Watu 17 wafariki dunia kufuatia mafuriko ya ghafla Nepal
Takriban watu 17 wamefariki dunia na wengine karibu 400 hawajulikani walipo baada ya mafuriko ya ghafla na maporomoko ya udongo kusomba vijiji na kuharibu barabara pamoja na miundombinu katika eneo la mpakani kati ya Nepal na Tibet.
Mafuriko hayo yalitokea mapema Jumatano katika eneo la Rasuwa, kaskazini mwa Kathmandu, mji mkuu wa Nepal. Taarifa za awali zinaeleza kuwa huenda yalisababishwa na tetemeko la ardhi lililosababisha maporomoko ya theluji, na kusababisha maji ya theluji iliyoyeyuka kutiririka kwa nguvu kuelekea mto Bhote Koshi.
Shughuli za uokoaji zinaendelea pande zote mbili za mpaka kati ya Nepal na Tibet. Hadi sasa, watu 12 wameokolewa.
Vyombo vya habari vya serikali ya China, inayodhibiti Tibet, vimeripoti madhara makubwa, huku maafisa wa Nepal wakisema wanatarajia "hasara kubwa".
Bodi ya Utalii ya Nepal imesema juhudi zinaendelea kubaini walipo watalii 291 na raia 93 wa Nepal, wakiwemo waongoza watalii, ambao walikuwa katika eneo lililoathiriwa.
Miongoni mwa watu hao ni wasafiri 12 kutoka Uingereza, pamoja na raia wa Marekani, Malaysia, Afrika Kusini na India.
Picha za video zinaonyesha maji yakitiririka kwa nguvu na kusomba sehemu za vijiji. Msemaji wa Polisi ya Nepal, Abhi Narayan Kaphle, ameiambia BBC kuwa vikosi vyote vya usalama vinashirikiana katika shughuli za uokoaji.
Maeneo kadhaa yaliyo chini ya mkondo wa mto Bhote Koshi, unaotoka Tibet na kuingia Nepal, yako katika tahadhari kubwa. Barabara, mawasiliano na huduma za umeme zimekatizwa katika maeneo yaliyoathiriwa.
Mamlaka pia zimesema barabara kuu inayounganisha eneo hilo na Kathmandu imefungwa.