Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Milipuko yaripotiwa karibu na miji ya bandari, huku Iran ikishambulia meli za mafuta za UAE
Rais wa Marekani Donald Trump amesemaingawa mashambulizi yanaendelea kuna uwezekano wa kuafikia makubaliano na Iran.
Muhtasari
- EU yapiga marufuku uingizaji wa dhahabu kutoka Sudan
- Trump: Mojtaba Khamenei amekufa kwa asilimia 90
- Shambulio la Iran dhidi ya meli za mafuta ni ishara kwamba bado ina uwezo
- Milipuko yasikika katika maeneo kadhaa - Vyombo vya habari vya serikali ya Iran
- Rubio azindua kampeni ya kupinga Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC
- Trump asema makubaliano na Iran bado yanawezekana
- El Niño kali yatishia kuleta mafuriko makubwa Afrika Mashariki na Asia
- Kiongozi wa RSF Hamdan Dagalo ahukumiwa kifo bila kuwepo mahakamani
- Mwanamke atuhumiwa kumuua mumewe kwa dawa ya kusafishia choo
- Iran yajibu pendekezo la Trump la ushuru wa Hormuz
- UN yapinga mpango wa Trump wa kutoza ada meli zinazopita Hormuz
- Marekani yatangaza kurejesha kizuizi cha majini dhidi ya Iran katika Mlango wa Hormuz
- UAE yashutumu Iran kwa shambulio la meli za mafuta huku Marekani ikiendeleza mashambulizi
- Trump ataka mataifa ya Ghuba yalipie ulinzi wa Marekani dhidi ya Iran
Moja kwa moja
Na Mariam Mjahid & Ambia Hirsi
Netanyahu: Shambulio lolote la Iran dhidi ya Israel litajibiwa 'vikali zaidi'
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anasema nchi yake italipiza kisasi kwa "nguvu zaidi" endapo iltashambuliwa na Iran.
"Nawaambia viongozi wa Iran: Msitegemee tutasalia kimya mkitushambulia," alisema kwenye video iliyochapishwa kwenye mtandao wake wa kijamii.
Ameonya kuwa jibu la Israel halitakuwa sawa na wakati wa mwisho iliposhambuliwa na Iran, ingawa inasadikiwa ilikuwa "kali" kutokana na kiwango cha uharibifu na maafa yaliyoshuhudiwa.
"Siku za kupigwa na kusalia kimya zimepita, tutalipiza kisasi mara mbili," aliongeza kusema.
Huku hayo yakijiri watu saba wameuawa akiwemo afisa mkuu katika shambulio la anga la Israel dhidi ya kituo cha polisi kinachomilikiwa na Hamas huko Gaza kwa mijibu wa maafisa wa afya na polisi.
Walioshuhudia shambulio hilo waliiambia BBC kwamba ndege isiyo na rubani ya Israel ilirusha makombora manne kwenye kituo hicho karibu na soko lenye shughuli nyingi katika eneo la Jabalia kaskazini mwa Gaza.
Wizara ya mambo ya ndani ya eneo la Palestina inayoongozwa na Hamas ilisema mkuu wa kituo cha polisi cha eneo hilo, Kanali Mohammed Marwan Salem, na maafisa wengine kadhaa ni miongoni mwa waliouawa katika kile ilichokitaja kuwa "mauaji".
Pia unaweza kusoma:
Iran yailaani Uingereza kwa kuipiga marufuku IRGC
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeikosoa vikali serikali ya Uingereza kwa kuiorodhesha Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, kama mashirika yaliyopigwa marufuku.
Taarifa hiyo ilisema: "Ofisi ya Mambo ya Nje inalaani kitendo cha uadui cha serikali ya Uingereza ya kuikitaja IRGC kama tishio chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa ya nchi hiyo na inaiona kama kitendo kisicho cha haki, kinachokiuka kanuni za sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na kanuni uhuru wa mataifa na kanuni ya kutoingilia mambo ya ndani ya nchi."
Taarifa hiyo imelitaja Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi kama "sehemu muhimu ya jeshi rasmi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran" na imesema "kuitaja taasisi ya usalama kuwa taasisi rasmi ya nchi huru kuwa ni kitendo cha kipuuzi na cha uchochezi ambacho kinakiuka sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa."
Taarifa hiyo ilisisitiza haki ya serikali ya Uingereza "kuchukua hatua za kukabiliana na makosa" na kuweka jukumu la hili kwenye "baraza" lake linaloongoza.
Wakati huo huo, Ismail Kowsari, mjumbe wa Tume ya Usalama wa Kitaifa na Sera ya Kigeni ya Bunge, leo ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje "kumwita balozi wa Uingereza ili kumwajibisha."
Soma pia:
Mashirika ya ndege ya Ulaya yaonywa dhidi ya safari katika mataifa ya Ghuba
Shirika la Usalama wa Anga la Umoja wa Ulaya (EASA) linaonya mashirika ya ndege dhidi ya kusafiri kwenye anga ya Bahrain, Kuwait, Qatar, UAE, na juu ya maji ya Ghuba ya Oman.
Linasema "matukio ya kijeshi yasiyotabirika, pamoja na uwezekano wa matumizi ya makombora, ndege zisizo na rubani, ndege za kivita na mifumo ya ulinzi wa anga" ndani ya eneo hilo ni "hatari" kwa safari za ndege.
EASA inasema ushauri huu utaendelea kudumishwa hadi tarehe 29 Julai, ikiongeza kuwa itafuatilia hali hiyo kwa karibu.
EU yapiga marufuku uingizaji wa dhahabu kutoka Sudan
Umoja wa Ulaya (EU) umepiga marufuku ununuzi, uagizaji na usafirishaji wa dhahabu kutoka Sudan, ukisema biashara hiyo imekuwa chanzo muhimu cha ufadhili wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo vilivyozuka Aprili 2023.
Mvutano kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa Rapid Response Forces (RSF) umesababisha moja ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani, na kulazimisha zaidi ya watu milioni 14 kukimbia makwao.
Sudan ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika na akiba yake kubwa imekuwa chanzo muhimu cha mapato kwa pande zote mbili, kulingana na makundi ya haki za binadamu.
Mawaziri wa mambo ya nje wa EU waliidhinisha hatua hizo pamoja na marufuku ya mauzo ya nje ya zebaki na sianidi kwenda Sudan, kemikali zinazotumika sana katika uchimbaji wa dhahabu.
Kulingana na wataalamu wa Umoja wa Mataifa na wachambuzi wengine, zaidi ya nusu - na kwa makadirio mengine hadi 70% - ya dhahabu ya Sudan husafirishwa nje ya nchi kwa njia ya magendo kila mwaka.
RSF inadhibiti maeneo mengi ya dhahabu huko Darfur na Kordofan - katika maeneo ya magharibi na katikati ya nchi, huku jeshi la Sudan likisimamia uzalishaji katika maeneo ya kaskazini na mashariki.
Dhahabu hiyo mara nyingi husafirishwa kupitia nchi jirani, ikiwa ni pamoja na Misri, Chad na Libya, kabla ya kufika Dubai katika Falme za Kiarabu (UAE), kitovu kikuu cha kimataifa cha kusafisha na kufanya biashara ya dhahabu.
Soma Zaidi:
Trump: Mojtaba Khamenei amekufa kwa asilimia 90
Rais wa Marekani Donald Trump ameiambia kituo cha habari cha Fox News kwamba: "Khamenei amekufa, na mwanawe amekufa kwa asilimia 90."
Tangu kuanza kwa vita, hakuna picha, sauti, wala video ya Mojtaba Khamenei iliyochapishwa, na hajaonekana hadharani.
Siku mbili zilizopita, picha mpya ilichapishwa kwenye tovuti ya Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu, lakini hakukuwa na dalili yoyote inayoonyesha kuwa ilipigwa hivi karibuni.
Katika mahojiano na Fox News Rais Trump alisisitiza tena kuwa jeshi la majini, jeshi la anga, na vikosi vya ulinzi vya Iran vimelemazwa na viongozi wake wameuawa.
Rais huyo wa Marekani pia alisema kuwa "makubaliano yalifikiwa kuhusu kila kitu" jana baada ya "mkutano wa saa 11," akirejelea suala la Iran.
Hakutaja maelezo ya mkutano huo. Aliongeza: "Kazi yao huwa inachukua saa 11 wakati inapaswa kuchukua dakika moja tu... lakini walipotoka chumbani, walipiga simu tena na kusema kuwa kuna mabadiliko yaliyohitajika kufanywa."
Donald Trump aliongeza: "Siku zote huwa kuna mabadiliko. Unajua, wao ni wataalamu wa mazungumzo, hiyo ndio kazi yao. Sisemi kwamba wanaimudu vyema kazi hiyo... Hawakupata chochote kutoka kwangu."
Bw. Trump alisema siku chache zilizopita kuwa Iran imekubali kila kitu, lakini saa chache baadaye walishambulia meli ya kibiashara katika Mlango-bahari wa Hormuz.
Anaituhumu Iran kwa kucheza michezo ya hila dhidi ya marais wa Marekani, akiwemo Bill Clinton, George Bush na Barack Obama, katika kipindi cha miaka 47 iliyopita, huku akimtaja Bw. Obama kuwa "mbaya zaidi kuliko wote."
Soma zaidi:
Shambulio la Iran dhidi ya meli za mafuta ni ishara kwamba bado ina uwezo
Mbinu ya Iran ya kushambulia tena meli , ikiwa ni pamoja na meli za mafuta, inachangia lengo lake kubwa la kimkakati la kutaka kudumisha udhibiti wa Mlango-Bahari wa Hormuz.
Mashambulizi haya yanaonyesha uwezo wa Tehran, licha ya mashambulizi makubwa ya mabomu ya Marekani na Israel dhidi yake mapema mwaka huu.
Hilo linaashiria mambo mawili. Juhudi kubwa za mabomu hazikufanikiwa kuharibu silaha hizo za Iran kama ilivyotarajiwa, au Iran kwa namna fulani sasa inaweza kuimarisha hifadhi yake kutoka kwingineko. Hatujui.
Tunachojua ni kwamba kuna malengo zaidi yanayojitokeza kwa Marekani kuendelea kushambulia - kutoka angani na, cha kufurahisha zaidi, kutoka baharini.
Matumizi ya Marekani ya magari ya uso yasiyo na wafanyakazi ya njia moja kushambulia Kituo cha Wanamaji cha Bandar Abbas yanatukumbusha matumizi ya teknolojia kama hiyo na Ukraine katika vita vyake na Urusi, mgogoro ambao kwa kiasi kikubwa umebadilisha jinsi vita vinavyopiganwa.
Lakini, tukiangalia mashariki zaidi, ni sheria ya matokeo yasiyotarajiwa ambayo imeonyesha tena jinsi kudumisha ushawishi juu ya Mlango-Bahari wa Hormuz kumethibitika kuwa silaha yenye ufanisi zaidi ya Iran.
Milipuko yasikika katika maeneo kadhaa - Vyombo vya habari vya serikali ya Iran
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran, milipuko kadhaa imesikika karibu na mji wa bandari wa Bandar Abbas.
Shirika la habari la serikali, IRNA, pia limesema kuwa maeneo manne katika mji wa Bushehr yalishambuliwa kwa makombora, huku shirika la habari la Fars likiripoti kuwa wakazi wamesema wamesikia milipuko kadhaa.
Tumewasiliana na Kamandi Kuu ya Marekani (US Central Command) ili kupata maoni yao kuhusu suala hili.
Habari za hivi punde, Watatu wauawa katika mashambulizi ya Marekani nchini Iran - vyombo vya habari vya serikali
Watu watatu wameuawa katika mashambulizi ya Marekani ya usiku kucha nchini Iran, kulingana na vyombo vya habari vya serikali vya Iran.
Shambulio hilo lilitokea katika jimbo la Hormozgan, shirika la habari la Fars linasema, ambalo liko kusini mwa nchi.
Shirika la habari la serikali la IRIB limeandika katika chapisha kwenye mtandao wa Telegram, kuwa familia ya mwanamazingira mmoja ndio iliyoathiriwa vibaya na shambulio hilo.
Rubio azindua kampeni ya kupinga Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema serikali ya Marekani imeanzisha kampeni ya kupinga Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), akidai kuwa mahakama hiyo inatishia mamlaka ya nchi yake kwa kuwaruhusu wanajeshi na maafisa wa Marekani kufunguliwa mashtaka.
Kwa mujibu wa Rubio, Washington itazishawishi nchi washirika wake kukataa mamlaka ya ICC.
Pia amesema mataifa yatakayoendelea kuiunga mkono mahakama hiyo yanaweza kukabiliwa na hatua mbalimbali kutoka Marekani, zikiwemo vikwazo, masharti ya utoaji visa na marufuku za kusafiri.
Marekani kwa muda mrefu imekuwa ikipinga mamlaka ya ICC dhidi ya raia wake, ikisema haifungwi na Mkataba wa Roma ulioanzisha mahakama hiyo kwa kuwa si mwanachama wake.
Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wa sheria wamekosoa kauli za Rubio, wakisema ICC hailengi Marekani pekee na kwamba juhudi za kuidhoofisha zinaweza kuathiri uwajibikaji wa kimataifa kwa watuhumiwa wa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilianzishwa mwaka 2002 kwa lengo la kuwafikisha mbele ya sheria watu wanaotuhumiwa kwa makosa makubwa ya kimataifa pale ambapo mahakama za kitaifa haziwezi au haziko tayari kufanya hivyo.
Pia Soma:
Trump asema makubaliano na Iran bado yanawezekana
Rais wa Marekani Donald Trump amesema bado anaamini kuna uwezekano wa kufikiwa makubaliano kati ya Marekani na Iran, licha ya kuendelea kwa mashambulizi ya kijeshi na kurejeshwa kwa kizuizi cha majini dhidi ya Tehran.
"Ndiyo, naamini makubaliano bado yanawezekana," alisema Trump alipoulizwa ikiwa bado anaona nafasi ya mazungumzo.
Hata hivyo, Trump alisema Marekani itaendelea kuishambulia Iran huku ikiongeza shinikizo kwa kurejesha kizuizi cha majini kinacholenga biashara ya Iran.
"Tunawashambulia kwa nguvu kubwa na tutaendelea kufanya hivyo. Tunaharibu uwezo wao wote wa kushambulia," alisema.
Rais huyo alisema kizuizi hicho kinaihusu Iran pekee, akisisitiza kuwa meli zinazofanya biashara na Iran hazitaruhusiwa kupita, huku meli nyingine zikiendelea kutumia njia za baharini.
"Yeyote anayefanya biashara na Iran hataweza kupita, lakini wengine wataweza," alisema.
Trump aliongeza kuwa anaamini kizuizi hicho kinaweza kuwa na athari kubwa hata kuliko mashambulizi ya kijeshi, lakini akasema hatua hizo mbili zikichanganywa ndizo zitakazoongeza shinikizo dhidi ya Iran.
El Niño kali yatishia kuleta mafuriko makubwa Afrika Mashariki na Asia
Hali ya hewa ya El Niño inayoongezeka kwa kasi inatishia kusababisha mafuriko makubwa, kuenea kwa magonjwa na ukame katika baadhi ya jamii zilizo hatarini zaidi duniani, hususan Afrika Mashariki na Asia, shirika la misaada ya kibinadamu limeonya.
Jumatatu, Shirika la Kimataifa la Uokoaji (International Rescue Committee, IRC) lilisema Kenya, Uganda, Somalia, Bangladesh, Pakistan na Afghanistan ni miongoni mwa nchi zilizo katika hatari kubwa zaidi. Baadhi ya mataifa hayo tayari yanakabiliwa na migogoro ya kibinadamu inayoendelea.
"Tunashuhudia majanga kadhaa yakitokea kwa wakati mmoja, na maeneo yenye uwezo mdogo wa kukabiliana na mshtuko mwingine ndiyo yanayokabiliwa na hatari kubwa zaidi," alisema Bob Kitchen, afisa mwandamizi anayeshughulikia masuala ya dharura katika IRC.
Kituo cha Marekani cha Utabiri wa Hali ya Hewa (US Climate Prediction Center) kilisema Julai 9 kuwa El Niño inaongezeka kwa kasi, ikiwa na uwezekano wa asilimia 81 kuwa miongoni mwa matukio makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1950.
Kituo hicho kiliongeza kuwa El Niño inatarajiwa kufikia kilele chake kati ya miezi ya Oktoba na Desemba.
Maelezo zaidi:
Kiongozi wa RSF Hamdan Dagalo ahukumiwa kifo bila kuwepo mahakamani
Mahakama nchini Sudan imemhukumu adhabu ya kifo kiongozi wa wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), Mohamed Hamdan Dagalo, kwa makosa ya uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari yanayohusishwa na machafuko katika eneo la Darfur Magharibi.
Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti, alihukumiwa bila kuwepo mahakamani pamoja na maafisa wengine 15 wa RSF, ambao pia walihukumiwa adhabu hiyo.
Kesi hiyo ilisikilizwa katika mji wa Port Sudan, unaodhibitiwa na jeshi la Sudan.
RSF haijatoa tamko kuhusu hukumu hiyo. Hata hivyo, kundi hilo limekuwa likikanusha mara kwa mara tuhuma za uhalifu wa kivita.
Kesi hiyo ilijikita katika madai ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika mji wa El Geneina, ikiwemo mauaji ya aliyekuwa gavana wa Darfur Magharibi, Khamis Abbakar, mwezi Juni 2023.
Mahakama pia iliwapata washtakiwa hao na hatia ya kuharibu na kupora mali pamoja na kushambulia raia, shule, maeneo ya ibada na makazi.
Soma Zaidi:
Mwanamke atuhumiwa kumuua mumewe kwa dawa ya kusafishia choo
Mwanamke mmoja nchini India amekamatwa kwa tuhuma za kumuua mumewe kwa kushirikiana na wanaume wengine wawili, katika tukio ambalo polisi wanasema lilihusisha kumpa dawa za kumlewesha, kumtupa kutoka kwenye roshani na kumdunga dawa ya kusafishia choo.
Onyo: Habari hii ina maelezo ambayo yanaweza kuwasumbua baadhi ya wasomaji.
Inspekta Suresh Kumar wa wilaya ya Nazimabad katika jimbo la Telangana alisema watuhumiwa walidaiwa kutekeleza mpango huo baada ya kuamini kuwa mume huyo, aliyekuwa amerejea hivi karibuni kutoka Saudi Arabia, angezuia uhusiano wa mwanamke huyo na mpenzi wake.
"Tulimkamata mwanamke mmoja pamoja na wanaume wawili kwa tuhuma za kumpa dawa za kulevya mume wa mwanamke huyo, kumtupa kutoka kwenye roshani na kumdunga dawa ya kusafishia choo ili kumuua," alisema Inspekta Suresh Kumar.
Polisi wanasema watuhumiwa walijaribu kumuua mwanaume huyo mara mbili ndani ya kipindi cha saa 24 kabla ya kufariki dunia tarehe 30 Juni.
Kwa mujibu wa polisi na familia ya marehemu, Dayani Prashant mwenye umri wa miaka 36 alifunga ndoa ya kupangwa na Scindia miaka 12 iliyopita. Wawili hao walikuwa na watoto wawili, wa miaka tisa na saba.
Kabla ya ndoa, Scindia alikuwa amepata mafunzo ya uuguzi na alikuwa akifanya kazi kama muuguzi katika hospitali binafsi mjini Nazimabad.
Polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku watuhumiwa wakikabiliwa na tuhuma za mauaji.
Iran yajibu pendekezo la Trump la ushuru wa Hormuz
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amejibu pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la kutoza ushuru wa asilimia 20 kwa meli za kibiashara zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, akisema kiwango hicho ni kikubwa mno huku akisisitiza kuwa Iran imekuwa mlinzi wa njia hiyo muhimu ya baharini.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Araghchi alionekana kujibu kwa kejeli pendekezo la Trump.
“Rais wa Marekani yuko sahihi kabisa. Yeyote anayehakikisha meli za kibiashara zinapita kwa usalama katika Mlango wa Bahari wa Hormuz anapaswa kulipwa kwa huduma hiyo'', aliandika kwa ukurasa wake.
Vile vile akaendelea kusisitiza msimamo wa Iran kuhusu njia hiyo ya kimkakati kwa kusema, “Iran imekuwa mlinzi wa Mlango wa Hormuz siku zote na itaendelea kuwa hivyo milele.”
Akirejelea moja kwa moja pendekezo la Trump, Araghchi aliongeza, “Asilimia 20 bila shaka ni kubwa mno. Tutatoza ada za bei nafuu.”
