Trump: Mojtaba Khamenei hajafariki, amejeruhiwa vibaya

"Kila kitu kinaelekea kwenye ushindi mkubwa sana. Hivi karibuni tutapata ushindi mkubwa Iran," amesema Trump.

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx
  • Dangote

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula & Sarafina Robi

  1. Na kufikia hapo tunakamilisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Usiku mwema.

  2. Rais Samia aongoza kikao maalum cha Kamati Kuu ya CCM

    D

    Chanzo cha picha, IKULU TZ

    Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, CCM, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameongoza kikao maalum cha Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM jijini Dar es Salaam Jumatano, Agosti 26, 2026.

    Kikao hicho kimefanyika siku moja baada ya Makamu wa Rais, Emmanuel Nchimbi, kutangaza kujiuzulu na kustaafu siasa pamoja na utumishi wa umma. Uamuzi huo utaanza rasmi Septemba 4, 2026, na Rais Samia amekubali kujiuzulu kwake.

    Katika taarifa yake, Nchimbi alisema alimwandikia Rais Samia kumjulisha kuhusu uamuzi huo, akirejea masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanayohusu kujiuzulu kwa Makamu wa Rais.

    Nchimbi amesema pia ameamua kustaafu siasa na utumishi wa umma, chini ya mwaka mmoja tangu aliposhika nafasi ya Makamu wa Rais.

    Hatua hiyo sasa inaacha wazi nafasi ya Makamu wa Rais, ambayo kwa mujibu wa Katiba inapaswa kujazwa na Rais ndani ya siku 14 baada ya nafasi hiyo kuwa wazi, huku uteuzi ukihitaji kuidhinishwa na Bunge.

    E

    Chanzo cha picha, IKULU TZ

  3. Trump: Ninaamini Kiongozi Mkuu wa Iran bado yuko hai

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema anaamini Kiongozi Mkuu wa Iran, Mojtaba Khamenei, bado yuko hai, licha ya kutoweka hadharani tangu alipochukua madaraka baada ya kuuawa kwa baba yake mwezi Februari.

    "Sidhani kama amefariki," Trump alimwambia mtangazaji wa Marekani mwenye msimamo wa kihafidhina, Glenn Beck. Alisema Khamenei alijeruhiwa vibaya upande wa kushoto wa mwili wake, ukiwemo mkono na mguu.

    Mojtaba Khamenei bado anaongoza Iran wakati mashambulizi ya Marekani na Israel yakiendelea. Hata hivyo, kutokuwepo kwake hadharani na kuongezeka kwa ushawishi wa viongozi waandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, IRGC, kumeibua uvumi kuhusu hali yake na uwezo wake wa kuongoza.

    Baba yake, Ayatollah Ali Khamenei, aliuawa katika mashambulizi ya mabomu yaliyoashiria kuanza kwa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Trump amesema mara kadhaa kuwa Marekani inaelekea kupata ushindi dhidi ya Iran. Hata hivyo, Marekani bado haijafanikiwa kuhakikisha Iran inafungua kikamilifu Mlango wa Hormuz au kukabidhi silaha na vifaa vyake vya nyuklia.

    Katika mahojiano hayo, Trump alisisitiza kuwa shinikizo la kijeshi na kiuchumi dhidi ya Iran linaendelea kuleta matokeo.

    "Kila kitu kinaelekea kwenye ushindi mkubwa sana. Hivi karibuni tutapata ushindi mkubwa hapa," alisema.

    Kuhusu Mlango wa Hormuz, ambao Iran imezuia kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa meli, Trump alisema njia hiyo iko wazi na kwamba meli nyingi sasa zinaruhusiwa kupita.

    Alisema migodi ya baharini katika eneo hilo imeondolewa na Marekani inaendelea kusaidia meli kupita.

    Trump pia alisisitiza kuwa Marekani haiwezi kuruhusu Iran kupata silaha ya nyuklia, akisema hilo ndilo suala muhimu zaidi katika mzozo huo.

