Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Wasafiri kutoka nchi 130 wataingia Kenya bila kuwekwa karantini, Tanzania haimo

Kenya imetoa orodha ya nchi 130 ambazo raia wake wataruhusiwa kuingia nchini humo bila masharti ya raia hao kukaa karantini ndani ya taifa hilo

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi

  1. Na huo ndio mwisho wa matangazo yetu ya moja kwa moja kwa leo, tukutane tena kesho...

    Nakuacha na habari ya mvulana huyu mchezaji wa Ballet kutoka Ghana Athony Mmesoma...unamkumbuka?

    Baada ya video yake akicheza Ballet kusambaa mtandaoni, sasa amepata ufadhili wa Masomo nchini Marekani.

  2. ECOWAS yaangalia uwezekano wa kuwawekea vikwazo waliopanga mapinduzi Mali

    Viongozi wa Mataifa yaliyoko magharibi wa Afrika watafanya kikao cha video leo juu ya mzozo unaoendelea nchini Mali.

    Kikao hicho kitakachofanyika mjini Niamey kinakuja siku moja baada yaJumuiya ya kiuchumi ya Mataifa yaliyoko maghraribi mwa Africa ECOWAS kuchukua hatua ya kusitisha shughuli zake za kiuchumi na Mali.

    Nchi 15 wanachama wa ECOWAS zimetangaza kufunga mipaka yake na Mali, kusitisha shughuli zote zinazohusiana na masuala ya kifedha na kuiondolea uanachama .

    Umoja wa Mataifa umelaani mapinduzi ya kijeshi ya Mali yaliyomlazimisha RaisBoubacar Keïta aondoke madarakani.

  3. Walinzi sita wa Makamu wa rais wa Sudan Kusini wauawa

    Walinzi sita wa Makamu wa rais wa Sudan KusiniJames Wani Igga wamepigwa risasi hadi kufa na wengine wawili kujeruhiwa baada ya msafara wao wa magarikuvamiwa na waasi , msemaji wake ameiambia BBC

    Bwana Wani hakuwa katika msafara huo wakati uliposhambuliwa kwa risasi katika kijiji alikozaliwa cha Lobonok,Kusini mwa mji mkuu, Juba, Jumatano jioni, amesema Bwana Lado .

    Gari la walinzi waMakamu wa rais lilikua likisafiri na liliharibiwa na kuchomwa na waasi kutoka kundi la National Salvation Front (NAS), aliongeza.

    Kundi hilo halijatoa taarifa yoyote juu ya shambulio hilo.

    Bwana Igga ni mmoja wa Makamu wa rais watano nchini Sudan. Anahusika masuala uchumi.

    Sudan Kusini ilipata uhuru wake kutoka kwa Sudan Kaskazini mwaka 2011, lakini imekuwa katika migogoro ya mara kwa mara.

  4. Mwana FA, Gwajima wapitishwa kugombea Ubunge CCM

    Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima nchini Tanzania Josephat Gwajima pamoja na mwanamuziki wa Bongo Flava Hamisi Mwinyi marufu Mwana FA wamepitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

    Gwajima na Mwana FA walishindwa katika kura za maoni katika majimbo ya Kawe na Muheza mtawalia mwezi uliopita.

    Hata hivyo vikao vya juu vya chama hicho vimewapitisha wao badala ya walioshinda katika ngazi ya jimbo ili kukiwakilisha chama kwenye uchaguzi wa ubunge mnamo Oktoba 28.

    Wawili hao ni baadhi ya wanasiasa ambao majimbo yao yamefanyiwa mabadiliko ya washindi.

  5. Mwandishi wa habari wa Kenya aachiliwa Ethiopia

    Mwandishi wabari wa Kenya Yassin Juma ameachiliwa huru kutoka mahabusu nchini Ethiopia – takriban wiki moja baada ya wakili wake kusema kuwa alipatwa na maambukizi ya virusi vya corona gerezani.

    Amehamishiwa kwenye hospitali ya serikali kwa ajili ya matibabu, na ataruhusiwa kusafiri kurejea nyumbani Kenya baada ya kupona.

    Bwana Juma,ambaye ni mwandishi huru wa habari, alikamatwa katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa, mwezi wa Julai, kufuatia ghasia zilizoibuka baada ya kuuawa kwa mwanamuziki maarufu wa jamii ya Oromo Hachalu Hundessa .

    Maafisa nchini Ethiopia wiki hii waliamuru kuachiliwa kwake, wakisema “alikamatwa kimakosa”.

    Wizara ya Mambo ya nje ya Kenya ilisema kuwa aliachiliwa baada ya ubalozi wake nchini Ethiopia kuingilia kati na ambao ulipinga kushikiliwa kwake.

  6. Zimbabwe yataka kujua msimamo wa Vatican juu ya ukosoaji wa Maaskofu

    Serikali ya Zimbabwe imewasiliana na muwakilishi wa Vatican Askofu Mkuu Marek Zalewski kupata maelezo juu ya ukosoaji wa maaskofu waKikatoliki dhidi yake.

    Hivi karibuni maaskofu hao walitoa barua ya kitume wakielezea ufisadi, umasikini na ukiukaji wa haki za binadamu vilivyokithiri nchini humo. Walitoa wito wa kutatuliwa haraka wa matatizo ya kiuchumi na kisiasa nchini humo.

    Waziri wa sheria Ziyambi Ziyambi anasema serikali inataka kujua iwapo maaskofu hao walizungumza kwa niaba ya serikali ya Vatican.

    " Serikali inataka kuzungumza na Vatican kuelewa iwapo taarifa ya aina hiyo inaonyesha msimamo rasmi wa mkuu wa Vatican kuelekea utawala wa Zimbabwe au haya ni maoni ya watu ," alisema.

    Bwana Ziyambi amesema kuwa Waziri wa Mambo ya nje Sibusiso Moyo atakutana na muwakili wa Vatican nchini humo.

  7. Magufuli awataka wajumbe wa CCM Tanzania kuweka maslahi ya nchi mbele

      • Author, Aboubakar Famau
      • Nafasi, BBC Swahili, Dar es Salaam

    Rais John Pombe Magufuli amewataka wajumbe kufanya uteuzi kwa kuweka maslahi ya nchi mbele bila kutumia kigezo cha ukanda, udini, udugu na kuendelea.

    Rais huyo wa Tanzania ambae pia ni Mwenyekiti wa Chama Tawala CCM alikuwa akifungua kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama hicho kitakachofanya uteuzi wa wabunge na wawakilishi watakaopeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

    Katika ufunguzi huo, rais Magufuli amesema kazi kubwa tayari imefanywa siku mbili zilizopita ambapo mafaili 1367 yaliangaliwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM.

  8. Huenda Kenya ikaanza kujaribu tiba ya corona

      • Author, Rhoda Odhiambo
      • Nafasi, BBC Africa,Nairobi

    Huenda Kenya ikaanza kujaribu kuwatibu wagonjwa wa Covid-19 kwa kutumia plasma. Plasma ni sehemu ya maji maji ya damu ambayo inabakia wakati seli zote nyeupe na nyekundu za damu pamoja na ute mweupe vinapoondolewa.

    Dokta Mercy Mwangangi kutoka Wizara ya Afya anasema kuwa watalaam wanandaa miongozo ambayo itawaruhusu madakatari kutumia sehemu hii ya damu kama tiba ya corona.

    'Katika uchunguzi huu, watalaam, watakuwa wanachunguza uwezekano wa kuchukua damu ya mtu ambaye amepona baada ya kuambukizwa corona na kuitumia damu hiyo kumtibu yeyote ambaye amepatikana na maambukizi hayo,” Dokta Mwangagi aliwaelezea wanahabari.

    Mbinu hiyo ya kutumia damu kumtibu mtu mwingine ni matibabu ya kale.

    Dawa hii inapunguza uvimbe wa mwili kulingana na homoni inayotengenezwa ndani ya mwili. Katika janga hili, dawa hili hutumika kwa wale ambao wako katika hali mahututi na hawawezi kupuma vizuri.

    Plasma inatumiwa kwasababu ina kinga ya mwili. Lakini, kwa sasa wataalam hawajui kinga hiyo inadumu kwa muda ngapi au siku ngapi.

    Kuna zaidi ya majaribio 80 ambayo yanalenga kuwasajili wagonjwa kushiriki katika uchunguzi huu kote duniani.

  9. Viongozi wa mapinduzi Mali wazungumza na upinzani

    Viongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Mali wamefanya mazungumzo na viongozi wa upinzani ambao wamepongeza kung’olewa madarakani kwa Ibrahim Boubacar Keïta.

    Wamemlaumu kwa kushindwa kukomesha mashambulio ya jihad na kuporomoka kwa uchumi wa nchi.

    Muungano wa upinzani umesema unatambua utashi wa jeshi wa kuundwa kwa serikali ya mpito ya kiraia.

    Kanali wa jeshi , Assimi Goita, amejitokeza kama kiongozi mpya wa jeshi la nchi hiyo. .

    Amewataka wafanyakazi wa umma kurejea kazini.

    Baraza la usalama la Umoja wa Maraifa limelaani mapinduzi nchini Mali.

    Viongozi wa Afrika Magharibi wametangaza kufunga mipaka yao na Mali na wanatarajia kufanya mkutano kwa njia ya video kujadili hatua zaidi dhidi ya Mali.

  10. Raia wa nchi 130 kuingia Kenya bila Karantini

    Mamlaka nchini Kenya zimetoa orodha mpya ya raia wa nchi 130 ambao wataruhusiwa kuingia nchini humo bila kukaa karantini.

    Hata hivyo, Taifa jirani la Tanzania halimo katika orodha hiyo. Kwa nchi za Afrika Mashariki ni Rwanda na Uganda ndizo zilizomo kwenye orodha hiyo.

    Kenya ilifungua anga lake Agosti Mosi na Tanzania pia haikuwemo kwenye orodha ya awali. Hali hiyo ilisababisha mamlaka za Tanzania kuzuia ndege za Shirika la Ndege la Kenya kutua nchini humo.

    Licha ya viongozi wa pande zote mbili kusema wanafanya mazungumzo, bado undani ama matokeo ya mazungumzo hayo havijawekwa wazi.