Kauli hiyo imekuja baada ya ripoti kwamba Rais Trump alipendekeza kutozwa ushuru wa asilimia 20 kwa meli za mizigo zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambao ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa bidhaa duniani.
Mlango huo hupitisha sehemu kubwa ya mafuta ghafi na gesi asilia inayosafirishwa duniani, hivyo ukiwa na umuhimu mkubwa kwa biashara na usalama wa nishati duniani.
Kauli za Araghchi zinaweza kuongeza mvutano kati ya Tehran na Washington kuhusu usalama na udhibiti wa njia hiyo muhimu ya baharini.
Hadi sasa, Marekani haijatoa tamko rasmi kujibu kauli za Araghchi, lakini mabadilishano hayo yanaonyesha kuendelea kwa mvutano kati ya mataifa hayo mawili kuhusu Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Soma Zaidi:
UN yapinga mpango wa Trump wa kutoza ada meli zinazopita Hormuz
Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO), ambalo ni wakala wa Umoja wa Mataifa, limesema linapinga utozwaji wa ada kwa meli zinazopita katika njia za kimataifa za baharini, likijibu tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Trump alikuwa ametangaza kuwa Marekani itarejesha kizuizi cha majini dhidi ya Iran na kutoza ushuru wa asilimia 20 kwa shehena zote zitakazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Akijibu tangazo hilo, msemaji wa IMO alisema shirika hilo linafahamu taarifa hiyo na linasubiri maelezo zaidi.
"Msimamo wetu kuhusu ada za kupita umekuwa wazi siku zote. Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini linapinga vikali kutozwa ada kwa meli zinazopita katika milango ya bahari inayotumika kwa usafiri wa kimataifa. Hakuna msingi wa kisheria wa kuweka ada za lazima kwa meli kwa sababu tu zinapita katika mlango huo wa bahari," alisema.
Tamko hilo linakuja wakati mvutano kati ya Marekani na Iran kuhusu udhibiti wa Mlango wa Bahari wa Hormuz ukiendelea kuongezeka, huku njia hiyo ikiendelea kuwa muhimu kwa usafirishaji wa mafuta na bidhaa duniani.
Soma Zaidi:
Marekani yatangaza kurejesha kizuizi cha majini dhidi ya Iran katika Mlango wa Hormuz
Jeshi la Marekani kupitia Kamandi Kuu ya Marekani, CENTCOM, limesema litarejesha kizuizi cha majini dhidi ya Iran kuanzia Jumanne, Julai 14, kikilenga meli zinazoelekea bandari na maeneo ya pwani ya Iran.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, CENTCOM imesema hatua hiyo itaanza kutekelezwa saa 4:00 mchana kwa saa za Mashariki mwa Marekani.
Jeshi hilo limesema litaendelea kuruhusu usafiri wa meli katika maji ya eneo hilo kwa meli ambazo hazitakiuka masharti ya kizuizi hicho.
Rais Donald Trump alikuwa ametangaza awali kwamba Marekani ingerudisha mara moja kizuizi dhidi ya bandari za Iran.
Aidha, Trump ametangaza kuwa Marekani itaweka tozo ya asilimia 20 kwa meli zitakazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz kama sehemu ya hatua mpya za kuzuia usafiri wa majini katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa CENTCOM, hatua hiyo inafuatia kipindi cha awali cha utekelezaji wa kizuizi hicho kilichodumu kuanzia Aprili 13 hadi Juni 18.
Kwa upande wake, Iran imesema imeufunga Mlango wa Bahari wa Hormuz hadi itakapotangaza vinginevyo, kufuatia mapigano ya siku za karibuni.
Msemaji wa Makao Makuu ya Khatam al Anbiya amesema Iran haitaruhusu Marekani kuingilia usimamizi wa Mlango wa Hormuz kwa hali yoyote.
Unaweza kusoma;
UAE yashutumu Iran kwa shambulio la meli za mafuta huku Marekani ikiendeleza mashambulizi
Falme za Kiarabu (UAE) zimeishutumu Iran kwa kile ilichokiita shambulio la "kijasiri" dhidi ya meli mbili za mafuta katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, lililosababisha kifo cha mfanyakazi mmoja raia wa India na kujeruhi wengine wanane.