    Alidai kuwa tayari amewahi kuzuia Iran kupata silaha hiyo mara mbili hapo awali.

  4. Meta yafikia makubaliano na majimbo yaliyoishutumu

    N

    Chanzo cha picha, Reuters

    Habari kutoka Marekani zinaeleza kuwa Meta, kampuni inayomiliki Facebook na Instagram, imefikia makubaliano na majimbo 29 ya Marekani yaliyoishutumu kwa kuwadhuru watoto.

    Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinaashiria kuwa Meta inaweza kulipa hadi dola bilioni 17, ingawa kampuni hiyo imekanusha kufanya kosa lolote.

    Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama zilizotajwa na shirika la habari la Reuters, Meta itaweka kikomo cha muda ambao vijana hutumia kwenye jukwaa hilo na pia itazuia matumizi yake wakati wa usiku.

    Majimbo hayo yaliishutumu Meta kwa kubuni huduma zinazowafanya watoto kuwa na uraibu, na kwa kuficha matokeo ya utafiti kuhusu suala hilo.

  5. Tanzania na Kenya zatoa tahadhari ya El Niño inayotarajiwa

    D

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamlaka za hali ya hewa Kenya na Tanzania zimewaonya wananchi kujiandaa kwa mvua kubwa zinazotarajiwa katika msimu wa Oktoba hadi Desemba, huku hali ya El Niño ikitarajiwa kuathiri maeneo ya Afrika Mashariki.

    Nchini Tanzania, mamlaka ya hali ya hewa imetoa utabiri kuhusu uwezekano wa mvua zinazohusishwa na El Niño.

    Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, amewataka Watanzania kuchukua tahadhari na kuhifadhi vizuri chakula walichovuna, kutokana na uwezekano wa mabadiliko ya hali ya hewa.

    Mamlaka za hali ya hewa zinasema mvua hizo zinaweza kuwa na athari chanya na hasi katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, mifugo, maji, afya na miundombinu.

    Kwa hiyo, licha ya mvua hizo kuwa muhimu kwa uzalishaji wa chakula na kujaza vyanzo vya maji, mamlaka zinaonya kuwa maandalizi mapema ni muhimu ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi.

    Wakati huo huo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Kenya, KMD, pia imewahimiza Wakenya kujiandaa kwa mvua za juu ya wastani kuanzia wiki ya mwisho ya Septemba hadi Desemba.

    Katika utabiri wake wa msimu wa Oktoba hadi Desemba uliotolewa Jumatano, Agosti 26, KMD imesema mvua hizo zinaweza kuwa kubwa na kusababisha mafuriko pamoja na maporomoko ya ardhi.

    KMD imesema mvua za juu ya wastani zinatarajiwa katika kaunti zote 47 nchini Kenya, huku kiwango chake kikiongezeka hatua kwa hatua, hasa katika maeneo ya Kati, Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria na Magharibi mwa Kenya.

    Baadhi ya kaunti zinatarajiwa kuanza kupata mvua mapema mwezi Septemba, huku nyingine zikitarajiwa kuanza kupata mvua kuanzia wiki ya pili ya Oktoba.

  6. Mzozo wa Sudan: Watu 27 wauawa, wakiwemo watoto wanne

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Takriban watu 27, wakiwemo watoto wanne, wamefariki dunia katika wimbi jipya la ghasia katika eneo la Kordofan Kusini nchini Sudan.

    Ripoti zinaonyesha kuwa mashambulizi hayo yalifanyika katika maeneo ya Qardud na Abu Hamama, ambako jamii ya Otoro inaishi, na wanawake kadhaa pia walijeruhiwa.

    Chama cha Madaktari cha Sudan kililituhumu kundi la waasi la SPLM-N, linaloongozwa na Abdel Aziz al-Hilu, kwa kuhusika na mashambulizi hayo.

