Zambia itaelekea kwenye uchaguzi baada ya siku mbili, ambapo wananchi watapiga kura kumchagua Rais, wabunge na viongozi wa mabaraza ya serikali za mitaa.
Uchaguzi huo umetajwa kwa kiasi kikubwa kuwa ni ushindani wa wagombea wawili wakuu, kufuatia kuibuka kwa mgombea mmoja wa muungano wa upinzani.
Kwa mujibu wa Reuters, kura za maoni pamoja na wawekezaji wengi wanatarajia Rais Hakainde Hichilema kushinda muhula mwingine wa miaka mitano, akimshinda mpinzani wake Brian Mundubile, anayeongoza upinzani uliogawanyika.
Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi ya Zambia inakabiliwa na moja ya mitihani yake mikubwa zaidi, huku ikisimamia uchaguzi wa kwanza unaotumia daftari jipya la wapiga kura na unaofanyika katika majimbo mapya ya uchaguzi. Masuala ya usalama wa kura, mvutano wa kisiasa na wasiwasi wa umma kuhusu uaminifu wa mchakato wa uchaguzi pia yameibua changamoto kwa tume hiyo.
Uchaguzi huo wa Agosti 13 umejikita katika ushindani kati ya miungano miwili mikuu ya kisiasa.
Muungano unaoongozwa na chama tawala cha United Party for National Development, UPND, unaungwa mkono na vyama vidogo 15.
Upande wa pili ni Tonse Pamodzi Alliance, unaoongozwa na mgombea urais Brian Mundubile na mgombea mwenza Makebi Zulu.
Muungano huo unajumuisha vyama vidogo visivyo na uwakilishi bungeni pamoja na sehemu kubwa ya miundo iliyosalia ya chama cha Patriotic Front, PF.
Mundubile aliwahi kuwa mwanachama wa PF, chama kilichoondolewa madarakani katika uchaguzi wa mwaka 2021.
Kwa mujibu wa sheria za Zambia, miungano ya kisiasa haiwezi kusajiliwa kama vyombo vya uchaguzi. Hivyo, wagombea wa miungano hiyo hulazimika kugombea kupitia chama kimoja, huku wakiungwa mkono na muungano usio rasmi.
Kuundwa kwa miungano ya upinzani si jambo jipya nchini Zambia. Takriban kila uchaguzi umekuwa ukishuhudia mazungumzo ya kuunganisha vyama vya upinzani, ingawa ni miungano michache iliyofanikiwa kudumu hadi wakati wa uchaguzi.
Mwaka huu, vyama vya upinzani viliungana katika hatua za mwisho za maandalizi ya uchaguzi, vikidai kukabiliwa na kile vinachokiita kuingiliwa kwa kiasi kikubwa na serikali.
Licha ya changamoto hizo, upinzani unasema una matumaini ya kushinda uchaguzi.
Jumla ya wagombea 14 wanawania urais, ingawa ni vyama vichache vinavyotambulika kwa kiasi kikubwa na wapiga kura.
Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30, hakuna chama chochote kilichowahi kuwa madarakani kinachowakilishwa kwenye karatasi ya kura ya urais. Soma Zaidi: