nyalandu amezuiwa kutoka nchini kupitia mpaka wa Tanzania na Kenya wa Namanga.

Moja kwa moja

Lizzy Masinga

  1. Mchezaji wa zamani mashuhuri wa soka Samuel Eto'o anusurika kwenye ajali ya gari

    Mshindi mara nne wa tuzo ya mchezaji bora AfrikaSamuel Eto’o amenusurika katika ajali siku ya Jumapili wakati akielekea mji wa kibiashara nchini Cameroon wa Douala, kwa mujibu wa wanafamilia wake.

    Alikuwa akirejea kutoka mji wa Bafoussam, Magharibi mwa Cameroon, ambako alihudhuria tamasha mwishoni mwa juma.

    Dereva alisema kuwa alishindwa kulidhibiti gari na kuyagonga magari mawili yaliyokuwa kwenye msafara wa Eto’o.

    Msemaji wake alizungumza na BBC idhaa ya Pidgin kuwa anaendelea vizuri na kuwa gari lake liliharibika.

    Alikataa kujibu maswali zaidi.

  2. Kampeni kuelekea uchaguzi Uganda zaanza

    Kampeni za kuelekea uchaguzi kumpata rais ajaye zimeanza nchini Uganda.

    Wagombea 11 akiwemo rais aliyekaa madarakani kwa muda mrefu, Yoweri Museveni ambaye atawania tena nafasi hiyo katika uchaguzi utakaofanyika katika kipindi cha miezi miwili.

    Masharti makali ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona vimewekwa kwenye kampeni, lakini utekelezaji wake umekuwa mgumu.

    Rais Museveni ameanza kampeni katika eneo liitwalo Luweero triangle, eneo ambalo lilikuwa kitovu cha vita vya msituni vya miaka mitano vilivyomuweka madarakani mwaka 1986.

    Mwanamuziki ambaye sasa ni mwanasiasa Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine yuko njiano kuelekea mji wa West Nile, kuanza kampeni siku ya Jumanne.

    Polisi mji wa Mashariki wa Jinja umewatawanya wafuasi wa chama cha Forum for Democratic Change(FDC) cha mgombea Patrick Amuriat Oboi kwa kutumia vitoa machozi. Walikusanyika njiani kumshangilia akielekea eneo la Mashariki kuanza kampeni yake.

    Masharti ya afya wakati huu wa kampeni yanawataka wanasiasa kuepuka mikusanyiko mikubwa kwa kuwa na mkutano wa watu wasiozidi 70.

    Lakini suala hili limeonekana kuwa gumu kama ilivyoshuhudiwa wakati wa uteuzi juma lililopita, wakati wafuasi wa karibu wagombea wote walipokusanyika kwa wingi kwenye mitaa mbalimbali na kwenye vituo vya biashara.

    Kinyang’anyiro cha urais pia kinawahusisha majenerali wawili wa jeshi na mhitimu wa Chuo kikuu mwenye miaka 24 ambaye hana ajira.

    Raia wa Uganda watapiga kura kuchagua rais na wawakilishi tarehe 14 mwezi Januari.

  3. Lazaro Nyalandu azuiwa kuvuka mpaka wa Namanga

    Aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Singida Kaskazini, kwa tiketi ya Chadema, Lazaro Nyalandu amezuiwa kutoka nchini kupitia mpaka wa Tanzania na Kenya wa Namanga baada ya kukosa nyaraka muhimu.

    Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi Mkuu wa Wilaya Longido, Frank Mwaisumbe amesema mwanasiasa huyo alikuwa akitaka kuondoka nchini humo lakini hakuwa na nyaraka zinazohitajika.

    "Ni kweli maofisa wa uhamiaji mpakani wamemzuia kutoka nchini, kwani alikuwa hana nyaraka kadhaa ikiwamo za gari na vitu vingine ambavyo alikuwa anaondoka navyo,"Mwananchi lilimnukuu Mkuu huyo wa Wilaya.

    Amesema kwa sasa vitu alivyotaka kuvuka navyo bado vinashikiliwa mpaka wa Namanga na ametakiwa kuwasilisha nyaraka zake.

    "Tumemtaka alete nyaraka muhimu zinazohitajika na tumemuachia akalete, lakini akishindwa atafikishwa mahakamani,"alilieleza gazeti la Mwananchi.

  4. Vijana wa Nigeria watishia kufanya maandamano mapya

    Ripoti za kuwepo kwa maandamano mapya nchini Nigeria zimechapishwa na vyombo vya habari vya nchini humo.

    Vitisho hivyo vya maandamano mapya dhidi ya ukatili wa polisi vimejitokeza baada ya mahakama kutoa amri kuipa haki mamlaka Benki Kuu ya Nigeria kuzuia akaunti za watu 19 na kampuni zilizohusishwa na maandamano ya #EndSARS.

    Makundi tofauti, ikiwemo ya haki ya kiislamu (Muric), wamewataka watu wasishiriki kwenye maandamano mapya.

    Serikali ya Lagos pia imetahadharisha wakazi wake kutoshiriki maandamano.

    Jopo liliundwa kuchunguza matukio ya ukatili wa polisi limekuwa likiwasikiliza waathirika.

    Polisi imetoa tahadhari kuwa hairuhusu maandamano nchini humo.

  5. Mchekeshaji Elsa Majimbo ashinda tuzo za watu za E!

    Mchekeshaji wa Kenya Elsa Majimbo amewapiku wasanii kutoka nchi mbali mbali Afrika na kupata ushindi katika tuzo za E! people’s kipengele cha Nyota wa mitandao ya kijamii Afrika.

    Mwanadada huyo machachari alikuwa akiwania kipengele hicho na watu saba akiwemo msanii nyota wa Afrika Kusini Sho Madjozi huku wengine ni Karl Kugelmann, Dimma Umeh, Wian, Lydia Forson, Thuso Mbedu na Zozi Tunzi.

    Tuzo hizo ambazo hufanyika nchini Marekani mwaka huu zilifanyika kupitia mkutano wa Video utokana na janga la virusi corona.

  6. Godbless Lema akamatwa baada ya kukimbilia Kenya

    Bw. Lema alikamatwa wakati akiendeshwa na mwanasheria wake katika mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi.

    Alikuwa amefuatana na mke wake na watoto.

    Polisi wa Kenya waliwakamata katika eneo karibu kilometa 45 (maili 28) kutoka mpakani baada ya kutahadharishwa na wenzao wa Tanzania, gazeti la Standard linaripoti.

    Mbunge huyo wa zamani anaripotiwa kukataa kutoa pasi yake ya kusafiria kwa maafisa wa uhamiaji wa Tanzania.

    Mwanasheria, George Luchiri Wajackoyah, alinukuliwa na gazeti akisema alitaka kumpeleka mwanasiasa huyo kwenye ofisi ya tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNHCR).

    ‘’Sasa hivi , niko na mke wanguNeema, mtoto wangu wa kiume mwenye miaka 14 Allbless, Brilliance( binti) kitindamimba wangu Terrence. Sijui kesho yetu itakuwaje. Sasa ninatafuta hifadhi,’’ Bwana Lema alinukuliwa na gazeti hilo akisema

    Bw. Lema alikuwa miongoni mwa viongozi watatu walioachiwa juma lililopita baada baada ya kuitisha maandamano kutaka kufanyika upya kwa uchaguzi.

  7. Kiongozi wa Tigray aitaka AU kuingilia kati mzozo wa Ethiopia

    Kiongozi wa jimbo la Tigray Kaskazini mwa Ethiopia ametoa wito kwa Umoja wa Afrika kuingilia kati mgogoro nchini humo usifikie hatua ya kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

    Katika taarifa aliyoitoa kwa njia ya televisheni, Debretsion Gebremichael alisema Tigray itaendelea kujitetea mpaka pale serikali itakapokubali kufanya mazungumzo.

    Lakini Waziri Mkuu wa Ethiopia , Abiy Ahmed, amesema kuwa vitendo vya viongozi wa Tigray vilivyovuka mpaka vimemfanya achukua hatua za kijeshi.

    Ripoti kutoka mji jirani wa Amhara zinasema wanajeshi 100 wa serikali walikuwa wakipatiwa tiba ya majeraha.

    Awali, Bwana Abiy bila kutoa maelezo amewafuta kazi mkuu wa jeshi, mkuu wa idara ya Intelijensia na waziri wa mambo ya nje

    Mkuu mpya wa jeshi Berhanu Jula amesema kuwa vikosi vya serikali vimedhibiti miji minne Magharibi mwa Tigray.

  8. Matokeo ya uchaguzi Marekani 2020: Polisi yawafurusha waandamanaji Georgia

    Polisi katika mji mkuu wa jimbo la Georgia, Tbilisi, wamewafurusha makundi ya watu waliokuwa wakiandamana kupinga matokeo ya wabunge katika uchaguzi wa juma lililopita.

    Maelfu ya watu walikusanyika nje ya jengo la Tume ya uchaguzi kutaka mchakato wa kura kufanyika upya, baada ya kushutumu chama tawala wa wizi wa kura.

    Chama cha Dream cha Georgia kimekana shutuma za udanganyifu.

    Waangalizi wa kimataifa wamesema “kura zimepigwa kwa kuheshimu uhuru” lakini walikosoa sehemu ya mchakato

    Chama cha Dream,ambacho kilianzishwa na bilionea Bidzina Ivanishvili , kilichokuwa madarakanitangu mwaka 2012, kilipata 48% ya kura kwenye uchaguzi wa tarehe 31 mwezi Oktoba.

    Ushindi huo unakipa chama hicho haki ya kuunda serikali ijayo.

    Lakini maelfu ya waandamanaji walioandamana Tbilisi walikataa matokeo na kutaka ,mkuu wa polisi na wa tume kujiuzulu.

  9. Habari! karibu katika matangazo ya moja kwa moja Jumatatu 09.11.2020