    Shirika hilo lilisema kuwa mashambulizi hayo dhidi ya raia yalitokea huku kukiwa na ongezeko la mapigano kati ya kundi hilo na jamii ya Otoro.

    Shirika hilo lilisema kuwa mashambulizi hayo yalisababisha watu wengi kuyahama makazi yao, huku wengi wakikimbilia maeneo ya Abu Hitan na Kadugli.

    Pia lilionya kuwa mashambulizi yanayoendelea dhidi ya raia kwa misingi ya tofauti za kikabila yanaweza kuzidi na kuwa mzozo mpana zaidi wa kikabila.

    Lilisema kuwa mashambulizi dhidi ya wanawake na watoto wasio na silaha ni ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

  7. Viongozi wa Afrika waomba fedha zaidi ili kukabiliana na Ebola

    S

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mkurugenzi wa Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), Dkt. Jean Kaseya, pamoja na viongozi wa Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Uganda, wameitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada wa kifedha ili kudhibiti kuenea kwa Ebola.

    Katika taarifa ya pamoja, viongozi hao walisema kuwa michango ya kifedha inapaswa kuendana na kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo, ambao umesababisha vifo vya watu zaidi ya 2,600 na kuambukiza zaidi ya watu 5,500 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

    Aidha, walieleza kuwa kuchelewa kwa fedha kunaweza kukwamisha usambazaji wa dawa na vifaa vya kujikinga kwa wahudumu wa afya. Pia waliwataka wafadhili kutimiza ahadi zao, zenye thamani ya takriban dola bilioni 1.3, ili kuimarisha hatua zinazochukuliwa kupambana na ugonjwa huo.

  8. Mazungumzo ya amani kati ya Iran na Marekani huenda yakagonga mwamba - Netanyahu

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema haamini kuwa makubaliano ya kidiplomasia yanaweza kufikiwa na viongozi wa Iran, akisema ana mashaka kuhusu uwezekano wa kutatua tofauti kati ya Tehran na nchi za Magharibi kupitia mazungumzo.

    Akirejelea mkutano wake wa hivi karibuni na Trump, Netanyahu alisema walijadili uwezekano wa diplomasia na Iran, lakini akaongeza,

    "Nina shaka kama makubaliano yanaweza kufikiwa na kundi hilo la Iran, ni watu katili. Nawaambia, hakuna makubaliano yanayoweza kufikiwa."

    Katika mkutano uliofanyika Jumanne jioni, akirejelea mazungumzo yake ya hivi karibuni na Trump, alisema kuwa pande hizo mbili zilijadili uwezekano wa kupata suluhu ya kidiplomasia kwa suala la Iran.

    Katika siku za hivi karibuni, juhudi za kidiplomasia zinazofanywa na wapatanishi, akiwemo Pakistan, ili kutatua mvutano kati ya Iran na Marekani zimeongezeka tena.

    Soma Zaidi Hapa:

  9. Watu 17 wafariki dunia kufuatia mafuriko ya ghafla Nepal

    d

    Chanzo cha picha, Shaktimaya Tamang

    Takriban watu 17 wamefariki dunia na wengine karibu 400 hawajulikani walipo baada ya mafuriko ya ghafla na maporomoko ya udongo kusomba vijiji na kuharibu barabara pamoja na miundombinu katika eneo la mpakani kati ya Nepal na Tibet.

    Mafuriko hayo yalitokea mapema Jumatano katika eneo la Rasuwa, kaskazini mwa Kathmandu, mji mkuu wa Nepal. Taarifa za awali zinaeleza kuwa huenda yalisababishwa na tetemeko la ardhi lililosababisha maporomoko ya theluji, na kusababisha maji ya theluji iliyoyeyuka kutiririka kwa nguvu kuelekea mto Bhote Koshi.

    Shughuli za uokoaji zinaendelea pande zote mbili za mpaka kati ya Nepal na Tibet. Hadi sasa, watu 12 wameokolewa.

