Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rais Magufuli atafanya nini katika miaka mitano ijayo?
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
- Iliyochapishwa
Kuna mambo makubwa mawili ambayo yamekuwa bayana katika miaka mitano ya kwanza ya Rais John Magufuli; Mosi kwamba washindani wake naWatanzania wengi hawakuwa wakimfahamu vizuri na Pili uwezo wake kama mwanasiasa ulikuwa ukidharauliwa.
Katika lugha ya Kiswahili cha mitaani; mtu unaweza kusema kwamba washindani wa kisiasa wa Rais Magufuli walikuwa na wameendelea 'kumchukulia poa'.
Miaka mitano iliyopita, nikiwa Mhariri wa Gazeti la Kiswahili la kila wiki la Raia Mwema, niliandika kwa mara ya kwanza habari kuwa Magufuli; wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi, angejitosa katika kinyang'anyiro cha kuwania Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wakati huo, Edward Lowassa - Waziri Mkuu wazamani wa Tanzania, ndiye aliyekuwa akionekana kama mtafuta urais kinara miongoni mwa wana CCM na mmoja wa watu wake wa karibu aliandika katika ukurasa wake binafsi wa mtandao wa facebook kuwa; "Raia Mwema mmeishiwa stori, mnatafuta hata watu wasio na nia ili mradi tu kumwekea vikwazo Lowassa".
Kwa mfuasi huyo wa Lowassa na wengi wa wana CCM wengine waliokuwa katika kinyang'anyiro hicho; Magufuli hakuwa tishio. Miezi mchache baadaye, mgombea huyo ambaye alikuwa hajawahi hata kuwa kiongozi wa ngazi ya shina wa CCM - chambilecho Profesa Mark Mwandosya, akapitishwa na CCM kuwa mgombea wake.
Ni kwa sababu ya kutomjua huku na kwa sababu ya kutofahamu hasa mawanda ya upeo wake wa kisiasa; ni vigumu kubashiri ni Tanzania ya namna gani itakuwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo ya urais wa Magufuli ambayo inaanza rasmi leo kwa kuapishwa baada ya kutangazwa mshindi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliofanyika Oktoba 28 mwaka huu.
Pasi na shaka yoyote, kichwani kwake, Rais Magufuli ana mpango kamili wa nini amepanga kufanya katika kipindi cha miaka ijayo hasa baada ya ushindi wake mkubwa wa asilimia 84 katika uchaguzi huo - ambao ni rekodi kwa mgombea wa CCM tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini.
Nini hutokea kihistoria katika Awamu ya Pili?
Kabla ya Magufuli, Tanzania imewahi kuwa namarais wengine wanne; Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete. Ukiondoa Nyerere ambaye ni kama aliongoza kwa vipindi vitano, waliomfuatia wote wameongoza kwa muda wa vipindi viwili viwili vya miaka mitano.
Kama kuna jambo moja la kujirudiarudi miongoni mwa marais waliomtangulia Magufuli katika miaka ya nyuma ni kuwa katika awamu ya pili, marais hufanya jambo kubwa ambalo ama hawakulisema mapema au halikuwa likipewa umuhimu mkubwa kwenye kampeni.
Mzee Mwinyi aliruhusu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania mnamo mwaka 1992 wakati akiwa katika awamu yake ya pili. Ukifuatilia hotuba zake za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1990, jambo hilo wala halikuwa miongoni mwa ajenda zake kwa wananchi.
Kimsingi, Watanzania wenyewe - wakati huo, kupitia maoni yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Francis Nyalali, walionyesha kutotaka mfumo wa vyama vingi; takwimu zikitaja asilimia 80 kupendelea kubaki kwenye mfumo wa chama kimoja.
Awamu ya pili ya Rais Mkapa ilitawaliwa na zoezi la ubinafsishaji wa mashirika ya umma; jambo ambalo wala halikuwa msingi wa kampeni zake za mwaka 2000.
Sera za ubinafsishaji zilikuwa na upinzani mkali hata ndani ya CCM kwenyewe kiasi kwamba Mwalimu Nyerere aliwahi kutamka hadharani kwamba pasipo na umakini, serikali inaweza kujikuta ikibinafsisha hadi magereza.
Kwa upande wa Kikwete, yeye alitumia awamu yake ya pili kuanzisha mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Tanzania kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba. Katika kampeni za Kikwete za mwaka 2010, suala la kuwa na katiba mpya wala halikuwa ajenda ya maana.
Mapendekezo ya Katiba Mpya yaliyotolewa na Tume ya Jaji Warioba, yalitupiliwa mbali na Bunge la Katiba; upinzani mkubwa ukitoka ndani ya CCM yenyewe ambayo baadhi ya vigogo wake hawakuwa wamefurahishwa na mapendekezo ya kuundwa kwa Serikali Tatu; ikimaanisha kupunguza nguvu za kimamlaka alizonazo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa.
Kwa mtiririko huo, kuna uwezekano wa Rais Magufuli kufanya jambo ambalo huenda hajawahi kulizungumza au kulipa uzito mkubwa kwenye hotuba zake za nyuma lakini lina maslahi makubwa kwa Watanzania.
