Iran yakanusha madai ya kutumia ndege za kiraia kusafirisha askari na silaha Yemen

Chanzo cha picha, EPA
Naibu mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amekanusha madai yoyote kwamba Iran inatumia safari za ndege za kiraia kusafirisha askari au vifaa vya kijeshi kwenda Yemen.
Katika barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na rais wa zamu wa Baraza la Usalama, Gholamhossein Darzi alipinga madai ya Marekani kuhusu nafasi ya Iran katika kuvuruga utulivu nchini Yemen na matumizi ya kijeshi ya safari za ndege za Iran kuelekea Sanaa.
Akirejelea athari za kibinadamu zinazotokana na vikwazo vya muda mrefu dhidi ya uwanja wa ndege wa Sanaa, alisisitiza kuwa safari hizo za ndege zilifanyika kwa madhumuni ya "kibinadamu".
Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa pia alikosoa hatua za kijeshi za Marekani nchini Yemen, akiishutumu Washington kwa kukiuka mamlaka na ukamilifu wa ardhi ya nchi hiyo pamoja na kuchochea mivutano katika eneo hilo.
Mwezi mmoja uliopita, serikali ya Yemen inayoungwa mkono na Saudi Arabia na yenye makao yake Aden ililenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa jiji hilo ili kuzuia ndege ya shirika la Mahan kutua Sanaa, na shambulio hilo lilisababisha wimbi jipya la mapigano kati ya Wahouthi na Saudi Arabia.
Serikali ya Yemen inaona safari ya ndege ya Mahan kwenda Sanaa kuwa ukiukaji wa anga yake.
Wahouthi, ambao ni washirika wa Iran, wanaona "zingiro la anga" dhidi ya Sanaa kuwa kinyume cha sheria. Iran na Wahouthi wamesema kuwa safari hizo za ndege zitaendelea.


