    Vyombo vya habari vya serikali ya China, inayodhibiti Tibet, vimeripoti madhara makubwa, huku maafisa wa Nepal wakisema wanatarajia "hasara kubwa".

    Bodi ya Utalii ya Nepal imesema juhudi zinaendelea kubaini walipo watalii 291 na raia 93 wa Nepal, wakiwemo waongoza watalii, ambao walikuwa katika eneo lililoathiriwa.

    Miongoni mwa watu hao ni wasafiri 12 kutoka Uingereza, pamoja na raia wa Marekani, Malaysia, Afrika Kusini na India.

    Picha za video zinaonyesha maji yakitiririka kwa nguvu na kusomba sehemu za vijiji. Msemaji wa Polisi ya Nepal, Abhi Narayan Kaphle, ameiambia BBC kuwa vikosi vyote vya usalama vinashirikiana katika shughuli za uokoaji.

    Maeneo kadhaa yaliyo chini ya mkondo wa mto Bhote Koshi, unaotoka Tibet na kuingia Nepal, yako katika tahadhari kubwa. Barabara, mawasiliano na huduma za umeme zimekatizwa katika maeneo yaliyoathiriwa.

    Mamlaka pia zimesema barabara kuu inayounganisha eneo hilo na Kathmandu imefungwa.

  10. Trump aagiza bendera za Marekani kupeperushwa nusu mlingoti kumuenzi Dolly Parton

    d

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump ameagiza bendera za Marekani kupeperushwa nusu mlingoti kwa wiki moja, kwa heshima ya mwimbaji mashuhuri Dolly Parton, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80.

    Mwandishi wa BBC America, Anthony Zurcher, amesema hatua hiyo ni nadra sana nchini Marekani.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump alisema kifo cha Parton ni "hasara kubwa kwa mamilioni ya watu", akiongeza kuwa "hakujawahi kuwa na mtu kama yeye, na hakutakuwa na mtu kama yeye tena."

    Alimalizia ujumbe wake kwa kusema: "Dolly, pumzika kwa amani. Dunia inakupenda."

    Marais wote wa zamani wa Marekani ambao bado wako hai pia wametoa salamu za rambirambi, wakisifu muziki wa Parton, kazi zake za hisani na mchango wake katika utamaduni wa Marekani.

    Bill Clinton

    Rais wa zamani Bill Clinton alimwelezea Parton kama mtunzi wa nyimbo na msanii "wa kipekee", aliyesimulia maisha ya Wamarekani wa kawaida kwa uhalisia, unyenyekevu na hisia za dhati.

    Clinton alisema yeye na mkewe, Hillary Clinton, wamekuwa mashabiki wa Parton tangu walipokutana naye mwaka 1974. Pia alisifu mchango wake katika kuendeleza elimu ya kusoma na kuandika.

    George W Bush

    Rais wa zamani George W Bush alisema yeye na mkewe Laura walivutiwa na muziki na mtindo wa mavazi wa Parton.

    Alisema Parton alikuwa msanii aliyewaburudisha wengi, lakini zaidi ya yote alikuwa "mtu mwenye moyo wa upendo".

    Pia alisifu juhudi zake za kuendeleza elimu ya kusoma na kuandika, kuhamasisha maisha yenye afya na kusaidia jamii.

    Barack Obama

    Rais wa zamani Barack Obama alisema ni vigumu kumfikiria mtu mwingine aliyekuwa na ushawishi mkubwa kama Dolly Parton.

    Obama alitaja baadhi ya shughuli zake za hisani pamoja na tuzo nyingi alizopokea katika kipindi cha maisha yake.

    Joe Biden

    Rais wa zamani Joe Biden alisema Parton alikuwa "mtetezi asiyechoka wa haki za wanawake na usawa".

    Aliongeza kuwa, zaidi ya mafanikio yake katika muziki na kazi za kijamii, Parton alikuwa mtu aliyewatendea wengine kwa "wema na heshima".

  11. Ajuza wa miaka 101 akamatwa kwa kuuza bangi

    d

    Chanzo cha picha, NDLEA

    Ajuza, ambaye mamlaka zinaamini kuwa na umri wa miaka 101, amekamatwa nchini Nigeria kwa madai ya kuuza bangi, katika tukio lililowavutia wengi.

    Esther Ogunmabo, anayefahamika kama bibi mkongwe, alikamatwa Jumamosi katika Jimbo la Ogun, kusini-magharibi mwa nchi hiyo, kulingana na taarifa ya Shirika la Kitaifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya (NDLEA).

    Femi Babafemi, Mkurugenzi wa mawasiliano wa shirika hilo, alisema kuwa mwanamke huyo mwenye umri wa zaidi ya miaka 100 alikutwa akiwa na "vifurushi vilivyokusudiwa kwa ajili ya kuuzwa rejareja vya 'skunk', aina ya bangi yenye uzito wa gramu 90, ambayo anadai kuwauzia wakazi wa eneo hilo."

    Shirika la NDLEA lilieleza kuwa mtuhumiwa aliwaambia wachunguzi kuwa alianza kujihusisha na biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya baada ya duka lake kuteketezwa kwa moto.

    Aliachiwa kwa dhamana.

  12. Marekani yasitisha kwa muda utoaji wa viza

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amesitisha kwa muda, utoaji wa viza, kwa wanaotaka kusafiri nchini humo kutoka maeneo tofauti duniani.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wa Marekani, amesema kuwa wizara hiyo imeanzisha mpango wa kutoa mafunzo katika balozi zake kote duniani, na watarekebisha jinsi huduma ya kutoa viza inavyoendeshwa.

    Marekani imekuwa ikiendeleza kampeni kali ya kuwafurusha wahamiaji wasio na vibali vya kuishi nchini humo.

    Kulingana na Marekani, hii ni mojawapo ya hatua za kuimarisha usalama wa ndani wa taifa hilo.

    Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Marco Rubio, ametetea msimamo mkali wa serikali ya taifa hilo, akisema kuingia Marekani kunapaswa kuamuliwa kwa kuzingatia maslahi ya kitaifa ya nchi hiyo.

    Hatua hiyo inakuja miezi kadhaa baada ya Washington kutangaza mipango ya kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya balozi za taifa hilo zilizoko barani Afrika.

    Soma pia:

  13. Takriban watoto 14 wameteketea wakiwa hospitalini, nchini Pakistan

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Takriban watoto wachanga 14 wamefariki baada ya moto kuteketeza wodi ya watoto katika hospitali moja mjini Islamabad, nchini Pakistan.

    Moto huo unasemekana kusababishwa na hitalafu ya mfumo wa kiyoyozi.

    Moto huo ulianza mapema leo asubuhi katika Taasisi ya Sayansi za Tiba ya Pakistan (PIMS), kwenye ghorofa la tatu lenye wodi ya mama na mtoto.

    Tukio hilo ni miongoni mwa matukio mabaya zaidi ya moto kuwahi kutokea katika hospitali nchini Pakistan.

    Kulikuwa na watoto wachanga 16 katika wodi hiyo wakati moto huo ulipozuka, mmoja aliokolewa.

    Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amezitaka mamlaka husika kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu tukio hilo.

    “Wahusika wanapaswa kutambuliwa na hatua kali zaidi zichukuliwe,”

    Soma pia:

  14. Mlango Bahari wa Hormuz bado umefungwa - Iran

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Kazem Gharibabadi, amejibu madai ya Rais wa Marekani Donald Trump kuwa Marekani “imeondoa kabisa mabomu ya baharini” katika Mlango Bahari wa Hormuz.

    Gharibabadi amesema kuwa “Ikiwa kweli Marekani imeondoa mabomu hayo, kwa nini hakuna meli ambayo imeweza kupita katika Mlango wa Hormuz hadi sasa?”

    Ameongezea kuwa madai ya Marekani ni “uongo na propaganda”.

    Naibu huyo wa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, pia alitishia kwamba ikiwa meli za Marekani za kuondoa mabomu ya baharini zitaingia katika eneo hilo, zitalengwa na Iran

    Kauli yake imekuja wakati Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Oman yuko mjini Tehran, huku kukiwa na makubaliano kati ya Oman na Iran kuhusu kuanzishwa kwa njia mbadala ya kupitisha meli za kibiashara katika Mlango bahari wa Hormuz.

    Gharibabadi alisema hata kama makubaliano kati ya Tehran na Muscat yatakamilika, haimaanishi kuwa Mlango wa Hormuz utafunguliwa mara moja.

    Iran na Oman zimekubaliana nini kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz?

    Akieleza kuhusu makubaliano hayo,Gharibabadi alisema njia ya kuingia katika Ghuba ya Uajemi itapitia katika maji ya Iran, huku njia ya kutoka ikipitia katika maji ya Oman. Hata hivyo, meli zinazosafiri katika pande zote mbili zitapita katika maji ya Iran.

    Kulingana na shirika la habari la Iran, IRNA, Naibu Waziri huyo alisema njia hiyo itakuwa kama “barabara kuu yenye njia mbili”

    Hata hivyo, alisisitiza kuwa njia hiyo iliyokubaliwa kati ya Iran na Oman ni ya muda, na kwamba nchi hizo mbili zitafanya mazungumzo ndani ya siku 30 hadi 60 ili kuamua njia mpya ya kudumu.

    Gharibabadi,alisema kuwa baada ya makubaliano hayo, njia ya kusini ya Mlango bahari wa Hormuz itafungwa. Oman pia imekubali kufungwa kwa njia hiyo na itaarifu Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini kuhusu suala hilo.

    Kiongozi huyo wa Iran pia amesema kuwa iwapo hakutakuwa na maelewano ya kudumu, Mlango Bahari wa Hormuz utaendelea kufungwa.

    Soma pia:

  15. Baraza la amani Gaza laonya Hamas kuhusu kuchochea vita

    .

    Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images

    Baraza linalosimamia amani eneo la Gaza, linaloongozwa na Marekani, limeionya kundi la Hamas, dhidi ya kurusha tiara au ndege za karatasi, baada ya Israel kutishia kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi.

    “Shughuli zozote za kijeshi huko Gaza lazima zisitishwe, ikiwemo kurusha ndege za karatasi,” afisa mmoja wa Baraza la Amani, ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema. “Tumewasilisha ujumbe huu moja kwa moja kupitia utaratibu uliopo.”

    Aliongezea kuwa “Israel nayo lazima iheshimu usitishaji mapigano.”

    Ndege za karatasi zilizorushwa kutoka Ukanda wa Gaza siku za hivi karibuni zimeongeza tena mvutano katika maeneo yanayopakana na Gaza.

    Kulingana na vyombo vya habari vya Israel, takriban ndege 10 za karatasi zimepatikana au kuzuiwa katika siku za hivi karibuni, huku Israel pia ikiripoti kurusha ndege zisizo na rubani.

    Hamas imekanusha kuhusika na urushaji wa ndege hizo za karatasi, ikisema watoto walioko Gaza ndio waliozirusha.

    Shirika la Utangazaji la Israel, Kan, lilinukuu jeshi la Israel lilolosema kuwa ndege hizo zilizopatikana hazikuwa na vilipuzi wala vitu vya kutiliwa shaka.

    Soma pia:

  16. Canada yalipiza kisasi kwa kuongeza ushuru kwa bidhaa za Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Canada imetangaza ushuru wa kulipiza kisasi wa hadi asilimia 50 dhidi ya bidhaa mbalimbali kutoka Marekani, ikiwa ni hatua ya kujibu ushuru mpya kwa bidhaa za Canada, uliotangazwa na Rais Donald Trump mwishoni mwa wiki iliyopita.

