Moja kwa moja, Trump ataka mataifa ya Ghuba yalipie ulinzi wa Marekani dhidi ya Iran

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Iran ingekuwa tayari imepata silaha ya nyuklia ndani ya mwezi mmoja kama Marekani isingefanya mashambulizi dhidi ya miundombinu yake ya nyuklia.

Skip Video and continue reading
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote
  • xx
  • Lydia Wanjiku

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Trump asema makubaliano na Iran bado yanawezekana

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema bado anaamini kuna uwezekano wa kufikiwa makubaliano kati ya Marekani na Iran, licha ya kuendelea kwa mashambulizi ya kijeshi na kurejeshwa kwa kizuizi cha majini dhidi ya Tehran.

    "Ndiyo, naamini makubaliano bado yanawezekana," alisema Trump alipoulizwa ikiwa bado anaona nafasi ya mazungumzo.

    Hata hivyo, Trump alisema Marekani itaendelea kuishambulia Iran huku ikiongeza shinikizo kwa kurejesha kizuizi cha majini kinacholenga biashara ya Iran.

    "Tunawashambulia kwa nguvu kubwa na tutaendelea kufanya hivyo. Tunaharibu uwezo wao wote wa kushambulia," alisema.

    Rais huyo alisema kizuizi hicho kinaihusu Iran pekee, akisisitiza kuwa meli zinazofanya biashara na Iran hazitaruhusiwa kupita, huku meli nyingine zikiendelea kutumia njia za baharini.

    "Yeyote anayefanya biashara na Iran hataweza kupita, lakini wengine wataweza," alisema.

    Trump aliongeza kuwa anaamini kizuizi hicho kinaweza kuwa na athari kubwa hata kuliko mashambulizi ya kijeshi, lakini akasema hatua hizo mbili zikichanganywa ndizo zitakazoongeza shinikizo dhidi ya Iran.

  2. El Niño kali yatishia kuleta mafuriko makubwa Afrika Mashariki na Asia

    d

    Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    Hali ya hewa ya El Niño inayoongezeka kwa kasi inatishia kusababisha mafuriko makubwa, kuenea kwa magonjwa na ukame katika baadhi ya jamii zilizo hatarini zaidi duniani, hususan Afrika Mashariki na Asia, shirika la misaada ya kibinadamu limeonya.

    Jumatatu, Shirika la Kimataifa la Uokoaji (International Rescue Committee, IRC) lilisema Kenya, Uganda, Somalia, Bangladesh, Pakistan na Afghanistan ni miongoni mwa nchi zilizo katika hatari kubwa zaidi. Baadhi ya mataifa hayo tayari yanakabiliwa na migogoro ya kibinadamu inayoendelea.

    "Tunashuhudia majanga kadhaa yakitokea kwa wakati mmoja, na maeneo yenye uwezo mdogo wa kukabiliana na mshtuko mwingine ndiyo yanayokabiliwa na hatari kubwa zaidi," alisema Bob Kitchen, afisa mwandamizi anayeshughulikia masuala ya dharura katika IRC.

    Kituo cha Marekani cha Utabiri wa Hali ya Hewa (US Climate Prediction Center) kilisema Julai 9 kuwa El Niño inaongezeka kwa kasi, ikiwa na uwezekano wa asilimia 81 kuwa miongoni mwa matukio makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1950.

    Kituo hicho kiliongeza kuwa El Niño inatarajiwa kufikia kilele chake kati ya miezi ya Oktoba na Desemba.

  3. Kiongozi wa RSF Hamdan Dagalo ahukumiwa kifo bila kuwepo mahakamani

    h

    Chanzo cha picha, Anadolu Agency via Getty Images

    Mahakama nchini Sudan imemhukumu adhabu ya kifo kiongozi wa wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), Mohamed Hamdan Dagalo, kwa makosa ya uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari yanayohusishwa na machafuko katika eneo la Darfur Magharibi.

    Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti, alihukumiwa bila kuwepo mahakamani pamoja na maafisa wengine 15 wa RSF, ambao pia walihukumiwa adhabu hiyo.

    Kesi hiyo ilisikilizwa katika mji wa Port Sudan, unaodhibitiwa na jeshi la Sudan.

    RSF haijatoa tamko kuhusu hukumu hiyo. Hata hivyo, kundi hilo limekuwa likikanusha mara kwa mara tuhuma za uhalifu wa kivita.

    Kesi hiyo ilijikita katika madai ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika mji wa El Geneina, ikiwemo mauaji ya aliyekuwa gavana wa Darfur Magharibi, Khamis Abbakar, mwezi Juni 2023.

    Mahakama pia iliwapata washtakiwa hao na hatia ya kuharibu na kupora mali pamoja na kushambulia raia, shule, maeneo ya ibada na makazi.

    Soma Zaidi:

  4. Mwanamke atuhumiwa kumuua mumewe kwa dawa ya kusafishia choo

    g

    Chanzo cha picha, GETT

    Mwanamke mmoja nchini India amekamatwa kwa tuhuma za kumuua mumewe kwa kushirikiana na wanaume wengine wawili, katika tukio ambalo polisi wanasema lilihusisha kumpa dawa za kumlewesha, kumtupa kutoka kwenye roshani na kumdunga dawa ya kusafishia choo.

    Onyo: Habari hii ina maelezo ambayo yanaweza kuwasumbua baadhi ya wasomaji.

    Inspekta Suresh Kumar wa wilaya ya Nazimabad katika jimbo la Telangana alisema watuhumiwa walidaiwa kutekeleza mpango huo baada ya kuamini kuwa mume huyo, aliyekuwa amerejea hivi karibuni kutoka Saudi Arabia, angezuia uhusiano wa mwanamke huyo na mpenzi wake.

    "Tulimkamata mwanamke mmoja pamoja na wanaume wawili kwa tuhuma za kumpa dawa za kulevya mume wa mwanamke huyo, kumtupa kutoka kwenye roshani na kumdunga dawa ya kusafishia choo ili kumuua," alisema Inspekta Suresh Kumar.

    Polisi wanasema watuhumiwa walijaribu kumuua mwanaume huyo mara mbili ndani ya kipindi cha saa 24 kabla ya kufariki dunia tarehe 30 Juni.

    Kwa mujibu wa polisi na familia ya marehemu, Dayani Prashant mwenye umri wa miaka 36 alifunga ndoa ya kupangwa na Scindia miaka 12 iliyopita. Wawili hao walikuwa na watoto wawili, wa miaka tisa na saba.

    Kabla ya ndoa, Scindia alikuwa amepata mafunzo ya uuguzi na alikuwa akifanya kazi kama muuguzi katika hospitali binafsi mjini Nazimabad.

    Polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku watuhumiwa wakikabiliwa na tuhuma za mauaji.

  5. Iran yajibu pendekezo la Trump la ushuru wa Hormuz

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amejibu pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la kutoza ushuru wa asilimia 20 kwa meli za kibiashara zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, akisema kiwango hicho ni kikubwa mno huku akisisitiza kuwa Iran imekuwa mlinzi wa njia hiyo muhimu ya baharini.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Araghchi alionekana kujibu kwa kejeli pendekezo la Trump.

    “Rais wa Marekani yuko sahihi kabisa. Yeyote anayehakikisha meli za kibiashara zinapita kwa usalama katika Mlango wa Bahari wa Hormuz anapaswa kulipwa kwa huduma hiyo'', aliandika kwa ukurasa wake.

    Vile vile akaendelea kusisitiza msimamo wa Iran kuhusu njia hiyo ya kimkakati kwa kusema, “Iran imekuwa mlinzi wa Mlango wa Hormuz siku zote na itaendelea kuwa hivyo milele.”

    Akirejelea moja kwa moja pendekezo la Trump, Araghchi aliongeza, “Asilimia 20 bila shaka ni kubwa mno. Tutatoza ada za bei nafuu.”

    Kauli hiyo imekuja baada ya ripoti kwamba Rais Trump alipendekeza kutozwa ushuru wa asilimia 20 kwa meli za mizigo zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambao ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa bidhaa duniani.

    Mlango huo hupitisha sehemu kubwa ya mafuta ghafi na gesi asilia inayosafirishwa duniani, hivyo ukiwa na umuhimu mkubwa kwa biashara na usalama wa nishati duniani.

    Kauli za Araghchi zinaweza kuongeza mvutano kati ya Tehran na Washington kuhusu usalama na udhibiti wa njia hiyo muhimu ya baharini.

    Hadi sasa, Marekani haijatoa tamko rasmi kujibu kauli za Araghchi, lakini mabadilishano hayo yanaonyesha kuendelea kwa mvutano kati ya mataifa hayo mawili kuhusu Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Soma Zaidi:

  6. UN yapinga mpango wa Trump wa kutoza ada meli zinazopita Hormuz

    G

    Chanzo cha picha, Reuters

    Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini (IMO), ambalo ni wakala wa Umoja wa Mataifa, limesema linapinga utozwaji wa ada kwa meli zinazopita katika njia za kimataifa za baharini, likijibu tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Trump alikuwa ametangaza kuwa Marekani itarejesha kizuizi cha majini dhidi ya Iran na kutoza ushuru wa asilimia 20 kwa shehena zote zitakazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Akijibu tangazo hilo, msemaji wa IMO alisema shirika hilo linafahamu taarifa hiyo na linasubiri maelezo zaidi.

    "Msimamo wetu kuhusu ada za kupita umekuwa wazi siku zote. Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini linapinga vikali kutozwa ada kwa meli zinazopita katika milango ya bahari inayotumika kwa usafiri wa kimataifa. Hakuna msingi wa kisheria wa kuweka ada za lazima kwa meli kwa sababu tu zinapita katika mlango huo wa bahari," alisema.

    Tamko hilo linakuja wakati mvutano kati ya Marekani na Iran kuhusu udhibiti wa Mlango wa Bahari wa Hormuz ukiendelea kuongezeka, huku njia hiyo ikiendelea kuwa muhimu kwa usafirishaji wa mafuta na bidhaa duniani.

    Soma Zaidi:

  7. Marekani yatangaza kurejesha kizuizi cha majini dhidi ya Iran katika Mlango wa Hormuz

    g

    Chanzo cha picha, US Central Command via Getty Images

    Jeshi la Marekani kupitia Kamandi Kuu ya Marekani, CENTCOM, limesema litarejesha kizuizi cha majini dhidi ya Iran kuanzia Jumanne, Julai 14, kikilenga meli zinazoelekea bandari na maeneo ya pwani ya Iran.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, CENTCOM imesema hatua hiyo itaanza kutekelezwa saa 4:00 mchana kwa saa za Mashariki mwa Marekani.

    Jeshi hilo limesema litaendelea kuruhusu usafiri wa meli katika maji ya eneo hilo kwa meli ambazo hazitakiuka masharti ya kizuizi hicho.

    Rais Donald Trump alikuwa ametangaza awali kwamba Marekani ingerudisha mara moja kizuizi dhidi ya bandari za Iran.

    Aidha, Trump ametangaza kuwa Marekani itaweka tozo ya asilimia 20 kwa meli zitakazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz kama sehemu ya hatua mpya za kuzuia usafiri wa majini katika eneo hilo.

    Kwa mujibu wa CENTCOM, hatua hiyo inafuatia kipindi cha awali cha utekelezaji wa kizuizi hicho kilichodumu kuanzia Aprili 13 hadi Juni 18.

    Kwa upande wake, Iran imesema imeufunga Mlango wa Bahari wa Hormuz hadi itakapotangaza vinginevyo, kufuatia mapigano ya siku za karibuni.

    Msemaji wa Makao Makuu ya Khatam al Anbiya amesema Iran haitaruhusu Marekani kuingilia usimamizi wa Mlango wa Hormuz kwa hali yoyote.

    Unaweza kusoma;

  8. UAE yashutumu Iran kwa shambulio la meli za mafuta huku Marekani ikiendeleza mashambulizi

    H

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Falme za Kiarabu (UAE) zimeishutumu Iran kwa kile ilichokiita shambulio la "kijasiri" dhidi ya meli mbili za mafuta katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, lililosababisha kifo cha mfanyakazi mmoja raia wa India na kujeruhi wengine wanane.

    Wizara ya Ulinzi ya UAE imesema raia sita wa India na wawili wa Ukraine walijeruhiwa, huku majeruhi wanne wakiwa katika hali mbaya.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, wizara hiyo imesema shambulio hilo ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na linahatarisha usalama na utulivu wa eneo hilo.

    Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump alisema Marekani imeanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran kwa usiku wa tatu mfululizo.

    "Tunaishambulia Iran kwa nguvu kubwa," alisema Trump.

    Pia alitangaza kuwa Marekani itaweka tozo ya asilimia 20 kwa meli zitakazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz kama sehemu ya hatua mpya za kuzuia usafiri wa majini katika eneo hilo.

    Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema Tehran itaendelea kuwa "mlinzi" wa Mlango wa Bahari wa Hormuz, akijibu tangazo la Marekani kuhusu hatua hizo.

    Baadaye, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) lilidai kuhusika na shambulio hilo, likisema meli hizo zilipuuzia maonyo, zilizima mifumo yao na kujaribu kupita katika njia iliyokuwa imewekewa mabomu ya baharini.

    IRGC ilisema hatua hiyo ilikuwa onyo kwamba ushirikiano na "adui mvamizi" utasababisha madhara zaidi na unaweza kuchelewesha kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz, pamoja na kuchochea mgogoro wa nishati duniani.

    Mvutano kuhusu udhibiti wa Mlango wa Bahari wa Hormuz unaendelea kuongezeka huku Marekani na Iran zikiendelea kubadilishana mashambulizi na vitisho katika eneo hilo.

    Unaweza kusoma;

  9. Trump ataka mataifa ya Ghuba yalipie ulinzi wa Marekani dhidi ya Iran

    f

    Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema mataifa ya Ghuba ya Uajemi yanapaswa kulipia ulinzi ambao Marekani inayatoa dhidi ya vitisho kutoka Iran.

    "Ndani ya mwezi mmoja tangu siku tulipowashambulia, wangekuwa na silaha ya nyuklia kama tusingefanya hivyo. Kama wangekuwa na silaha ya nyuklia, Israel huenda isingekuwapo tena, na pengine hata Mashariki ya Kati isingekuwa salama."

    Akizungumza na waandishi wa habari, Trump amesema Marekani imekuwa ikitumia fedha nyingi kulinda eneo hilo na kwamba ni wakati wa washirika wake kubeba sehemu ya gharama hizo.

    "Nataka tulipwe kwa sababu tunalinda sehemu tajiri sana ya dunia. Tunatumia fedha nyingi, hivyo nchi tunazozilinda zinapaswa kutulipa kwa ulinzi huo."

    Trump ametaja Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Qatar, Bahrain na Kuwait kuwa miongoni mwa mataifa yanayonufaika na ulinzi wa Marekani katika eneo la Ghuba.

    Trump pia amedai kuwa Iran ilirusha makombora kuelekea mataifa hayo matano, akisema hatua hiyo inaonesha kuwa viongozi wa Tehran ni "hatari" na kwamba Marekani haitakubali hali hiyo iendelee.

    Aidha amesema Marekani itafanya "shambulio jingine kubwa" dhidi ya Iran usiku huo, huku akidai kuwa Tehran sasa inataka kufikia makubaliano baada ya miaka mingi ya mazungumzo.

    "Tutafanya shambulio jingine kubwa usiku wa leo. Wanataka kufanya makubaliano... Tumekuwa tukifanya mazungumzo kwa miaka 47, lakini hakuna aliyewahi kuwashambulia kijeshi. Sisi tunawashambulia kwa nguvu sana."

    Kauli hiyo imekuja huku mvutano kati ya Marekani na Iran ukiendelea kuongezeka, baada ya mashambulizi ya kijeshi ya pande zote na vitisho vinavyoendelea kuhusu usalama wa usafiri wa majini katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Trump pia amedai kuwa Iran ilikaribia kupata silaha ya nyuklia kabla ya mashambulizi ya Marekani, akisema Washington itaendelea kuchukua hatua za kijeshi ikiwa itahitajika.

    Iran haijajibu mara moja kauli za Trump. Tehran imekuwa ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani na imekuwa ikipinga mashambulizi ya Marekani dhidi ya miundombinu yake.

    Soma Zaidi:

  10. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.