Wanaharakati walaani kufungwa kwa mtandao wa X Tanzania

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeeleza kusikitishwa kwake na pia kimelaani uamuzi wa hivi karibuni wa Serikali ya Tanzania wa kufunga mtandao wa kijamii wa X (zamani wa Twitter).

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi, Dinah Gahamanyi & Asha Juma

  1. Wanaharakati walaani kufungwa kwa mtandao wa X Tanzania

    Mtandao wa X

    Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeeleza kusikitishwa kwake na pia kimelaani uamuzi wa hivi karibuni wa Serikali ya Tanzania wa kufunga mtandao wa kijamii wa X (zamani wa Twitter).

    Hatua hiyo imethibishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia,Jerry Silaa wakati wa mahojiano na kituo cha televisheni.

    Kwa mujibu wa Slaa, uhalali wa serikali kwa hatua hii unatokana na sera za maudhui za jukwaa, ambazo zinadaiwa kuruhusu maudhui yanayokiuka sheria na maadili ya Tanzania.

    Wanaharakati hao wamesema ingawa wanaunga mkono umuhimu wa kudhibiti maudhui ya mtandaoni kwa mujibu wa sheria za kitaifa, ''tunasisitiza kwa nguvu zote kwamba hatua hizo lazima ziwe na uwiano, uwazi, na kuheshimu haki za msingi za binadamu hasa haki za uhuru wa kujieleza na kupata habari''.

    Wanaharakati wanadai kurejeshwa mara moja kwa X, Clubhouse Telegramu na majukwaa mengine yoyote yaliyowekewa vikwazo

    Wameitaka serikali kuhakikisha kunakuwa na uwazi katika michakato ya udhibiti wa kidijitali kwa kushirikisha wadau katika kuunda sera za udhibiti wa maudhui zinazoheshimu haki za binadamu.

    Pia kuzingatia wajibu wa kikatiba na kimataifa kulinda uhuru wa kujieleza, upatikanaji wa habari na haki za kidijitali.

    ''Tunawaomba wadau wote, ikiwa ni pamoja na jumuiya ya kimataifa, kuendelea kuwa macho na kuunga mkono juhudi za kulinda uhuru wa kidijitali nchini Tanzania''. Ilieleza taarifa ya LHRC.

    Unaweza kusoma;

  2. Gaza imekuwa mbaya zaidi kuliko 'jehanamu' duniani, Shirika la Msalaba Mwekundu laambia BBC

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Gaza imekuwa mbaya zaidi kuliko jehanamu Duniani, rais wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), amesema.

    Akizungumza katika mahojiano na BBC katika makao makuu ya ICRC mjini Geneva, Spoljaric alisema ubinadamu haupo tena.

    Mataifa hayafanyi vya kutosha kumaliza vita, mateso ya Wapalestina na kuwaachilia mateka wa Israeli, aliongeza.

    Wapalestina, anasema, wamevuliwa utu wa kibinadamu lakini sheria ya kimataifa ya kibinadamu haionekani tena kuchukua mkondo wake.

    Kinachotokea Gaza, alisema, kinazidi chochote kinachokubalika kisheria, kimaadili na kiutu.

    ICRC ni shirika la kimataifa linalofanya kazi katika maeneo ya vita likiwa na zaidi ya wafanyakazi 300 huko Gaza, wengi wao wakiwa Wapalestina.

    Soma zaidi:

  3. Nyota wa TikTok alipigwa risasi na kufa nyumbani kwake - polisi

    .

    Chanzo cha picha, Sanayousaf22

    Mwanamume mwenye umri wa miaka 22 amekamatwa nchini Pakistan na kukiri kumuua msichana mwenye umri wa miaka 17 aliyekuwa mshawishi wa mitandao ya kijamii Sana Yousaf, kulingana na polisi.

    Mamlaka inasema inaamini kuwa Umar Hayat alimuua Bi Yousaf nyumbani kwake huko Islamabad siku ya Jumatatu baada ya kukataa kile walichokiita "kutaka awe naye urafiki".

    Inadaiwa pia alijaribu mara kwa mara na akashindwa, kukutana naye.