    Ushuru huo wa Canada utatozwa kwa bidhaa za Marekani zenye thamani ya karibu dola bilioni 28 za Canada, sawa na dola bilioni 20 za Marekani, kuanzia bidhaa za chuma hadi samani,pamba na Samaki aina ya tuna.

    Orodha ya bidhaa za Marekani zitakazolengwa imeandaliwa ili kuendana na bidhaa za Canada ambazo zimewekewa ushuru na Marekani. Ushuru huo wa Canada utaanza kutekelezwa tarehe 8 mwezi Septemba.

    Hatua hii inajiri baadaya kuongezeka kwa mvutano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili, baada ya mazungumzo ya kibiashara kati ya Marekani na Canada kugonga mwamba wiki iliyopita.

    Soma pia:

  17. Tumeondoa mabomu yote ya baharini katika Mlango wa Hormuz - Trump

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema Jeshi la Wanamaji la Marekani limeondoa na kulipua mabomu yote ya baharini katika Mlango Bahari wa Hormuz,ambayo ni njia muhimu ya majini ambayo Iran kwa kiasi kikubwa imeifunga tangu kuanza kwa vita Mashariki ya Kati.

    “Iran imearifiwa kwamba meli au boti yoyote itakayoweka mabomu mapya ya baharini itateketezwa mara moja,” Trump alisema kupitia mtandao wake wa Truth Social.

    Kufungwa kwa Mlango huo kumesababisha kupanda kwa bei ya mafuta katika masoko ya dunia. Trump amekuwa akisema mara kwa mara kwamba Marekani inadhibiti eneo hilo, huku Iran ikifyatulia risasi meli zilizojaribu kuvuka bila idhini yake.

    Soma pia:

  18. Gwiji wa muziki wa country Dolly Parton afariki dunia akiwa na miaka 80

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanamuziki mashuhuri wa muziki wa country, Dolly Parton, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80, familia yake imetangaza kupitia mitandao yake ya kijamii.

    "Maumivu yako kwetu, si kwa Dolly," alisema mpwa wake, Brian Seaver, katika video iliyotangaza kifo chake.

    Parton, aliyekulia katika Milima ya Smoky katika jimbo la Tennessee, atakumbukwa kwa nyimbo zake zilizokuwa zikisimulia hadithi za maisha, zikiwemo Coat of Many Colors, Jolene na I Will Always Love You.

    Gwiji huyo wa muziki wa country aliuza zaidi ya rekodi milioni 100 duniani kote na aliandika zaidi ya nyimbo 3,000.

    Parton aliuchukulia uandishi wa nyimbo kwa uzito mkubwa na alijitambulisha zaidi kama mtunzi wa nyimbo.

    "Ni njia yangu ya kujieleza. Ni tiba yangu," aliwahi kusema.

    Mbali na muziki, Parton alikuwa mfanyabiashara mahiri. Ucheshi na haiba yake vilimsaidia kudumu katika tasnia ya burudani kwa zaidi ya miaka 60.

    "Dolly aliishi katika mwanga na sasa yuko mikononi mwa Yesu, bila shaka," alisema mpwa wake.

    Dolly Parton alizaliwa mwaka 1946 katika familia maskini ya wakulima iliyokuwa ikiishi katika nyumba ndogo yenye chumba kimoja kando ya Mto Little Pigeon huko Tennessee.

    Alikuwa wa nne kati ya watoto 12. Baba yake, Robert Lee Parton, alikuwa mkulima wa tumbaku na alilipa misionari kwa gunia la unga wa mahindi ili amsaidie kumleta duniani.

    Parton alisema mama yake, Avie Lee, alikuwa akiimba nyimbo za jadi mara kwa mara. Pia alipewa msukumo na shangazi yake, aliyekuwa akipiga gitaa na kutunga nyimbo.

  19. Hujambo natumai umzima karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 26/08/2026.