Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Iran yatishia kufunga njia zingine baharini, Marekani ikianzisha mashambulizi mapya

Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kushambulia miundombinu ya Iran wiki ijayo nchi hiyo isiporejea katika mazungumzo.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Ambia Hirsi

  1. Tunakomea hapo kwa leo. Kwaheri.

  2. Kikosi maalum cha polisi kuchunguza mauaji ya kiongozi wa kundi linalopinga wahamiaji Afrika Kusini

    Kikosi maalum cha polisi kimeanza kuchunguza mauaji ya kiongozi wa wa kundi linalopinga wahamiaji nchini Afrika Kusini.

    Polisi wamethibitisha kwamba Andile Mvuyelwa Somgxada, kiongozi wa mkoa wa Gauteng wa March and r, alipigwa risasi nje ya nyumba yake mashariki mwa Johannesburg mapema mwezi huu, akafariki siku kadhaa baadaye akipokea matibaby hospitalini.

    "Ni kitendo cha kulipiza kisasi," msemaji wa March and March Sandile Dube aliiambia BBC, akielezea jinsi vugu vugu hilo lilivyoamini alilengwa kwa sababu ya kampeni yake ya kuwashinikiza wahamiaji wasio na vibali waondoke nchini.

    Alisema viongozi wengine wa Marchi and March, ambao wamekuwa wakiandaa maandamano dhidi ya wahamiaji kote nchini, hivi karibuni walipokea vitisho vya mauaji.

    "Tukio hilo linaonekana kama mauaji yaliyopangwa," Dube aliambia BBC, akitoa wito kwa mamlaka kushughulikia suala hilo kikamilifu.

    Kaimu mkuu wa polisi Luteni Jenerali Puleng Dimpane ametangaza jopo la polisi wenye taaluma mbalimbali kuchunguza kisa hicho, kusisitiza jinsi polisi ilivyojitolea ikishughulikia kesi hiyo.

    "Tumejitolea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini mazingira yanayozunguka mauaji haya na kuwawajibisha waliohusika," alisema katika taarifa Jumanne jioni.

    Soma zaidi:

  3. Sierra Leone yamuondolea mashtaka ya uhaini rais wa zamani Ernest Bai Koroma

    Serikali ya Sierra Leone imeondoa mashtaka ya uhaini, dhidi ya Rais wa zamani Ernest Bai Koroma, ambaye alikamatwa kuhusiana na jaribio la mapinduzi takriban miaka mitatu iliyopita.

    Mashtaka hayo yaliondolewa kwa sababu za kiafya, Waziri wa Habari Chernor Bah aliambia BBC.

    Rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 72 amekuwa akikanusha kuhusika katika jaribio la mapinduzi la Novemba 2023, ambapo watu wenye silaha walivamia ghala la silaha la jeshi na magereza kadhaa, na kuwaachilia huru takriban wafungwa 2,000.

    Katika taarifa yake siku ya Jumanne, Koroma alimshukuru Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio, Rais wa Nigeria Bola Tinubu na jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS, kwa uungaji mkono wao.

    Baada ya Koroma kushtakiwa na kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani, ECOWAS ilisimamia makubaliano na serikali ya Sierra Leone, yaliyomruhusu rais huyo wa zamani kwenda uhamishoni nchini Nigeria na kupata matibabu.

    Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliwasilisha ombi la kusitisha kwa kesi dhidi ya Koroma na kumuondolea mashtaka hayo, Bah alisema.

    "Kwa hivyo, rais huyo wa zamani yuko huru kurejea Sierra Leone wakati wowote anaotaka na kuendelea na shughuli zake za kawaida," aliongeza.

    Koroma aliiongoza Sierra Leone kwa miaka 11 hadi mwaka 2018, wakati Rais wa sasa Julius Maada Bio alipochaguliwa.