    Wanasema alivamia nyumbani kwake, akafyatua risasi mbili, akaiba simu yake na kutoroka.

    Babake Bi Yousaf, Syed Yousaf Hassan, aliambia BBC kwamba alikuwa binti yake wa pekee, na alikuwa "jasiri sana". Familia yake imekusanyika Chitral, ambapo Bi Yousaf amezikwa.

  4. Ujerumani inahamisha raia 20,000 kutegua mabomu ya Vita vya Pili vya Dunia

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Mji wa Cologne nchini Ujerumani unawahamisha takriban watu 20,500 kutoka eneo kubwa katikati mwa jiji ili wataalamu waweze kutegua mabomu matatu ambayo hayakulipuka katika Vita vya Pili vya Dunia.

    Mabomu hayo ya Marekani yaligunduliwa siku ya Jumatatu katika kitongoji cha Deutz, mji huo ulisema katika taarifa.

    Mabomu ambayo hayajalipuka bado yanaweza kusababisha hatari na jiji limefunga eneo hilo lililo na ukubwa wa mita 1,000 (3,280ft), katika kile ilichoelezea kama "operesheni kubwa zaidi tangu mwisho wa WW2".

    Nyumba, maduka, hoteli na shule zimeagizwa kuhama, pamoja na hospitali kubwa na kituo kikuu cha gari moshi.

  5. Kiongozi Mkuu wa Iran akosoa pendekezo la Marekani la makubaliano ya nyuklia

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amekosoa pendekezo la Marekani la makubaliano mpya ya nyuklia, akisisitiza kwamba haitaacha kurutubisha madini ya urani.

    Wapatanishi wa Iran wanatazamiwa kujibu katika siku zijazo kwa kile Ikulu ya Marekani ilichokiita "mpango wa kina na unaokubalika" uliowasilishwa kwenye mazungumzo Jumamosi iliyopita.

    Ripoti za Marekani zinasema inapendekeza kuwa Iran isitishe uzalishaji wa madini yote ya uranium yaliorutubishwa - ambayo yanaweza kutumika kutengeneza fyueli ya kinu na pia silaha za nyuklia - na badala yake itegemee muungano wa kikanda kwa ajili ya usambazaji.

    Akiwa kiongozi mkuu, Khamenei ana usemi wa mwisho juu ya masuala muhimu zaidi ya nchi, ikiwa ni pamoja na makubaliano ya nyuklia.

    Katika hotuba ya kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, Ayatollah Ruhollah Khomeini, alisema "Hilo linakinzani kwa asilimia 100 na wazo la 'Tunaweza'" - kauli mbiu maarufu ya Khomeini.

    "Urutubishaji wa madini ya Urani ndio ufunguo wa mpango wetu wa nyuklia na maadui wamekodolea macho urutubishaji huo," aliongeza.

    "Viongozi wasio na adabu na wenye kiburi wa Marekani wanadai mara kwa mara kwamba tusiwe na mpango wa nyuklia. Wewe ni nani kuamua kama Iran inapaswa kuwa na madini yaliyorutubishwa?"

    Khamenei alikuwa akizungumza siku chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusisitiza kwamba Iran italazimika kusitisha urutubishaji wa madini ya uranium.

    Soma zaidi:

  6. Mwandishi wa Kenya ashtakiwa kwa kuandika kitabu kuhusu binti wa rais

    ,

    Chanzo cha picha, Francis Odee

    Watetezi wa uhuru wa kujieleza na mawakili nchini Kenya wamelaani kushtakiwa kwa mwandishi kwa wasifu ambao haujaidhinishwa wa binti ya Rais wa Kenya William Ruto.

    Charlene Ruto alimshutumu Webster Ochora Elijah kwa "kutumia vibaya" jina lake kwa kuandika kitabu bila kwanza kuomba kibali kutoka kwake.

    Siku ya Jumanne, mwandishi huyo alikamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kuiga kuwa binti wa rais kwenye kitabu kilichoitwa Beyond the Name: Charlene Ruto and the Youth Uprising.

    Hata hivyo, alikanusha mashtaka hayo na kuachiliwa kwa dhamana.

    Charlene Ruto aliambia wanahabari kuwa ameripoti kisa hicho kwa polisi na anafuata taratibu za kisheria. Ameorodheshwa kama mlalamishi kwenye karatasi ya mashtaka.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Afrika Kusini: Mwanasiasa afutwa kazi kwa kumtembelea Nabii Bushiri

    .

    Chanzo cha picha, Gallo Images via Getty Images

    Afisa wa ngazi ya juu katika mojawapo ya vyama vikubwa zaidi vya kisiasa nchini Afrika Kusini amefutwa kazi baada ya kumtembelea mchungaji wa Malawi mwenye utata mnamo mwezi Aprili.

    Floyd Shivambu amefutwa kazi kama katibu mkuu wa chama cha uMkhonto weSizwe (MK) baada ya miezi sita tu kwa kuhudhuria ibada ya Pasaka katika kanisa la Nabii milionea wa Malawi Shepherd Bushiri.

    Bw Bushiri, kutoka Malawi, alikuwa mmoja wa wahubiri maarufu kusini mwa Afrika alipokamatwa na kushtakiwa kwa udanganyifu nchini Afrika Kusini mwaka wa 2020.

    Baada ya kuachiliwa kwa dhamana, alifanikiwa kukimbilia nchini mwake katika mazingira yasiyoeleweka. Afrika Kusini imekuwa ikijaribu kumrejesha nchini humo tangu wakati huo.

    Bw Bushiri amekanusha kufanya makosa yoyote.

    Chama cha MK, ambacho kiliasisiwa na Rais wa zamani Jacob Zuma, kilisema katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano kwamba kuondolewa kwa Bw Shivambu kumetokea baada ya vitendo vyake "kuonekana kuwa kinyume na mwelekeo na maagizo ya katiba ya chama cha MK".

    "Rais na maafisa wa kitaifa hawakuwa na chaguo jingine ila kuchukua hatua haraka," mwenyekiti wa kitaifa wa MK Nathi Nhleko alisema.

    Aliongeza kuwa safari hiyo "haikuwa mpango ulioidhinishwa rasmi na chama hicho".

    Hata hivyo, Bw Shivambu anasalia kuwa mwanachama wa chama na badala yake atawakilisha MK katika Bunge la Kitaifa.

    Soma zaidi:

  8. Vituo vya misaada vya Gaza vyafungwa kwa siku huku Israeli ikionya barabara ni 'maeneo ya mapigano'

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Vituo vya usambazaji wa misaada huko Gaza vitafungwa leo baada ya jeshi la Israel kuonya barabara zinazoelekea kwenye maeneo hayo zitachukuliwa kuwa "maeneo ya mapigano" .

    Wakfu wa misaada ya Kibinadamu wa Gaza (GHF), mtandao wenye utata unaoungwa mkono na Marekani na Israel ambao ulianza kufanya kazi wiki iliyopita, unasema kuwa unafunga tovuti zake kwa ajili ya "kusasisha, shirika na kazi za kuboresha ufanisi".

    Katika taarifa tofauti, Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) linasema watu "watapigwa marufuku" kuingia kwenye vituo vya usambazaji au kusafiri kwenye barabara zinazoelekea kwao.

    Hii ni baada ya Wapalestina wasiopungua 27 kuuawa na moto uliosababishwa na mashambulio ya Israeli karibu na kituo cha usambazaji siku ya Jumanne, kulingana na Shirika la Ulinzi la kiraia linaloendeshwa na Hamas. IDF inasema wanajeshi wake walifyatua risasi baada ya kuwatambua washukiwa ambao walisogea kwao "wakitoka kwenye njia zilizowekwa".

    Lilikuwa tukio la tatu la mauti ndani ya siku nyingi kutokea kwenye njia ya kwenda kwenye eneo la shirika la GHF.

    Umoja wa Mataifa umeonya kuwa zaidi ya watu milioni mbili wako hatarini kukumbwa na njaa huko Gaza, baada ya Israel kupiga marufuku usafirishaji wa chakula na misaada mingine uliodumu kwa wiki 11.

  9. Kenya yatuhumiwa kutumia sheria ya uhalifu mtandao kukandamiza upinzani

    Rose Njeri

    Chanzo cha picha, Vocal Africa/X

    Gazeti la The Standard, nchini Kenya limeripoti kuwa serikali imekuwa ikitumia Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandao kukandamiza ushiriki wa raia na harakati za kidijitali

    Serikali ilimkamata mwanaharakati wa kidijitali Rose Njeri kwa kuunda programu ya mtandaoni iliyoruhusu Wakenya kutuma barua pepe kwa kamati ya bunge wakielezea maoni yao dhidi ya Mswada wa Fedha wa 2025.

    Upande wa mashtaka ulidai kuwa barua pepe hizo nyingi zilivuruga mifumo ya kamati hiyo.

    Njeri aliwakilishwa mahakama hiyo na aliyewakilishwa Jaji Mkuu David Maraga, Wakili Mwandamizi Kalonzo Musyoka, Seneta Dan Maanzo miongoni mwa mawakili wengine wakuu waliodai kuwa kesi hiyo ni jaribio la kuzima upinzani.

    Mswada wa Sheria ya Fedha wa 2024 ulisababisha maandamano makubwa kote nchini huku Wakenya wakikabiliwa na hali mbaya ya gharama ya maisha.

  10. Shirikisho la mchezo wa ndondi duniani laomba msamaha baada ya kumtaja Khelif katika tangazo la kupima jinsia

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Imane Khelif wa Algeria anasherehekea ushindi dhidi ya Liu Yang wa Uchina.

    Shirikisho la Mchezo wa Ngumi wa Dunia umeomba radhi baada ya Imane Khelif kutajwa katika tangazo lao la kupima jinsia kwa lazima kwa mabondia wote katika mashindano yake, akisema faragha ya mshindi wa medali ya dhahabu ya Olimpiki ya Paris ilipaswa kulindwa.

    Baraza la kimataifa, litakalosimamia mashindano ya ndondi katika Michezo ya Olimpiki ya 2028 baada ya kupewa kutambuliwa kwa muda na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, lilitoa tangazo hilo wiki iliyopita, chini ya mwaka mmoja baada ya Khelif kushinda dhahabu mjini Paris huku kukiwa na mzozo kuhusu jinsia.

    Tangazo hilo lilisema bodi hiyo ilituma barua kwa Shirikisho la Ndondi la Algeria ikisema Khelif "hatashiriki katika kitengo cha wanawake" katika mashindano yoyote ya duniani hadi atakapofanya kipimo cha utambuzi wa jinsia yake.

    Hata hivyo, chanzo kilisema rais wa ndondi duniani Boris van der Vorst amemuandikia barua rais wa Shirikisho la Ndondi la Algeria Abdelkader Abbas kuomba radhi kwa kujumuisha jina la Khelif.

    Van der Vorst alisema World Boxing ilipaswa kufanya juhudi kubwa kulinda usiri wa Khelif.

    Soma zaidi:

  11. Watu watano wauawa katika shambulizi dhidi ya msafara wa misaada ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan

    .

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Watu watano waliokuwa kwenye msafara wa Umoja wa Mataifa uliokuwa umebeba msaada kuelekea mji unaokumbwa na vita wa el-Fasher nchini Sudan wameuawa katika shambulio, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema.

    Watu kadhaa pia walijeruhiwa na malori mengi kuteketezwa katika shambulio la Jumatatu usiku, lililotokea karibu na El-Koma katika jimbo la Darfur Kaskazini, waliongeza.

    Pande mbili zinazozana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan - Kikosi Vikosi vya waasi na jeshi la Sudan - zimeshtumiana kwa kishambulia msafara wa Umoja wa Mataifa kwa kutumia ndege zisizo na rubani.

    Umoja wa Mataifa haukueleza jinsi shambulio hilo lilivyotokea, lakini umetaka uchunguzi wa haraka ufanyike na wahusika wachukuliwe hatua.

    Msafara huo ulijumuisha malori 15 kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa ya chakula na watoto, ambao walisema ni "uharibifu" na kwamba wanasikitika msaada haukuwafika watu "wanaokumbwa na njaa" huko El-Fasher.

    El-Fasher ni eneo kuu la mwisho huko Darfur Kaskazini chini ya udhibiti wa jeshi.