Kwa sababu yeye ni mtu anayeweka karata zake karibu na kifua chake, ni vigumu kubashiri ni jambo gani hasa linaweza kuwa liko kifuani kwake kwa sasa. Hata hivyo, kwa mazingira ya uchaguzi wa mwaka huu; kama kuna jambo linaweza kumpa Rais Magufuli heshima ya kipekee ni kumalizia mchakato wa Katiba mpya; ukianzia alipoishia Kikwete na kufika mwisho.
Kwa tukio hilo moja, Rais Magufuli anaweza kujikuta ameacha alama (legacy) ya kudumu ya uongozi wake kwa Watanzania kwa kuwaachia jambo litakaloongoza maisha yao kwa muda mrefu kutoka sasa.
Hata hivyo, kama nilivyosema awali - ni vigumu kupanga Rais Magufuli anawaza nini wakati huu ingawa ni wazi kwamba kuna jambo litafanyika katika awamu yake ya pili kwa kufuata mtiririko wa watangulizi wake.
Mwendelezo wa miaka mitano iliyopita
Hakuna Rais wa Tanzania, kabla ya Magufuli, ambaye alibadilika katika awamu ya pili na kufanya mambo ambayo hakuwa akiyafanya katika awamu iliyotangulia. Jambo kubwa kwa Rais anayekwenda kumaliza muda wake ni kuhakikisha anamaliza vizuri muda wake na kukamilisha mambo ya kukamilisha.
Kwa hiyo, kwa vyovyote vile, kwa mambo ambayo yalitokea katika miaka mitano ya kwanza ya Magufuli, yataendelea kuwa yaleyale. Jambo la pekee litakalobadilika ni kwa msisitizo mkubwa zaidi kuhakikisha miradi mikubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano inakamilika kwa wakati.
Kwa sababu hiyo, maisha kwa wanasiasa wa upinzani, asasi za kiraia na vyombo vya habari binafsi yataendelea kuwa na changamoto kama ilivyokuwa katika miaka mitano ya kwanza.
Tutarajie kukamilika kwa mradi wa Reli ya Mwendokasi (Standard Gauge Railway), Bwala la Umeme la Mwalimu Nyerere (Stiegler Gorge) na kuwa na Shirika la Ndege la Air Tanzania imara Zaidi kuliko lilivyokuwa wakati Magufuli akiingia madarakani mwaka 2015.
Kama dunia itakuwa imeingia katika mtikisiko wauchumi kutokana na janga la ugonjwa wa Corona - wakati ambao nchi wahisani wa Tanzania zikiwa zinaingia tena katika kujifungia (lockdown), ni wazi kuwa maeneo itabidi yapunguziwe mafungu na badala yake fedha zielekezwe katika miradi muhimu kwa hiba ya rais anayemaliza muda wake.
Rais Magufuli, bila shaka, atapenda kukumbukwa kama kiongozi aliyeacha nchi ikiwa na reli ya mwendokasi na yenye umeme wa uhakika kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Simwoni Magufuli akiruhusu aondoke madarakani bila kukamilisha miradi hiyo miwili mikubwa.
Kumuandaa mrithi
Katika miaka miwili ya mwisho ya utawala wa Rais Magufuli, kuanzia mwaka 2023, kinyang'anyiro cha kutafuta mtu atakayemrithi kitaanza kuonekana dhahiri.
Haitakuwa siri tena kuwa ni akina nani wanataka nafasi hiyo.
Kumekuwa na maoni kwa baadhi ya wana CCM kuwa Rais Magufuli anapaswa kuendelea na muhula wa tatu, japo yeye mwenyewe amelipinga jambo hilo hadharani mara kadhaa.
Kama Rais Magufuli atabadili mawazo na kuamua kuendelea na urais - jambo hili likihitaji kubadili Katiba ya Tanzania ambayo imeweka ukomo wa vipindi viwili vya miaka mitano mitano, kunaweza kuwa na vuta nikuvute ndani na nje ya CCM.
Katika mazungumzo ambayo nimewahi kufanya nammoja wa marais wastaafu wa Tanzania; kuna mambo mawili makubwa ambayo hutawala akili ya rais aliye madarakani katika miaka yake ya mwisho ya utawala.
Jambo la kwanza linahusu kupata mrithi ambaye hatamsumbua wala kumvunjia heshima na pili kuhakikisha CCM haivunjiki wakati yeye akiwa kiongozi wake.
Kwa sababu hiyo, katika awamu yake ya pili ya uongozi, Rais Magufuli atahakikisha anafanya mambo mawili ambayo waliomtangulia waliyafanya pia - kuona kwamba mbadala wake anakuwa mtu atakayekipa chama chake ushindi na kutomsumbua mbele ya safari na pili kuiacha CCM iliyo imara kuliko alivyoikuta.
Katika moja ya ubashiri maarufu wa Mwalimu Nyerere miaka mingi iliyopita, alisema kwamba jambo pekee linaloweza kuitoa CCM madarakani ni endapo utatokea mpasuko ndani ya chama chenyewe. Kwamba upinzani dhidi ya CCM utatoka ndani ya CCM yenyewe.
Katika jambo lolote ambalo Rais Magufuli atapanga kulifanya kati ya sasa na mwaka 2025, wazo lake la kwanza litakuwa endapo jambo hilo litaleta mpasuko ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa sababu mimi 'simchukulii poa' Rais Magufuli, sidhani kama anaweza kufanya jambo linaloweza kuharakisha ubashiri wa Baba wa Taifa.