Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Gambia: Jammeh akubali kuachia madaraka

Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi walikuwa wamempa Yahya Jammeh fursa ya mwisho kuachia madaraka, huku wanajeshi wa Senegal wakiingia nchini Gambia.

Moja kwa moja

  1. Watu 45,000 waikimbia Gambia

    Raia 45,000 wa Gambia wameikimbia nchi hiyo na kuingia Senegal kutokana na mzozo wa kisiasa unaoendelea, shirika la UN linalowashughulikia wakimbizi limesema.

    Taifa jirani la Senegal linaweza kuwahudumia hadi wakimbizi 100,000, msemaji wa UNHCR  Babar Baloch amesema.

  2. Jammeh atawaambia nini Conde na Abdel Aziz?

    Mwandishi wa BBC Thomas Fessy aliye mjini Banjul anasema maandalizi ya kuwalaki marais wa Guinea na Mauritania uwanja wa ndege, Alpha Conde na Mohamed Ould Abdel Aziz.

    Wanajeshi uwanjani wanatabasamu na kuonesha urafiki.

    Mjumbe wa UN Afrika Magharibi Mohamed Ibn Chambas ambaye amemtaka Jammeh kung’atuka tayari amewasili.

    Jijini, kimya kimetanda na biashara nyingi zimefungwa.

    Wengi wanaamini mwisho wa mzozo wa sasa wa kisiasa unakaribia lakini wanasubiri Jammeh atawaambiaje marais hao wanaofika kumshawishi kuondoka kwa Amani.

    Mwenyekiti wa tume ya Ecowas, Marcel de Souza, amependekeza Jammeh apelekwe Guinea kabla ya hatima yake kuamuliwa.

    Mauritania si mwanachama wa Ecowas.

    Rais wa Guinea Alpha Conde amekuwa akipinga pendekezo la majeshi kutumia kumuondoa Jammeh. Anasema diplomasia inafaa kutumiwa.

  3. Hakuna aliye tayari kufa kwa ajili ya Jammeh

    Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Gambia Sidath Diop ameambia BBC kwamba Bw Jammeh amekataa ushauri wa viongozi wa Afrika Magharibi kwa sababu anaamini wanajeshi watampigania.

    Hata hivyo, amesema wanajeshi wengi hawana imani na Bw Jammeh.

    "Jammeh anaamini anamili Gambia," amesema Diop, na kuongeza kuwa kiongozi huyo hajui afanye nini utawala wake unapofikia kikomo.

  4. Yahya Jammeh amevunja baraza la mawaziri

    Taarifa zinasema Yahya Jammeh amevunja baraza la mawaziri baada ya mawaziri wake wengi kujizulu.

    Anapanga kusimamia shughuli zote za wizara za serikali.

    • Mawaziri watatu zaidi wajiuzulu Gambia
    • Makamu wa rais wa Gambia ajiuzulu

    Makamu wake wa rais ni miongoni mwa waliojizulu.

    Amechukua hatua hiyo siku moja tu baada ya Adama Barrow kuapishwa kuwa rais mpya wa Gambia ubalozini Senegal.

  5. Wanajeshi wako tayari kumtoa kwa nguvu

    Juhudi za mwisho za kumshawishi Bw Jammeh kuondoka kwa hiari, ambazo zinaongozwa na Rais wa Guinea Alpha Conde, zinatarajiwa kufanyika Ijumaa asubuhi.

    Mwenyekiti wa tume ya Ecowas, Marcel Alain de Souza, alisema iwapo mkutano huo utakaoongozwa na Bw Conde hautafaulu, basi hatua ya kijeshi itafuata.

    "Iwapo kufikia saa sita mchana, yeye (Bw Jammeh) hatakubali kuondoka Gambia chini ya Rais Conde, tutaingilia kijeshi," amesema.

    Hatua ya Ecowas kutaka kumtoa kwa nguvu Jammeh inaungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15, ingawa baraza hilo lilisisitiza kwamba suluhu ya amani inafaa kupoewa kipaumbele.  

  6. Jammeh ana hadi saa sita mchana kuondoka

    Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi wamempa Yahya Jammeh fursa ya mwisho kuachia madaraka, huku wanajeshi wa Senegal wakiingia nchini Gambia.

    Bw Jammeh amepewa hadi saa sita mchana Ijumaa (saa tisa Afrika Mashariki) kuachia madaraka la sivyo aondolewe kwa nguvu na wanajeshi wa nchi za Afrika Magharibi wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

    Wanajeshi hao wametakiwa kusubiri hadi makataa hayo yamalizike.

    Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) inaunga mkono Adama Barrow, ambaye aliapishwa kuwa rais mpya wa Gambia katika ubalozi wa nchini hiyo nchini Senegal.

  7. Hujambo!

    Hujambo! Karibu kwa taarifa za moja kwa moja kuhusu yanayojiri nchini Gambia. Rais Yahya Jammeh amepewa makataa ya mwisho kuondoka madarakani.