    Soma zaidi:

  4. Wahouthi warusha makombora Saudi Arabia

    Kundi la Wahouthi nchini Yemen limerusha makombora kuelekea nchini Saudi Arabia baada ya kuishutumu kwa kulipua uwanja wa ndege unaodhibitiwa na kundi hilo, hatua ambayo inakiuka makubaliano ya kusitisha mapigano ya miaka minne kati ya pande hizo mbili.

    Shambulio hilo linaashiria mwisho wa kipindi cha kushuka kwa uchumi kati ya Saudi Arabia na Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran na limeibua wasiwasi kwamba Tehran itatumia washirika wake wa Wahouthi kuzuia Mlango Bahari wa Bab al-Mandab.

    Bab al-Mandab ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za meli duniani na njia ya kuelekea maji makuu, na kufungwa kwake kutaathiri biashara ya baharini duniani, baada ya kuvurugika kwa Mlango Bahari wa Hormuz.

    Maelezo zaidi:

  5. Iran yatishia kufunga njia zaidi za baharini, Marekani ikianzisha mashambulizi mapya

    Iran imetishia kuzuia njia zaidi za usafiri wa majini katika eneo hilo, baada ya Marekani kuanzisha wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya ngome zake za kijeshi.

    Vikosi vya Walinzii wa Mapinduzi wa Iran IRGC vimesema Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kufungwa hadi Marekani itakapokomesha "vitendo vyake vya uchokozi".

    IRGC pia imetishia kufunga njia zingine za usafirishaji wa mafuta na gesi za kikanda.

    Tishio hilo limekuja baada ya Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (Centcom) kutangaza kuwa imefanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani, angani na majini dhidi ya jeshi la majini la Iran Jumatano asubuhi, katika operesheni ya usiku kucha.

    Uhasama mpya kati ya Marekani na Iran katika siku za hivi karibuni umesaidia kusisitiza umuhimu wa kimkakati wa Mlango wa Hormuz kwa uchumi wa dunia.

    Mashambulizi hayo mapya pia yamesababisha kupanda kwa kasi kwa bei ya mafuta, huku safari ya meli za mafuta kupitia njia hiyo muhimu ya majini ikikaribia kukwama.

    Mashambulizi ya Jumatano asubuhi "yalizidi kupunguza uwezo wa Iran kushambulia meli za kibiashara katika Mlango wa Hormuz," Centcom ilisema katika taarifa.

    Wimbi la dakika 90 lilitumika kulenga ulinzi wa pwani ya Iran na maeneo ya kuhifadhi makombora na kurusha makombora kwenye Kisiwa cha Greater Tunb, maafisa wa Centcom waliongeza.

    Siku ya Jumanne, Rais wa Marekani Donald Trump aliapa kushambulia madaraja na mitambo ya umeme ya Iran wiki ijayo ikiwa nchi hiyo haitarejea kwenye mazungumzo.

    Soma Zaidi Hapa:

  6. Urusi yashambulia meli mbili zilizokuwa na bendera ya Tanzania na Liberia katika Bahari Nyeusi

    Vikosi vya Urusi vimeshambulia meli mbili za kibiashara zilizokuwa zikihudumu chini ya bendera za mataifa ya Tanzania na Liberia katika Bahari Nyeusi.

    Nahodha wa moja ya meli hizo aliuawa katika shambulio hilo.

    Mkuu wa Utawala wa Kijeshi wa Oblast Oleh Kiper, Mamlaka ya Bandari ya Ukraine (USPA),alisema Urusi imekuwa ikishambulia kiholela meli za kiraia.

    "Adui anaendelea kushambulia meli za raia kimakusudi katika Bahari Nyeusi. Lengo la mshambuliaji lilikuwa meli mbili za kibiashara zilizokuwa zikisafiri kando ya ukanda wa bahari chini ya bendera za Tanzania na Liberia," alisema Kiper

    Wafanyakazi wa watu 11 walihamishiwa ufukweni,huku watatu kati yao wakijeruhiwa katika shambulio hilo.