    Raia na wanajeshi katika eneo hilo wamekuwa wakishambuliwa na waasi wa RSF kwa zaidi ya mwaka mmoja.

    Soma pia:

  12. Jeshi la Israel lafanya mashambulizi ya anga dhidi ya Syria

    h

    Chanzo cha picha, Waangalizi wa Syria

    Jeshi la Israel lilitangaza kwamba lilifanya mashambulizi ya anga yaliyolenga "silaha za utawala wa Syria kusini mwa nchi."

    Gazeti la Observatory limeripoti kuwa milipuko mikali ilisikika katika mji wa Quneitra na maeneo ya vijijini ya Daraa kusini mwa Syria kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel. Ilibainisha kwamba walilenga Kikosi cha 175 karibu na mji wa Izra, jirani na Tal al-Mal kaskazini mwa Daraa, na Tal al-Shaar karibu na Quneitra.

    Bado hakuna taarifa iliyothibitishwa kuhusu majeruhi wowote.

    Observatory iliongeza kuwa uvamizi huo wa Israel ulikuja kujibu makombora mawili yaliyorushwa kutoka Syria kuelekea Israel.

    Kwa upande wake, jeshi la Israel lilithibitisha kwamba ndege yake "ilipiga silaha za utawala wa Syria kusini mwa Syria," ikiuwajibisha utawala wa Syria kwa kile ilichokitaja kuwa "hali ilivyo."

    Taarifa hiyo iliongeza kuwa utawala wa Syria "utaendelea kubeba madhara yake iwapo shughuli za uhasama zitaendelea kufanyika kutoka katika ardhi yake."

  13. Raia wa China watuhumiwa kuingiza kimagendo 'kiini hatari' nchini Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Raia wawili wa China wanatuhumiwa kuingiza nchini Marekani kuvu ambayo maafisa wanasema ni "kiini hatari cha kibaolojia".

    Yunqing Jian, 33, na Zunyong Liu, 34, wameshtakiwa kwa kula njama, kusafirisha bidhaa, kutoa taarifa za uongo na ulaghai wa viza, Ofisi ya Mwanasheria wa Marekani wa Michigan ilitangaza Jumanne.

    Waendesha mashtaka wanadai kuwa Bw Liu alijaribu kuingiza kuvu hiyo n chini kupitia uwanja wa ndege wa Detroit ili aweze kuofanyia utafiti katika maabara ya Chuo Kikuu cha Michigan ambako mpenzi wake, Bi Jian, alifanya kazi.

    Kuvu inayofahamika kisayansi kama Fusarium graminearum inasababisha magonjwa kwa mimea ya ngano, shayiri, mahindi na mchele ambayo inaweza kuangamiza mazao na kusababisha kutapika na uharibifu wa ini ikiingia kwenye chakula.

    Kuvu hiyo kisayansi ni kama "silaha inayoweza kuwa ya ugaidi wa kilimo", kulingana na Ofisi ya Mwanasheria wa Marekani, ikiongeza kuwa inaweza kusababisha hasara ya "mabilioni ya dola kote duniani kila mwaka."

    Maafisa zaidi wanadai kuwa Bi Jian alipokea ufadhili kutoka kwa serikali ya China kwa ajili ya utafiti wake kuhusu ugonjwa huo nchini China. Pia wanadai kuwa yeye ni mwanachama wa Chama cha Kikomunisti cha China.

    Mwanasheria wa Marekani Jerome F Gorgon Jr alielezea madai hayo kama "wasiwasi mkubwa zaidi wa usalama wa taifa".

    "Wageni hawa wawili wameshtakiwa kwa kusafirisha kuvu ambayo imefafanuliwa kama 'silaha inayoweza kutumika kama ugaidi wa kilimo' katika eneo la Marekani, inaonekana walikusudia kutumia maabara ya Chuo Kikuu cha Michigan kuendeleza mpango wao."

    Uchunguzi huo ulikuwa juhudi za pamoja kati ya FBI naIdara ya Forodha ya Marekani na Ulinzi wa Mipaka.

    BBC imewasiliana na Chuo Kikuu cha Michigan na ubalozi wa China mjini Washington DC kwa maoni.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.