Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Kimbunga Kenneth kimefifia

Kasi imepungua ya kimbunga Kenneth na upepo wake, hatahivyo mvua kubwa bado inatarajiwa katika utabiri wa siku zijazo.

Moja kwa moja

  1. "Kimbunga kutua Ijumaa alfajiri"

    Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imetoa taarifa mpya juu ya mwenendo wa kimbunga Kenneth na kusema kuwa kinatarajiwa kutua Ijumaa alfajiri au asubuhi.

    Katika Taarifa ya video iliyopakiwa kwenye mtandao wa kijamii wa You Tube, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt Agness Kijazi amesema kufikia sa tisa mchana wa leo kimbunga kitakuwa umbali wa kilomita 177 kutoka pwani ya Mtwara kikiwa na kasi ya kilometa 140 kwa saa.

    Kutokana na kasi hiyo kimbunga kinatarajiwa kutua nchini Msumbiji kuanzia Alfajiri ya Ijumaa kikiwa na kasi kilomita 100 kwa saa.

    Hata hivyo, kitakapotua kimbunga hicho ni karibu na mpaka wa Tanzania kwa kilomita 230, na athari zake zinatarajiwa kukumba maeneo yaliyo ndani ya kilomita 600.

    "Nchini mwetu, maeneo ya mpaka Lindi na Ruvuma yataathirika sana," amesema Kijazi na kuongeza, "wakazi hususani wa Mtwara kwa sasa wanaweza wakaona tu kuna mvua zinanyesha lakini waendelee kuchukua tahadhari. Kadri muda unavyosidi kusonga ndiyo kimbunga kinazidi kukaribia nchi kavu."

  2. Ni jioni, watu wanarudi nyumbani

    Wakaazi waliokuwa wamepiga kambi katika uwanja wa ndege mchana kutwa kama mojawapo ya maeneo salama ya kujikinga na dhoruba ya kimbunga Kenneth ambacho bado kinatarajiwa kutua, sasa wameanza kurudi nyumbani kwao pasi kuhofia hatari ambayo huenda ikawepo.

    Mwandishi wa BBC Eagan Salla aliyepo katika eneo hilo anasema 'giza limeanza kuingia na watu wanahisi njaa'

  3. 'Kimbunga Kenneth kupiga eneo ambalo halijawahi kukumbwa na dhoruba'

    Shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO linaendelea kuonya kuwa Kimbunga Kenneth ni hatari sana na kinaelekea kupiga eneo ambalo halijawahi kukumbwa na tufani toka picha za satelaiti zianze kuchukuliwa.

    Picha za satelaiti kwa mara ya kwanza zilianza kuchukuliwa toka angani kuanzia miaka ya 1940, na picha ya kwanza kwa utabiri wa hali ya hewa ilipigwa mwaka 1960 na chombo cha TIROS-1 cha shirika la anga la Marekani NASA.

  4. 'Kama siwezi kujiokoa, basi ndio itakuwa mwisho wangu'

  5. Kimbunga Kenneth kinatarajiwa kupita maeneo haya

  6. Usafiri wa baharini wasitishwa Zanzibar

    Mamlaka visiwani Zanzibar, Tanzania zimesitisha usafiri wa baharini kama sehemu ya tahadhari dhidi ya Kimbunga Kenneth.

    Visiwa vya Zanzibar vinategemea usafiri wa majini kama njia kuu ya mawasiliano na biashara baina ya visiwa vikuu viwili vya Pemba na Unguja pamoja na miji ya Tanzania bara hususani Dar es Salaam, Tanga na Bagamoyo.

  7. Wakaazi kusubiri msaada

      • Author, Eagan Salla
      • Nafasi, BBC Swahili, Mtwara, Tanzania

    Baadhi ya picha kutoka Mtwara zilizopigwa na mwandishi wetu zinaonyesha wakaazi wa eneo hilo wanavyoelekea kutafuta hifadhi salama katika shule ya Sabasaba sekondari Mtwara.

    Mwalimu mkuu katika shule hiyo, Julia Kariati ameiarifu BBC kwamba kufikia sasa wamepokea wakaazi 1,083 ambao ni mchanganyiko pamoja na wanachuo.

