Mwendesha mashtaka wa mahakama ya ICC akosoa madai ya kuilenga Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, inakabiliwa na changamoto zinazoongezeka kutoka kwa baadhi ya nchi, hususan barani Afrika.
Katika mazingira hayo, Naibu Mwendesha Mashtaka wa ICC, Msenegali Mame Mandiaye Niang, amekuwa Dakar kama sehemu ya ziara yake katika nchi wanachama wa Mkataba wa Roma. Lengo lake ni kueleza jukumu la mahakama hiyo na kujibu shutuma zinazoikabili.
Akizungumza na BBC News Africa, Niang amekanusha madai kwamba ICC inalenga Afrika, akisema mahakama hiyo imeanzisha uchunguzi kadhaa barani humo kwa ombi la nchi zinazohusika.
Amesema ICC inazingatia kanuni ya ukamilishano, ambapo mahakama ya kimataifa huingilia pale mifumo ya kitaifa inaposhindwa au kutokuwa tayari kushughulikia uhalifu mkubwa.
Niang pia amekataa tuhuma kwamba ICC inaingilia mamlaka ya nchi, akisisitiza kuwa waathiriwa wa ukatili barani Afrika bado wanahitaji haki.
“Bado kuna watu wanaoteseka, kuna waathiriwa wengi. Na kama hatuwezi kuwarudishia kila kitu walichopoteza, basi angalau tunapaswa kuwapatia haki kwa kiasi fulani'', anasema Mame Mandiaye.
Kuhusu baadhi ya nchi za Afrika, zikiwemo wanachama wa Muungano wa Nchi za Sahel, AES, kutangaza kujiondoa ICC, Niang amesema ni jambo la kusikitisha kuona kutokuelewana kuhusu jukumu la mahakama hiyo.
Amesema licha ya vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya baadhi ya maafisa wa ICC, mahakama hiyo haitarudi nyuma katika kutekeleza majukumu yake.
“Ni vikwazo tunavyovijutia, lakini havitatufanya turudi nyuma,” amesema Niang.
Soma Zaidi:























