Uturuki yaagiza kukamatwa kwa Netanyahu kufuatia shambulio la Fotilla
Uturuki imesema itaomba Interpol kutoa ilani nyekundu ya kimataifa ya kumtafuta na kumkamata Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika kesi inayohusiana na shambulio dhidi ya wanaharakati waliokuwa wakijaribu kupeleka misaada ya kibinadamu Gaza.
Waziri wa Sheria wa Uturuki, Akin Gurlek, amesema hati za kukamatwa zimetolewa dhidi ya Netanyahu na mshukiwa mwingine kwa tuhuma zikiwemo mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mateso.
Kesi hiyo inawahusisha watu 35 kufuatia hatua ya Israel kuingilia boti za Global Sea Flotilla katika maji ya kimataifa, ambazo zilikuwa zikielekea Gaza kupeleka misaada.
Uturuki ni miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa operesheni za kijeshi za Israel Gaza na imekuwa ikitaka hatua za kimataifa zichukuliwe dhidi ya Israel. Israel inakanusha tuhuma za ukiukaji wa sheria za kimataifa na haki za binadamu.