Moja kwa moja, Tutadhibiti Mlango bahari wa Hormuz-Trump

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa Marekani "huenda ikaudhibiti" Mlango wa Bahari wa Hormuz, akidai kwamba Iran "imevunja" makubaliano.

Skip Video and continue reading
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote
  • xx
  • Lydia Wanjiku

Moja kwa moja

Na Mariam mjahid & LizzyMasinga

  1. Tutadhibiti Mlango bahari wa Hormuz-Trump

    Trump

    Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa Marekani "huenda ikaudhibiti" Mlango wa Bahari wa Hormuz, akidai kwamba Iran "imevunja" makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa kati ya nchi hizo mbili.

    Akizungumza na kituo cha habari cha Fox News, Trump amesema:

    "Tunachukua udhibiti wa mlango huo wa bahari. Hawana chochote. Hawana kitu."

    Pia amesema kwamba Marekani ilishambulia Iran kwa nguvu kubwa usiku uliopita, akirejelea mashambulizi kadhaa yaliyofanywa na Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) dhidi ya mali na vifaa vya kijeshi nchini Iran.

    Trump ameongeza:

    "Tunawadhibiti. Wako katika hali ngumu. Sehemu kubwa ya vifaa vyao vya kijeshi imeharibiwa. Mifumo yao ya ulinzi wa anga imeondolewa."

    Mapema Jumatatu, Ubalozi wa Iran nchini Uingereza ulisema kuwa Iran imeanzisha ukanda wa muda wa usalama wa usafiri wa baharini, ambao ni bila vikwazo vya kiufundi na vya kijeshi, katika Mlango wa Bahari wa Hormuz ili kuruhusu meli kupita kwa usalama.

    Hata hivyo, ubalozi huo ulisema kuwa hatua za kijeshi za Marekani zimeugeuza Mlango wa Bahari wa Hormuz kuwa eneo lenye hatari kubwa, na hivyo kuongeza wasiwasi kuhusu usalama wa usafiri wa baharini katika eneo hilo.

    Unaweza kusoma;

  2. Rais Samia: Hakuna mtu aliye juu ya sheria

    Rais Samia

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Na Lizzy Masinga

    Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba yeyote atakayevunja atashughulikiwa.

    Ameyasema hayo alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali (TPBA), jijini Arusha.

    Rais Samia amesema Tanzania iko vizuri kwenye masuala ya haki za binadamu na uzuri ni kwamba hakuna aliye juu ya sheria, anayevunja sheria anashughulikiwa.

    ''Tanzania tuko vizuri, waendelee kusema hakuna haki,tunavunja haki, lakini hakuna aliye juu ya sheria''.

    "Tunashuhudia mataifa yakihujumiana, tunashuhudia vijana kulaghaiwa na kumezeshwa sumu dhidi ya mataifa yao na kushawishiwa kuhujumu chumi zao zilizojengwa kwa nguvu kubwa".

    "Vilevile kuna wimbi la kuwaaminisha vijana kwamba serikali zao hasa za Afrika, hazifuati au zinakiuka haki za binaadamu". Alisema Rais Samia.

    "Sasa hapa ninataka tukumbushe tu ulimwengu lakini na watu wetu wajue kwamba kwa upande wa Tanzania, sisi ni wafuasi wazuri sana wa haki za binadamu.'' Mtakumbuka kwamba sisi Tanzania tuliweka kwa mara ya kwanza kwenye Katiba yetu, mtiririko wa haki za binadamu tulipobadili sheria mwaka 1984 na tukatanua wigo wa haki hizo.

    Rais Samia amewataka mawakili kutekeleza kwa weledi majukumu yao na kutoa majawabu kwa changamoto zinazojitokeza.

    "Niseme nyinyi ni walinzi muhimu wenye ujuzi wa kisheria za ndani na za kimataifa, nimesema hali ilivyo duniani sasa hivi, lazima tuwe na weledi wa matamko, itifaki na mambo mengine ya kimataifa yanayotoka huko, kuyaangalia kwa haraka, kuyatafsiri katika hali yetu na kutoa majawabu kwa haraka ili kuuhami uhuru wetu". Alisema.

    Unaweza kusoma;

  3. Waziri wa zamani nchini Tanzania ashauri Lissu aachiwe huru

    Anna Tibaijuka

    Chanzo cha picha, Anna Tibaijuka

    Na Lizzy Masinga

    Aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka ametoa ushauri kwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani CHADEMA, Tundu Lissu aachiwe huru kwani kesi haikamiliki.

    ''Hekima na busara iliyokufanya kutangaza sera ya 4RS mara ulipoingia madarakani ikuongoze katika jambo hili''. Aliandika katika ukurasa wake wa X.

    Amesema simulizi za kutisha za vyombo vya habari vya kimataifa, zinaibua hisia kali hasa kwa vijana, hata wazee wamekumbushwa kadhia ya operesheni sogeza iliyounda vijiji vya ujamaa mwaka 1974-1976.

    Kitengo cha uchunguzi cha BBC Afrika Eye kimechapisha makala maalumu ya Tundu Lissu ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu kukamatwa kwake.

    Lissu ambaye ni kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, anakabiliwa na kesi ya uhaini.

    Lissu, mwenye umri wa miaka 58, alikamatwa mwezi Aprili 2025 wakati akifanya kampeni chini ya kaulimbiu ya chama chake Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), "Hakuna Mageuzi, Hakuna Uchaguzi."

    Mamlaka zilielezea kuwa kampeni hiyo ilikuwa ikichochea umma kupinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

    Bi. Tibaijuka amesema kuwa taarifa hizi zinaathiri kikubwa taswira ya taifa la Tanzania na maslahi yake.

    "Athari ni kubwa. Tutafute mufaka kupitia uwajibikaji na maridhiano. Tuwe na hofu ya Mungu na kutambua miujiza yake, mfano wa risasi16 kushindwa kukomesha uhai ingawa maumivu ni makubwa". Aliandika.

    Unaweza kusoma;

  4. Hatutasita kuchukua hatua za kujilinda-Iran

    Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje Esmail Baghaei

    Chanzo cha picha, Reuters

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa makubaliano kati ya Marekani na Iran "yameingia katika mgogoro."

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vinamnukuu Esmail Baghaei akisema kwamba "mashambulizi ya kujihami" ya Iran yamelenga tu kambi na vituo vilivyotumiwa na Marekani kushambulia nchi hiyo.

    "Hatutasita kujilinda," ameongeza, akisema kuwa Iran haiwezi kuruhusu Marekani kutumia njia ya usafiri kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz kuhatarisha mamlaka na usalama wa nchi hiyo.

    Baghaei amesema kuwa mazungumzo ya Jumamosi yalihusu tu njia hiyo muhimu ya baharini, akiongeza kuwa lengo la Iran lilikuwa kuhakikisha meli zinapita kwa usalama. Hata hivyo, amesema kuwa shinikizo la Marekani kwa Oman limekwamisha juhudi hizo.

    Kwa ukumbusho, takwimu za ufuatiliaji wa meli zinaonesha kuwa hakuna meli iliyopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz tangu jana jioni.

    Kuhusu Hati ya makubaliano yenye vipengele 14 yaliyotiwa saini tarehe 17 Juni, Baghaei amesema kuwa Iran haitatekeleza wajibu wake ikiwa Marekani haitaheshimu makubaliano hayo.

    Unaweza kusoma;

  5. Iran yasema imezishambulia kambi za kijeshi za Marekani Mashariki ya Kati

    s

    Chanzo cha picha, Morteza Nikoubazl/NurPhoto via Getty Images

    Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limesema limefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani nchini Bahrain, Kuwait na Jordan.

    Kwa mujibu wa IRGC, mashambulizi hayo yalifanyika kujibu hatua za kijeshi za Marekani zilizotekelezwa Jumapili na Jumatatu.

    IRGC imedai kuwa makombora na droni ziliharibu miundombinu muhimu ya kijeshi, ikiwemo maghala ya makombora na matangi ya mafuta katika Kituo cha Anga cha Prince Hassan nchini Jordan, na kusababisha moto.

    Jeshi hilo pia limesema Kituo cha Anga cha Sheikh Isa nchini Bahrain kililengwa, kikidai kuwa mashambulizi hayo yaliharibu kituo cha matengenezo ya helikopta za Jeshi la Marekani, banda la ndege ya kivita ya kielektroniki aina ya P 8 na kituo cha uongozi na udhibiti wa droni.

    Madai hayo ya IRGC hayajathibitishwa kwa kujitegemea, na hadi sasa Marekani haijatoa tamko kuhusu taarifa hizo.

  6. Bei ya mafuta duniani yapanda baada ya Marekani na Iran kuzidisha mashambulizi

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Bei ya mafuta katika soko la dunia imepanda kwa zaidi ya asilimia nne kufuatia hatua ya Marekani kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran na Tehran kujibu kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi.

    Mafuta ghafi aina ya Brent yalipanda kwa asilimia nne na kufikia dola 79.11 kwa pipa, huku mafuta ghafi ya Marekani aina ya West Texas Intermediate (WTI) nayo yakiongezeka kwa asilimia nne na kufikia dola 74.36 kwa pipa, kwa mujibu wa Reuters.

    Kupanda kwa bei hizo kunafuatia wasiwasi kuhusu usalama wa usafirishaji wa mafuta katika eneo la Ghuba, ambalo ni moja ya njia muhimu zaidi za biashara ya nishati duniani.

    Pia unaweza kusoma:

  7. ODM haitasimamisha mgombea urais katika uchaguzi wa 2027

    Kiongozi wa Chama cha ODM nchini Kenya

    Chanzo cha picha, ODM/Mitandaoni

    Maelezo ya picha, Kiongozi wa Chama cha ODM nchini Kenya

    Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) hakitasimamisha mgombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, kwa mujibu wa kiongozi wake, Oburu Oginga, ambaye amesema chama hicho kinalenga kumuunga mkono Rais William Ruto kuwania muhula wa pili.

    "Katika mazungumzo ya muungano tunayofanya, tunajua safari hii ODM haitasimamisha mgombea urais. Kwa hiyo, tutamuunga mkono Rais William Ruto kuwania muhula wa pili," amesema Oburu.

    Akizungumza katika harambee iliyofanyika Kanisa Katoliki la St Pascal's Chiga, Kaunti ya Homa Bay, Oburu amesema uamuzi huo ni sehemu ya mazungumzo ya kisiasa yanayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya ODM na serikali ya Rais Ruto.

    Aidha, amesema ODM itaingia katika ushirikiano huo kwa masharti yatakayohakikisha sera na vipaumbele vyake vinajumuishwa katika ajenda ya serikali, pamoja na kuwepo kwa mfumo unaobainisha nafasi na ushiriki wa chama hicho.

    Kauli hiyo imeongeza uzito kwa ishara za kuimarika kwa ushirikiano kati ya ODM na utawala wa Rais Ruto, uliokuwa umejengwa kupitia kile kinachoitwa serikali ya ushirikiano mpana, baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo kati ya viongozi wa pande hizo mbili.

    Hata hivyo, kauli hiyo huenda ikaibua mjadala wa kisiasa ndani na nje ya ODM, hasa ikizingatiwa kuwa chama hicho kwa muda mrefu kimekuwa kikisimamisha mgombea wake au kumuunga mkono mgombea wa upinzani katika chaguzi za urais nchini Kenya.

    Soma zaidi:

  8. Jaji Mwislamu atishiwa kuuawa baada ya kuwahukumu waliofanya mauaji kwa madai ya kulinda ng'ombe

    h

    Chanzo cha picha, narmadapuram.dcourts.gov.in

    Jaji Tabassum Khan wa jimbo la Madhya Pradesh nchini India anakabiliwa na vitisho vya kuuawa na kampeni ya chuki kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuwahukumu kifungo cha maisha watu 14 waliopatikana na hatia ya mauaji ya umati yaliyofanywa kwa madai ya "kulinda ng'ombe".

    Washitakiwa hao walitiwa hatiani kwa makosa yakiwemo mauaji, jaribio la mauaji, kufanya vurugu na kuwazuia watu kinyume cha sheria.

    Kesi hiyo ilihusu tukio la mwaka 2022 ambapo Nazir Ahmed aliuawa baada ya yeye na wenzake wawili kushambuliwa na kundi lililodai kuwa linawalinda ng'ombe, likiwashuku kusafirisha mifugo kinyume cha sheria.

    Wenzake walinusurika na kutoa ushahidi mahakamani, huku Jaji Khan akieleza katika hukumu yake kuwa tukio hilo lilikuwa mfano wa wazi wa mauaji yanayotekelezwa na umati wa watu.

    Baada ya hukumu hiyo, maandamano yalifanyika nje ya mahakama, huku baadhi ya makundi ya Wahindu wenye msimamo mkali yakipinga uamuzi huo.

    Video zilizosambazwa mitandaoni zilionyesha watu wakitoa matusi na vitisho vya kuuawa dhidi ya Jaji Khan, huku wengine wakitaka waliohukumiwa waachiwe huru.

    Aliyekuwa jaji wa Mahakama ya Juu ya India, Markandey Katju, amesema mashambulizi hayo yanalenga kudhoofisha uhalali wa jaji huyo kwa kuzingatia dini yake badala ya misingi ya kisheria.

    Vyama vya mawakili wa Mahakama ya Juu pia vimelaani vitisho hivyo na kusisitiza kuwa majaji wanapaswa kutekeleza wajibu wao bila hofu wala shinikizo.

    Polisi wamesema watu wawili wamekamatwa kuhusiana na vitisho hivyo na uchunguzi unaendelea kuwabaini wengine waliosambaza ujumbe wa uchochezi mtandaoni.

    Wakati huo huo, Mahakama Kuu ya Madhya Pradesh imeagiza ulinzi wa polisi kwa Jaji Tabassum Khan uendelee huku ikitaka serikali kueleza hatua ilizochukua kuhakikisha usalama wake.

    Soma Zaidi:

  9. Zaidi ya raia wa kigeni elfu 50 wakimbia vurugu Afrika Kusini

    s

    Chanzo cha picha, EMMANUEL CROSET / AFP via Getty Images

    Zaidi ya raia wa kigeni 53,000 wameondoka au kurejeshwa katika nchi zao tangu Afrika Kusini ilipoanzisha operesheni maalumu ya kusimamia uhamiaji wiki tano zilizopita, mamlaka za nchi hiyo zimesema.

    Maafisa wa serikali wanasema wengi wa waliorejeshwa wanatoka Malawi, Zimbabwe na Msumbiji. Wengine bado wanazuiliwa katika vituo vya muda wakisubiri kukamilika kwa taratibu za kurejeshwa makwao.

    Operesheni hiyo ni miongoni mwa hatua kubwa zaidi kuwahi kuchukuliwa dhidi ya wahamiaji wasio na vibali nchini Afrika Kusini katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Inafuatia wiki kadhaa za maandamano ya kupinga uhamiaji yaliyogubikwa na vurugu, vitisho na matukio ya uporaji.

    Waandamanaji wanaitaka serikali kuimarisha ulinzi wa mipaka na kuwafukuza wahamiaji wasio na vibali, wakidai kuwa wamechangia kuongezeka kwa ukosefu wa ajira, uhalifu na kuzorota kwa huduma za umma.

    Hata hivyo, Umoja wa Mataifa umeonya dhidi ya kuwalaumu wahamiaji kwa changamoto za kijamii na kiuchumi zinazoikabili Afrika Kusini.

    Makundi yanayopinga uhamiaji yameahidi kuendelea na maandamano ya kila wiki hadi serikali itakapotekeleza madai yao. Hali hiyo imeibua hofu ya kuzuka kwa vurugu zaidi.

    Waandamanaji walikuwa wametoa kile walichokiita tarehe ya mwisho isiyo rasmi ya Juni 30 kwa wahamiaji wasio na vibali kuondoka nchini, hatua iliyowafanya maelfu ya wageni kuondoka kwa hofu ya kushambuliwa au kutishiwa.

    Katika majuma ya hivi karibuni, nchi kadhaa zikiwemo Ghana, Nigeria, Uganda na Kenya zimewarejesha raia wao waliokuwa nchini Afrika Kusini.

    Unaweza kusoma;

  10. Watu 27 wafariki dunia katika moto ulioteketeza baa jijini Bangkok

    D

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takriban watu 27 wamefariki dunia baada ya moto mkubwa kuzuka katika baa moja jijini Bangkok, Thailand, kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Anutin Charnvirakul.

    Vikosi vya zimamoto vilifika eneo la tukio muda mfupi baada ya saa sita usiku wa kuamkia Jumapili. Maafisa walisema wateja walikuwa wakijaribu kutoroka kupitia mlango wa kuingilia, ambao tayari ulikuwa umeteketezwa na moto, wakati waokoaji walipowasili.

    Video zilizosambaa mitandaoni, ambazo hazijathibitishwa na vyanzo huru, zinaonyesha moto ukilipuka kutoka ndani ya jengo huku watu wakikimbia kujiokoa. Katika moja ya video hizo, mwanamke anaonekana akianguka chini katikati ya taharuki kabla ya kuinuka na kukimbia.

    Akizungumza eneo la tukio, Waziri Mkuu alisema watu 27 wamefariki huku wengine kadhaa wakipelekwa hospitalini kwa matibabu. Alisisitiza kuwa chanzo cha moto huo bado kinachunguzwa.

    Alisema pia alizungumza na mmoja wa wanamuziki waliokuwa wakitumbuiza wakati moto ulipozuka. Kwa mujibu wa mwanamuziki huyo, moto ulianza kutokana na hitilafu ya umeme kabla ya kuenea kwa kasi.

    Baa hiyo, inayojulikana kwa jina la Rong Bir Na Lat Phrao, ipo katika eneo la Chatuchak jijini Bangkok na ni miongoni mwa maeneo maarufu ya burudani na migahawa katika mji mkuu wa Thailand, kwa mujibu wa gazeti la Daily News la Thailand.

    Soma zaidi:

  11. Iran yajibu wito wa Umoja wa Mataifa wa kusitisha mashambulizi

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghai

    Chanzo cha picha, Iran Press

    Maelezo ya picha, Ni msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghai

    Iran imesema haijafanya mashambulizi dhidi ya nchi yoyote, ikisisitiza kuwa hatua zake dhidi ya vituo na mali za kijeshi za Marekani katika pwani ya kusini ya Ghuba ya Uajemi ni sehemu ya haki yake ya kujilinda kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

    Akizungumza baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, kutoa wito kwa Iran na Marekani kusitisha mashambulizi na kurejea kwenye mazungumzo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghai, alisema lawama hazipaswi kuelekezwa kwa Iran.

    "Iran haijashambulia popote. Hatua tulizochukua dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani ni utekelezaji wa haki yetu ya kujilinda chini ya sheria za kimataifa," alisema.

    Baghai pia alizitaka nchi zinazoruhusu Marekani kutumia maeneo na kambi zake za kijeshi kuwajibika kwa nafasi yao katika mzozo huo.

    "Waulizeni nchi zinazotoa ardhi na kambi zao kwa Marekani," alisema.

    Aidha aliikosoa Umoja wa Mataifa kwa kile alichodai ni kuilaumu Iran badala ya kuishutumu Marekani kwa kukiuka sheria za kimataifa.

    Katika kauli yake, Baghai pia alikosoa matumizi ya neno "Ghuba" yaliyotumiwa na msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric, akisisitiza kuwa jina sahihi kwa mujibu wa nyaraka za Umoja wa Mataifa ni Ghuba ya Uajemi.

    Awali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alikuwa ametoa wito kwa Iran na Marekani kusitisha mashambulizi ya karibuni na kurejea kwenye mazungumzo ya kumaliza mzozo huo. Pia alitaja mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran, mashambulizi ya Iran dhidi ya meli katika Mlango wa Hormuz na mashambulizi dhidi ya vituo vya washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

    Soma Zaidi:

  12. Marekani yasema imekamilisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran

    b

    Chanzo cha picha, Reuters

    Jeshi la Marekani kupitia Kamandi Kuu ya Marekani Mashariki ya Kati (CENTCOM) limesema limekamilisha operesheni mpya za kijeshi dhidi ya Iran usiku wa Julai 12 hadi 13, likidai kuwa makumi ya maeneo yalilengwa ili kudhoofisha uwezo wa Iran wa kushambulia meli zinazopita katika Mlango wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa CENTCOM, operesheni hizo zilihusisha matumizi ya ndege za kivita, meli za kijeshi, ndege zisizo na rubani na, kwa mara ya kwanza, droni za majini.

    Jeshi hilo limesema droni za angani na za majini zilitumika kutekeleza mashambulizi yaliyolenga mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran, vituo vya rada za pwani, uwezo wa makombora na droni pamoja na boti ndogo.

    CENTCOM imeeleza kuwa Mlango wa Hormuz ni njia muhimu ya usafirishaji wa bidhaa duniani na kusisitiza kuwa Iran haina mamlaka ya kuudhibiti.

    "Vikosi vya Marekani vimewekwa tayari kuhakikisha uhuru wa usafiri wa baharini unaendelea kuwepo kwa meli za kibiashara, licha ya kile ilichokitaja kuwa uchokozi, vitisho na hatua za upande mmoja za Iran," ilisema CENTCOM.

    Soma Zaidi:

  13. Iran na Marekani zazidisha mashambulizi ya kulipizana

    D

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani mashambulizi mapya ya Marekani na kuonya kuwa mataifa ya Ghuba yatakayoshirikiana katika kile ilichokiita "uchokozi wa kijeshi dhidi ya Iran" yatakuwa shabaha halali za vikosi vya jeshi la Iran.

    Tamko hilo lilichapishwa na vyombo rasmi vya habari vya Iran Jumatatu asubuhi, Julai 13.

    Katika taarifa hiyo, Iran iliishutumu Marekani kwa kukiuka makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni ya kusitisha vita.

    "Katika muda wa siku 25 tu tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kumaliza vita, utawala wa Marekani umekiuka wazi karibu masharti yote ya makubaliano hayo na umetenda uhalifu mkubwa wa kivita kwa kushambulia miundombinu ya usafiri ya Iran, boti za uvuvi, meli za mizigo, vituo vya hali ya hewa na miundombinu mingine," ilisema taarifa hiyo.

    Wizara hiyo pia ilisema kuwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa, nchi jirani zina wajibu wa kuhakikisha maeneo yao hayatumiwi kutekeleza mashambulizi dhidi ya Iran.

    "Nchi jirani zina wajibu chini ya sheria za kimataifa kuzuia eneo lao au miundombinu yao kutumiwa kwa uchokozi wa kijeshi dhidi ya Iran. Eneo lolote litakalotumiwa kupanga au kutekeleza mashambulizi dhidi ya Iran litachukuliwa kuwa shabaha halali ya mashambulizi ya kujihami ya vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," taarifa hiyo iliongeza.

    Wakati huo huo, mamlaka mpya inayosimamia usafiri katika Mlango wa Hormuz imesema shughuli za usafirishaji kupitia njia hiyo zimesimamishwa kutokana na mashambulizi ya kijeshi na kuongezeka kwa shughuli za kijeshi za Marekani katika maji ya Ghuba ya Uajemi.

    Mamlaka hiyo ilitangaza kuwa Mlango wa Hormuz utaendelea kufungwa hadi itakapotolewa taarifa nyingine.

    Soma Zaidi Hapa:

  14. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 12 Julai 2026.