    Kwa siku ya tano mfululizo, Urusi imeendelea kufanya mashambulizi dhidi ya miundombinu ya bandari ya Greater Odesa na meli za raia.

    ''Adui anatumia makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani, kushambulia usiku na mchana bandari, meli za raia na mabaharia," USPA iliongeza kusema.

    Shambulio la hivi karibuni dhidi ya chombo cha kiraia kilichokuwa kikisafiri chini ya bendera ya Tanzania lilisababisha kifo cha mtu mmoja.

    USPA iliripoti kwamba watu tisa wameuawa tangu kuanza kwa wimbi hili la mashambulizi ya Urusi.

  7. Marekani yazuia mali za kidijitali za 'zaidi ya dola milioni 130' zinazohusishwa na Iran

    Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Besant ametangaza kufungia mali za kidijital za Iran zilizo na thamani ya "zaidi ya dola milioni 130".

    "Idara ya Fedha ya Marekani imejitolea kudhibiti shughuli haramu za kifedha za Iran, ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya mali za kidijitali,"Scott Besant alisema katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii X

    Aliongeza kusema: "Idara ya Udhibiti wa Mali za Kigeni ya Wizara ya Fedha ya Marekani iliidhinisha kuzuiliwa kwa akaunti kadhaa za kidijitali zilizounganishwa na Benki Kuu ya Iran, na kusababisha kufungiwa kwa zaidi ya dola milioni 130."

    "Tutaendelea kufuatilia na kudhibiti utakasaji wa pesa na kuinyima serikali ya Iran ufikiaji wa mapato ya programu zake haramu."

    Idara ya Udhibiti wa Mali za Kigeni ya Marekani hivi karibuni iliwekea vikwazo masoko kadhaa makubwa ya Iran ambayo, kulingana na idara hiyo, yalihamisha mabilioni ya dola kila mwaka kwa niaba ya benki za Iran zilizowekewa vikwa kutumia mtandao wa makampuni ya siri kuficha shughuli haramu za kifedha za serikali.

    Maelezo zaidi:

  8. Mwanajeshi wa Israel ahukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kufanyia Iran upelelezi

    Mahakama ya kijeshi nchini Israel imemhukumu askari kifungo cha miaka mitano jela kwa madai ya kutoa taarifa nyeti kwa "wakala wa Iran" ili kupata malipo.

    Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama, askari huyo—ambaye jina lake halijatolewa hadharani—alituma video zinazoonyesha makombora mawili yakizuiliwa kwa "wakala wa Iran" wakati wa vita vifupi vilivyotokea mwaka jana kati ya Israel na Iran.

    Mamlaka za mahakama nchini Israel zilikuwa zimeomba adhabu kali zaidi kwa askari huyo, lakini mahakama ilitoa hukumu hafifu zaidi ikizingatia kuwa alisitisha kwa hiari uhusiano wake na "wakala wa Iran," kisha akatoa taarifa kwa makamanda wake na kukiri kosa la upelelezi.

    Mbali na kifungo cha miaka mitano jela, askari huyo pia alihukumiwa kulipa faini na kushushwa cheo hadi askari wa kawaida.

    Soma pia:

  9. Mahakama yakataa ombi la Jumuiya ya rastafari kutumia bangi katika ibada

    Mahakama Kuu nchini Kenya imekataa ombi la Chama cha Warastafari Kenya lililotaka kuruhusiwa kutumia bangi kwa shughuli za ibada, ikisema marufuku ya dawa hiyo nchini haikiuki haki za kikatiba.

    Katika uamuzi uliotolewa Jumatano, Jaji Bahati Mwamuye alitupilia mbali ombi hilo, akisema waombaji hawakuwasilisha ushahidi wa kutosha unaothibitisha kuwa matumizi ya bangi ni sehemu ya msingi ya dini ya Kirastafari.

    Chama hicho kilikuwa kimeiomba mahakama kuwaruhusu waumini wake kulima, kumiliki na kutumia bangi katika nyumba binafsi na maeneo maalumu ya ibada bila kukabiliwa na hatua za kisheria.

    Warastafari walisisitiza kuwa hawakuwa wanataka bangi ihalalishwe kwa matumizi ya umma, bali walikuwa wanaomba msamaha wa matumizi yake kwa madhumuni ya ibada pekee.

    Serikali ilipinga ombi hilo kwa hoja kwamba kutoa msamaha wa kidini kungeathiri utekelezaji wa sheria za kupambana na dawa za kulevya na kufungua mianya ya biashara haramu ya bangi.

    "Waombaji hawakuwasilisha ushahidi wa kutosha na unaoendana unaothibitisha kuwa matumizi ya bangi ni sehemu muhimu au ya lazima ya dini ya Kirastafari," alisema Jaji Bahati Mwamuye.

    Shauri hilo lililowasilishwa mwaka 2021 lilitaka mahakama iamue ikiwa kuhalalisha adhabu za matumizi ya bangi kunakiuka haki za Warastafari, zikiwemo haki ya uhuru wa kuabudu, faragha, utu, usawa na uhuru wa kujumuika.

    Uamuzi huo unakuja miaka saba baada ya Mahakama Kuu kutambua dini ya Kirastafari kama dini inayolindwa na Katiba, katika kesi iliyohusu mwanafunzi aliyefukuzwa shule kwa sababu ya nywele zake za rasta.

    Bangi inaendelea kuwa haramu nchini Kenya, ambapo mtu anayepatikana na hatia ya kuimiliki anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 10 jela.

    Soma pia:

  10. Ripoti yasema Kenya iko katika hatari kubwa ya kushuhudia vurugu za uchaguzi wa 2027

    Kenya inakabiliwa na uwezekano wa asilimia 84.1 wa kutokea kwa aina fulani ya vurugu zinazohusiana na uchaguzi wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Taasisi ya Kofi Annan.

    Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia hiyo ni tathmini ya kiwango cha hatari na si uhakika kwamba vurugu zitatokea. Hivyo, inatoa wito kwa serikali, viongozi wa kisiasa, asasi za kiraia na wananchi kuchukua hatua mapema ili kuimarisha juhudi za kudumisha amani na kuzuia vurugu kabla hazijatokea.

    "Takwimu hizi ni tathmini ya hatari, si uhakika wa kitakachotokea. Zinapaswa kuwa mwito wa kuchukua hatua mapema ili kuimarisha juhudi za amani na kuzuia vurugu kabla hazijatokea," imeongeza ripoti hiyo.

    Kwa mujibu wa Taasisi ya Kofi Annan, uchaguzi unaweza kuwa fursa ya kuimarisha demokrasia, lakini pia unaweza kuongeza mvutano iwapo kutakuwa na mgawanyiko wa kisiasa, taasisi dhaifu au kupungua kwa imani ya wananchi katika mchakato wa uchaguzi.

    Ripoti hiyo imeeleza kuwa Kielezo cha Hatari ya Uchaguzi kinatumia viashiria vya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutawala kutathmini mazingira ya uchaguzi na kutoa tahadhari ya mapema kwa watunga sera, wasimamizi wa uchaguzi na wadau wengine.

    Kenya ni miongoni mwa nchi 10 zilizofanyiwa uchambuzi wa kina katika ripoti hiyo, ambao unachanganya tathmini ya takwimu na uchambuzi wa mazingira ya kisiasa, changamoto za uchaguzi na hatua zinazoweza kuchukuliwa kupunguza hatari ya vurugu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

  11. Majaribio ya dawa ya kuzuia Ebola yaanza DR Congo na Uganda

    Shirika la Afya Duniani, WHO, limetangaza kuanza kwa majaribio ya kwanza ya kitabibu ya dawa ya kuzuia Ebola kwa watu waliokaribiana na walioambukizwa virusi hivyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Uganda.

    Majaribio hayo, yanayojulikana kama EBO PEP, yanalenga kutathmini uwezo wa dawa ya obeldesivir kuzuia maambukizi ya aina ya Bundibugyo Ebola kwa watu waliowahi kukutana na wagonjwa waliothibitishwa kuwa na virusi hivyo.

    Dawa hiyo ya majaribio, inayotengenezwa na kampuni ya Marekani ya Gilead Sciences na kutumiwa kwa njia ya kumeza, imeonyesha matokeo ya kutia matumaini katika tafiti za awali.

    Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuanza kwa majaribio hayo ni hatua muhimu katika juhudi za kukabiliana na Ebola.

    "Kila mafanikio huanza na matumaini. Ikiwa dawa hii itathibitika kuwa na ufanisi kwa watu walio katika hatari kubwa baada ya kuathiriwa, inaweza kuwa hatua kubwa mbele katika kuzuia maambukizi ya Ebola," alisema Tedros.

    WHO imesema iwapo dawa hiyo itafanikiwa, inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuwalinda wahudumu wa afya, wanafamilia na jamii wakati wa milipuko ya Ebola.

  12. Rwanda yasaini mkataba wa udhamini na Aston Villa kupitia kampeni ya Visit Rwanda

    Klabu ya Aston Villa imetangaza kampeni ya utalii ya Visit Rwanda kuwa mdhamini mkuu wa jezi za nyumbani kwa msimu wa 2026 hadi 2027 wa Ligi Kuu ya England.

    Chini ya makubaliano hayo, nembo ya Visit Rwanda itaonekana mbele ya jezi za timu za wanaume, wanawake na vijana.

    Aidha, kampeni hiyo itakuwa mshirika wa utalii wa klabu hiyo pamoja na msambazaji wa kahawa.

    Mkurugenzi wa Biashara wa Aston Villa, Francesco Calvo, amesema ushirikiano huo unaashiria kuendelea kwa ukuaji wa klabu hiyo.

    “Huu ni ushirikiano mkubwa kwa Aston Villa. Kuna fursa nyingi za kushirikiana, kujifunza na kuleta ubunifu. Tunafurahia kufanya kazi na Visit Rwanda kuanzisha shughuli zenye manufaa kupitia utalii, uwekezaji na maendeleo ya michezo.”

    Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda, Jean Guy Afrika, amesema ushirikiano huo utaiwezesha Rwanda kujitangaza kwa mamilioni ya watu duniani.

    “Ushirikiano huu unatupa fursa kubwa ya kuisogeza Rwanda karibu na mamilioni ya watu duniani, kwa kuwaalika kutembelea, kuwekeza, kufanya biashara na kugundua fursa zilizopo nchini mwetu.”

    Mkataba huu unakuja baada ya ushirikiano wa Visit Rwanda na Arsenal kumalizika mwishoni mwa msimu uliopita.

    Makubaliano hayo yalikuwa yamekumbwa na ukosoaji kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa Arsenal kutokana na madai ya kuhusika kwa Rwanda katika mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, madai ambayo Rwanda imekuwa ikiyakanusha.

    Aston Villa ilimaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu ya England katika nafasi ya nne.

  13. Trump: Iran isiporejea kufanya mazungumzo, tutashambulia mitambo ya umeme na madaraja

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema jeshi lake litalenga mitambo ya kuzalisha umeme na madaraja nchini Iran wiki ijayo ikiwa Tehran haitarejea kwenye meza ya mazungumzo.

    Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Fox News, Trump amesema hatua hiyo itachukuliwa iwapo Iran haitakubali kuendelea na mazungumzo.

