Syria sio tishio kwa ulimwengu, kiongozi wa waasi wa Syria aiambia BBC

Kiongozi wa serikali isiyo rasmi wa Syria, Ahmed al-Sharaa, amesema nchi hiyo imechoshwa na vita na si tishio kwa majirani zake wala kwa nchi za Magharibi.
Katika mahojiano na BBC mjini Damascus, ametaka vikwazo dhidi ya Syria viondolewe.
"Sasa, baada ya yote yaliyotokea, vikwazo lazima viondolewe kwa sababu vililengwa kwa utawala wa zamani. Mwathiriwa na mdhalimu hawapaswi kutendewa sawa," alisema.
Sharaa aliongoza mashambulizi yaliyoangusha utawala wa Bashar al-Assad chini ya wiki mbili zilizopita. Yeye ni kiongozi wa Hayat Tahrir al-Sham (HTS), kundi kubwa katika muungano wa waasi, na hapo awali alijulikana kwa jina la Abu Mohammed al-Jolani.
Alisema HTS inapaswa kuondolewa kwenye orodha ya yale yanayotambulika kama mashirika ya kigaidi. HTS Imetajwa kuwa moja wapo na Umoja wa Mataifa, Marekani, EU na Uingereza, miongoni mwa mengine mengine, kwani lilianza kama kundi lililogawanyika la al-Qaeda, ambalo lilijitenga nalo mwaka 2016.
Sharaa alisema HTS sio kundi la kigaidi.
Hawakuwalenga raia au maeneo ya kiraia, alisema. Isitoshe, waliwachukulia kuwa wahanga wa uhalifu wa utawala wa Assad.
Alikanusha kuwa alitaka kubadilisha Syria kuwa kama Afghanistan.
Sharaa alisema nchi hizo ni tofauti kabisa, na vile vile, zenye mila tofauti. Afghanistan ilikuwa jamii ya kikabila. Nchini Syria, alisema, kuna mawazo tofauti.
Aliongeza kuwa anaamini katika elimu kwa wanawake.
Raia wengi wa Syria hawamwamini.
Vitendo vya watawala wapya wa Syria katika miezi michache ijayo vitaonyesha aina ya nchi wanayotaka Syria iwe - na jinsi wanavyotaka kuitawala.
Soma zaidi:
