Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani yaanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran huku Trump akiionya Tehran kuishi kwa nidhamu

Trump aiambia Iran kuwa "Sipendi kuweka muda wa mwisho, lakini wanafahamu hali ilivyo. Ni vyema wakaishi kwa nidhamu."

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Marekani yawazuia wasafiri kutoka DRC kuingia nchini kutokana na Ebola

    Ubalozi wa Marekani mjini Kinshasa umetangaza kuwa raia wa Marekani watakaoondoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) hawataruhusiwa kupanda ndege zinazoelekea Marekani hadi watakapokaa nje ya DRC kwa siku 21, kufuatia mlipuko wa Ebola unaoendelea mashariki mwa nchi.

    Hatua hiyo inafuatia tahadhari iliyotolewa na Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), iliyosema wasafiri kutoka DRC, Uganda na Sudan Kusini watafuatiliwa kiafya kwa siku 21.

    Kwa mujibu wa CDC, watu wanaoondoka DRC wanaweza kuwekewa amri ya "Kutoabiri", inayowazuia kupanda ndege zinazoelekea Marekani hadi kipindi hicho cha ufuatiliaji kitakapokamilika.

    Wasafiri watakaoruhusiwa kuingia Marekani wataendelea kufanyiwa uchunguzi wa afya katika viwanja maalumu vya ndege, ikiwa ni pamoja na kupimwa joto la mwili na kufuatiliwa hali yao ya kiafya.

    Ubalozi wa Marekani umeonya kuwa raia wake walioko DRC wanapaswa kutarajia ucheleweshaji wa safari na huenda wakalazimika kupita katika nchi nyingine kabla ya kurejea Marekani. Hata hivyo, baadhi ya misamaha inaweza kutolewa kwa misingi ya kibinadamu.

    Wakati huo huo, Kituo cha Uendeshaji wa Dharura za Afya ya Umma cha DRC kimesema mlipuko wa Ebola unaendelea kuongezeka. Kufikia Julai 13, kulikuwa na wagonjwa 2,011 waliothibitishwa na vifo 754 katika majimbo matano, huku jimbo la Ituri likiwa na idadi kubwa zaidi ya maambukizi mapya.

    Maafisa wa afya pia wamesema maambukizi mapya katika jimbo la Haut Uélé yanaashiria kuwa mlipuko huo unaendelea kusambaa katika maeneo mapya.

    Kiwango cha vifo kutokana na mlipuko huo kimefikia asilimia 37.5, hali inayoonyesha ukubwa wa athari za aina ya Bundibugyo ya virusi vya Ebola.

  2. Spishi mpya ya nyani wenye midomo ya rangi ya chungwa yagunduliwa msituni DRC

    Nyani mwenye midomo ya rangi ya waridi inayokaribia chungwa, uso mweusi na anayeishi katika misitu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) amethibitishwa kuwa spishi mpya kwa sayansi.

    Nyani huyo mwenye manyoya meusi alionekana na kupigwa picha akiwa amejificha kwenye matawi ya juu ya miti katika msitu mnene wa kitropiki wa Hifadhi ya Taifa ya Lomami, iliyoko mashariki ya kati mwa DRC.

    Wahifadhi wa mazingira wanaofanya kazi katika eneo hilo waliripoti kumuona mnyama huyo wa kipekee kwa mara ya kwanza mwaka 2008, lakini wakati huo walifanikiwa kupata picha moja tu isiyoeleweka vizuri.

    Baada ya kuonekana tena miaka 10 baadaye, timu ya kimataifa ya watafiti ilianzisha msako wa kumtafuta na kumchunguza, na hatimaye kuthibitisha kuwa alikuwa spishi ambayo haikuwa imewahi kutambuliwa na sayansi.

    Hii ni spishi ya tano pekee ya nyani barani Afrika kugunduliwa katika kipindi cha miaka 75 iliyopita.

    Junior Amboko, mwanafunzi wa shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Florida Atlantic, aliongoza sehemu ya utafiti huo uliotumia kurekodi sauti, upigaji picha na uchambuzi wa kina wa vinasaba.

    Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika jarida la kisayansi la PLoS One.

    Akizungumza na BBC News, Amboko alisema ilikuwa "hisia ya kipekee" kutazama uso wa mnyama ambaye watu wachache sana duniani walijua uwepo wake.

  3. Iran yadai kuidungua ndege isiyo na rubani ya Marekani

    Iran imesema imeidungua na kuharibu ndege isiyo na rubani ya Marekani aina ya MQ 9, ambayo inadai ilikuwa ikiruka juu ya mji wa Andimeshk.

    Kwa mujibu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ndege hiyo ilidunguliwa kwa kutumia mfumo wa kisasa wa ulinzi wa anga.

    Shirika la habari la Tasnim, linalohusishwa na IRGC, liliripoti kuwa operesheni hiyo ilifanikiwa, lakini halikutoa ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.

    Hadi sasa, Marekani wala Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) hawajathibitisha rasmi madai ya Iran kwamba ndege hiyo ya MQ 9 ilidunguliwa.

    Soma Zaidi Hapa:

  4. Jeshi la Marekani kuanza uchunguzi wa upungufu wa homoni ya testosterone kwa wanajeshi

    Wizara ya Ulinzi ya Marekani imetangaza kuwa wanajeshi wote wenye umri wa miaka 30 na zaidi wataanza kufanyiwa uchunguzi wa upungufu wa homoni ya testosterone kama sehemu ya vipimo vyao vya afya vya kila mwaka.

    Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, alisema katika video aliyochapisha kwenye mtandao wa X kwamba ameidhinisha mpango huo ili kuhakikisha wanajeshi wanakuwa na kiwango kinachofaa cha homoni hiyo na hivyo kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi wa juu.

    Wanajeshi watakaobainika kuwa na kiwango cha chini cha testosterone watapewa fursa ya hiari ya kupata tiba ya kuongeza homoni hiyo. Kwa wanajeshi walio chini ya umri wa miaka 30, vipimo hivyo vitakuwa vya hiari.

    Hegseth hakufafanua iwapo mpango huo utawahusu pia wanawake, ambao viwango vya ostrojeni pia hupungua kadiri umri unavyoongezeka.

    "Tunawajibika kuwapatia wanajeshi wetu huduma bora zaidi za afya duniani, na mpango huu unatekeleza wajibu huo," alisema Hegseth.

    Aliongeza kuwa kulinda afya ya muda mrefu kunamaanisha kuhakikisha wanajeshi wanabaki imara, wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto na tayari kutekeleza majukumu yao, si tu katika operesheni zinazofuata bali pia baada ya kustaafu utumishi wa kijeshi.

    Matumizi ya testosterone kwa sababu zisizo za kitabibu, kama vile kuongeza misuli bila agizo la daktari, yamepigwa marufuku ndani ya jeshi la Marekani.

    Hegseth alisisitiza kuwa mpango huo haukusudii kuongeza uwezo wa mwili kwa njia isiyo ya kawaida, bali unalenga kuboresha huduma za afya kwa wanajeshi.

    Msemaji wa Pentagon, Sean Parnell, alisema mpango huo utaanza kutekelezwa mara moja kwa wanajeshi wote walio katika utumishi wa moja kwa moja na wa akiba wenye umri wa miaka 30 na zaidi.

    Alisema uchunguzi huo utaiwezesha Wizara ya Ulinzi kupata taarifa za msingi kuhusu afya ya wanajeshi na kutoa matibabu yanayolengwa kwa wale wenye upungufu wa testosterone, kwa lengo la kudumisha jeshi lenye afya, uwezo na utayari wa kutekeleza majukumu yake.

    Pentagon haikujibu iwapo wanawake pia watafanyiwa vipimo hivyo au kama watapatiwa tathmini ya tiba ya homoni ya oestrogen wanapoanza kipindi cha kuelekea ukomo wa hedhi.

    Soma zaidi:

  5. Kombe la Dunia: Argentina yafuzu fainali kwa shangwe, England yaondoka kwa majonzi

    Argentina imefuzu fainali kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuiondoa England katika mchezo wa nusu fainali ulioshuhudia hisia tofauti kwa timu hizo mbili.

    Baada ya filimbi ya mwisho, wachezaji wa Argentina walipiga magoti uwanjani wakisherehekea ushindi na tiketi ya kuelekea fainali, huku wachezaji wa England wakijilaza uwanjani kwa huzuni baada ya ndoto yao ya kutwaa ubingwa kuyeyuka.

    Argentina sasa itachuana na Uhispania katika fainali itakayopigwa Jumapili mjini New Jersey, ikilenga kutwaa taji hilo.

    Kwa upande wa England, itaelekeza nguvu zake katika pambano la kuwania nafasi ya tatu dhidi ya Ufaransa, baada ya kushindwa tena kufika fainali.

    Soma Zaidi:

  6. Shirika la habari la Fars: Makombora ya Marekani yamedondoka karibu na hospitali ya watoto wenye saratani

    Shirika la habari la Iran, Fars News Agency, limesema makombora ya Marekani yamedondoka karibu na hospitali inayowahudumia watoto wenye saratani katika mji wa Ahvaz, kusini magharibi mwa nchi.

    Kwa mujibu wa shirika hilo, milipuko kadhaa ilisikika katika maeneo mbalimbali ya mji huo katika saa za hivi karibuni.

    Fars ilisema baadhi ya makombora hayo yalidondoka karibu na Hospitali ya Baghaei, ambayo hutoa huduma za tiba ya kemikali kwa wagonjwa wa saratani, hasa watoto.

    "Katika moja ya mashambulizi hayo, makombora kadhaa yalidondoka karibu na Hospitali ya Baghaei, inayotoa huduma za tiba ya saratani kwa watoto," ilisema Fars.

    BBC haijaweza kuthibitisha kwa njia huru madai hayo kutokana na ukosefu wa fursa ya kupata taarifa moja kwa moja kutoka ndani ya Iran.

    Soma Zaidi Hapa:

  7. Trump asema Iran itashindwa vitani huku Marekani ikiongeza mashambulizi

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema Iran “inataka sana” kufikia makubaliano na Marekani, lakini akasisitiza kuwa Washington ndiyo itakayoamua iwapo mazungumzo hayo yataendelea.

    Akizungumza Jumatano mjini Carlisle, Pennsylvania, Trump alisema pia kuwa Iran “itashindwa karibuni,” bila kutoa maelezo zaidi kuhusu kauli hiyo.

    Kauli yake imejiri wakati mvutano wa kijeshi kati ya Marekani na Iran ukiendelea kuongezeka.

    Jeshi la Marekani lilisema limeanzisha wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya malengo ya kijeshi ya Iran, likidai yamelenga kupunguza uwezo wa Tehran wa kutishia meli zinazopita katika Mlango wa Hormuz.

    Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema mashambulizi hayo yalianza saa 19:00 GMT na yalilenga miundombinu ya kijeshi inayohusishwa na vitisho dhidi ya usafiri wa baharini katika eneo hilo.

    Wakati huo huo, shirika la habari la Mehr la Iran liliripoti kuwa milipuko ilisikika katika mji wa Bandar Abbas, kusini mwa Iran, na baadaye likasema makombora ya Marekani yaligonga eneo karibu na mji huo.

    Iran haikuwa imetoa taarifa rasmi kuhusu kiwango cha uharibifu au idadi ya walioathiriwa kufikia wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hii.

    Soma Zaidi Hapa:

  8. Marekani yaanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran huku Trump akiionya Tehran kuishi kwa nidhamu

    Marekani imesema imeanzisha wimbi jipya la mashambulizi dhidi ya Iran ikiwa ni usiku wa tano mfululizo, huku Rais Donald Trump akiionya Tehran kwamba "ni vyema ikaishi kwa nidhamu".

    Jeshi la Marekani limesema mashambulizi hayo yalilenga uwezo wa kijeshi wa Iran uliokuwa ukitumiwa kutishia meli zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz. Pia limesema lilishambulia meli iliyodaiwa kujaribu kuvunja marufuku mpya ya usafirishaji kupitia bandari za Iran.

    Hatua hiyo imekuja baada ya Iran kudai kuwa ilishambulia maeneo ya kijeshi ya Marekani katika eneo la Ghuba, yakiwemo Bahrain na Kuwait, huku siku ya tano ya mapigano mapya ikizidi kuhatarisha makubaliano ya awali yaliyolenga kumaliza vita.

    Mjadala mkuu wa Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, ameiambia vyombo vya habari vya serikali kuwa Tehran "haina sababu" ya kuendelea kuheshimu makubaliano hayo ikiwa hayatakuwa na manufaa kwa nchi hiyo.

    Jumanne usiku, Trump alitishia kushambulia madaraja na miundombinu ya uzalishaji wa umeme nchini Iran iwapo Tehran haitarejea kwenye mazungumzo wiki ijayo.

    Alipoulizwa na waandishi wa habari Jumatano usiku iwapo angeweka muda wa mwisho kabla ya kuchukua hatua hiyo, Trump alisema:

    "Sipendi kuweka muda wa mwisho, lakini wanafahamu hali ilivyo. Ni vyema wakaishi kwa nidhamu."

    Baadaye, akihutubia mkutano wa viongozi wa masuala ya ulinzi, Trump alisema Iran haijafurahishwa na hali ya sasa.

    "Wanataka kufikia makubaliano kwa udi na uvumba. Hawafurahishwi na kile tunachofanya. Tutaona kama tutafikia makubaliano nao au kama tutamaliza suala hili kabisa," alisema.

    Soma Zaidi Hapa:

  9. Hujambo, natumai umzima karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.