Wizara ya Ulinzi ya UAE imesema raia sita wa India na wawili wa Ukraine walijeruhiwa, huku majeruhi wanne wakiwa katika hali mbaya.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, wizara hiyo imesema shambulio hilo ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na linahatarisha usalama na utulivu wa eneo hilo.
Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump alisema Marekani imeanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran kwa usiku wa tatu mfululizo.
"Tunaishambulia Iran kwa nguvu kubwa," alisema Trump.
Pia alitangaza kuwa Marekani itaweka tozo ya asilimia 20 kwa meli zitakazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz kama sehemu ya hatua mpya za kuzuia usafiri wa majini katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema Tehran itaendelea kuwa "mlinzi" wa Mlango wa Bahari wa Hormuz, akijibu tangazo la Marekani kuhusu hatua hizo.
Baadaye, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) lilidai kuhusika na shambulio hilo, likisema meli hizo zilipuuzia maonyo, zilizima mifumo yao na kujaribu kupita katika njia iliyokuwa imewekewa mabomu ya baharini.
IRGC ilisema hatua hiyo ilikuwa onyo kwamba ushirikiano na "adui mvamizi" utasababisha madhara zaidi na unaweza kuchelewesha kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz, pamoja na kuchochea mgogoro wa nishati duniani.
Mvutano kuhusu udhibiti wa Mlango wa Bahari wa Hormuz unaendelea kuongezeka huku Marekani na Iran zikiendelea kubadilishana mashambulizi na vitisho katika eneo hilo.
Unaweza kusoma;
Trump ataka mataifa ya Ghuba yalipie ulinzi wa Marekani dhidi ya Iran
Rais wa Marekani Donald Trump amesema mataifa ya Ghuba ya Uajemi yanapaswa kulipia ulinzi ambao Marekani inayatoa dhidi ya vitisho kutoka Iran.
"Ndani ya mwezi mmoja tangu siku tulipowashambulia, wangekuwa na silaha ya nyuklia kama tusingefanya hivyo. Kama wangekuwa na silaha ya nyuklia, Israel huenda isingekuwapo tena, na pengine hata Mashariki ya Kati isingekuwa salama."
Akizungumza na waandishi wa habari, Trump amesema Marekani imekuwa ikitumia fedha nyingi kulinda eneo hilo na kwamba ni wakati wa washirika wake kubeba sehemu ya gharama hizo.
"Nataka tulipwe kwa sababu tunalinda sehemu tajiri sana ya dunia. Tunatumia fedha nyingi, hivyo nchi tunazozilinda zinapaswa kutulipa kwa ulinzi huo."
Trump ametaja Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Qatar, Bahrain na Kuwait kuwa miongoni mwa mataifa yanayonufaika na ulinzi wa Marekani katika eneo la Ghuba.
Trump pia amedai kuwa Iran ilirusha makombora kuelekea mataifa hayo matano, akisema hatua hiyo inaonesha kuwa viongozi wa Tehran ni "hatari" na kwamba Marekani haitakubali hali hiyo iendelee.
Aidha amesema Marekani itafanya "shambulio jingine kubwa" dhidi ya Iran usiku huo, huku akidai kuwa Tehran sasa inataka kufikia makubaliano baada ya miaka mingi ya mazungumzo.
"Tutafanya shambulio jingine kubwa usiku wa leo. Wanataka kufanya makubaliano... Tumekuwa tukifanya mazungumzo kwa miaka 47, lakini hakuna aliyewahi kuwashambulia kijeshi. Sisi tunawashambulia kwa nguvu sana."
Kauli hiyo imekuja huku mvutano kati ya Marekani na Iran ukiendelea kuongezeka, baada ya mashambulizi ya kijeshi ya pande zote na vitisho vinavyoendelea kuhusu usalama wa usafiri wa majini katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.
Trump pia amedai kuwa Iran ilikaribia kupata silaha ya nyuklia kabla ya mashambulizi ya Marekani, akisema Washington itaendelea kuchukua hatua za kijeshi ikiwa itahitajika.
Iran haijajibu mara moja kauli za Trump. Tehran imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani na imekuwa ikipinga mashambulizi ya Marekani dhidi ya miundombinu yake.
Soma Zaidi:
Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.