    "Ikiwa Iran haitarejea kwenye meza ya mazungumzo, tutalenga mitambo yao ya umeme na madaraja wiki ijayo," alisema Trump.

    Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuanzisha operesheni ya vikosi vya ardhini, Trump hakutoa jibu la moja kwa moja.

    "Sitazungumzia hilo kwa undani. Wakati mwingine operesheni ya ardhini inahitajika, lakini kuna watu wengine watakaoitekeleza kwa niaba yetu," alisema.

    Kauli hiyo imekuja wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ukiendelea kuongezeka, huku pande zote zikiendeleza mashambulizi na vitisho vya kijeshi.

    Soma Zaidi Hapa:

  14. Hispania yafuzu fainali baada ya kuichapa Ufaransa

    Beki wa Hispania na mchezaji bora wa mechi, Pedro Porro, amesema kufuzu kwa timu yake ni ndoto aliyokuwa akiisubiri kwa muda mrefu.

    "Hii ni ndoto iliyotimia kwangu. Ilikuwa ndoto yangu kubwa zaidi. Nina furaha sana kwa timu. Tulicheza vizuri kuanzia mwanzo hadi mwisho na leo tulifanya kila tulichoweza ili kufuzu," alisema Porro.

    Akizungumzia ushindi dhidi ya Ufaransa, Porro alisema walijua wangekutana na mpinzani mgumu lakini walitekeleza mpango wao ipasavyo.

    "Tulijua tunakutana na timu ngumu sana. Huu ni ushindi wa timu nzima, si wangu pekee. Nawapongeza wachezaji wote kwa kiwango walichoonyesha."

    Kuhusu jinsi walivyowadhibiti Wafaransa, Porro alisema umiliki wa mpira ulikuwa sehemu muhimu ya mkakati wao.

    "Tulijua kumiliki mpira kungetusogeza karibu na ushindi. Mashambulizi yao ya kushtukiza ndiyo silaha yao kubwa, na kuyazuia ilikuwa jambo muhimu."

    Porro pia alisema alitolewa uwanjani baada ya kuhisi hangeweza kuendelea kuchangia zaidi, akisisitiza kuwa ushindi huo ulitokana na mchango wa kikosi kizima.

    "Nilihisi siwezi kuchangia zaidi. Ushindi huu umeletwa na wachezaji wote 26. Sasa tunaelekeza nguvu zetu kwenye fainali."

    Alimalizia kwa kusema kuwa licha ya uchovu, Hispania itajipanga upya na kupambana kwa nguvu zote katika mchezo wa fainali.

    Soma Zaidi:

  15. Maseneta wa Democratic wazuia muswada wa ulinzi wa Marekani kupinga vita na Iran

    Maseneta wa Chama cha Democratic nchini Marekani wamekwamisha kupitishwa kwa Muswada wa Mwaka wa Sera ya Ulinzi, wakionyesha kupinga kuendelea kwa vita dhidi ya Iran.

    Muswada huo, unaojulikana kama National Defense Authorization Act (NDAA), umeshindwa kusonga mbele baada ya kuungwa mkono na maseneta 50 huku 46 wakipinga.

    Ingawa bado unahitaji hatua nyingine kabla ya kuwa sheria, matokeo hayo yanaonyesha mgawanyiko mkubwa katika Seneti kuhusu sera ya Marekani dhidi ya Iran na athari zake kwa bajeti ya Wizara ya Ulinzi.

    Seneta Richard Blumenthal, mwanachama wa chama cha Democratic na kiongozi wa upinzani katika Kamati ya Seneti ya Huduma za Kijeshi, alisema muswada huo kwa sasa unaendeleza ufadhili wa vita dhidi ya Iran.

    "Kwa mtazamo wangu, sheria hii inaendeleza ufadhili wa vita, huku utawala wa sasa ukikosa uwajibikaji," alisema.

