Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya uchaguzi Tanzania 2020: Rais Magufuli aapishwa
John Pombe Magufuli hii leo ameapishwa kuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muhula wa pili.
Moja kwa moja
Asha Juma
Matukio ya uchaguzi Marekani 2020:'Malaika kutoka Afrika' waombwa kumsaidia Trump kushinda uchaguzi
Mshauri wa kidini wa Rais wa Marekani Donald Trump, Paula White-Cain anasema "malaika wameshukishwa" kutoka Afrika na Marekani Kusini kumsaidia Trump kuibuka na ushindi.
Katika ibada ya maombi, anasema: "Nasikia sauti za ushindi. Mungu anasema tayari ameshatenda. Ninachokisia ni ushindi, ushindi, ushindi kutoka mbinguni." Kiongozi huyo wa dini anaongezea "malaika wameshatumwa" kutoka Afrika hadi Marekani Kusini.
"Wanakuja hapa kwa jina la Yesu... nguvu za malaika," alisema hivyo kwa nguvu za ajabu kiasi cha kujipata anaanza "kukemea mapepo wanaojaribu kuiba kura za Trump".
Video zake zimesambaa katika mitandao ya kijamii – pengine zimechochewa na mamilioni ya watu wanaosubiri kusikia kuhusu taarifa zaidi za majimbo ambayo bado kura zinahesabiwa.
Rais Magufuli alipokuwa anakula kiapo cha kuwa rais muhula wa pili
Matokeo ya uchaguzi Marekani 2020:Uchaguzi ‘umechafuliwa’ na madai ya wizi wa kura
Ujumbe wa kimataifa umesema uchaguzi wa Marekani ‘umechafuliwa’ na madai ya wizi wa kura na majaribio ya kwanza kabisa ya kushusha imani ya umma“.
Shirika la Usalama na Ushirikiano Ulaya limesema kuwa uchaguzi wenyewe ulikuwa wa “ushindani na ulisimamiwa vizuri” licha ya changamoto za ugonjwa wa corona.
Katika taarifa za matokeo ya awali, ujumbe huo umesema “madai yasio na msingi ya mapungufu ya mfumo, yaliyotolewa na rais wa sasa, ikiwemo usiku wa uchaguzi, kunaathiri uaminifu wa umma katika taasisi za kidemokrasia”.
Katika hotuba yake ya usiku wa siku ya kupiga kura, Donald Trump alisema upigaji kura ni "kudanganya raia wa Marekani".
Kampeni ya Trump sasa inataka kusitisha shughuli ya kuhesabu kura kwa majimbo ya Pennsylvania, Wisconsin, Georgia na Michigan, – bila ushahidi wowote – kwamba kulikuwa na udanganyifu wa kura.
Magufuli kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa
Baada ya kuapishwa katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma nchini Tanzania.
Rais John Magufuli ametoa shukrani kwa Watanzania wote kwa kumuamini na kumchagua kwa mara nyingine kuliongoza taifa hilo kwa miaka mingine mitano.
Katika hotuba yake amesisitiza kuwa ushindi aliopata si wa chama tawala cha Mapinduzi (CCM) bali ni ushindi kwa Watanzania wote.
"Ushindi huu ni wa Watanzania wote. Nawapongeza sana Watanzania kwa kuonesha utulivu mkubwa katika kipindi chote cha uchaguzi. Tumepita kwenye mitihani mingi lakini mara zote Mungu ametuvusha salama" Magufuli amesema.
Pia ameipongeza Tume ya uchaguzi Tanzania (NEC) kwa kusimamia vyema uchaguzi huo.
Aidha, Bwana Magufuli amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwavusha katika janga la corona.
Rais John Magufuli amesisitiza kwamba sasa uchaguzi umekwisha na kuwa jukumu kubwa ni kuendeleza jitihada za kuleta maendeleo katika taifa hilo.
"Nitashirikiana nanyi nyote bila kujali itikadi na utofauti wetu" Magufuli amesema.
"Tutazidisha mapambano dhidi ya rushwa, wizi na ubadhirifu" Magufuli ameongeza.
Amemshukuru Mungu kwa fursa ya yeye kuwa rais wa kwanza kuapishwa katika jiji la Dodoma.
Matokeo ya uchaguzi Marekani 2020:Wafuasi wa Trump waandamana nje ya kituo cha Arizona
Kituo cha kuhesabu kura eneo la Maricopa huko Arizona, kimejikuta kikiwa na wakati mgumu wa kufanya maamuzi ya kusitisha shughuli zake baada ya kundi la wafuasi wa Republican kukusanyika nje - wakijibu madai ya mitandao wa kijamii kuwa kura ambazo zinasemekana kuwa za Trump hazitahesabiwa.
Baadhi ya waandamanaji waliingia ndani ya kituo hicho wakisindikizwa na maafisa wa usalama.
Asilimia 82 ya kura katika eneo la Maricopa zimehesabiwa huku Joe Biden akiongoza.
Hata hivyo, maafisa wanasema wana zaidi ya masanduku 400,000 ya kura ambazo bado hazijahesabiwa.
Eneo hilo halijajumuisha eneo la Phoenix, kwa muda mrefu limekuwa likichukuliwa kuwa ngome ya Republican.
Maelezo zaidi:
Matokeo ya uchaguzi Marekani 2020: Wafuasi wa Trump wafungua kesi Georgia
Wafuasi wa Donald Trump wanatafuta kusitisha shughuli ya kuhesabiwa kwa kura katika baadhi ya sehemu za Georgia – jimbo muhimu katika uchaguzi ambao bado halijatabiriwa nani anaweza kuibuka na mshindi.
Madai ya mashtaka wanayotaka kufungua ni kwamba muangalizi wa Republican alimshuhudia mhudumu wa uchaguzi akiongeza masanduku ya kura 53 yaliopigwa kwa njia ya posta ambayo yaliwasili kuchelewa katika kituo cha kuhesabu kura kaunti ya Chatham.
Huko Georgia, masanduku ya kupiga kura yanastahili kuwasili kabla ya saa moja usiku siku ya kupiga kura ili kuhesabiwa.
Hilo ni jimbo muhimu la nne ambapo rais amefungua kesi.
Bwana Trump ameahidi kusitisha uhesabu wa kura katika maeneo ambayo anasema kuna udanganyifu unaoendelea.
Hata hivyo hadi kufikia sasa, hakuna ushahidi wowote alioutoa kuthibitisha madai hayo.
Maelezo zaidi:
Magufuli tayari ameapishwa kuwa rais wa Tanzania
Jamuhuri ya muungano wa Tanzania tayari imemuapisha John Pombe Magufuli kuwa rais wa taifa hilo kwa awamu ya pili.
Rais Magufuli ametetea nafasi yake baada ya kushinda kwa kishindo Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28.10.2020.
Magufuli alishinda kwa kupata kura 12,516,252 ambayo ni asilimia 84 ya kura zote zilizopigwa. Tundu Lissu kutoka chama cha upinzani cha Chadema ameshika nafasi ya pili kwa kupata kura 1,933,271 ya kura zote ziizopigwa.
Jumla ya watu 15,91950 walipiga kura hizo wakati waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 29,754,699 kwa mujibu wa Tume ya taifa ya Uchaguzi (NEC).
Hii ni awamu ya pili kwa rais Magufuli kuongoza Tanzania, yeye ndiye alikuwa rais wa tano kuiongoza Tanzania kuanzia mwaka 2015 mpaka 2020.
Na sasa anatarajia kuongoza mpaka mwaka 2025.
Matokeo ya uchaguzi Marekani 2020: Joe Biden achukua jimbo la Michigan
Mgombea wa urais wa Democrat Joe Biden hadi kufia sasa amefanikiwa kupata kura milioni 71.5.
Awali, Joe Biden alisema kuwa ni wazi kwamba atashinda majimbo ya kutosha tu kumuwezesha kuwa Rais lakini bado kura zinaendelea kuhesabiwa katika majimbo mengine.
"Uhesabu wa kura ukimalizika tunaamini kwamba tutakuwa washindi," Bwana Biden amesema katika taarifa fupi aliyotoa kabla ya dalili kuanza kuonesha kuwa ana uwezekano mkubwa wa kuchukua ushindi katika jimbo la Michigan.
BBC ilitaarifiwa kuwa Bwana Biden atashinda jimbo la Michigan huku vyombo vya habari vya Marekani vikionesha kwamba ameshinda huko Wisconsin.
Maelezo zaidi:
Magufuli kuapisha leo kuwa rais kwa awamu ya pili
Rais mteule wa Tanzania John Pombe Magufuli anatarajiwa kuapishwa leo jijini Dodoma
Magufuli anatarajiwa kuanza kuitumikia nchi yake kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Rais Magufuli ameibuka kidedea katika uchaguzi mkuu ukiofanyika wiki iliyopita na kujizolea ushindi wa asilimia 84.4 na kuwashinda wapinzani wake 14 kutoka vyama mbalimbali vya upinzani.
Kwa mara ya kwanza jiji la Dodoma linashuhudia kufanyika kwa sherehe za kuapishwa kwa rais.
Kuanzia saa kumi na mbili asubuhi milango ya uwanja wa Jamhuri ilikuwa wazi kwa ajili wa wananchi waliofurika kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Viongozi mbalimbali kutoka nchi zaidi ya 12 huku wawakilishi kutoka jumuiya kama vile SADC na AU wakitarajiwa kuhudhuria.
Rais Magufuli anaanza kuwatumikia Watanzania katika kipindi cha pili cha uongozi wake baada ya kutangazwa mshindi katika uchaguzi ambao kwa asilimia kubwa umepingwa na upinzani kwa madai kuwa haukuwa wa huru na haki.
Tuhuma ambazo zimekuwa zikipingwa na Tume ya uchaguzi nchini humo.
Kutokana na madai hayo, vyama vikuu vya upinzani nchini Tanzania Chadema na ACT Wazalendo waliitisha maandamano ya amani ya nchi nzima kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu.
Hata hivyo, Polisi ilisema maandamano hayo sio halali, hatua iliyosababisha baadhi ya viongozi wa upinzani kufunguliwa kesi za kuitisha maandamano yanayodaiwa kuwa lengo la kuvunja amani.
Kwa maelezo zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja hii leo ikiwa ni Alhamisi tarehe 5.11.2020.