Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi
Mutuse alijipata katika hali ngumu siku ya Jumatano wakati alipokuwa
akihojiwa ndani ya Seneti katika kesi ya kuondolewa madarakani aliyowasilisha kwa bunge dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Naibu Rais Rigathi Gachagua kupitia mawakili wake
wazoefu wanaoongozwa na Wakili Paul Muite wanapambana kuhakikisha haondolewi
mamlakani baada ya Bunge la taifa mnamo Oktoba 8 kupiga kura kuidhinisha
kutimuliwa kwake.
Mutuse alipata kibarua kigumu kujibu maswali makali ya
wakili wa Gachagua Elisha Ongoya ambaye aliupinga ushahidi wake mkuu dhidi ya
Bw Gachagua.
Miongoni mwa tuhuma ambazo wanasheria wa Gachagua
walitaka kuzifuta ni pamoja na kuihujumu serikali kwa kupinga hadharani sera
zake za kuwahamisha wafanyabiashara kutoka soko la wakulima na kuwapeleka
katika eneo jipya katika Barabara ya Outering na ubomoaji wa majengo katika
maeneo ya mabondeni.
Timu ya Gachagua ilitumia kanda za video kuwadhihirishia
maseneta kuwa alitoa matamshi akiiomba serikali kuwatendea raia utu na zile
zilizoonyesha kuwa baadhi ya kauli zilizotajwa kuchochea ukabila zimekuwa
zikitumiwa tangu awali pia na Rais william Ruto na kwamba zilikuwa msingi wa ugavi wa madaraka katika serikali ya sasa ya Kenya Kwanza .
Mawakili wa Gachagua walitoa video ambapo alitoa
matamshi akiiomba serikali kuwatendea raia utu kwa kuzingatia ahadi zake za
kabla ya kampeni.
“Naibu Rais
anasema ‘Tusiwe na vita na Wananchi.’. Je, unaona jambo lolote la kuudhi katika
taarifa hiyo?” Ongoya alimuuliza, Mutuse aliyejibu , hapana.
"Anatoa
wito wa huruma kwa wananchi. Je, unaona jambo lolote la kukera katika sehemu hiyo?” wakili aliuliza.
Wakati mmoja kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea wakili wa Gachagua, alicheza kanda ya video ambapo Rais Ruto alionekana kwenye mkutano akiwaambia wananchi wa eneo la Mlima Kenya kuwa wana 'share' (hisa) katika serikali- kauli ambayo bunge linasema imekuwa ikitumiwa na Gachagua na inachochea ukabila. Gachagua alisema alijifunza kutumia kauli hiyo kutoka kwa Rais Ruto.
Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea kusikilizwa na seneti leo asubuhi.