    Ameeleza kwamba, maafisa wa usalama wamesema wanakwenda kupanga utaratibu kwa maana ya kwamba wanakwenda kutafuta utaratibu ili waweze kutoa mwelekeo wa huduma muhimu kama chakula na malazi kwa wananchi

  8. Mambo 5 muhimu wakati wa kimbunga Kenneth

    James Mbatia ni mbunge nchini Tanzania na mtaalamu wa kudhibiti na kupambana na majanga amezungumza na BBC na kushauri mambo matano yafuatayo;

    • Taarifa sahihi ziendelee kutolewa na mamlaka za serikali pamoja na vyombo vya habari.
    • Nguvu ielekezwe kuokoa maisha kwanza, miundombinu baadae.
    • Watu waliopo katika sehemu zisizo salama mathalan mabondeni au karibu na bahari wahamishwe.
    • Majengo imara kama misikiti, makanisa, magorofa, shule na kambi za jeshi zitumike kuhifadhi watu.
    • Kitengo cha kupambana na majanga kiwezeshwe kifedha na rasilimali watu ili kuratibu uokozi.
  9. Jeshi la zimamoto na uokoaji Tanzania linasema lipo imara kutoa usaidizi

    Idara za dharura na uokoaji nchini Tanzania zinasema zipo tayari kutoa usaidizi kwa wakaazi watakao athiriwa na mvua kubwa na upepo mkali unaotarajiwa katika maeneo ya pwani kusini mwa Tanzania.

    Katika taarifa ya wizara ya mambo ya ndani ya nchi, Jeshi la zimamoto na uokojaji linasema lipo 'imara na limejipanga kuhakikisha linatoa huduma bora, sahihi na kwa wakati'.

    Mamlaka ya hali ya hewa nchini TMA ilitoa utabiri wa wiki nzima na kutahadharisha kuwa siku ya Ijumaa, Aprili 26 kunategemewa mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makubwa baharini katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Lindi na Mtwara.

    "Tafadhali chukua hatua, uwezekano wa kutoke ni mkubwa na kiwango cha athari zinazoweza kutokea ni mkubwa," taarifa hiyo ya (TMA).

    Shirika la msalaba mwekundu Tanzania (TRCS) limesema limeviarifu vikosi vyake Lindi na Mtwara na limesema lipo tayari kutoa usaidizi mara moja.

  10. Kimbunga Kenneth hatari kubwa: laonya shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani

    " Upepo mkali wenye uharibifu, tufani, mvua kubwa na mafuriko " linaonya shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO

  11. Zimbabwe yatoa tahadhari ya athari za kimbunga Kenneth

    Taarifa ya wizara ya habari Zimbabawe imeeleza kwamba Kimbunga Kenneth kinachotarajiwa kutua Msumbiji Malawi na baadhi ya maeneo ya Zimbabawe, kimeshuhudiwa visiwani Comoros.

    Imeeleza kwamba kutokana na uzoefu wa mkasa na athari ya kimbunga Idai mwezi uliopita, watu wote wanaoishi katika maeneo yalio katika hatari ya kukumbwa na mafuriko kama Mbire Muzarabani na maeneo ya chini ya jimbo la Masvingo na kwingineko, wanapaswa kujihadhari pakubwa.

  12. Kimbunga Kenneth kimefika daraja la nne

    Kimbunga Kenneth kimefika daraja la nne kikiambatana na upepo wa kasi ya 130 mph karibu na eneo la kati na kinaarifiwa kuelekea Msumbiji katika jimbo la Cabo Delgado.

  13. Wakaazi watakiwa kuelekea maeneo ya juu Mtwara

    Mkuu wa mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa ameagiza wakaazi wasiende kazini na shuleni hii leo na ametoa tahadhari kwa wakazi wanaoishi pembezoni mwa bahari kuyahama makazi yao, kwa hofu ya kukumbwa na kimbunga Kenneth

  14. Kimbunga Kenneth kimefika wapi

    Kimeonekana umbali wa -11.6,41.8 na upepo wenye kasi ya 145mph

  15. Kimbunga Kenneth kina tofauti gani na Kimbunga Idai?

    Wataalamu wa hali ya hewa wanaonya kuwa Kimbunga Kenneth kinatazamiwa kuwa na nguvu sawa na Kimbunga Idai ambacho kilizikumba nchi tatu Msumbiji, Zimbabwe na Malawi mwezi uliopita.

    Na hata kama kutakuwa na tofauti, basi makali ya Kenneth yatakuwa madogokidogo ikilinganishwa na Idai.

    Kimbunga Idai kimesababisha madhara makubwa kwa mataifa tajwa, ambapo watu Zaidi ya 900 wamefariki dunia.

    Kwa mujibu wa Kamati ya Dharura ya Majanga ya Uingereza watu 960 walipoteza maisha kutokana na athari za kimbunga hicho. Watu milioni tatu kwenye nchi hizo bado wanahitaji misaada ya kibinaadamu kama chakula, dawa, malazi na makazi.

    Tofauti na Idai, Kenneth kinatazamiwa kupunguza makali baada ya kutua lakini kinatarajiwa kuendelea kujikusanya mpaka kwa kipindi cha wiki moja. Katika kipindi chote hicho kinatarajiwa kuambatana na mvua za ukubwa wa mililita 600.

    Kutokana na ukubwa wa mvua hizo, madhara makubwa ya mafuriko, maporomoko ya udongo yatakuwa makubwa kama Idai au hata kuwa makubwa zaidi.

    Kimbunga Kenneth kinatarajiwa kutua nchini Msumbiji katika eneo ambalo ni kilomita 200 tu kutoka mpakani na Tanzania. Kwa Msumbiji maeneo yatakayoathirika zaidi ni majimbo ya Pemba na Montepuez.

    Kwa upande wa Tanzania, mikoa mitatu ya Mtwara, Ruvuma na Lindi inatazamiwa kuathirika zaidi.

  16. Je unafahamu vimbunga vinavyopewa majina duniani?

    Umewahi kusikia vimbunga vikiwa na majina ya kushangaza:

    • Idai kilichosababisha uharibifu mkubwa katika baadhi ya maeneo nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe mwezi uliopita Machi.
    • Matthew ambacho kilikumba maeneo ya Haiti, Jamaica, Jamhuri ya Dominika, Bahamas na baadhi ya majimbo ya Marekani mwezi Oktoba mwaka 2016
    • Hermine ambacho kilisababisha uharibifu mkubwa jimbo la Florida.
    • Katrina ambacho kiliathiri sana majimbo ya Louisiana, Mississippi na Alabama nchini Marekani.
  17. Wanafunzi wakielekea katika maeneo ya juu

    Wanafunzi wa chuo cha ufundi Mtwara wakielekea katika maeneo ya juu kama walivyoagizwa.

    Chuo hicho kipo kilomita mbili tu umbali na bahari.

  18. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania yathibitisha ujio wa upepo mkali

    Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA) imetangaza kuwa Kimbunga Kenneth kimeongezeka kasi na kinatarajiwa kufika pwani ya kusini ya Tanzania na kaskazini mwa Msumbiji kuanzia usiku wa kuamkia leo Alhamisi. Kimbunga hicho kinatarajiwa kuongeza nguvu zaidi Alhamisi mchana ambapo kitakuwa kinasafiri kwa kilomita 170 kwa saa na kitakuwa kilomita 150 kutoka pwani ya Mtwara. Kwa mujibu wa TMA, kimbunga hicho kitatua nchini Msumbiji, kikiwa na kasi ya kilomita 100 kwa saa. Eneo hilo litakuwa kilomita 200 kutoka pwani ya Mtwara. Hata hivyo, mkoa wa Mtwara na maeneo jirani hususani mikoa ya Lindi na Ruvuma yataathirika pakubwa (athari zinategemewa kufikia umbali mpaka wa kilomita 500 kutoka Mtwara).

    Kwa mengi zaidi: Bonyeza

  19. Mtwara imeamkaje leo?

    Asubuhi hii mvua inanyesha kwa wepesi katika eneo la Mtwara na upepo unapiga. Tayari waandishi wa BBC wamekita kambi kukujulisha hali inavyotukia.

    'Wasafiri sio wengi kwenye ndege tulikuwa abiria wasiozidi 15 licha ya kwamba hatuwezi kusema iwapo ni kutokana na hofu ya kimbunga hicho', anasema mwandishi wa BBC Eagan Salla.