    Blumenthal alisema hataunga mkono muswada huo hadi utawala wa Rais Donald Trump utoe mkakati wazi kuhusu Iran na upate idhini ya Bunge kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Vita.

    Naye Seneta Tammy Duckworth alisema asingepigia kura muswada huo kusonga mbele isipokuwa marekebisho aliyopendekeza yapitishwe, yakilenga kuzuia fedha zaidi kutumika kufadhili operesheni za kijeshi za kushambulia Iran.

    Soma Zaidi Hapa:

  16. Trump afuta pendekezo la tozo ya asilimia 20 kwa meli zinazopita Hormuz

    Rais wa Marekani Donald Trump ameondoa pendekezo lake la kutoza ada ya asilimia 20 kwa mizigo yote inayopitia Mlango wa Bahari wa Hormuz, akisema badala yake atategemea mikataba mikubwa ya biashara na uwekezaji kutoka mataifa ya Ghuba.

    Hatua hiyo imekuja saa chache kabla ya Jeshi la Marekani kupitia Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) kurejesha kizuizi dhidi ya bandari za Iran na kuanzisha duru mpya ya mashambulizi dhidi ya malengo ya Iran.

    CENTCOM ilisema mashambulizi hayo yanalenga kudhoofisha uwezo wa Iran wa kushambulia meli za kibiashara zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Mashambulizi hayo yanafuatia mapigano mapya kati ya Marekani na Iran, ambayo yamesababisha bei ya mafuta kupanda huku shughuli za usafirishaji wa mafuta kupitia Hormuz zikipungua kwa kiasi kikubwa.

    Iran ilisema imelenga vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Bahrain na Jordan, baada ya awali kushambulia meli mbili za Umoja wa Falme za Kiarabu.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema:

    "Nimeamua kuondoa tozo ya asilimia 20 ya Marekani na badala yake mataifa ya Ghuba yatawekeza na kufanya mikataba mikubwa ya biashara nchini Marekani."

    Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi kuhusu mpango huo.

    Trump pia alisema Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kuwa wazi kwa meli zote isipokuwa zile zinazofanya biashara na Iran.

    Baadaye, akizungumza mjini Washington, Trump alisema hakupendelea wazo la kutoza ada kwa meli zinazopita Hormuz, lakini akaongeza kuwa si haki kwa Marekani kubeba jukumu la kulinda njia hiyo muhimu ya baharini kwa manufaa ya dunia nzima.

    Kwa upande wake, Iran imesema itaendelea kusimamia Mlango wa Bahari wa Hormuz licha ya hatua za Marekani.

    Unaweza kusoma;

  17. Iran yasema makubaliano ya kusitisha mapigano na Marekani yamevunjika

    Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa masuala ya kisheria Iran Kazem Gharibabadi amesema hakuna tena kinachoitwa Makubaliano ya Islamabad kati ya Tehran na Washington, akidai kuwa mashambulizi mapya ya Marekani yameharibu kabisa msingi wa maelewano yaliyokuwapo.

    Kauli hiyo imekuja baada ya Marekani kuanzisha mashambulizi mapya katika pwani ya kusini mwa Iran na Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) kutangaza kurejesha kizuizi cha majini dhidi ya bandari za Iran.

    "Hakuna tena kinachoitwa Makubaliano ya Islamabad. Msingi wa maelewano kati ya Iran na Marekani umeharibiwa kabisa," alisema Naibu Waziri huyo.

    Mapema Jumatano, milipuko kadhaa iliripotiwa katika maeneo ya kusini mwa Iran kufuatia mashambulizi ya Marekani.

    Kwa kujibu mashambulizi hayo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na jeshi la Iran yalisema yamelenga vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Kuwait, Bahrain na Jordan kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani.

    Mvutano kati ya Iran na Marekani umeendelea kuongezeka huku pande zote zikiendeleza mashambulizi na hatua za kijeshi katika eneo la Ghuba.

    Soma Zaidi:

  18. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.